Kuna usemi wa Kiswahili unaosema: “Ukishangaa ya Mussa utayaona ya Firauni.” Mnamo Septemba 2021, wanajeshi walitwaa madaraka nchini Guinea na kumuangusha Rais Alpha Condé aliyekuwa akiongoza taifa hilo la Afrika ya Magharibi. Kuna walioshangaa na kushtushwa, lakini kuna waliosema, kama wanavyosema Waswahili wa Pwani, “Astahili yake, kayataka.”
Kwa miaka mingi, Conde alikuwa mpinzani wa utawala wa kimapinduzi wa Rais Ahmed Sékou Touré, Baba wa vuguvugu lililoongoza harakati za kupigania uhuru wa Guinea, ambapo mwaka 1958, taifa hilo liliukataa ukoloni kwa kupiga kura ya hapana dhidi ya ukoloni wa Ufaransa na kuamua kuwa huru.
Sékou Touré alitawala hadi alipofariki 1984. Siku chache baadaye, katika kile kilichoonekana kuwa kinyang’anyiro cha kuwania madaraka, jeshi, likiongozwa na Lansana Conté, likachukuwa madaraka.
Kuna tetesi kwamba hatua hiyo ilifanyika kumzuwia Ismail Toure, ndugu wa baba mmoja wa Sékou Touré, kushika hatamu za uongozi wa nchi. Ismail, aliyeiongoza Idara ya Usalama wa Taifa ya Guinea, alifahamika kama mtu aliyehusika na kamata kamata ya maadui wa mapinduzi na kuwekwa gerezani. Pia, inaaminika kwamba alihusika katika kifo cha Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU), Diallo Telli.
Conté alifariki mwaka 2008, lakini Guinea ikabakia tena mikononi mwa wanajeshi baada ya mapinduzi yalioongozwa na Kapteni Moïse Dadis Camara. Camara naye hakudumu madarakani. Mnamo mwaka 2009, alinusurika katika jaribio la kuuwawa na kukimbizwa Morocco kwa matibabu na sasa anaishi uhamishoni nchini Burkina Faso.
Guinea iliingia katika mfumo wa siasa ya vyama vingi mnamo mwaka 2010, wakati jeshi lilipoachia madaraka, kutokana na shinikizo la raia wake walioungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa. Alpha Condé alishinda uchaguzi huo na akachaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka miatano mwaka 2015.
Madaraka matamu
Ulipofika muda wa kuondoka, Condé, 83, aliwashangaza wengi aliposhurutisha kifungu kifungu cha kikatiba kilichoweka ukomo wa madraka wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, kibadilishwe na kufanya madaraka ya urais yasiwe na ukomo. Akawaachia kazi wapambe wake ambao walifanikisha hilo kutokea.
Bunge likayapitisha mabadiliko hayo. Condé, aliyeishi uhamishoni nchini Ufaransa kwa miaka mingi na kumkosoa Ahmed Sékou Touré akimwita dikteta, akageuka mbinafsi na kuwa dikteta mpya. Akafanya yale yale aliyodai yakifanywa na utawala aliouita muovu wa Ahmed Sékou Touré .
Condé aliwadhibiti wapinzani wake, akahakikisha Tume ya Uchaguzi na Mahakama ziko upande wake, kwa kuwateuwa wale waliokuwa wakimuunga mkono. Hatimaye, wakati jamii ya Waguinea ikiwa inakabiliwa na kitisho cha kugawanywa na mivutano ya kikabili na kimajimbo, mnamo Septemba 5, 2021, jeshi likajiingiza kati na kumpindua.
Mapinduzi hayo yaliongozwa na Kanali Mamady Doumbouya, mwanajeshi wa zamani wa kikosi cha Ufaransa nchi za nje maarufu kama Legionnaire. Doumbouya alikuwa ameitwa na Condé mwaka 2018 arudi nyumbani kukiongoza kikosi kipya cha ulinzi wa Rais, Guinean Special Forces Group, kwa maana nyengine, kikosi maalum cha kumlinda Condé. Karata aliyoicheza Condé haikuwa turufu nzito!
Doumbouya ndiye aliyemng’oa Condé madarakani. Tangu yafanyike mapinduzi hayo, Doumbouya amemteuwa kuwa Waziri Mkuu, akiahidi kuirejesha Guinea katika utawala wa kidemokrasia, baada ya kuandikwa Katiba Mpya kwa kushirikisha wadau wote. Pia, akatangaza kwamba yeyote aliye na wadhifa katika Serikali ya mpito hatokuwa na haki ya kugombea wadhifa wowote pale uchaguzi utakapofanyika.
Waguinea waliopoteza matumaini na Condé, waliyakaribisha mabadiliko hayo. Doumbouya, kwa upande wake, ahakusita kutafuta mbinu za kukubalika na tabaka zote za jamii. Alifika nyumbani kwa mjane wa Rais wa kwanza Ahmed Sékou Touré, akionesha heshima zake kwa kiongozi huyo aliyemwita mkombozi wa taifa la Guinea.
Waguinea, na hasa kizazi kipya, leo wanamkumbuka Sékou Touré, wakivutiwa na hotuba zake alizokuwa akizitoa na msimamo wake wa kuliweka taifa hilo mbele, licha ya njama nyingi za mkoloni wa zamani Ufaransa za kutaka kumuondoa madarakani.
Ufaransa iliwatumia hata viongozi walioonekana ni vibaraka wake katika nchi jirani kama Félix Houphouët-Boigny wa Côte d’Ivoire kutimiza masilahi yake. Duru zinasema hata Léopold Sédar Senghor wa Senegal alitumika kufanikisha njama na mipango hiyo ya Ufaransa ya ‘kumshughulikia’ Sékou Touré.
Hiki kilikuwa ni kipindi cha Vita Baridi, kipindi ambacho mvutano kati ya wa Kambi ya Mashariki na Kambi ya Magharibi ulikuwa umepamba moto. Sékou Touré aliandamwa zaidi walipopinduliwa Kwame Nkrumah wa Ghana na Modibo Keïta wa nchini Mali.
Condé amuacha mkono sahibu yake
Kupinduliwa kwa Condé bila shaka kumemtia wasiwasi rafiki yake mkubwa Rais Alassane Ouattara wa Côte d’Ivoire. Wote wawili ni kama waliovinjari pamoja kuzikanyaga katiba za nchi zao husika. Ouattara kwanza aliamua kuheshimu Katiba na kuonesha ishara ya kwamba angeondoka madarakani mara muda wake utakaomalizika.
Alikwisha ongoza kampeni ya kumpata mrithi wake, akimchagua Waziri Mkuu Amadou Coulibaly. Coulibaly alifariki ghafla kwa kile kilichotajwa kuwa ni matatizo ya moyo. Ouattara akabadili msimamo na kuanza kutekeleza mkakati mpya.
Alishikilia kwamba Katiba haimzuwii kugombea kipindi cha tatu kwa kuwa kipindi cha kwanza kilitokana na mgogoro alipomshinda hasimu yake Laurent Gbagbo aliyeyakataa matokeo yaliotangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Mapigano yaliozuka kati ya wapiganaji waliomsaidia Ouattara, wakiongozwa na kiongozi wa waasi waliojenga ngome yao Kaskazini, na majeshi yaliomuunga mkono Gbagbo, hatimaye yakapelekea Gbagbo kukamatwa, kwa msaada wa majeshi ya Ufaransa.
Ufaransa imekuwa na kambi kubwa ya kijeshi nchini humo, baada ya ile ilioko Chad. Matokeo hayo yaliashiria kuwa Ouattara, ambaye sasa ana umri wa miaka 79, ni mtu wao.
Gbagbo amerudi tena katika ulingo wa siasa, tangu alipoachiwa huru na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, alikokuwa akishtakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu alipokataa kuwa ameshindwa na Ouattara, kupelekea taifa hilo kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Alikabidhiwa kwa Mahakama hiyo mwaka 2011 punde tu baada ya kutiwa nguvuni. Alikutwa asiye na hatia mwaka 2019 na kuruhusiwa kurudi nyumbani mwaka 2020.
Gbagbo hakujifunza?
Tangu arudi nyumbani mnamo Juni 2020, baada ya kuishi kwa muda Ubeligiji, kiongozi huyo ameingia kwenye mvutano na wenzake katika chama alichowaachia alipokuwa akizuiliwa huko The Hague.
Inaelekea washirika wake wa zamani wanaona hana mchango wa kukisaidia tena chama hicho baada ya matukio ya 2010-2011 na angefaa apumzike. Lakini, wimbo unaonekana ni ule ule, “madaraka matamu.”
Akiziona ishara za kushindwa vita hivyo, Gbagbo ameamua kuunda chama kipya, akisema kwanza hataki kupoteza muda katika mvutano wa kisheria, na pili ameazimia kuendelea kuwa katika siasa hadi kifo. Katika siasa, mahasimu wa jana wanaweza ghafla kuwa marafiki wa leo.
Gbagbo ameshakutana na Ouattara kwa mazungumzo yaliotajwa na wote wawili kuwa ya manufaa na kirafiki. Mazungumzo hayo yamefanyika katika wakati ambapo Ouattara ana uhasama na mshirika wake wa zamani aliyemsaidia kuingia madarakani Guillaume Soro.
Awali ilikubalika kwamba Soro awe mgombea baada ya Ouattara kumaliza mhula wa pili, lakini mapatano yao hayakuzaa matunda. Soro, aliyewahi wakati mmoja kuwa Waziri Mkuu na baadae Spika wa Bunge, sasa anaishi uhamishoni. Ushirika wa Ouattara na Rais wa zamani Henri Konan Bedie pia ulivunjika.
Tukiyatathimini ya Condé nchini Guinea, Ouattara na Gbagbo Cote d´Ivoire, nadhani tunaweza kukubaliana kwamba matukio haya yanavunja moyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watu hawa walikuwa ni wapigania mageuzi kabla ya kushika madaraka na kuanza kurudia madhila ya watangulizi wao au zaidi.
Udhaifu wa Umoja wa Afrika
Kauli kwamba matatizo ya Afrika yatatuliwe na Waafrika wenyewe, kimsingi inavutia. Lakini uhalisia wake hauendi sambamba na matarajio yetu. Mzunguko wa matukio ya kisiasa ya kusikitisha katika nchi kadhaa barani Afrika, unaashiria udhaifu wa Umoja wa Afrika na dira ya kulipeleka usoni bara hilo.
Matumaini juu ya demokrasia kama msingi wa maendeleo na hatua za kuondokana na matukio ya wizi wa kura na mapinduzi ya kijeshi yanazidi kutoweka.
Mafanikio ya kubadilishwa kwa vifungu vya Katiba kuongeza mihula ya watawala, nchini Rwanda, Burundi, Uganda, Djibouti, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Comoro kwa kuzitaja chache, kumewafungulia milango watawala hao kuchaguliwa tena bila upinzani.
Kwa upande mwengine, Waraka wa Umoja wa Afrika na tangazo la Lome linalopinga mabadiliko ya Serikali kinyume na Katiba, vimetoa ufafanuzi wa wazi jinsi ya kukabiliana na mapinduzi ya kijeshi na wanaokataa kuondoka madarakani wanaposhindwa uchaguzi.
Lakini matokeo yake Umoja wa Afrika umeshikwa na kigugumizi katika kutekeleza matakwa ya miongozo hii. Sababu kubwa ni kulindana. AU imegeuka kilabu ya maneno matupu, tafrija za kupokezana kijiti cha uenyekiti wa mwaka na kupongezana.
Mabadiliko ya kweli ya kidemokrasia, ikiwa ni zaidi ya nusu karne baada ya uhuru kwa sehemu kubwa ya nchi za bara la Afrika, bado ni ndoto. Afrika kwenye eneo la demokrasia unaweza kusema bado tuko mguu mmoja ndani, mguu mmoja nje.
Mohamed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.