The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwanahistoria Mohamed Said: Miaka 60 ya Uhuru Lakini Hatuijui Historia Yetu

Nguli huyo wa historia nchini anabainisha umuhimu wa watu kujua historia yao akisema kwamba mtu akinyang’anywa historia yake ndio amenyang’anywa utu wake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnamo Oktoba 9, 2021, The Chanzo, ilikutana na kufanya mahojiano maalum na mwahistoria na mwandishi wa vitabu, ambaye ametumia maisha yake mengi kuweza kuwasilisha historia ambayo unaweza kusema ina utofauti fulani na ile historia ambayo imekuwa ikifundishwa na shuleni na vyuoni. Na huyu si mwingine bali Sheikh Mohamed Said.

Mazungumzo kati ya The Chanzo na nguli huyu wa historia ya Tanzania yalifanyika ikiwa taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, na bila shaka Tanzania baada ya muungano wa mwaka 1964, na tulikuwa na shauku ya kutaka kupata mtazamo wake kuhusiana na safari hii ya miongo sita ya shubiri na asali katika historia ya Tanzania. 

Kama ulikuwa hufahamu, moja ya mambo makubwa tu ambayo Mohamed ameyafanya kwenye maisha yake ni kuandika kitabu kuhusu maisha ya mwanaharakati na mpigania uhuru wa Tanganyika Abdulwahid Skyes ambacho kinaitwa Maisha Na Nyakati Za Abdulwahid Sykes (1924-1968): Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati Za Waislam Dhidi Ya Ukoloni Wa Waingereza Katika Tanganyika.

Kitabu hicho cha kwanza kilichapishwa mwaka 1998, ambacho kilichapishwa kwa lugha ya Kiingereza lakini kipo pia cha Kiswahili, na vitabu vyote hivi vinapatikana kwenye maktaba zetu zote nchini. Yafautayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya The Chanzo na Sheikh Mohamed Said. Endelea … 


The Chanzo: Tunashukuru sana kupata fursa hii ya kuzungumza na wewe. Labda kwa kuanzia tu, na kwa niaba ya watu ambao hii ni mara yao ya kwanza kukufahamu, kama ungepewa fursa ya kuelezea maisha yako ndani ya sentensi moja, ungejielezea vipi?

Mohamed Said: Mimi Mohamed Said ni mtoto wa mjini Dar es salaam. Ningesema hivyo tu.

The Chanzo: Sasa kama nilivyotangulia kusema kwenye utangulizi wangu, mnamo Disemba 9 mwaka huu [wa 2021], Tanganyika itakuwa inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kingereza. Nilikuwa nataka kupata tathmini yako kama mwanahistoria, unaitazama vipi miaka hii 60 ya Tanganyika huru, na baada ya muungano na Zanzibar mwaka 1964,  Tanzania, ipi tathmini yako katika safari yote hii, hususani katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na kijamii?

Mohamed Said: Mimi huko kwenye uchumi sijui kitu, labda nitazungumza kwenye siasa na historia na ndio jamii yenyewe hiyo. Nitakwambia kitu nje ya swali ulilouliza kuwa tunasherehekea miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, kama ulivyosema, mimi nimeandika kitabu cha Abdu Sykes na kilichonisukuma ni ile kuwa nikimfahamu marehemu Abdu alikuwa rafiki wa baba yangu na ujana wao unakwenda leo sasa ni miaka 100, toka wanazaliwa [Mtaa wa] Kipata, [jijini Dar es Salaam] pale wako pamoja mpaka wamehitimishana. 

Ile Disemba 9, alinihadithia mwanae [Abdu anayeitwa] Kleist, anasema: “Siku ile mimi na baba tulikuwa uani kwetu tunasikiliza redio, sherehe za uhuru zimepamba moto, bendera ya Mwingereza inashuka na bendera ya Tanganyika inapanda.” Kleist alikuwa mdogo maana kazaliwa mwaka 1950, kwa hiyo, mwaka 1961, alikuwa kijana wa kama miaka 10 hivi. 

Anasema: “Ilivyokuwa bendera ya Tanganyika inapanda, baba alijiinamia machozi yakawa yanamtoka.” Nikamuuliza Kleist, “baba alikuwa analia?” Akasema, “Naam, alikuwa analia.” Kipi kilikuwa kinamliza? Anasema [Kleist], “Mimi nimekuwa mkubwa sasa, nadhani kilichokuwa kinamliza ni kuwa juhudi yote ile aliyokuwa amefanya kwenye [Tanganyika African Association] TAA” — na TAA alianzisha baba yake [Kleist mwaka] 1929 akiwa katibu na mfadhili wa African Association na jamaa wengine. 

Anasema [Kleist], “Baba nadhani alikuwa analia kuwa bendera ya Tanganyika inapanda na swahibu wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anachukua uongozi wa nchi yeye Abdu Sykes hajaalikwa kwenye sherehe zile.” [Kleist] anasema anadhani baba [yake] kilikuwa kinamliza hiki. Mimi nikamwambia inawezekana vile vile ni kilio cha furaha. Akasema, “Sidhani kwa sababu nilikuwa naona  sura ya baba ilikuwa si ya kuonesha furaha.” 

Ndio, lazima ufurahi nchi umekomboa lakini vipi kuwa leo Mwalimu anapokea nchi, wale watu ambao alikuwa nao hawapo jirani yake? Kuna sura nyingine? Wewe hujui. Abdu Sykes ndio alimuweka Nyerere kwenye yale madaraka aje akamate nafasi ya Rais wa TAA 1953 na mwaka 1954 wanaunda TANU wakidai nchi yao. Na ukitaka ushahidi kuwa kadi namba moja ni ya Nyerere, kadi namba mbili ni ya Ali Sykes na kadi namba tatu ni ya Abduwahid Kleist Sykes. 

Kwa hiyo, nadhani kwa maelezo hayo mafupi kidogo umeelewa. Sasa nilikuwa nimekutangulizia kuwa miaka 60 lakini hatuijui historia yetu kuwa tumefika fika vipi mpaka tukaweza kuichukuwa nchi yetu kutoka mikononi mwa Waingereza. Wale waliohangaika, wazalendo wenyewe hawafahamiki.

The Chanzo: Na hapo umenileta kwenye swali langu jingine na umeelezea vizuri kwamba historia yetu hatuifahamu. Labda kwa mtazamo wako wewe ni nini kinakosekana  kwenye historia tunayofundishwa kuhusu taifa la Tanganyika, na baadae Tanzania, ambacho unadhani kimepelekea hali hiyo? Ni nini kama utakuwa na uwezo wa kuainisha mambo yanayokosekana kwenye historia yetu ambayo yamejenga uelewa uliopo?

Mohamed Said: Khalifa swali hili naulizwa kila siku. Hakai mtu kunihoji mimi, hasa akiwa amekwishakisoma kitabu wa Abdu Sykes, [asiseme], “Ah! Ndio mambo yalikuwa namna hii, mbona historia hii sio tunayoijua sisi?”  Mimi nakupa wewe changamoto, swali hili ukiniuliza mimi utanionea. Nitakujibu nini? Kawaulize — maana umesema unafanya kipindi na watu mbalimbali — hebu waulize watu [au] viongozi wa [chama tawala, Chama cha Mapinduzi] CCM, kwa sababu wao wameandika historia ya TANU toka mwaka 1954 mpaka 1977. 

Hawa ndio warithi wa African Association, warithi wa TAA, warithi wa TANU. TANU imeanzishwa katika jengo la African Association ambalo limejengwa kati ya mwaka 1929 hadi 1933. Na waliojenga hili jengo ni kina baba yake [Kleist], na yeye anasema alipokuwa mdogo alikuwa anaenda pale na baba yake, maana walikuwa wanajenga kwa kujitolea.  

Waulize [CCM], mbona historia ya chama chenu imekuwa hivi? Wazalendo wenu mbona hatuoni picha zao hapa? Hatuwasomi, hatuwajui? Mbona hatuoni picha ya Mzee Kleist hapa? Mbona hatuoni picha ya Mzee Iddi  Musubi hapa? Mbona hatuoni picha ya Abdu? Mbona hatuoni picha ya Joseph Kimalandu? Mbona hatuoni picha ya Joseph Kasela Bantu hapa? Mbona hatuoni picha ya fulani fulani, vipi? Nyie hamuwathamini hawa watu kama [wazee] waliopigania uhuru? Hiyo ni Dar es salaam.

Twende labda Kanda ya Ziwa. Ali Vigeyo mbona haonekani? Hatumuoni Paul Bomani. Kina mama pia. Mbona hatumuoni hapa Bi Tatu binti Mzee? Mbona hatumuoni Titi Mohamed? Mbona hatumuoni Bi Chiku binti Kisusa? Mbona hatumuoni Halima Serengia? Mbona hatumuoni Lucy Lameck? Namna hiyo. Waambie mbona hiyo historia mmeiacha hivyo hivyo watu hawaijui? Sasa jibu lake litakuwa jibu kamili. Sasa ukiniuliza mimi nitakwambia nini?

The Chanzo: Mimi nakuhaidi nitajaribu kuuliza lakini nataka na wewe uniambie. Huwezi kulikwepa hili swali.

Mohamed Said: Nitakujibu lakini Khalifa wewe hutalipenda jibu langu.

The Chanzo: Mimi nimejiandaa kwa majibu yoyote mpaka nimeamua kuja hapa. Nataka uniambie imetokeaje tokeaje mpaka hali ikawa hivyo unavyozungumzia wewe, kwamba hao watu wote ambao umewataja hawapo kwenye historia rasmi ya Chama cha Mapinduzi. Nina shauku ya kutaka kufahamu.

Mohamed Said: Nitakwambia jibu langu. Kuna mtu nilimpa jibu hili hakupenda, akanambia, “Mohamed mimi nakuuliza maswali ya maana wewe unaniletea majibu ya kitoto bwana.” [Jibu nililompa ni kwamba] inawezekana Mwalimu Nyerere mwenyewe hakuwa anaijua historia kabla yake. Hakuwa anawajua kina Sykes na mchango wao. Hakuwa anamjua Abdu, ndio maana yakatokea haya. Akadhani labda mambo yalianza na yeye mwaka 1954. Maana hata ile 1953 hajasema. Hivi unajua Nyerere aligombea urais wa TAA ukumbi wa Anatouglou na Abdu Sykes?

The Chanzo: Hapana, sijui.

Mohamed Said: Na Nyerere akashinda kwa tabu sana, na katika uongozi akawa yeye ndio Rais, Makamu wa Rais akawa Abdu Sykes, Kasela Bantu akawa Katibu Mkuu, Mzee [John] Rupia akawa Mweka Hazina, Ali Sykes akawa Mweka Hazina mdogo. [Mwalimu] hajasema haya. Kwa hiyo, shida ndio inakuwa hii. 

Sasa huenda yeye [Mwalimu] hakuwa anajua kabla yake yeye. Na wala hasemi kuwa Rais wa TAA alitakiwa kuwa Chief Abdalah Makwaia, ndio Abdu alikuwa anamtaka na walishazungumza 1950 ile. Hajasema kuwa mabadiliko hasa ya TAA yalikuja 1950 baada ya kuondolewa wazee waliokuwa wameshika chama. Walikuwa Mzee Mwalimu Thomas Plantan, hajasema. Uongozi ukaingia mpya, Vedasto Kyaruzi akawa Rais na Abdu Sykes akawa Katibu nafasi ile ile aliyoishika baba yake. 

Shinikizo kubwa lilitoka kwa Schneider Plantan. Unajua hawa  kina Plantan na kina Sykes ni ndugu. Unajua kulikuwa na familia hapa zikiendesha mambo katika mji wa Dar es salaam. Kulikuwa na kina Sykes, kuliwa na kina Plantan alafu kuna kina Chaurembo.  Hawa kina Chaurembo hata kwenye dini walikuwa na elimu kubwa, kulikuwa na Chaurembo, Liwali wa Dar es Salaam, kama Hakimu pale Mahakama ya Mwanzo.  

The Chanzo: Kwa hiyo, unataka kuniambia kwamba hali hiyo imetokea kibahati mbaya? 

Mohamed Said: Sasa, hiyo utajiambia wewe mwenyewe, usiniulize mimi. Wewe mwenyewe pima, inawezekana vipi ikaandikwa historia [ya nchi na chama] hawa niliokutajia hata kwenda kuwahoji hawakwenda kuwahoji? Lakini nitakwambia kitu kimoja. Mwanzo hapo kabla hatujaanza kipindi nimekwambia habari za Hasano Peka ambaye alikuwa kwenye jopo la kuandika historia ya TANU.

[Huyu] ameniambia mwenyewe [kilichotokea wakati wa mchakato huo wa uandishi] na kwenye kitabu nimesema. Nilimuuliza haya unayoniambia. [Nilimuuliza,] “Kaka, unaniruhusu nikutaje, nisije nikatoa habari nzito kama hizi halafu nisiwe na chanzo cha maana?” Akanambia, “Wewe kaka nitaje tu hakuna tatizo.” 

Anasema, “mimi nimekuwa TANU toka mwaka 1956, nimekuwa kachero [wa TANU] na nimefanya mahojiano na Abdu Sykes vipi TANU imekuja. Siku zile wakati tunaandika historia ya TANU, mimi nilizipeleka notes kwa kiongozi wetu’ — naweza nikamtaja jina kwa sababu hata kwenye kitabu nimemtaja — Dk Mayanje Kiwanuka, yeye ndio alikuwa anaongoza utafiti na uandishi ule. 

Alivyompatia zile notes, [Kiwanuka] akamwambia [Peka]: “Tunayoandika ni historia ya TANU [na historia hii] haina uhusiano wowote na Abdu Sykes.” [Peka] anasema akashituka maana alipokuwa akiingia ofisi za TANU alikuwa anamkuta pale na ndio katika viongozi wa juu wa TANU.  Anasema historia gani ya TANU itakuwa bila kumtaja Abdu Sykes, [mtu mwenye] kadi namba tatu? Mtu aliyemkaribisha Mwalimu Nyerere Dar es salaam na akaishi naye nyumbani?   Na [aliyeshiriki] mikutano yote ya siri mpaka kunyanyuka kwa TANU, [ukiwemo] mkutano wa siri wa kwenda [Umoja wa Mataifa] UNO [ambayo yote] ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Abdu?

Lakini mimi akanisaidia kitu kimoja, akanambia nakupa majina ya watu maktaba Dodoma nenda ukawaone hawa na waambie mimi nimekutuma, wao wakitaka wataniuliza.  Na kweli walinipa msaada mkubwa. Kila faili ambalo nililiomba nililetewa, lakini kwa bahati mbaya ndani kulikuwa hamna kitu. Mimi nimeletewa faili la Abdu Sykes Makao Makuu ya CCM, Dodoma. Nimeona faili la Mzee Mwapachu. Lakini ni faili tu juu, ndani hamna kitu. 

The Chanzo: Hii yote kusema ukweli, namaanisha nikijaribu kusema nilichokipata kwenye maelezo yako, inaonesha hii hali haikuwa ya bahati mbaya. Ni kitu kilipangwa. Kwa nini unafikiria walifanya hivyo?

Mohamed Said: We Khalifa matata sana, nilijua wewe Khalifa utakuja kunipa shida wewe. Tangu nilipokuona nilijua huyu, mimi sina salama na Khalifa. Mimi sichopoki hapa, toka mwanzo nilivyokujua. Si nina uzoefu wa kuhojiwa? [Anacheka].

The Chanzo: Wewe mwenyewe umenambia, maana ndio tumekuja hapa.

Mohamed Said: Nitakwambia. Kleist alipounda African Association, yeye pamoja na wenzake kama saba hivi, anasema kuwa wengi wao walikuwa ni Waislamu. Kwa sababu Kleist ameandika muswaada wa kitabu. Aliacha muswaada wa kitabu kabla hajafariki mwaka 1949. Kwa mkono wake ameandika, akamwachia mwanae Abdu. 

Na sijui kwa nini wakati huo hakuchapa kitabu, sijui kwa nini. Sasa ile AA ikawa na ushawishi mkubwa sana wa Uislamu ndani yake. Ilipofika mwaka 1933, manung’uniko mengi ya Waislamu yalikuwa yanapitishwa African Association. Sasa akaona hii si sawa kwa sababu hiki chama tunataka kiwe cha watu wote. Sasa hiki chama cha watu wote na nyie mambo yenu ya dini mnaleta mule inakuwa si sawa. 

Kwa hiyo, yeye na Mzee Bin Sudi, ambaye alikuwa Rais wa AA wakati ule, wakaamua kuanzisha chama kingine pembeni ya African Association, [kikaitwa] Ayatullah Islamia Tanganyika, [yaani kwa Kiswahili ikiwa na maana ya] Umoja wa Waislamu Tanganyika. Wakajenga shule na ofisi yao ikawa pale, siku zile ukiitwa Mtaa wa Stanley na New Street, halafu baadae ukaitwa Aggrey na sasa Makisi Mbwana 

The Chanzo: Unaitwa?

Mohamed Said: Makisi Mbwana, ni kati ya wazee wa TANU. Alikuwa kwenye Baraza la Wazee wa TANU, walikuwa na nguvu sana wazee wa TANU. Sasa na ile ushawishi wa Waislamu katika kudai uhuru wa Tanganyika haukuondoka. Hata ukitazama picha, wewe tazama picha zote za Mwalimu Nyerere wakati wa kudai uhuru, utakuta amezungukwa na Waislamu watupu. Aghalabu ukute wametokea wengine wako naye, zote tazama. 

Na mwenyewe siku ya kwanza anasema, mimi niliaminika mapema sana na wazee, lakini pale kama ameruka, ilikuwa aseme mimi walioniaminisha walikuwa ni Abdu na Hamza Mwapachu na vijana wengine kina Steven Muhando ndio walikuwa naye. Wakina Kasela Bantu hawa ndio walikuwa naye pamoja. Lakini hao wengine walikuwa wageni, waliokuwa wenye mji ndio hao kina Ali, Dossa ndio wenye mji wao. Ujue ile Dar es Salaam ya 1950s sio Dar es salaam unayoiona siku hizi.   

Sasa nadhani hofu imekuja, kwa sababu uhuru ulipokuja ulikuja na changamoto kubwa, na changamoto ya kwanza ilikuwa ndani ya halmashauri ya TANU pale Lumumba. Walikuja watu wawili Rajab Diwani na Selemani Kitundu, ndani ya Halmashauri Kuu wakasema kuwa, maana Waislamu walikuwa na taasisi nyingine ina nguvu sana ya East African Muslim Welfare Society ambayo ilikuwa  imejenga shule karibu nchi nzima. 

Agha Khan huyo, Agha Khan alikuwa anasema, Muislamu ukichangia shillingi na mimi nitachangia shilingi. Kwa hiyo, kwa mwaka labda tuseme Waislamu wamekusanya milioni moja, Agha Khan anatoa millioni moja kuwatia nguvu watu kufanya mambo yao wenyewe. Ilipokuja uhuru sasa, 1961 ile, 1962 Sheikh Hassan bin Amir, huyu alikuwa katika kamati ya ndani TANU, na ndio alikuwa Mufti wa Tanganyika lakini Mzanzibari, na yeye alikuwa anasimama bega kwa bega na Nyerere. Kwa hiyo, watu walikuwa wakimuona Sheik Amir wanasema hiki chama chetu hakuna wasiwasi huyu mtu wetu, Mufti mwenyewe yuko naye. 

Kwa hiyo, ile nguvu ikatia hofu. Kwa hiyo, mwaka 1962 Sheik Amir aliitisha mkutano ulioitwa Muslim Congress, zilikuwa mbili, ya 1962 na 1963, na katika maazimio waliokuja nayo, moja, kama sio mawili, ilikuwa East African Muslim Welfare Society ijenge shule wilayani, mikoani na mwisho ijenge Chuo Kikuu kwa sababu Waislamu walichelewa sana, walicheleweshwa na ukoloni, waliwadhulumu katika elimu. Sasa likaja suala ndani ya 1963 ndani ya Halmashauri Kuu ya TANU kwamba Agha Khan anataka kutawala nchi hii na [hili lililetwa na] Waislamu, [akina] Rajab Diwani na Selemani Kitundu. Titi akasimama upande wa Waislamu.

The Chanzo: Bibi Titi Mohammed?

Mohamed Said: Bibi Titi Mohammed. Akasema haiwezekani hii East African Muslim Welfare Society ilikuwepo kabla ya TANU na inasaidia Waislamu. Hayo yanayosemwa sio ya kweli. Kama wanaushahidi watoe. Sasa pale siku ile …

The Chanzo: Madai yalikuwa sio ya kweli? 

Mohamed Said: Yalikuwa si kweli.

The Chanzo: Ndio.

Mohamed Said: Ukisoma kitabu utaona sio kweli. Hapo unaweza kudhani wale [akina Diwani na Kitundu] walitumwa au kwa fikra yao. Pale pakapishana maneno baina ya Nyerere na Bibi Titi, maneno makali. 

The Chanzo: Nyerere alikuwepo kwenye kikao?

Mohamed Said: Ah, [alikuwa ndio] mwenyekiti. Bibi Titi akamwambia Nyerere sikiliza bwana, mimi simuogopi mtu yoyote, mimi  namwogopa Allah peke yake. Sasa, hiyo kanambia mwenyewe [Titi] uso kwa macho wallah, nakwambia!

The Chanzo: Bibi Titi? 

Mohamed Said: Mwenyewe. Kaniambia, “Mimi tulianza kugombana na Mwalimu toka mwaka 1963, na tatizo lilikuwa hili la East African Muslim Welfare Society.” Lakini alikataa kunipa mahojiano kamili, alikataa kabisa. Aliyenipeleka alikuwa kaka Ali Sykes, kipindi hicho [Titi] ndio alikuwa amerudishiwa nyumba yake pale Upanga pale mkabala na ilipo Makao Makuu ya Jeshi [la Wananchi]. Ana nyumba ghorofa moja, nyumba nzuri, nimekwenda pale ndio akaniambia hivyo. Sasa, hii 1963 wakati Baraza la Wazee wa TANU ambalo mwenyekiti wake alikuwa ni Tulio, maana Sheikh Takadir ni historia nyingine hiyo alifukuzwa TANU kwa masuala haya ya Uislamu.

The Chanzo: Pale mwanzo umegusia kwamba hii nguvu ili wapa hofu [baadhi wa wakuu ndani ya TANU].

Mohamed Said: Swadakta.

The Chanzo: Hofu ya nini sasa?

Mohamed Said: Kuwa Uislamu utaimarika sasa. Kwa sababu unaona nguvu yao katika kupigania Uhuru wa Tanganyika. Ukisoma kitabu utaona kulikuwa na jitihada za mapambano za Waislamu. Utaona hiyo.

The Chanzo: Sasa utajiuliza hilo lina uhusiano gani na kutolewa watu kwenye historia rasmi ya upatikanaji wa Uhuru wa Tanganyika?

Mohamed Said: Kwa sababu watu wakijitambua-, laba niseme kwa n ini mimi ninasema kwa kujiamini? Kwa nini historia ninayosema wala jina langu sijifichi? 

The Chanzo: Kwa nini?

Mohamed Said: Kwa sababu wazee wangu ndio wameunda chama cha African Association, iliyozaa chama cha TAA, yote haya mimi nimeishi katika historia hii ingawa nilikuwa bado mdogo. Nimewasikia wazee wangu wakizungumza, nimepata umri nimewauliza wamenihadithia kila kitu. Wewe hujapata kusikia. Wewe ulikuwa unajua kama hizo namba, we ulikuwa unajua kadi ya Adu Sykes namba tatu na Ali Sykes namba mbili?

The Chanzo: Hapana.

Mohamed Said: Namba nne Dossa Azizi. Namba tano Denis Pombea. Namba sita Budoe. Huyu Pombea kutoka Nyasa na Budoe Mluya kutoka Kenya. Abbasi Sykes namba saba, ndugu watatu wote kwenye chama na baba yao ni mwasisi wa chama. Hayo umekuwa hujayasikia kwa sababu mtu ukimnyang’anya historia yake ndio umemnyang’anya utu wake.

The Chanzo: Na si kweli kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa anakusudia kujenga taifa la ki-secular, [taifa] ambalo halina dini na pengine Waislamu walikuwa wamedhamiria kujenga taifa la Kiislamu?

Mohamed Said: Wala hapakuwa na dhamira ya kuunda taifa la Kiislamu. Kama kungekuwa na dhamira ya kuunda taifa la Kiislamu, Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Abdu Sykes, hawa wote waliomuunga mkono, wasingemuunga mkono Nyerere. Wangemuambia Hamza, na kumwambia wewe kaa pale, Abdu kaa pale. 

Lakini katika sifa mabayo Hamza Mwapachu anamwambia Abdu kwa nini Nyerere achukue nafasi ya urais ni kuwa ni Mkristo. Tunataka chama hiki kiwe chama cha watu wote. Chama kikiwa cha watu wote, nchi unaiweka mahali pazuri. Watu wote wataona haki zao ni sawa, usiwatie watu hofu. 

Wazee wetu walipata fundisho India. Mohammad Ali Jinnah [muasisi wa taifa la Pakistan] na [Jawaharlal] Nehru, [Waziri Mkuu wa zamani wa India]. [Wazee] walikuwa wanajua historia ya India. [India] walipopata uhuru siku hiyo hiyo walianza kupigana [na kupelekea kuanzishwa kwa taifa la Pakistan]. Kwa hiyo, wazee walipata fundisho. Tatizo watu wanadhani hawa wazee wetu walikuwa wajinga. Hawa watu walikuwa wasomi. Sheikh Hassan bin Amir [alikuwa] msomi. Sheikh Selemani Takadir alikuwa msomi. Watu wamesoma Quran. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa bingwa wa kusoma Quran, wametafsiri Quran, atakuwaje zuzu mtu kama huyo? 

Katika kutoa mapendekezo ya Katiba, Edward Twining mwaka 1950, tazama ile rasimu ipo sahihi ya Sheikh Hassan bin Amir, ipo sahihi ya Sheikh Said Chaurembo. Hawa si watu ambao walikuwa hawajui mambo. Lakini watu wanaaminishwa kwamba hawa watu hawakuwepo na kama walikuwepo hawajui chochote, hawana mchango wowote isipokuwa aliyeleta mambo yakawa, akagombea nchi ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Itakuwa vipi? Sasa hapa ndio ikawa tatizo la historia likaanza kutokea hapo.

The Chanzo: Hili suala la Serikali au dola kupindisha historia za uanzishwaji wake … 

Mohamed Said: Mimi nimekuambia walikuwa hawajui historia hiyo, wewe ndio unasema walipindisha.

The Chanzo: Ndio, mimi nasema walipindisha au kuandika upya.

Mohamed Said: Halafu katika mchakato ule wa kuandika historia mpya [aliouagiza Rais John] Magufuli, na mimi nilichukuliwa katika ile kamati ya kuandika historia mpya ile ya Magufuli, nilikuwa mule ndani.

The Chanzo: Mchakato ulifikia wapi?

Mohamed Said: Mama Samia [Suluhu Hassan] aliufuta ule mchakato. Niliyoyaona mule ndani [ya kamati] nilichoka. Niliyoyaona mule ndani ya ile kamati. Mimi nilikuwepo, tulikuwa watu wengii karibu waandishi hamsini [wa historia]. Muswaada ulikuwa umeshaandikwa, sisi tulikuwa tunapitia tu. Mimi mambo mengi nilikuwa nawasahihisha, nasema hili si kweli na hili si kweli.

The Chanzo: Hiyo kamati?

Mohamed Said: Aah tumekaa pale nanii, Taasisi ya Elimu pale. Mimi nilikwenda baada kamati imeshakaa kama muda wa wiki mbili [au] wiki tatu. Kuna mtu akanipigia simu, wala simjui, akasema Mohamed mbona nasikia wewe haupo kwenye uandishi wa historia hii ya Magufuli? Aakasema mi nimempigia kule mkurugenzi mmoja nikamwambia Mohamed Said na Husseni Bashiri hawa ndio wataalamu wa historia wetu sisi atakwambieni mambo mengi nyie hamuyajui.

The Chanzo: “Wetu sisi” anamaanisha nini?

Mohamed Said:  Ana maana sisi watu wa pwani, [pwani] yote hii. Nyinyi hamjui habari zetu, mtaandika habari sio, maana si anajua historia iliyopita. Akasema hawa wapo watakusaidieni.

The Chanzo: Unasema ulichoka?

Mohamed Said: Nilichoka.

The Chanzo: Kwa nini?

Mohamed Said: Sio historia ya Tanzania ile [waliyokuwa wanataka kuandika], sio historia ya Tanzania kabisa ile.

The Chanzo: Kama kuna kitu ambacho kilikuchokesha zaidi ni kipi kati ya ulivyo viona?

Mohamed Said: Wamenambia tunataka mchango wa Tanganyika katika Vita ya Pili ya Dunia, [yaani] nini kilitokea.

The Chanzo: Walikuuliza wewe?

Mohamed Said: Eh, maana yake ndio wanajadili katika ule mswaada. Nikasema mimi nasoma zile shajara za Abdu Sykes, nyaraka za Abdu Sykes [na] anasema kitu kikubwa kilichowasaidia Watanganyika [kwenye] vita ile ilikuwa kwanza kujitambua. Maana walikuwa wanasema, “Sisi tumekuja huku Burma” — maana alikuwa kwenye Burma infantry —  

The Chanzo: Siku hizi inaitwa Myanmar.

Mohamed Said: Eeh [Anacheka]. Mi nitaita Burma tu kama tulivyokuwa tunaita. [Wakawa wanasema], “Sisi tumekuja huku kumpigania Mwingereza aendelee kututawala?” Ilikuwa inaitwa sixth battalion [kikosi cha sita], walikuwa Wanyasa kutoka Malawi, Wakenya, Waganda, Watanganyika na Wazanzibari. 

Akasema sisi tukirudi kwetu lazima hawa Waingereza tuwaondoe, lazima tufungue chama cha siasa, Abdu huyo. Tarehe 24 kuamkia 25 mwaka 1945 wako nje ya Bombay [sasa Mumbai] kambi inaitwa Kalieni Camp wanafanyiwa wazungu wanaita repatriation, wanarudi kwenye nchi zao, Abdu aliitisha kikao pale. 

Akasema jamani kama tulivyokubaliana, tusifike nchini kwetu tukabweteka, sote tufanye juhudi tufungue vyama, Waingereza waachie hizi nchi zetu. Nawaeleza [wajumbe wa kikao] tulikuwa tumekaa kwenye ukumbi lakini kila watu wamekaa peke yao peke yao. Sasa mimi nikizungumza meza ya pili utasikia wanasema, “Msikilize huyu anasema nini?” Mimi nilikuwa na laptop yangu, nikatoa picha …

The Chanzo: Kama walikuwa wanakutilia wasiwasi?

Mohamed Said: Hapana, wanataka kuniuliza. 

The Chanzo: Anha, wana shauku!

Mohamed Said: Eeh, wanauliza na mimi nikawa nawapa jibu kuwa katika hisani kubwa tulofanyiwa na Vita ya Pili ya Dunia ni kuwa wazee wetu ile [vita] iliwatia hamasa zaidi kuwa kwa nini sisi tukafe kwa kulipigania taifa jingine. Tuna shida gani sisi na Wajerumani mpaka Waingereza waje watupiganishe? Nikatoa picha moja mimi, Abdu Sykes amevaa sare za jeshi la Kiingereza na mdogo wake Ali amevaa sare za jeshi la Kiingereza lakini Abdul alikuwa ofisa utaona sare yake tofauti na ya Ali.  

Ali alikuwa na miaka 16 huwezi kuamini. Alitoroka nyumbani kwenda kuingia jeshini. Wazulu wana balaa bwana. Nikawaambia hii kama mlikuwa mnataka kuweka picha, maana walikuwa wanatafuta picha, nikawaambia wekeni picha hii. Hawa wawili, mmoja huyu Abdu ndio alipigania Nyerere achukue uongozi TAA yeye na mzee Mwapachu. Uongozi wa TAA alafu wakaunda TANU. Huyu Ali alikuwa mdogo wake yeye kadi yake namba mbili na kadi ya Nyerere namba moja kaandika huyu. 

Wao [wajumbe wengine wa kamati] wanasema tuweke picha ya Bisimin, Askari Monument ile picha ya sanamu ya askari iliyopo makutano ya barabara ya Azikiwe na Samora jijini Dar es Salaam. Nikawaambia picha ya Bisimini ina maana gani? Akasema hii inaweza kuwa na tatizo la hakimiliki. Nikasema haina tatizo la hakimiliki, mimi hizi nyaraka nilikabidhiwa na Bwana Ali, zote nifanye ninavyotaka. 

Na hivi ninavyokwambia kuna nyaraka mimi nimewapa Kigoda cha Mwalimu Nyerere kina [Issa] Shivji. Kwenye maonesho yao walikuwa wanaonesha hiyo nyaraka niliyowapa mimi, umuhimu wake ulikuwa wanapeleka barua ya pongezi kwa Queen Elizabeth kwa kutawazwa kuwa Malkia. Sasa viongozi wote pale, Mwalimu Nyerere sahihi yake ipo, Abdu Sykes, makamu wa Mwalimu Nyerere, sahihi yake ipo, Mzee Rupia, Dosa, Ali Sykes, wote pale, Budoi sahihi yake ipo.  

[Kigoda cha Mwalimu Nyerere] wakaipenda, walikuja hapa nikawaonesha, wakasema hii tunaiomba nikawapa. Wakaitia fremu nzuri, nikawaambia nyie ionesheni, wakawa wanaionesha katika maonesho yao. Ukiitazama hiyo nyaraka wameandika hii nyaraka inatoka kwa Mohamed Said. Mi nikawaandikia rasmi, nikasema hiyo itakuwa vibaya kwa sababu wenyewe wako hai, watasema hizi nyaraka kumpa Mohamed Said zishakuwa zake tena? Bora mseme mmezikuta kwangu lakini hizi nyaraka zote ni za akina Sykes. Niliwaeleza pale.

The Chanzo: Haya yote wajumbe wenzako walikuwa hawayafahamu?

Mohamed Said: Walikuwa hawafahamu. Lakini kiongozi wetu yule [kwenye kikundi chetu] alikataa kata kata. Hakutaka kuweka picha zile. Nikasema ndio yale yale. Hofu. Nikasema Bismini ni nani, Bismini hana jina yule nimekupa watu ambao nimekupa sifa zao hawa, wakakataa.

The Chanzo: Sasa hii ilikuwa ni fursa nzuri ya kurekebisha mambo kwa nini Rais Samia ameiondosha?

Mohamed Said: Ah, hairekebishi mi nakuelezea, hapo katika uandishi wenyewe ndio haya hawayataki. Ama hujanielewa Khalifa.

The Chanzo: Nakuelewa.

Mohamed Said: Vipi utakuja usikie, maana wao pengine wamefanya utafiti hii historia ina maana, bila shaka wakaona historia yenyewe ndio hiyo hiyo itakuwa haina tofauti na historia zilizopita. 

The Chanzo: Itakula tu pesa za walipa kodi. 

Mohamed Said: Alhamdulillah tumekula kiasi, tumekuwa pale tukaenda Kigulunyembe  na wamekuwa wakituweka vizuri.

The Chanzo: Mlikuwa mnakula vizuri?

Mohamed Said: Sana sana, kwa hilo nawasifia. Walikuwa-, hatupati shida yoyote. Saa nne tu chai imekuja. Saa sita chakula kimekuja. Saa kumi na moja imekuja chai na vitafunwa. 

The Chanzo: Na posho?

Mohamed Said: Na posho walitupa. Posho nzuri. 

The Chanzo: Na usafiri?

Mohamed Said: Usafiri nadhani ilikuwa kwenye posho, kwa wale waliokuwa wanatoka [Tanzania] Bara waliwapa tiketi.

The Chanzo: Kwa hiyo, mchakato utakuwa umekufa kabisa?

Mohamed Said: Aah, umekufa nashangaa Khalifa ulikuwa hujui, umekufa ule. 

The Chanzo: Mimi nilimsikia hayati John Magufuli aliposema kwamba watu wafundishwe somo la historia wakati najua somo la historia lipo kumbe kukawa kuna mambo yanaendelea?

Mohamed Said: Ni historia nyingine. Wakati mmoja [mwenyekiti wa kamati] akasema msiweke nyaraka zozote hizi za Serikali. Maana tulimaliza ile kazi na tukatia sahihi lakini mimi niliwaambia naweka sahihi tu lakini hakuna mambo kama haya. Sikuyasema gizani niliwaambia mimi hawa wazee wangu ninayoyasema nayajua, lakini kama nyinyi mna historia yenu wekeni. 

The Chanzo: Aisee, hiyo nilikuwa siijui na wenzangu  walikuwa hawajui. Basi sawa, tukirudi kwenye lile swali langu la mwanzo, hii tabia ya  mataifa au Serikali kuandika upya historia za mataifa … 

Mohamed Said: Khalifa wewe king’ang’anizi wewe [Anacheka].

The Chanzo: Ni jambo la kawaida, halikutokezea kwa Tanganyika tu.

Mohamed Said: Ni kweli.

The Chanzo: Hata ukiangalia Zanzibar kuna historia zinakinzana, hata Marekani, hata Uingereza. Wewe ni mwanahistoria na bila shaka utakuwa umetafiti haya mambo. Dola linakuwa na maslai gani? Maslai yao ni nini hasa, wanalenga kufanikisha nini [zinapoamua kupindisha historia za nchi husika]?

Mohamed Said: Hadhi zao. Si unaona hapo Kenya, imechukua miaka mingi Dedani Kimath kuwekewa sanamu. Lakini unaweza wewe kuhadithia historia ya Kenya bila kuwataja Wakikuyu? Bila kumtaja Dedan Kimathi? Ndivyo inavyokuja Tanganyika, huwezi kutaja historia ya uhuru bila kutaja mchango maalum wa Waislamu. Huwezi. Utakuwa umefanya hiyana tu. Wala huwezi wewe ukamkwepa Abdu Sykes au familia yao, hata Mwalimu [Nyerere] akikueleza historia yake, alipofika Dar es salaam alipokelewa na nani? Alikaa na nani? Nani kampa funguo za kuingia katika ofisi ya TAA? Huwezi.

The Chanzo: Kuna kitu huwa najiuliza ila sijabahatika kupata majibu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaitwa Baba wa Taifa wa Tanganyika au Baba wa Taifa la Tanzania maana Tanzania sisi ni wawili, hii imekaaje?

Mohamed Said: Hilo mimi sitokujibu, lakini nataka nikwambie kitu kimoja. Hili la Nyerere kumuitwa Baba wa Taifa anastahili. Sio kwamba hastahili. Siku ya kwanza Nyerere akasimama kwenye jukwaa anazungumza na Watanganyika anawaambia kutawalaiwa ni fedheha, 1954 hiyo. Anakwenda Umoja wa Mataifa anarudi, hali ya siasa Tangayika ilibadilika. Nyerere alifanya kazi kubwa. Mimi kitu kimoja nasikitika, na baada ya kuchapa hiki kitabu, mimi nazijua dialogues za Abdu Sykes.

The Chanzo: Kitabu chenyewe ni hiki?

Mohamed Said: Hiki ni cha Kiingereza nadhani unakijua na hiki cha Kiswashili. Zile shajara zina kila kitu. Mimi nimesoma kwa jicho langu. Nilimwomba Sykes zile shajara nisome akanikatalia. Na zile shajara mpaka leo hazijasomwa na mtu yoyote, na waliokuwepo wanasema zile shajara ndani utakuta kila kitu. Maana kuna shajara nyingine alikuwa akiandika kwa lugha isiyo na kificho na nyingine akiandika kwa lugha ya kificho. Sykes anasema [kwenye] zile za zilizoandikwa kwa kificho, 1950s ndio harakati za siasa, nadhani alikuwa ana hofu kama watamvamia kikosi cha polisi wa siri wa kikoloni wapate tabu ya kuzisoma zile shajara sio wanasoma kila kitu.

The Chanzo: Kwenye maelezo yako ni kama vile Waislamu na machango wao katika kupigania uhuru wa taifa hili ni kama vile haupewi uzito?

Mohamed Said: Sawa sawa, haujapewa ile heshima inayostahili.

The Chanzo: Sasa kwa mfano itokezee fursa ya Serikali, sasa tuna Rais tukubali tukatae ni Muislamu, kwa mfano, anasikia haya mahojiano na akataka kurekebisha baadhi ya mambo, unadhani ni vitu gani vinapaswa kufanywa ili hili liweze kurekebishwa?

Mohamed Said: Hakuna jambo nyeti nchini kwetu kama jambo lolote linalohusu Waislamu. Uislamu na Waislamu ni jambo nyeti sana sana.

The Chanzo: Kwa nini?

Mohamed Said: Hofu.

The Chanzo: Nani wanahofu?

Mohamed Said: Waliokuwa madarakani. Unajua katika Serikali yetu …

The Chanzo: [Serikali yetu] haina dini.

Mohamed Said: Hapana, huwezi kusema haina dini. Kama Serikali, watu asilimia 80 ni watu wa dini moja, useme Serikali haina dini? Watu wanafanya kazi kwa fikra zao.

The Chanzo: Hiyo umeipataje?

Mohamed Said: Ndio hulka ya binadamu. Wewe huwezi kuniweka mimi nje ya ulingo katika Bunge tuko wachache, kila mahali, mawaziri wachache, halafu ukasema Serikali hii haina dini. Si kweli. Sisi tuna Muslim School, wazee wetu walijenga ile kwa msaada wa Agha Khan [mwaka] 1933, ni jengo moja tu, Serikali haijakubali kurudisha lile jengo lakini St Joseph School, ambayo mimi nimesoma, wamerudishiwa wenyewe Wakatoliki kwa sababu wao ndio wameshika dola, wameshika Serikali wanaweza kufanya chochote.

The Chanzo: Wakatoliki wameshika dola?

Mohamed Said: Ooh Sheikh wala sio siri, nakwambia. Na wao unaweza kuwauliza ingawa hawatopenda maswali hayo. 

The Chanzo: Hiyo umeijuaje? Yaani umepitia mchakato upi mpaka kufikia hitimisho hilo?

Mohamed Said: Zipo takwimu na ukitaka kuwapa mtihani waambie embu tufanye tuite majina katika Bunge tutizame uwiano wa dini mule. 

The Chanzo: Lakini Bunge si watu wanagombea? Waislamu wanapaswa wagombee, Wakristo wanapaswa wagombee?

Mohamed Said: Na mimi nitakujibu, unapomnyima mtu elimu ndio umemuwezesha yeye kushika madaraka? Wewe unajua katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, miaka 40, 50 [sasa tangu kianzishwe], Waislamu hawajafika asilimia 10 [ya] wanafunzi? 

The Chanzo: Hiyo inatokana na nini?

Mohamed Said: Nilikuambia mi leo sisalimiki kwenye kiti hiki. Hujasikia [kitu kinaitwa] Mfumo Kristu? Mfumo wenyewe haukubadilika hata tulipopata uhuru. Hata Mwalimu siku hiyo anaondoka anasema mimi naondoka tumeyarekebisha mambo, watu wote tuko sawa sawa. Katika mauaji ya Mwembechai, kitabu cha Prof Njozi anasema bora Mwalimu angenyamaza kimya si neno lile la kusema. Kwa sababu watu watakapoenda kusimama kutazama ule ukweli watatofautiana na kauli yake. 

The Chanzo: Wewe una amini kabisa Serikali inawanyima fursa ya elimu Waislamu?

Mohamed Said: Wajibu wao [Serikali] sasa kuwa, kuna manung’uniko Waislamu wanasema, nakufundisheni hilo swali kama vile hujui. Waislamu wanasema kuwa wameminywa [fursa] kwenye elimu, nafasi za siasa, Serikali nyie mnalitazamaje hili hebu wapeni jibu Waislamu.  

The Chanzo: Wao wataniuliza wananyimwa vipi, kwa hiyo naomba unisaidie?

Mohamed Said: Kama nilivyokwambia wewe, hebu fanyeni uchunguzi kwenye Bunge, Waislamu wangapi, Wakristo wangapi?

The Chanzo: Wao watakwambia Bunge mtu anagombea.

Mohamed Said: Kwa nini nakujibu hivyo sababu unapomnyima mtu elimu unategemea awe na nguvu ya kushika madaraka yoyote? Lakini wao kama wanaona ni jambo la kubabaisha, ni jambo sio la kufanyiwa kazi sawa.   

The Chanzo: Mimi nataka kufahamu ni kwa kiwango gani Serikali inajua …

Mohamed Said: Mimi nakusaidia kuwa kama wao hawajui, si wana rekodi zote pale watizame wataona.

The Chanzo: Kwamba?

Mohamed Said: Kuna upogo mkubwa sana, nenda pale Chuo Kikuu [cha Dar es Salaam] katazame.

The Chanzo: Upogo unamaanisha nini?

Mohamed Said: Upogo yaani utofauti, kwa Kiingereza sijui unasemaje.

The Chanzo: Kati ya Waislamu na Wakristo?

Mohamed Said: Ndiyo, kubwa sana. Nenda Chuo Kikuu [cha Dar es Salaam]. Nenda chuo chochote leo. Ndio sababu ya East African Muslim Welfare Society  kuvunjwa sababu walikuwa wanataka kujenga Chuo Kikuu, waliokuwa madarakani hawakutaka Waislamu waende Chuo Kikuu.

The Chanzo: Kwa sababu gani?

Mohamed Said: Nakwambia ni hofu tu, sababu wanafikiri Waislamu wakipanda juu basi dini yao itakuwa kwenye matatizo.

The Chanzo: Lakini kulikuwa  na Rais Muislamu hapa, Jakaya Mrisho Kikwete, na saa hizi kuna Rais pia Muislamu. Unadhani kuna fursa yoyote kwa Rais aliyepo kuweza kurekebisha hali ya mambo?

Mohamed Said: Kwanza wakubaliane tunalo tatizo.

The Chanzo: Wakubaliane na wewe, wakubali wao?

Mohamed Said: Wao kwanza watazame, waseme sisi hatuwezi kwenda namna hii, [kwamba] tunalo tatizo, lipo tatizo hapa. Kuna tatizo kwa sababu Waislamu wanasema tunabaguliwa [na] hili ni tatizo tulitazameni. Sasa wakiliona lipo tatizo dawa itapatikana lakini si kwa Rais afanye mambo kienyeji, hapana. Kwanza wakubali kuwa lipo tatizo. 

The Chanzo: Hiyo inanifikirisha sana.

Mohamed Said: Sana sana. Mimi nimeandika sana kuhusu hilo. Kuhusu haya nimeandika sana.

The Chanzo: Sasa ndio maana nilikuwa nataka kujua kutoka kwako, kama mtu uliyetafiti na kuandika. Tuchukulie leo kwa mfano Serikali ikakiri kuwa tatizo lipo, wewe unadhani ni hatua zipi Serikali inapaswa kuchukua kurekebisha mambo?

Mohamed Said: Wala sio mimi. Serikali ina wataalamu wote bwana, Serikali inajua kila kitu.

The Chanzo: Lakini hapa tunazungumza mimi na wewe, yaani kwa mtazamo wako pengine huwezi jua, maana ulipigwa simu ukaitwa kwenye kuandika historia.

Mohamed Said: Khalifa hili sio swali la kuwa mimi nikwambie nini. Nakupa jibu zuri kabisa, kwanza watambue. Kama walivyotambua kuna tatizo la wanawake kuwa nje lazima wanyanyuliwe kuwa juu, kwani walijua vipi?  Vile vile walivyofanya kwa wanawake tuwe na uwiano wa jinsia katika madaraka vile vile waweke. Kuna nchi zimeangamia kwa kudhani kuwa wanaweza wakapuuza hii. Wasione hali hii iko hivi, watu wanatembea vifua vina joto. Mengine hayasemeki.

The Chanzo: Lakini mtu anaweza kujiuliza, nisamehe sana … 

Mohamed Said: Wala. Uliza chochote, nakujibu.

The Chanzo: Nakuuliza kutoka katika mtazamo usiokuwa na hatia yoyote, wewe unasema Tanzania ina Mfumo Kristo, tunaondoka vipi kwenye hiyo hali? Kama wewe unaamini, pengine kunaweza kuwa na watu wengine nyuma yako wanaamini kama hivyo.

Mohamed Said: Amezunguka hapa nchi nzima, Sheikh Ilunga [Hassan Kapungu] akafanya mikutano ya wazi, ilikuwa inatisha wakati Kikwete yupo kwenye madaraka akaeleza hali ilivyo na bahati mbaya ulikuwa hujui habari hizo.

The Chanzo: Sijui chochote. Kwa hiyo, unadhani Rais Samia hawezi kutatua hiyo hali?

Mohamed Said: Kwanza si haki. Hawezi yeye akaamka tu na kuamua. Hapa Magufuli aliwahi kuchagua mawaziri 23, mawaziri 20 Wakristo, mawaziri watatu Waislamu. 

The Chanzo: Unadhani hiyo inafanyika kwa makusudi? 

Mohamed Said: Maswali hayo ndio utawauliza wao [Serikali].

The Chanzo: Mimi nakuuliza wewe?

Mohamed Said: Umeniuliza, mimi nakupa jibu, mimi ni nani? Mimi ni raia tu, na wala swali hili asijibu mtu mwingine. Naona JamiiForums wakati mwingine watu wanauliza.

The Chanzo: Ninachouliza mimi …

Mohamed Said: Nipe fursa kidogo.

The Chanzo: Naam.

Mohamed Said: Hili sio swali la mtu kwa mtu. Hili ni swali kwa Serikali kwamba haya tutizame tatizo halafu watakuja na jibu kama hakuna dhulma hapa kila mtu apate haki zao sawa, kwisha.

The Chanzo: Wao wanaweza wakasema haifanyiki kwa makusudi, si kwamba tunasema tuchague Wakristo.

Mohamed Said: Sijui kwa nini umekuwa uking’ang’ania hapo?

The Chanzo: Nataka tu kufahamu kwa sababu mtu anaweza akajitetea.

Mohamed Said: Soma kitabu cha  Jan P. van Bergen, Development and Religion in Tanzania [: Sociological Soundings on Christian Participation in Rural Transformation]. Hiki kitabu [Serikali] wamekipiga marufuku [kuuzwa Tanzania]. 

The Chanzo: Kinaitwa?

Mohamed Said: Jan P von Bergen, Development and Religion in Tanzania, mwaka 1981, Madras ndiko aliko kichapa kule na kinauzwa Kanisa Katoliki kwenye Cathedral bookshop pale, kilipigwa marufuku kimya kimya.

The Chanzo: Kilipigwa au mpaka sasa?

Mohamed Said: Kimya kimya hakiingizwi kile kitabu sababu yale maneno mule ndani yanatisha. Soma Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara, 1953 hadi 1985 cha John Sivalon. Nakupa rejea mbili hizo alafu uje umsome Hamza Mustafa Njozi [kwenye kitabu chake cha] Mwembechai Killings [, and the Political Future of Tanzania] ameeleza mambo mengi. 

Kilipigwa marufuku hicho, Serikali ilikuwa haina majibu. [Ukiwa huna majibu] njia nyepesi ni kukipiga marufuku, halafu siwezi sema unisome mimi. Mimi sehemu ya mwisho kabisa ya kitabu changu kuna sura inasema Conspiracies against Islam. Eeh, [yaani] njama dhidi ya Uislamu nimeandika vizuri mpaka leo hawajaweza kutoa jibu.  

The Chanzo: Hebu tuibie kidogo umeandika nini?

Mohamed Said: Nimeeleza njama zilizowekwa.

The Chanzo: Na nani?

Mohamed Said: Na waliokuwa madarakani.

The Chanzo: Dola?

Mohamed Said: Unajua lazima nizungumze kistaarabu, kwa sababu watu wanatusikiliza. Na ningependa usipate tabu kurusha kipindi chako. Ndio maana nazungumza kistarabu nikiamini wewe utanielewa na anayesikiliza atanielewa. Iliwekwa njama kwanza, East African Muslim Welfare Society lazima tuivunje, inajenga shule kila mahali, hilo sio jambo zuri kweli, ivunjwe hiyo. 

Na mradi wa Chuo kikuu uvunjwe. Ikishavunjwa East African Muslim Welfare Society kila kitu kitakufa. Wakaweka [Baraza Kuu la Waislamu Tanzania] BAKWATA, nimeweka historia nzima ya BAKWATA kuanzia mwanzo mpaka mwisho.  Ni watu wawili tu ndio wamefanya utafiti wa BAKWATA, ni huyu Mayanja Kiwanuka,  yule aliyekataa kupokea notes za Abdu Sykes, mwandishi wa historia na mimi ukisoma mule. 

Hii kwanza niliandika kama paper ya kujitegemea inaitwa Islam Politics in Tanzania – 1989, niliitoa kwenye kongamano moja Nairobi, [Kenya] halafu nikaingiza kama sehemu ya tatu kwenye kitabu cha Abdu Sykes, inaeleza kila kitu.  

The Chanzo: Kwa hiyo, hata kuletwa kwa BAKWATA ni moja ya njama dhidi ya Uislamu?

Mohamed Said: Profesa Haroub Othman sio mtu mjinga. Siku nilipokutana naye aliniambia Mohamed mimi nimesoma kitabu chako.

The Chanzo: Ni marehemu tayari?

Mohamed Said: Eh, marehemu. Alisema, mimi nimesoma kitabu chako, sikuweza kustahimili. Mimi nimekwenda kwa Mwalimu Nyerere, nikamwambia mimi nimesoma na naamini wewe umesoma kuhusu yeye, na vitabu viwili chake, changu mimi na cha Muhsin Barwani [kinachoitwa] Conflict and Harmony in Zanzibar. Nikamwambia Mwalimu hii ni legacy yako.

The Chanzo: Haroub anakwambia?

Mohamed Said: Anamwambia Mwalimu, mchango wa Abdu Sykes katika kuunda TANU, watu wanajua kama wewe uliunda TANU, Mohamed kasema wewe hukuunda TANU anasema TANU wameunda akina Abdu Sykes na akaeleza vipi umeingia kwenye TANU. Halafu amesema kuwa Waislamu wamedhulumiwa, mwalimu lazima na wewe ujibu. 

Mwalimu [Nyerere] akasema sasa hivi siwezi kujibu, siwezi kuandika. Nadhani wakati huo ameanza kuumwa. Lakini alichofanya Mwalimu akamwambia nitengenezee kamati, mimi nitakuja kuzungumza na nyie mtaandika. Katika kamati ile mmoja wapo ni Profesa Ahmed Muhidin. 

Mimi miaka miwili iliyopita nilimtembelea Mombasa, [Kenya] nyumbani kwake na alithibitisha, akasema Mwalimu alinipigia simu akasema Ahmed nisaidie kuandika maisha yangu. Na matokeo yake ndio kitabu hiki [Development as a Rebellion: A Biography of Julius Nyerere], kilichoandikwa na Issa Shivji, Ng’wanza Kamata na Saida Yahya-Othman] baada ya wao kushindwa kuandika kina Haroub Othman, ndio kikaandikwa kitabu hiki. Ukisoma kitabu hiki haya yote niliyokuambia humu wameyakwepa.

The Chanzo: Wameyakwepa?

Mohamed Said: Wameyakwepa, hata kumpa heshima Abdu kama mtu aliyestahili, aliyempokea Nyerere, mikutano ile waliyokuwa wakifanya na Hamza Mwapachu, [hawakuiweka]. 

The Chanzo: Kwa hiyo, Sheikh Mohamed, siku hizi kuna wanaharakati wa mambo ya kijinsia na haki za wanawake. Rais anapofanya uteuzi, waziri anapofanya uteuzi au wanapotangaza mkutano, wanaangalia wanawake wapo wangapi humu. Wakiona wanaume wapo nane na wanawake wawili wanasema inakuaje hapa. Kwa hiyo, na wewe linapotangazwa Baraza la Mawaziri unaangalia Waislamu wangapi?

Mohamed Said: Sana sana.

The Chanzo: Kwa nini hiyo ni muhimu?

Mohamed Said: Kwa sababu Waislamu wamebaguliwa [kwenye teuzi za] Serikali.

The Chanzo: Kwa kumalizia, tukiwa tunaelekea kuazimisha miaka 60 ya uhuru, wewe una furaha au huzuni?

Mohamed Said: Kwa kweli tunapoelekea kuazimisha miaka 60 ya uhuru, ndio tuko huru, lakini uhuru unataka uje na haki, ndio utakuwa uhuru wa kweli. Lakini kama kuna mtu yuko kwenye nchi huru lakini anaona anaonewa, anadhulumiwa hatakuwa na furaha. Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kutazama haya malalamiko [ya Waislamu kubaguliwa] na wakaangalia [kuna] ukweli katika hili? Na kama kweli tunafanya nini kuondoa hali hiyo? 

Ili kila mtu aishi kwa raha na mustarehe bila ya kuwa na kinyongo au joto ndani ya nafsi yake, katika kifua chake. [Hilo ni] muhimu sana, kwa sababu zipo nchi zimeangamia kwa kupuuza vitu hivi,  na [haya] sio mambo ya watu kuwa wanajibishana mitaani na kutunga majibu. Hili jambo Serikali waseme, tunalo tatizo wananchi lakini tunalifanyia kazi, watu wakae na matumaini. 

The Chanzo: Sheikh Mohamed, mimi nakushukuru sana kwa muda wako na matumaini yangu ni kwamba wahusika, mamlaka husika, zitapata wasaa wa kuangalia mazungumzo ambayo tumefanya hapa na kufanya kama ulivyopendekeza kwamba wachuje, wachunguze ili waone hayo madai kama yana ukweli au hayana ukweli na kuona wanaweza wakachukua hatua gani kuona wanaweza kurekebisha hali ya mambo. Ahsante sana, nimejifunza mengi, na Mungu akubariki sana.

Mohamed Said: Na mimi nashukuru kwa maswali yako chokonozi [Anacheka].

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Mahojiano Bora Kabisa yanayostahili kusomwa na kila Mtanzania,nchi ina mambo mengi sana ya kujifunza,hasa Historia yake

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts