The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Kitendo cha Moroko kuendelea kuikalia kwa mabavu Sahara Magharibi kinaonesha kwamba harakati dhidi ya ukoloni barani Afrika hazijaisha

subscribe to our newsletter!

Sahara Magharibi, eneo linalozozaniwa lililopo kwenye mwambao wa Kaskazini-Magharibi mwa ukanda wa Afrika ya Kaskazini na Afrika Magharibi, ilikuwa koloni la pili la Uhispania barani Afrika baada ya Guinea ya Ikweta, au Equtorial Guinea. Licha ya kwamba Uhispania ilishaondoka kwenye eneo hilo takriban miongo mitano sasa, bado wananchi wa Sahara Magharibi wanaendelea kubaki kwenye ukoloni huku taifa la Moroko likirithi nafasi ya Uhispania.

Kwa mujibu wa Serikali ya Tanzania, “Sahara Magharibi ni koloni la mwisho barani Afrika,” kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mnamo Oktoba 26, 2021, na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Kwa mujibu wa taifa hilo la Afrika Mashariki: [Sahara Magharibi] ni kesi ya kusikitisha ya mapambano dhidi ya ukoloni ambayo bado haijafika mwisho wake.”

Harakati za watu wa Sahara Magharibi kujikomboa kutoka kwenye ukoloni ni za muda mrefu, zikianza na utawala wa Uhispania iliyokua inawakalia watu hao na ambazo kwa sasa zinaendelea dhidi ya Moroco ambayo imekuwa ikiwakalia watu hao tangu mwaka 1976 baada ya Uhispania kuiachia Moroco kuitawala Sahara Magharibi. 

Tangu muda huo, watu wa Sahara Magharibi, chini ya vuguvugu lao la kupigania uhuru linaloitwa Polisario Front, wameendelea kupambana dhidi ya Moroko ili waweze kuwa huru na kujiamulia mambo yao wenyewe bila mafanikio huku Moroko ikiendelea kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa madai kwamba Sahara Magharibi ilikuwa ni sehemu ya Moroko hata kabla ya ukoloni wa Uhispania.

Kushindwa kwa AU

Lakini wadadisi wa mambo wanabainisha kwamba sababu kuu inayoifanya Moroko kuendelea kuikalia kwa mabavu Sahara Magharibi, hali ambayo imeendelea kuzigawa nchi za Afrika katika Umoja wa Afrika (AU), ni utajiri mkubwa wa madini ya Phosphate yanayodaiwa kuwepo Sahara Magharibi. 

AU, ambao zamani ulikuwa ukijulikana kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), umeshindwa kabisa kuja na suluhu endelevu ya mgogoro kati ya Sahara Magharibi na Moroko na hivyo kushindwa kutokomeza ukoloni na viasharia vyake barani Afrika kama ilivyokuwa lengo la kuanzishwa kwake. Tatizo moja la AU ambalo linaweza likawa limesababisha hali hii ni nia ya AU kutaka kukidhi matakwa ya kila upande, Moroco (mtawala) na Sahara Magharibi (mtawaliwa). 

Hii inadhirishwa na kitendo cha AU kuirejeshea uanachama wa chombo hicho nchi ya Moroko mnamo Januri 28, 2018, licha ya kwamba taifa hilo lilijitoa kwenye OAU mnamo mwaka 1984 kufuatia hatua ya OAU kukubali ushiriki wa Sahara Magharibi kwenye chombo hicho. Hatua hiyo ya AU ilikuja licha ya ukweli kwamba Sahara Magharibi bado ni mwanachama wa chombo hicho. Wengi wameielezea hatua hii kama usaliti wa AU kwa Sahara Magharibi.

Ni maoni yangu kwamba kurudi kwa Moroko kuwa mwanachama ni mkakati wa kidiplomasia wa taifa hilo wa kuhakikisha kwamba Sahara Magharibi itengwe na  hata kuendelea kuzingatiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Afrika kutakuwa sawa na kuwa na hadhi ya muangalizi tu kwa chama cha  Polisario.

Nasema hivi kwa sababu Mfalme Mohammed VI wa Moroko anaonekana kulivalia njuga suala la Sahara Magharibi. Kwa mfano, kati ya mwaka 2000 na 2017, kiongozi huyo mkuu wa Moroko amefanya ziara zaidi ya 50 katika nchi  zaidi ya 26. Lengo lake ni kuitafutia Moroko uungwaji mkono katika harakati zake za kutaka irudi  tena kuwa mwanachama wa Umoja wa Afrika, hatua iliyofanikishwa mwaka 2018.

Pia, Moroko imejaribu kuzirai Nigeria na Ethiopia zibakie  katika msimamo wao wa kutouunga mkono upande wowote katika mgogoro huo. Katika ziara yake ya siku tano nchini Tanzania, iliyoanza Oktoba 25, 2016, vyombo vya habari viliripoti kwamba nchi hizo mbili zilisaini mikataba 21 ya ushirikiano. 

Jitihada za Moroco zazaa matunda

Na kusema kweli jitihada za Mfalme Mohamed VI hazijawa za kazi bure. Kwa kiasi kikubwa jitihada hizo zimeishia kuzifanya nchi zilizofikiwa kujiweka karibu na Moroko na kujitahidi kulinda maslahi yake kwenye mgogoro unaoendelea kati yake na Sahara Magharibi. Na hii bila shaka inajumuisha Tanzania chini ya kiongozi wake wa awamu ya tano Hayati John Magufuli. 

Tanzania,  nchi iliyosifika katika kuwatetea watu wanaokandamizwa, ilishindwa kuweka msimamo wa wazi kuhusu suala la Sahara Magharibi. Tukio la kukumbukwa zaidi ni lile la Novemba 2018 lililovikutanisha vyama vya ukombozi barani Afrika katika mji mkuu wa Namibia wa Windhoek. Wajumbe wa mkutano, ambao walijumuisha Chama cha Mapinduzi (CCM), walitoka na azimio linaloelezea msimamo wao wa kushikamana na watu wa Sahara Magharibi na Palestine ambao wanakaliwa kimabavu na mataifa ya Moroko na Israel mtawalia. Hata hivyo, CCM ilikataa kushiriki kwenye azimio hilo. 

Utata kuhusu Sahara Magharibi unafanana na ule  juu ya  uungaji mkono kwa Wapalestina. Tanzania wakati wa utawala wa  Nyerere ilisimama kidete kukiunga mkono Chama cha Ukombozi wa Palestina maarufu kama PLO na  mapambano ya Wapalestina yakudai ardhi yao inayokaliwa na Israel na hatimaye kuwa na taifa lao. 

Hata hivyo, katika kipindi cha utawala wa Magufuli, Tanzania ilionekana kuunga mkono uamuzi wa Israel wa kuhamishia makao makuu yake Jerusalem kutoka Tel Aviv, hali iliyosababisha machafuko kati ya mataifa hayo mawili ya Mashariki ya Kati.

Tanzania si nchi pekee kwenye nchi za Kiafrika zinazoendelea kutumbukia katika mchezo wa masilahi unaotumiwa na mataifa ya kigeni kiasi cha hata kupoteza heshima ilizokuwa nazo katika siasa za dunia.  Chini ya kile kinachoitwa utandawazi na vitega uchumi, nchi  nyingi zimeshawishika na vitega uchumi kwa kile zinachokiona kuwa njia muwafaka  ya kujipatia maendeleo. 

Lakini badala ya  vitega uchumi kutumiwa kama  msingi wa ushirikiano utakaozinufaisha pande mbili husika,  vitega uchumi hivyo hutumiwa kama njia ya kurubuni nchi zinazoendelea na kuzifanya zitetee maslahi ya mataifa makubwa, muda mwengine kwa gharama hata za nchi wenzao zinazoendelea. Hili linadhihirika kwenye uungwaji mkono wa mataifa kama Israel na Moroko katika juhudi zao za kuzikalia Palestine na Sahara Magharibi kwa mabavu.

Uko wapi uhuru wa Afrika? 

Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika, bara zima la Afrika liko huru. Lakini suala hilo kimsingi linabakia  kuwa la mabishano. Mbali na jumuiya ya kimataifa  kuwapa haki wananchi wa Sahrawi kuamua hatima yao kwa kuitishwa kura ya maoni, jambo ambalo ni la  kujin´goa kutoka kwenye utawala wa Moroko, hatua hiyo bado haijafikiwa. 

Suala jengine linaloonesha kwamba Afrika bado haijawa huru linahusu kisiwa cha Comoro cha Mayotte. Maazimio yote ya Umoja wa Afrika tokea wakati wa OAU na yale ya Umoja wa Mataifa yanaitambua Mayotte kuwa sehemu ya muungano wa visiwa vya Comoro. Visiwa hivyo vilipiga kura kwa pamoja kuwa huru Disemba 1974. Haikuwa kura ya kisiwa  kimoja kimoja. 

Lakini Ufaransa imeendelea kukikalia kwa nguvu kisiwa hicho cha Mayote baada ya kutumia mbinu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukifanya kuwa sehemu ya ardhi yake kama ilivyofanya kwa mataifa ya Caribbean  ya  Guadelope na Martinique. Kwa sasa masuala hayo mawili yamepewa mgongo.

Kuhusu  Sahara Magharibi,  Moroko imeendelea kuhakikisha idadi ya  Wasahrawi inapungua kwa kuendesha sera ya kuwapeleka walowezi katika eneo hilo.  Wasahrawi wanazidi kuwa wachache ikisemekana ni asilimia 40 tu  wanaoishi Sahara Magharibi. Idadi kubwa ingali bado katika makambi katika mpaka wa Moroco na Algeria. 

Mfalme Mohammed VI anajizingatia kuwa mshindi. Katika kuadhimisha miaka 46 ya Matembezi ya Kijani wiki iliopita, Mfalme Mohammed VI alisema: “Sahara  Magharibi ni ardhi ya Moroko na hilo halina mjadala.”

Umoja wa Afrika umekosa kuwa na msimamo wa kueleweka  na huwenda wanaosema kwamba  hauna dira hawajakosea.  Lakini umoja huo utakuwa vipi na dira ikiwa wengi wa wanachama wake wanashindwa kuwa na msimamo unaoeleweka yanapokuja masuala yanayolihusu bara lao?

Mohamed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *