The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mawaziri Madini, Nishati na Viwanda Kikaangoni, Waelezea Miradi ya Kimkakati.

Miradi mipya ya madini yanye thamani ya trilioni 1.8 inategemewa

subscribe to our newsletter!

Dodoma imeendelea kupambamoto na wiki ya Azaki, tukio linalofanyika kila mwaka lenye kukutanisha asasi za kiraia mbalimbali toka mikoa yote ya Tanzania.

Moja kati ya matukio yaliyoongelewa zaidi  jana Oktoba 25,2021, ilikuwa ni mjadala uliowakutanisha mawaziri watatu; Waziri wa Madini Doto Biteko, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato  pamoja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe.

Mjadala huu ulioendeshwa na taasisi ya Hakirasilimali, ulilenga kuangazia ni kwa namna gani serikali imeweza kuwa na ulinganifu kwa kuangalia Tanzania inafaidika na utajiri wa rasimali iliyopo nchini, lakini pia kuvutia wawekezaji kuendelea kuja kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini.

Uwekezaji wa Trilioni 1.8 Unategemewa Kwenye Madini

Mwaka 2017, serikali ilileta mabadiliko ya sheria katika madini ikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Kudumu kwenye Utajiri wa Asili wa Rasilimali na Maliasili 2017 na Sheria ya Mikataba na Utajiri wa Maliasili na Rasilimali (Upitiaji na Uboreshaji Masharti Yenye Shaka) ya mwaka 2017. Sheria zote hizi ziliipa serikali nguvu zaidi, ikiwemo haki ya kupitia mikataba yote inayoonekana kuwa na shaka.

Mtendaji mkuu wa asasi ya Hakirasilimali, Rachel Chagonja alimuuliza Waziri Biteko juu ya manufaa ya mabadiliko haya.

Je Tanzania imepata faida gani kutoka kwenye sekta ya madini, tangu marekebisho ya sheria ya madini yaliyofanywa mwaka 2017?

Dotto Biteko: Ndugu zangu kama kuna wakati ambapo tunaweza tukasema mabadiliko haya yametuletea nafuu pamoja na hofu. Na mwanadamu yeyote mwenye akili timamu ni lazima awe na hofu, na mimi hofu niliyokuwa naiona kwenye asasi za kiraia,  kwenye vyombo vya habari, kwa wananchi na wawekezaji ilikuwa ni hofu ya msingi.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia watu kwamba sheria yeyote tunayoitengeneza siyo msaafu ipo kwaajili yetu tukiona kuna tatizo mahali fulani tutafanya marekebisho. Kwahiyo tumepata manufaa makubwa sana tulivyorekebisha sheria.

Sheria hii tulivyoirekebisha iliwapatia watanzania nafuu kubwa, watanzania kushiriki kwenye uchumi wa madini. Zamani wachimbaji wadogo walikuwa wanapewa majina ya hovyo kabisa waliitwa wachimbaji haramu , kwasababu tu sheria tulioyorithi ilikuwa na asili ya ukoloni ya kuharamisha wenye rasimali kushiriki kwenye uchumi wa madini na kuwafanya wageni kama wanufaika wakubwa.

Kwahiyo tukaangalia tufanyaje? tuangalie namna ya kuwapa nguvu wachimbaji wadogo waweze kushiriki kwenye uchumi wa madini na manufaa tumeyaona. Lakini vile vile hatuwezi kuchimba wenyewe  tunawahitaji wageni waje hapa wawekeze zaidi ili tuweze kupata nafuu.

Nafurahi kusema kwamba mchango wa wachimbaji wadogo umepanda sana mwaka 2017 kabla hatujafanya haya marekebisho ,ukichukuka mauzo yote nje ya madini  ya dhahabu , [mchango] wa wachimbaji wadogo ulikuwa ni 4% peke yake asilimia yote 96% ya mauzo nje zote zilikuwa ni za migodi mikubwa kama Barrick, GGM na kadhalika.

Lakini vile vile mapato yakaongezeka ,hivi ninavyozungumza ,tumepata rekodi ambayo hatujawahi kuipata ,mwaka juzi tulipangiwa kukusanya bilioni 526 lakini kabla ya mwaka huu wa fedha tulikusanya bilioni 586 kwenye rekodi ya nchi hatukuwahi kupata.

Sekta ya madini imeongoza kwenye ukuaji kwa mara ya kwanza kwa  mwaka 2019 ikakua kwa 17% ikifuatiwa na sekta ya ujenzi .Lakini kwenye kuleta fedha kutoka nje ya nchi, sekta hii ikaongoza vile vile ikaleta 51.9 % ya fedha zote zinazoleta ndani ya nchi. Lakini mauzo kutoka ndani kwenda nje iliyoongoza ikaonekana [ni] sekta ya madini.

Masikio yetu ya serikali yamekuwa wazi kwa wadau na kuona kwamba turekebishe wapi ili tuweze kuboresha . Nataka niwape taarifa [ndani] ya miaka 15 hatukuwahi kufungua mgodi mkubwa mmoja ,baada ya marekebisho haya wawekezaji wamekuja, tumefungua migodi mipya, nitawatajia mgodi wa kwanza ni mgodi wa Nyanzaga wa uchimbaji dhahabu, ni mgodi ambao utawekeza fedha za kimarekani dola milioni 499  na utaajiri watu kwa (direct empyoment) watu 1200 ,lakini kwenye ajira zisizo rasmi utaajiri watu kati ya watu 3000-5000 .

Lakini kuna mradi mwingine uko Ngwara kule Songwe na wenyewe utawekeza fedha za kimarekani dola milioni 196 na huu utaajiri zaidi ya watu 120 ambao watapata ajira za moja kwa moja kwaajili ya kuchimba madini .
Mradi mwingine ambao tunao ni mradi wa kabanga, utachimba madini ya Nickel kama manavyofahamu Nickel tuliyo nayo sisi ni daraja la kwanza, Nickel ambayo iko duniani na serikali imeshatoa kibali cha kutoa leseni, na mradi huu wenyewe utatuletea uwekezaji wa moja kwa moja dola za kimarekani dola milioni 112 na ajira za watanzania zitakuwa 1200 ajira za moja kwa moja na utakuwa mradi wa maisha ya miaka 30 serikali itapata 59% mwekezaji atapata 41%.

Mazungumzo ya Mradi wa LNG Kumalizika Ndani ya Miezi Mitatu

Toka mwaka 2014 kumekuwa na nenda rudi kuhusu mradi mkubwa wa gesi ya asilia wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 30. Mradi huu wa kimkakati unaotegemewa kujengwa huko Likong’o Lindi na makampuni ya Equinor na Shell sasa umeanza kujongea taratibu, Naibu Waziri Stephen Byabato  anazungumzia

 Je ni yapi maono ya wizara ya Nishati na mkakati kuhakikisha maslahi ya  watanzania yanapatikana kwa wakati unaofaa katika mradi wa mafuta na gesi ?

Stephen Byabato : Tumegundua gesi tangu mwaka 2010 lakini mpaka sasa bado hatujakamilisha uanzishaji wa mchakato wa kufanya gesi iweze kutoka na kwenda kule inapohitajika kwenye viwanda vya mbolea na mambo mengine.  Wizara ya Nishati inatambua kabisa jukumu lake kwenye gesi kwa niaba ya serikali ,inajua uwepo wa sheria,inajua uwepo wa kanuni na miongozo mbalimbali inayolenga na yenye nia kuhakikisha gesi hii inanufaisha Taifa kwa ujumla wake .

Sasa Wizara ya Nishati inafanya nini? niende moja kwa moja kwanza kwenye LNG, tulikuwa tumeanza kidogo kujadiliana na wenzetu wawekezaji , kama tulivyosema uwekezaji wa miradi mikubwa kama LNG sisi peke yetu watanzania hatujawa na mitaji mikubwa kufanya kila jambo lilipo humu.

Kwa mfano kwenye LNG tunatarajia kuwa na uwekezaji zaidi ya  dola bilioni 30 kwa kawaida ni pesa nyingi sana na tunahitaji tekinolojia kubwa sasa inatupelekea sisi tuwe na wabia ambao tunahitaji kufanya nao kazi. Tumeshaandaa kikosi kufanya majadiliano na wawekezaji wa mradi wa gesi (LNG) Lindi, ambapo majadiliano yataanza 08/11/2021. Pia, Rais ametoa miezi 3 majadiliano yakamilike ili utekelezaji uanze mwakani.

Wizara ya Viwanda na Biashara

Pamoja na ukuaji endelevu wa sekta ya madini na gesi, bado sekta hii haijaweza kuwafikia watu wengi, hasa katika kubadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja. Jitihada kadhaa zimeendelea kufanyika hasa katika kuhakikisha mnyororo wa thamani wa madini unagusa watu wengi zaidi na kuwanufaisha moja kwa moja.

Naibu Waziri wa Viwanda anaelezea juhudi zinazofanyika kufungamanisha maendeleo ya sekta za uziduaji na viwanda.

Pamoja na mambo mengine mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano  umelenga kukuza msingi wa viwanda kwa kutumia rasimali ,Je wizara inampango gani wa kufanya fungamanisho kati ya sekta ya mafuta, madini na  gesi ?

Exaud Kigahe: Mpango huu umelenga zaidi kuhakikisha sekta ya viwanda kama sekta chechemuzi ambayo itasaidia watanzania kunufaika na rasimali tulizonazo ,ikiwemo madini,mafuta na gesi katika nchi yetu.  Na nyinyi ni mashahidi ndugu zangu katika maendeleo ya sehemu zote duniani si uwepo tu rasimali zilizopo katika mahali husika ila ni namna ambavyo wazawa au nchi inatumia rasimali hizo  ili kujileta maendeleo.

Na ndio maana tumesema ni uchumi ambao utaangalia zaidi ushindani wake kwa kutegemea sekta ya viwanda bila kusahau  biashara,kwahiyo hili nilitaka kuliweka vizuri . Sisi kama sekta inayoratibu viwanda na biashara na uwekezaji kwa ujumla wake tumeweza kuandaa andiko ambalo limeweka mazingira wezeshi au kuboresha mazingira ya kufanya biashara,  ili kuhakikisha tunapunguza zile changamoto au vitu ambavyo vinapelekea uwekezaji wetu kutokuvutia .

Moja tunachokifanya sasa kuona namna gani bidhaa zinazozalishwa katika nchi yetu zinakuwa shindani .Sasa tunaandaa sera mpya ya ubora ambayo itaangalia kwa upana wake pamoja na kuendeleza sekta binafsi kuhakikisha wazawa wananufaika katika uzalishaji katika miradi hii, lakini pia bidhaa zinazozalishwa kwenye nchi hii ziwe kweli ni za ushindani ili na sisi tuweze kunufaika na uwepo wa eneo huru la biashara afrika.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *