Mwanahistoria Mohamed Said: Miaka 60 ya Uhuru Lakini Hatuijui Historia Yetu

Nguli huyo wa historia nchini anabainisha umuhimu wa watu kujua historia yao akisema kwamba mtu akinyang’anywa historia yake ndio amenyang’anywa utu wake.
Na Mwandishi Wetu22 October 2021214 min

Dar es Salaam. Mnamo Oktoba 9, 2021, The Chanzo, ilikutana na kufanya mahojiano maalum na mwahistoria na mwandishi wa vitabu, ambaye ametumia maisha yake mengi kuweza kuwasilisha historia ambayo unaweza kusema ina utofauti fulani na ile historia ambayo imekuwa ikifundishwa na shuleni na vyuoni. Na huyu si mwingine bali Sheikh Mohamed Said.

Mazungumzo kati ya The Chanzo na nguli huyu wa historia ya Tanzania yalifanyika ikiwa taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, na bila shaka Tanzania baada ya muungano wa mwaka 1964, na tulikuwa na shauku ya kutaka kupata mtazamo wake kuhusiana na safari hii ya miongo sita ya shubiri na asali katika historia ya Tanzania. 

Kama ulikuwa hufahamu, moja ya mambo makubwa tu ambayo Mohamed ameyafanya kwenye maisha yake ni kuandika kitabu kuhusu maisha ya mwanaharakati na mpigania uhuru wa Tanganyika Abdulwahid Skyes ambacho kinaitwa Maisha Na Nyakati Za Abdulwahid Sykes (1924-1968): Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati Za Waislam Dhidi Ya Ukoloni Wa Waingereza Katika Tanganyika.

Kitabu hicho cha kwanza kilichapishwa mwaka 1998, ambacho kilichapishwa kwa lugha ya Kiingereza lakini kipo pia cha Kiswahili, na vitabu vyote hivi vinapatikana kwenye maktaba zetu zote nchini. Yafautayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya The Chanzo na Sheikh Mohamed Said. Endelea … 


The Chanzo: Tunashukuru sana kupata fursa hii ya kuzungumza na wewe. Labda kwa kuanzia tu, na kwa niaba ya watu ambao hii ni mara yao ya kwanza kukufahamu, kama ungepewa fursa ya kuelezea maisha yako ndani ya sentensi moja, ungejielezea vipi?

Mohamed Said: Mimi Mohamed Said ni mtoto wa mjini Dar es salaam. Ningesema hivyo tu.

The Chanzo: Sasa kama nilivyotangulia kusema kwenye utangulizi wangu, mnamo Disemba 9 mwaka huu [wa 2021], Tanganyika itakuwa inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kingereza. Nilikuwa nataka kupata tathmini yako kama mwanahistoria, unaitazama vipi miaka hii 60 ya Tanganyika huru, na baada ya muungano na Zanzibar mwaka 1964,  Tanzania, ipi tathmini yako katika safari yote hii, hususani katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na kijamii?

Mohamed Said: Mimi huko kwenye uchumi sijui kitu, labda nitazungumza kwenye siasa na historia na ndio jamii yenyewe hiyo. Nitakwambia kitu nje ya swali ulilouliza kuwa tunasherehekea miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, kama ulivyosema, mimi nimeandika kitabu cha Abdu Sykes na kilichonisukuma ni ile kuwa nikimfahamu marehemu Abdu alikuwa rafiki wa baba yangu na ujana wao unakwenda leo sasa ni miaka 100, toka wanazaliwa [Mtaa wa] Kipata, [jijini Dar es Salaam] pale wako pamoja mpaka wamehitimishana. 

Ile Disemba 9, alinihadithia mwanae [Abdu anayeitwa] Kleist, anasema: “Siku ile mimi na baba tulikuwa uani kwetu tunasikiliza redio, sherehe za uhuru zimepamba moto, bendera ya Mwingereza inashuka na bendera ya Tanganyika inapanda.” Kleist alikuwa mdogo maana kazaliwa mwaka 1950, kwa hiyo, mwaka 1961, alikuwa kijana wa kama miaka 10 hivi. 

Anasema: “Ilivyokuwa bendera ya Tanganyika inapanda, baba alijiinamia machozi yakawa yanamtoka.” Nikamuuliza Kleist, “baba alikuwa analia?” Akasema, “Naam, alikuwa analia.” Kipi kilikuwa kinamliza? Anasema [Kleist], “Mimi nimekuwa mkubwa sasa, nadhani kilichokuwa kinamliza ni kuwa juhudi yote ile aliyokuwa amefanya kwenye [Tanganyika African Association] TAA” — na TAA alianzisha baba yake [Kleist mwaka] 1929 akiwa katibu na mfadhili wa African Association na jamaa wengine. 

Anasema [Kleist], “Baba nadhani alikuwa analia kuwa bendera ya Tanganyika inapanda na swahibu wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anachukua uongozi wa nchi yeye Abdu Sykes hajaalikwa kwenye sherehe zile.” [Kleist] anasema anadhani baba [yake] kilikuwa kinamliza hiki. Mimi nikamwambia inawezekana vile vile ni kilio cha furaha. Akasema, “Sidhani kwa sababu nilikuwa naona  sura ya baba ilikuwa si ya kuonesha furaha.” 

Ndio, lazima ufurahi nchi umekomboa lakini vipi kuwa leo Mwalimu anapokea nchi, wale watu ambao alikuwa nao hawapo jirani yake? Kuna sura nyingine? Wewe hujui. Abdu Sykes ndio alimuweka Nyerere kwenye yale madaraka aje akamate nafasi ya Rais wa TAA 1953 na mwaka 1954 wanaunda TANU wakidai nchi yao. Na ukitaka ushahidi kuwa kadi namba moja ni ya Nyerere, kadi namba mbili ni ya Ali Sykes na kadi namba tatu ni ya Abduwahid Kleist Sykes. 

Kwa hiyo, nadhani kwa maelezo hayo mafupi kidogo umeelewa. Sasa nilikuwa nimekutangulizia kuwa miaka 60 lakini hatuijui historia yetu kuwa tumefika fika vipi mpaka tukaweza kuichukuwa nchi yetu kutoka mikononi mwa Waingereza. Wale waliohangaika, wazalendo wenyewe hawafahamiki.

The Chanzo: Na hapo umenileta kwenye swali langu jingine na umeelezea vizuri kwamba historia yetu hatuifahamu. Labda kwa mtazamo wako wewe ni nini kinakosekana  kwenye historia tunayofundishwa kuhusu taifa la Tanganyika, na baadae Tanzania, ambacho unadhani kimepelekea hali hiyo? Ni nini kama utakuwa na uwezo wa kuainisha mambo yanayokosekana kwenye historia yetu ambayo yamejenga uelewa uliopo?

Mohamed Said: Khalifa swali hili naulizwa kila siku. Hakai mtu kunihoji mimi, hasa akiwa amekwishakisoma kitabu wa Abdu Sykes, [asiseme], “Ah! Ndio mambo yalikuwa namna hii, mbona historia hii sio tunayoijua sisi?”  Mimi nakupa wewe changamoto, swali hili ukiniuliza mimi utanionea. Nitakujibu nini? Kawaulize — maana umesema unafanya kipindi na watu mbalimbali — hebu waulize watu [au] viongozi wa [chama tawala, Chama cha Mapinduzi] CCM, kwa sababu wao wameandika historia ya TANU toka mwaka 1954 mpaka 1977. 

Hawa ndio warithi wa African Association, warithi wa TAA, warithi wa TANU. TANU imeanzishwa katika jengo la African Association ambalo limejengwa kati ya mwaka 1929 hadi 1933. Na waliojenga hili jengo ni kina baba yake [Kleist], na yeye anasema alipokuwa mdogo alikuwa anaenda pale na baba yake, maana walikuwa wanajenga kwa kujitolea.  

Waulize [CCM], mbona historia ya chama chenu imekuwa hivi? Wazalendo wenu mbona hatuoni picha zao hapa? Hatuwasomi, hatuwajui? Mbona hatuoni picha ya Mzee Kleist hapa? Mbona hatuoni picha ya Mzee Iddi  Musubi hapa? Mbona hatuoni picha ya Abdu? Mbona hatuoni picha ya Joseph Kimalandu? Mbona hatuoni picha ya Joseph Kasela Bantu hapa? Mbona hatuoni picha ya fulani fulani, vipi? Nyie hamuwathamini hawa watu kama [wazee] waliopigania uhuru? Hiyo ni Dar es salaam.

Twende labda Kanda ya Ziwa. Ali Vigeyo mbona haonekani? Hatumuoni Paul Bomani. Kina mama pia. Mbona hatumuoni hapa Bi Tatu binti Mzee? Mbona hatumuoni Titi Mohamed? Mbona hatumuoni Bi Chiku binti Kisusa? Mbona hatumuoni Halima Serengia? Mbona hatumuoni Lucy Lameck? Namna hiyo. Waambie mbona hiyo historia mmeiacha hivyo hivyo watu hawaijui? Sasa jibu lake litakuwa jibu kamili. Sasa ukiniuliza mimi nitakwambia nini?

The Chanzo: Mimi nakuhaidi nitajaribu kuuliza lakini nataka na wewe uniambie. Huwezi kulikwepa hili swali.

Mohamed Said: Nitakujibu lakini Khalifa wewe hutalipenda jibu langu.

The Chanzo: Mimi nimejiandaa kwa majibu yoyote mpaka nimeamua kuja hapa. Nataka uniambie imetokeaje tokeaje mpaka hali ikawa hivyo unavyozungumzia wewe, kwamba hao watu wote ambao umewataja hawapo kwenye historia rasmi ya Chama cha Mapinduzi. Nina shauku ya kutaka kufahamu.

Mohamed Said: Nitakwambia jibu langu. Kuna mtu nilimpa jibu hili hakupenda, akanambia, “Mohamed mimi nakuuliza maswali ya maana wewe unaniletea majibu ya kitoto bwana.” [Jibu nililompa ni kwamba] inawezekana Mwalimu Nyerere mwenyewe hakuwa anaijua historia kabla yake. Hakuwa anawajua kina Sykes na mchango wao. Hakuwa anamjua Abdu, ndio maana yakatokea haya. Akadhani labda mambo yalianza na yeye mwaka 1954. Maana hata ile 1953 hajasema. Hivi unajua Nyerere aligombea urais wa TAA ukumbi wa Anatouglou na Abdu Sykes?

The Chanzo: Hapana, sijui.

Mohamed Said: Na Nyerere akashinda kwa tabu sana, na katika uongozi akawa yeye ndio Rais, Makamu wa Rais akawa Abdu Sykes, Kasela Bantu akawa Katibu Mkuu, Mzee [John] Rupia akawa Mweka Hazina, Ali Sykes akawa Mweka Hazina mdogo. [Mwalimu] hajasema haya. Kwa hiyo, shida ndio inakuwa hii. 

Sasa huenda yeye [Mwalimu] hakuwa anajua kabla yake yeye. Na wala hasemi kuwa Rais wa TAA alitakiwa kuwa Chief Abdalah Makwaia, ndio Abdu alikuwa anamtaka na walishazungumza 1950 ile. Hajasema kuwa mabadiliko hasa ya TAA yalikuja 1950 baada ya kuondolewa wazee waliokuwa wameshika chama. Walikuwa Mzee Mwalimu Thomas Plantan, hajasema. Uongozi ukaingia mpya, Vedasto Kyaruzi akawa Rais na Abdu Sykes akawa Katibu nafasi ile ile aliyoishika baba yake. 

Shinikizo kubwa lilitoka kwa Schneider Plantan. Unajua hawa  kina Plantan na kina Sykes ni ndugu. Unajua kulikuwa na familia hapa zikiendesha mambo katika mji wa Dar es salaam. Kulikuwa na kina Sykes, kuliwa na kina Plantan alafu kuna kina Chaurembo.  Hawa kina Chaurembo hata kwenye dini walikuwa na elimu kubwa, kulikuwa na Chaurembo, Liwali wa Dar es Salaam, kama Hakimu pale Mahakama ya Mwanzo.  

The Chanzo: Kwa hiyo, unataka kuniambia kwamba hali hiyo imetokea kibahati mbaya? 

Mohamed Said: Sasa, hiyo utajiambia wewe mwenyewe, usiniulize mimi. Wewe mwenyewe pima, inawezekana vipi ikaandikwa historia [ya nchi na chama] hawa niliokutajia hata kwenda kuwahoji hawakwenda kuwahoji? Lakini nitakwambia kitu kimoja. Mwanzo hapo kabla hatujaanza kipindi nimekwambia habari za Hasano Peka ambaye alikuwa kwenye jopo la kuandika historia ya TANU.

[Huyu] ameniambia mwenyewe [kilichotokea wakati wa mchakato huo wa uandishi] na kwenye kitabu nimesema. Nilimuuliza haya unayoniambia. [Nilimuuliza,] “Kaka, unaniruhusu nikutaje, nisije nikatoa habari nzito kama hizi halafu nisiwe na chanzo cha maana?” Akanambia, “Wewe kaka nitaje tu hakuna tatizo.” 

Anasema, “mimi nimekuwa TANU toka mwaka 1956, nimekuwa kachero [wa TANU] na nimefanya mahojiano na Abdu Sykes vipi TANU imekuja. Siku zile wakati tunaandika historia ya TANU, mimi nilizipeleka notes kwa kiongozi wetu’ — naweza nikamtaja jina kwa sababu hata kwenye kitabu nimemtaja — Dk Mayanje Kiwanuka, yeye ndio alikuwa anaongoza utafiti na uandishi ule. 

Alivyompatia zile notes, [Kiwanuka] akamwambia [Peka]: “Tunayoandika ni historia ya TANU [na historia hii] haina uhusiano wowote na Abdu Sykes.” [Peka] anasema akashituka maana alipokuwa akiingia ofisi za TANU alikuwa anamkuta pale na ndio katika viongozi wa juu wa TANU.  Anasema historia gani ya TANU itakuwa bila kumtaja Abdu Sykes, [mtu mwenye] kadi namba tatu? Mtu aliyemkaribisha Mwalimu Nyerere Dar es salaam na akaishi naye nyumbani?   Na [aliyeshiriki] mikutano yote ya siri mpaka kunyanyuka kwa TANU, [ukiwemo] mkutano wa siri wa kwenda [Umoja wa Mataifa] UNO [ambayo yote] ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Abdu?

Lakini mimi akanisaidia kitu kimoja, akanambia nakupa majina ya watu maktaba Dodoma nenda ukawaone hawa na waambie mimi nimekutuma, wao wakitaka wataniuliza.  Na kweli walinipa msaada mkubwa. Kila faili ambalo nililiomba nililetewa, lakini kwa bahati mbaya ndani kulikuwa hamna kitu. Mimi nimeletewa faili la Abdu Sykes Makao Makuu ya CCM, Dodoma. Nimeona faili la Mzee Mwapachu. Lakini ni faili tu juu, ndani hamna kitu. 

The Chanzo: Hii yote kusema ukweli, namaanisha nikijaribu kusema nilichokipata kwenye maelezo yako, inaonesha hii hali haikuwa ya bahati mbaya. Ni kitu kilipangwa. Kwa nini unafikiria walifanya hivyo?

Mohamed Said: We Khalifa matata sana, nilijua wewe Khalifa utakuja kunipa shida wewe. Tangu nilipokuona nilijua huyu, mimi sina salama na Khalifa. Mimi sichopoki hapa, toka mwanzo nilivyokujua. Si nina uzoefu wa kuhojiwa? [Anacheka].

The Chanzo: Wewe mwenyewe umenambia, maana ndio tumekuja hapa.

Mohamed Said: Nitakwambia. Kleist alipounda African Association, yeye pamoja na wenzake kama saba hivi, anasema kuwa wengi wao walikuwa ni Waislamu. Kwa sababu Kleist ameandika muswaada wa kitabu. Aliacha muswaada wa kitabu kabla hajafariki mwaka 1949. Kwa mkono wake ameandika, akamwachia mwanae Abdu. 

Na sijui kwa nini wakati huo hakuchapa kitabu, sijui kwa nini. Sasa ile AA ikawa na ushawishi mkubwa sana wa Uislamu ndani yake. Ilipofika mwaka 1933, manung’uniko mengi ya Waislamu yalikuwa yanapitishwa African Association. Sasa akaona hii si sawa kwa sababu hiki chama tunataka kiwe cha watu wote. Sasa hiki chama cha watu wote na nyie mambo yenu ya dini mnaleta mule inakuwa si sawa. 

Kwa hiyo, yeye na Mzee Bin Sudi, ambaye alikuwa Rais wa AA wakati ule, wakaamua kuanzisha chama kingine pembeni ya African Association, [kikaitwa] Ayatullah Islamia Tanganyika, [yaani kwa Kiswahili ikiwa na maana ya] Umoja wa Waislamu Tanganyika. Wakajenga shule na ofisi yao ikawa pale, siku zile ukiitwa Mtaa wa Stanley na New Street, halafu baadae ukaitwa Aggrey na sasa Makisi Mbwana 

The Chanzo: Unaitwa?

Mohamed Said: Makisi Mbwana, ni kati ya wazee wa TANU. Alikuwa kwenye Baraza la Wazee wa TANU, walikuwa na nguvu sana wazee wa TANU. Sasa na ile ushawishi wa Waislamu katika kudai uhuru wa Tanganyika haukuondoka. Hata ukitazama picha, wewe tazama picha zote za Mwalimu Nyerere wakati wa kudai uhuru, utakuta amezungukwa na Waislamu watupu. Aghalabu ukute wametokea wengine wako naye, zote tazama. 

Na mwenyewe siku ya kwanza anasema, mimi niliaminika mapema sana na wazee, lakini pale kama ameruka, ilikuwa aseme mimi walioniaminisha walikuwa ni Abdu na Hamza Mwapachu na vijana wengine kina Steven Muhando ndio walikuwa naye. Wakina Kasela Bantu hawa ndio walikuwa naye pamoja. Lakini hao wengine walikuwa wageni, waliokuwa wenye mji ndio hao kina Ali, Dossa ndio wenye mji wao. Ujue ile Dar es Salaam ya 1950s sio Dar es salaam unayoiona siku hizi.   

Sasa nadhani hofu imekuja, kwa sababu uhuru ulipokuja ulikuja na changamoto kubwa, na changamoto ya kwanza ilikuwa ndani ya halmashauri ya TANU pale Lumumba. Walikuja watu wawili Rajab Diwani na Selemani Kitundu, ndani ya Halmashauri Kuu wakasema kuwa, maana Waislamu walikuwa na taasisi nyingine ina nguvu sana ya East African Muslim Welfare Society ambayo ilikuwa  imejenga shule karibu nchi nzima. 

Agha Khan huyo, Agha Khan alikuwa anasema, Muislamu ukichangia shillingi na mimi nitachangia shilingi. Kwa hiyo, kwa mwaka labda tuseme Waislamu wamekusanya milioni moja, Agha Khan anatoa millioni moja kuwatia nguvu watu kufanya mambo yao wenyewe. Ilipokuja uhuru sasa, 1961 ile, 1962 Sheikh Hassan bin Amir, huyu alikuwa katika kamati ya ndani TANU, na ndio alikuwa Mufti wa Tanganyika lakini Mzanzibari, na yeye alikuwa anasimama bega kwa bega na Nyerere. Kwa hiyo, watu walikuwa wakimuona Sheik Amir wanasema hiki chama chetu hakuna wasiwasi huyu mtu wetu, Mufti mwenyewe yuko naye. 

Kwa hiyo, ile nguvu ikatia hofu. Kwa hiyo, mwaka 1962 Sheik Amir aliitisha mkutano ulioitwa Muslim Congress, zilikuwa mbili, ya 1962 na 1963, na katika maazimio waliokuja nayo, moja, kama sio mawili, ilikuwa East African Muslim Welfare Society ijenge shule wilayani, mikoani na mwisho ijenge Chuo Kikuu kwa sababu Waislamu walichelewa sana, walicheleweshwa na ukoloni, waliwadhulumu katika elimu. Sasa likaja suala ndani ya 1963 ndani ya Halmashauri Kuu ya TANU kwamba Agha Khan anataka kutawala nchi hii na [hili lililetwa na] Waislamu, [akina] Rajab Diwani na Selemani Kitundu. Titi akasimama upande wa Waislamu.

The Chanzo: Bibi Titi Mohammed?

Mohamed Said: Bibi Titi Mohammed. Akasema haiwezekani hii East African Muslim Welfare Society ilikuwepo kabla ya TANU na inasaidia Waislamu. Hayo yanayosemwa sio ya kweli. Kama wanaushahidi watoe. Sasa pale siku ile …

The Chanzo: Madai yalikuwa sio ya kweli? 

Mohamed Said: Yalikuwa si kweli.

The Chanzo: Ndio.

Mohamed Said: Ukisoma kitabu utaona sio kweli. Hapo unaweza kudhani wale [akina Diwani na Kitundu] walitumwa au kwa fikra yao. Pale pakapishana maneno baina ya Nyerere na Bibi Titi, maneno makali. 

The Chanzo: Nyerere alikuwepo kwenye kikao?

Mohamed Said: Ah, [alikuwa ndio] mwenyekiti. Bibi Titi akamwambia Nyerere sikiliza bwana, mimi simuogopi mtu yoyote, mimi  namwogopa Allah peke yake. Sasa, hiyo kanambia mwenyewe [Titi] uso kwa macho wallah, nakwambia!

The Chanzo: Bibi Titi? 

Mohamed Said: Mwenyewe. Kaniambia, “Mimi tulianza kugombana na Mwalimu toka mwaka 1963, na tatizo lilikuwa hili la East African Muslim Welfare Society.” Lakini alikataa kunipa mahojiano kamili, alikataa kabisa. Aliyenipeleka alikuwa kaka Ali Sykes, kipindi hicho [Titi] ndio alikuwa amerudishiwa nyumba yake pale Upanga pale mkabala na ilipo Makao Makuu ya Jeshi [la Wananchi]. Ana nyumba ghorofa moja, nyumba nzuri, nimekwenda pale ndio akaniambia hivyo. Sasa, hii 1963 wakati Baraza la Wazee wa TANU ambalo mwenyekiti wake alikuwa ni Tulio, maana Sheikh Takadir ni historia nyingine hiyo alifukuzwa TANU kwa masuala haya ya Uislamu.

The Chanzo: Pale mwanzo umegusia kwamba hii nguvu ili wapa hofu [baadhi wa wakuu ndani ya TANU].

Mohamed Said: Swadakta.

The Chanzo: Hofu ya nini sasa?

Mohamed Said: Kuwa Uislamu utaimarika sasa. Kwa sababu unaona nguvu yao katika kupigania Uhuru wa Tanganyika. Ukisoma kitabu utaona kulikuwa na jitihada za mapambano za Waislamu. Utaona hiyo.

The Chanzo: Sasa utajiuliza hilo lina uhusiano gani na kutolewa watu kwenye historia rasmi ya upatikanaji wa Uhuru wa Tanganyika?

Mohamed Said: Kwa sababu watu wakijitambua-, laba niseme kwa n ini mimi ninasema kwa kujiamini? Kwa nini historia ninayosema wala jina langu sijifichi? 

The Chanzo: Kwa nini?

Mohamed Said: Kwa sababu wazee wangu ndio wameunda chama cha African Association, iliyozaa chama cha TAA, yote haya mimi nimeishi katika historia hii ingawa nilikuwa bado mdogo. Nimewasikia wazee wangu wakizungumza, nimepata umri nimewauliza wamenihadithia kila kitu. Wewe hujapata kusikia. Wewe ulikuwa unajua kama hizo namba, we ulikuwa unajua kadi ya Adu Sykes namba tatu na Ali Sykes namba mbili?

The Chanzo: Hapana.

Mohamed Said: Namba nne Dossa Azizi. Namba tano Denis Pombea. Namba sita Budoe. Huyu Pombea kutoka Nyasa na Budoe Mluya kutoka Kenya. Abbasi Sykes namba saba, ndugu watatu wote kwenye chama na baba yao ni mwasisi wa chama. Hayo umekuwa hujayasikia kwa sababu mtu ukimnyang’anya historia yake ndio umemnyang’anya utu wake.

The Chanzo: Na si kweli kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa anakusudia kujenga taifa la ki-secular, [taifa] ambalo halina dini na pengine Waislamu walikuwa wamedhamiria kujenga taifa la Kiislamu?

Mohamed Said: Wala hapakuwa na dhamira ya kuunda taifa la Kiislamu. Kama kungekuwa na dhamira ya kuunda taifa la Kiislamu, Sheikh Hassan bin Amir, Hamza Mwapachu, Abdu Sykes, hawa wote waliomuunga mkono, wasingemuunga mkono Nyerere. Wangemuambia Hamza, na kumwambia wewe kaa pale, Abdu kaa pale. 

Lakini katika sifa mabayo Hamza Mwapachu anamwambia Abdu kwa nini Nyerere achukue nafasi ya urais ni kuwa ni Mkristo. Tunataka chama hiki kiwe chama cha watu wote. Chama kikiwa cha watu wote, nchi unaiweka mahali pazuri. Watu wote wataona haki zao ni sawa, usiwatie watu hofu. 

Wazee wetu walipata fundisho India. Mohammad Ali Jinnah [muasisi wa taifa la Pakistan] na [Jawaharlal] Nehru, [Waziri Mkuu wa zamani wa India]. [Wazee] walikuwa wanajua historia ya India. [India] walipopata uhuru siku hiyo hiyo walianza kupigana [na kupelekea kuanzishwa kwa taifa la Pakistan]. Kwa hiyo, wazee walipata fundisho. Tatizo watu wanadhani hawa wazee wetu walikuwa wajinga. Hawa watu walikuwa wasomi. Sheikh Hassan bin Amir [alikuwa] msomi. Sheikh Selemani Takadir alikuwa msomi. Watu wamesoma Quran. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa bingwa wa kusoma Quran, wametafsiri Quran, atakuwaje zuzu mtu kama huyo? 

Katika kutoa mapendekezo ya Katiba, Edward Twining mwaka 1950, tazama ile rasimu ipo sahihi ya Sheikh Hassan bin Amir, ipo sahihi ya Sheikh Said Chaurembo. Hawa si watu ambao walikuwa hawajui mambo. Lakini watu wanaaminishwa kwamba hawa watu hawakuwepo na kama walikuwepo hawajui chochote, hawana mchango wowote isipokuwa aliyeleta mambo yakawa, akagombea nchi ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Itakuwa vipi? Sasa hapa ndio ikawa tatizo la historia likaanza kutokea hapo.

Na Mwandishi Wetu

2 comments

 • Sindika Fanuel

  22 October 2021 at 10:35 PM

  Mahojiano Bora Kabisa yanayostahili kusomwa na kila Mtanzania,nchi ina mambo mengi sana ya kujifunza,hasa Historia yake

  Reply

 • JOSHUA FABER

  2 September 2022 at 9:29 PM

  KITABU CHAKE CHA ABDUL WAHID SYKES KINAPATIAKANA WAPI

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved