Zuhura Yunus: Nimeandika Kitabu Kufuta Dhana Kwamba Wanawake wa Kizanzibari ni Legelege

Ni kitabu cha Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi, kilichozinduliwa Novemba 6, 2021.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Mwandishi wa habari mkongwe nchini Tanzania mwenye asili ya Zanzibar Zuhura Yunus amesema kwamba kilichomsukuma kuandika kitabu kuhusiana na simulizi ya mwanamke aliyeshiriki kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ni azma yake ya kutaka kufuta kwenye akili za watu wengi kwamba “wanawake wa Kizanzibari ni legelege.”

Mnamo Januari 12, 1964, vijana wa Kiafrika walifanya mapinduzi dhidi ya Serikali ya Kifalme chini ya Sultan Jamshid bin Abdullah, mwezi mmoja tu baada ya vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) kuunda Serikali ya mseto kufuatia ushindi walioupata kwenye Uchaguzi Mkuu wa Julai 1963, uchaguzi ambao Chama cha Afro-Shirazi (ASP) kiliamini kilishinda lakini hakikuruhusiwa kuunda Serikali.

Tukio hilo la Januari 12 ambalo uhalali wake umekuwa ukibishaniwa na makundi mbalimbali ya Wazanzibari pamoja na wanazuoni liliratibiwa kwa ukaribu na Chama cha Afro-Shirazi (ASP) pamoja na Chama cha Umma huku watu kama John Okello, raia wa Uganda, wakitajwa kama viongozi wa vuguvugu hilo lililopelekea Sultan Jamshid kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza huku nyuma yake Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiundwa chini ya Abeid Amani Karume akiwa Rais wake wa kwanza.

Mchango wa wanawake kusahaulika

Lakini wakati sasa ikikaribia miaka 57 tangu Mapinduzi ya Zanzibar yatokee, tukio hili muhimu katika historia ya Zanzibar limekuwa likionekana kama ni tukio la wanaume tu, huku wanawake waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba utawala wa Kisultan unaanguka visiwani humo wakipewa nafasi ndogo sana kwenye maandishi ya kihistoria ya tukio hilo au wakinyimwa kabisa fursa ya uwepo kwenye historia hiyo.

Zuhura Yunus mwenyewe kwa mfano kwenye kitabu chake hicho anaonesha kuhuzunishwa na hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo licha ya kutenga eneo maalum la kuwaenzi na kuwakumbuka waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar linalojulikana kama Mapinduzi Square, lakini karibia waasisi wote wanaokumbukwa ni wanaume huku wanawake wakionekana kwa tabu sana.

Mmoja kati ya wanawake hawa ni Biubwa Amour Zahor, mwanamapinduzi wa Kizanzibari aliyekuwa mstari wa mbele kwenye harakati za kimapinduzi visiwani humo. Biubwa ndiye muhusika mkuu katika kitabu hicho cha Zuhura Yunus kinachoitwa Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi kilichozinduliwa siku ya Jumamosi, Novemba 6, 2021, katika hoteli ya Golden Tulip, mjini Zanzibar.

“Nilianza mwaka 2017 kuandika [kitabu hiki] na kila mwaka nikija likizo [kutoka Uingereza ninakofanya kazi] nilikuwa naendelea kumuhoji [Biubwa] na kuzungumza nae,” Zuhura, Zuhura, mwandishi wa habari wa kwanza mwanamke kutangaza katika kipindi cha Dira ya Dunia TV kupitia idhaa ya BBC Swahili, aliwaambia wageni waalikwa waliofika kushuhudia uzinduzi wa kitabu chake cha kwanza kuandika. 

“Lengo  haswa la kuandika kitabu hiki ni kusimulia na kuwatambua wanawake wa Zanzibar ambao walijitoa na walikuwa sehemu ya Mapinduzi [ya Zanzibar] na pia nimeandika ili kuondoa dhana ya kuwa wanawake wa Zanzibar ni legelege kama wanavyosema watu,” aliongezea Zuhura.

Harakati za kumpata Biubwa

Kitabu hiki ambacho kimsingi ni wasifu wa Biubwa ni zao binafsi la jitihada za Zuhura kujisomea historia ya Zanzibar na kujidadisi endapo kama kunaweza kukawa na mwanamke aliyeshiriki harakati za mapinduzi kwani mpaka muda huo hakuwa amekutana na muhusika wowote mwanamke kwenye kujisomea kwake. 

Shauku hii ilimpelekea Zuhura kukutanishwa na mtoto wa Biubwa anayeitwa Salma Ali Hassan ambaye Zuhura alimuomba azungumze na mama yake kwa ajili ya kupata idhini ya kuandika kitabu kuhusu maisha yake.

Biubwa alikubali ombi hilo na matokeo yake ni kitabu chenye kurasa takriban 220 kinachoelezea maisha ya mama huyo na mchango wake katika harakati za kimapinduzi visiwani Zanzibar. 

Akigusia umuhimu wa kuwa na mageuzi katika mitazamo ya watu kuhusu ushiriki wa wanawake katika harakati za ukombozi wa mataifa yao, mwandishi na mwanaharakati wa haki za wanawake Salama Maoulidi alisema kwamba kitabu cha Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi kinatoa mchango mkubwa katika muelekeo huo.

Maudhui sugu ya ukatili wa kijinsia

“Simulizi ya [Biubwa Amour Zahor:] Mwanamke Mwanamapinduzi imefanya mageuzi kwenye simulizi za wanawake kwenye Mapinduzi [ya Zanzibar],” Salama, anayechapisha maandiko yake mengi kwenye mtandao wa Pambazuka News: Voices of Freedom and Justice, aliwaambia washiriki waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho. 

“Yaliyomo humu kwenye kitabu ni taswira ya maisha ya maudhui sugu ya ukatili wa kijinsia, ndoa za kulazimishwa na kunyimwa elimu kwa wanawake wa Kizanzibari,” aliongeza Salama.

Mwanazuoni huyo alikiri kwamba ni suala la kujivunia kuona historia za mwanamke wa Zanzibar inaandikwa na mzawa, tena nae akiwa ni Mzanzibar. Kwa mujibu wa maelezo yake: “Hiki ni kitu ambacho si agh-labu kutokea kwa sasa, mambo haya  [ya kuandika historia za watu] mara nyingi hufanywa na wageni.”

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dk Saada Mkuya Salum alikielezea kitabua hicho kama ni kitabu kinachohusu maisha ya mwanamapinduzi aliyesimamia kile alichokiamani.

Kitabu chamtoa machozi waziri

“Sehemu ambayo ilinitoa machozi kwenye kitabu hiki ni suala la unyanyasaji wa kijinsia,” alisema Dk Saada. “Kumbe mambo hayo yalikuwepo toka zamani. Ila ujasiri wa Biubwa kumsimuliza Zuhura na  yeye [Zuhura] akaweza kuandika si kitu kidogo.” 

Waziri huyo alibainisha kwamba kitabu hicho pia kinaonesha umuhimu wa suala la elimu kwa wanawake wa Kizanzibar na kama angepata nafasi ya kukuita jina jengine basi angekiita Nguvu ya Mwanamke.

Kitabu hiki kwa sasa kinapatikana kwa bei ya Sh45,000 kwa nakala ngumu na Sh30,000 kwa nakala laini. Baada ya kuzinduliwa Zanzibar, kitabu hicho pia kinatarajiwa kuzinduliwa Dar es Salaam mnamo Novemba 13, 2021. Kitabu kinapatikana kwenye maeneo haya kwa sasa. 

Nakala 150 zauzwa

Jumla ya nakala 150 za Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi ziliuzwa kwenye halfa ya uzinduzi uliohudhuriwa na mawaziri kutoka Serikali ya Zanzibar, mabalozi wanaowakilisha nchi zao Zanzibar na waandishi wakongwe wa fasihi pamoja na waandishi wa habari. 

Mama Shadiya Karume, mke wa aliyekuwa Rais wa awamu ya sita ya Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar Dk Amani Abeid Karume, pia alikuwa ni miongoni mwa wageni waalikwa kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho.

“Sijaweza kuandika kila kitu kwenye kwenye kitabu hiki,” Zuhura aliwatahadharisha watu waliokuwa wakimsikiliza kwa makini wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho. “Ikumbukwe pia hiki ni kitabu cha kihistoria, hivyo kukusanya tarehe, majina na mengineyo ilikuwa ni changamoto. Licha ya kuhaririwa mara 1,000, bado kunaweza kukawa na makosa kwenye kitabu hiki. Nilitaka pia kisiwe kikubwa ili watu waweze kusoma [kwa urahisi].”

Najjat Omar ni mwandishi wa habari za kijamii kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts