‘Harakati za Kudai Katiba Mpya Ziende Sambamba na Kudai Mabadiliko Kwenye Mfumo wa Elimu’

Mwanahabari huyo mkongwe nchini anadai elimu inayotolewa kwa sasa nchini haimjengi Mtanzania kuwa huru na kuweza kuiwajibisha Serikali yake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mwanahabari na mwanaharakati wa siku nyingi nchini Tanzania Dk Ananilea Nkya ameshauri kwamba harakati za kudai Katiba Mpya nchini zinapaswa ziende   sambamba na harakati za kudai mabadiliko kwenye mfumo wa elimu wa Tanzania ambao ameuita “janga kubwa” na ambao anadai haumjengi kijana wa Kitanzania kufahamu namna nchi yake inavyoendeshwa na nafasi yake kwenye mchakato huo mzima.

Dk Nkya, ambaye pia ni mshauri na mtafiti wa masuala ya vyombo vya habari nchini Tanzania, alitoa ushauri huo mwanzoni mwa wiki hii huko jijini Arusha alipokuwa mmoja wa waongeaji kwenye uzinduzi wa kitabu cha mwandishi mkongwe Jenerali Ulimwengu kinachoitwa Rai ya Jenerali: Juzuu ya III uliofanyika Novemba 9, 2021, chini ya udhamini wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

“Yaani elimu yetu tunayoitoa [Tanzania] haitolewi katika hali ambayo itamjengea kila mtoto wa Kitanzania aithamini Tanzania, aitumikie Tanzania, asimame kama mzalendo wa Tanzania kutetea maslahi yake ya Mtanzania na Watanzania wenzake,” Dk Nkya aliwaeleza washiriki wa hafla hiyo iliyojikita katika kujadili nafasi ya wananchi katika mapambano ya kudai Katiba Mpya. “Hapo ndio tuna shida kubwa sana kwenye elimu yetu na kama hatutaibadilisha hali hiyo hata kama tutakuwa na Katiba Mpya bado tutakuwa na tatizo kubwa sana, kubwa sana la uwajibikaji.”

Yafuatayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya Dk Nkya na Afisa Programu kutoka LHRC Tito Magoti ambayo yalilenga kupata mtazamo wa Dk Nkya wa changamoto zinazokwamisha juhudi za kudai Katiba Mpya nchini na mapendekezo yake juu ya nini kinapaswa kufanywa kukabiliana na changamoto hizo. Hapa Dk Nkya anaanza kwa kueleza changamoto ya wananchi kushindwa kupata taarifa sahihi kuhusiana na kinachoendelea kwenye nchi yao, hali inayowafanya kushindwa kushiriki kikamilifu katika uendeshwaji wake. Endelea …

Dk Ananilea Nkya: Mimi kama mwanahabari najua kwamba mtu anahitaji kwanza awe anafahamu hali ilivyo awe anafahamu, lakini kama anafahamu nani anastahili, anawajibu wa kumfahamisha mwananchi? Si kuna vyombo vyenye wajibu huo, si kuna taasisi zina wajibu huo, si kuna vyombo vya kitaifa, vya kiserikali, vya kijamii vinapaswa kuwafahamisha wananchi? Ni suala la kuuliza je, wananchi wanafahamishwa, wanashirikishwa kwa kupitia hivi vyombo kufahamu kwamba ni kitu gani leo kipo moto? 

Sijui kama wanafahamishwa na ninasema hivi kwa sababu nimekuwa hapa nchini kwetu wakati wa chama kimoja na wakati wa redio zikiwa ni za Serikali peke yake na za chama. Kwa hiyo, wakati ule kama ni jambo moja litazungumzwa katika hivyo vyombo vya Serikali, vyombo vya kitaifa, iwe ni redio itazungumza hilo jambo na wananchi watalifahamu. Kwa mfano, kama ni suala la kilimo, jinsi ya kuotesha mahindi na wakati gani waoteshe, ilikuwa linatangazwa na wananchi wanapata [taarifa] karibu nchi nzima. 

Mwananchi anakwambia nimesikia Redio Tanzania. Lakini baada ya [mwaka] 1992 tulivyoingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa tuliingia pia kwenye mfumo wa soko huria la vyombo vya habari tukasema kuna vyombo vya binafsi na kuna vyombo vya kiserikali. Lakini hatukuweka utaratibu kabisa [juu ya] ni masuala gani ya kitaifa ambayo ni lazima yawe yanabebwa na vyombo vyote vya habari. 

Kaka Jenerali [Ulimwengu] utanisahihisha maana yake sijapita sana kuona huko. Lakini je, kuliwekwa sheria ambayo inasema kuna masuala kama haya, haya, haya kila chombo chochote cha habari kitahakikisha kimetangaza jambo hilo? Kwa hiyo, kama hakuna ina maana kuna jambo litatangazwa [au] linaweza likatangazwa na chombo ambacho kinafikia watu wachache tu au kingine kabisa kikazuiliwa kisifikie watu wengi. 

Kwa hiyo, kuna wananchi wengi pengine wanakuwa wanaachwa hawana habari yoyote na jambo linalotokea katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ni jambo linalowahusu. Kwa hiyo, ile haki ya kupata taarifa imebaki kuwa kwenye Katiba lakini ukweli wa haki ya kupata taarifa muhimu zinazohusu maisha yao na hasa masuala ya kisiasa kwa sababu siasa inagusa kila kitu. Siasa ikiwa nzuri na uchumi unakuwa mzuri na mambo mengine yanakuwa mazuri. 

Kwa hiyo, hapo mimi naona tatizo moja lipo hapo katika kupata taarifa na tukifanya utafiti tu mdogo mdogo wa kuangalia vyombo vya habari vyombo vingi vya habari, tulisema sasa hivi tunajivunia kwamba tuna vyombo vingi vya habari mpaka kwenye ngazi ya jamii, mpaka vingine ngazi ya kijiji, ngazi ya mikoa kuna televisheni, kuna redio nyingi tu, lakini sikiliza maudhui. Maudhui yake ya kila siku. Kuna maudhui ya nyimbo za kucheza. Vitu vingine hata vya usiku vinaoneshwa mchana. Vya kitandani vinaoneshwa watoto. Hivo vipo ambavyo ndio watu wengi unakuta wanaviangalia. 

Lakini yanapokuja masuala muhimu, kwa mfano ya uwajibikaji wa viongozi, uwajibikaji wa wananchi wenyewe, utakuta hicho kitu hakipo. Kwamba ni namna gani, kwa mfano, wananchi wanaweza kuiwajibisha Serikali yao hata katika ngazi ya kijiji? Utakuta kama kuna redio ya jamii pale haitangazi habari hizo kwamba kuna mikutano ya kijiji kwa mfano ambayo inatakiwa ifanyike kila baada ya miezi minne kwa maana kuwe na miezi minne, mitatu, kama sikosei mikutano minne kwa mwaka, maana yake kila miezi mitatu ambapo wananchi wanakwenda kuhoji viongozi wao kwamba kilipangwa nini? 

Kwanza watapanga halafu wataangalia utekelezaji, si ndio? Sidhani kama Watanzania wengi wanajua kwamba wanawajibika kuhoji, kwanza kupanga, na kuhoji ile utekelezaji wa mipango. Kwa hiyo, na hizo redio za huko kwenye jamii ukisikiliza maudhui yake huwezi, nyingi hukuti zikizungumza habari hizo, na zikizungumza pengine ikafungiwa kwa sababu zikizungumza vitu hivyo maana yake zinaamsha wananchi waweze kuwawajibisha viongozi wao. 

Sidhani kama hiyo redio itakuwa rafiki sana na waliopo kwenye dola. Hilo ndio naliona tatizo kubwa na wananchi hatuhoji, si ndio? Na hata sisi [waandishi wa habari]. Kuna waandishi wa habari hapa hatufuatilii kutaka kuona vitu kama hivyo. Kwa hiyo, kuna tatizo kubwa la wananchi kupata taarifa na taarifa sahihi ya masuala muhimu ya kitaifa, masuala muhimu yanayohusu maisha yao. 

Mambo yanayowasilishwa zaidi kwenye redio na televisheni za kijamii ni yale mambo ambayo hayawezi kuleta mabadiliko makubwa ya kimfumo katika jamii na mengine ni yale ya burudani na mengine ni burudani zile ambazo za kuharibu jamii yetu kuwa jamii ambayo inaangalia tu masuala ya chini ya kiuno, si ndio? 

Au masuala ya michezo, sisemi kwamba michezo ni mibaya lakini ni kwa nini tuanze kumjua sana Ronaldo lakini hatumjui Mwenyekiti wetu wa Serikali ya mtaa? Yaani ukiuliza mwananchi niambie hata Mwenyekiti wako wa kitongoji hajui! Niambie hata kijijini kwako kwenye kitongoji chako mwaka huu kilipangwa kufanyika nini na kimefanyika nini na ambacho hakikufanyika ni kwa nini hakikufanyika? Muulize. Wengi watakwambia hawajui!

Tito Magoti: Lakini unafikiri ni bahati mbaya ama ni makusudi kwamba kumekuwa na msukumo wa kusababisha watu waone kwamba Serikali ni ujasiriamali, kwa mfano, ama watu waone kwamba ubunge ni ujasiriamali kwa hiyo mimi siwezi kujali mambo ya wajasiriamali? [Kwenye suala la] uenyekiti wa Serikali za mitaa. 

Mimi nilikuwa muangalizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2019, ninaweza kusema kwamba ule ulikuwa ni ujasiriamali wa kisiasa watu walitengenezeana nafasi na wakaishi. Sasa kwenye mazingira haya ambayo wananchi wanakata tamaa, wanajikatia tamaa, unafikiri kwamba hii kuyashutumu mazingira ya sasa inasimama peke yake ama kuna sababu nyingine ambazo tunatakiwa kuziona halafu tuzisahihishe ili tuwarudishe wananchi kwenye ushiriki?

Dk Ananilea Nkya: Nadhani kuna jambo kubwa la kutazamwa nalo linahusu mfumo wetu wa elimu kama nchi. Nadhani elimu yetu ya leo ni janga kubwa kweli kweli sasa, kesho na kesho kutwa na miaka ijayo. Ni janga kubwa sana kwa sababu haimjengi Mtanzania, [haimjengi] kijana wa Kitanzania kujua nchi yake inavyoendeshwa kuanzia pale alipo. Kujua wajibu wake yeye mwenyewe, [yaani] ana wajibu gani wa kuiwajibisha Serikali yake. Yeye mwenyewe ana wajibu gani wa kuijenga nchi yake. Hapo mambo hayo nadhani kuna nakisi kubwa, kubwa, kubwa kweli kweli. 

Kwa sababu, unaposema kwamba kuna mtu anamzuia [mwananchi kuihoji Serikali], hiyo ya kuzuia ingekuwa watu wamepata elimu ya kutosha ya uraia ya kuweza kufahamu yeye anawajibu gani kama raia wa Tanzania kuanzia shule ya msingi kwamba sauti yake ni muhimu katika kuongoza nchi [hicho kitu kisingewezekana]. 

Ukimsikiliza mwananchi hata wa kawaida anakwambia hii ni gari ya Serikali hahusishi na kodi yake, hahusishi kwamba hapa kuna kodi yetu wananchi, hapa kuna kodi yangu, hapa tunaponunua majani ya chai nalipa kodi kwa hii kodi inayokatwa hapa ndio imenunua ile gari ambalo huyo kiongozi anakwenda nalo badala ya kufanya shughuli za Serikali anafanya shughuli hizi. 

Yaani elimu yetu tunayoitoa haitolewi katika hali ambayo itamjengea kila mtoto wa Kitanzania aithamini Tanzania, aitumikie Tanzania asimame kama mzalendo wa Tanzania kutetea maslahi yake ya Mtanzania na Watanzania wenzake hapo ndio tuna tofauti kubwa sana kwa elimu yetu na kama hatutaubadilisha hali hiyo hata kama tutakuwa na Katiba Mpya bado tutakuwa na tatizo kubwa sana, kubwa sana la uwajibikaji.

Tito Magoti: Lakini mama, asante sana, lakini wanazuoni wanaoandaa vijana, kwa mfano, katika taasisi za elimu ya juu na vijana wenyewe kutoka muda na muda wanaothubutu kutumia elimu zao kufanya mambo fulani fulani kwa ajili ya taifa letu wanakumbana na misukosuko na wanapewa majina mabaya wengine wanateuliwa kuwa wahalifu, wanapewa kesi za kuchonga. 

Katika mazingira haya ambayo watu wanaoonekana wako mbele [kuisimamia na kuiwajibisha Serikali] wanapata shida namna ile na wewe umekuwa kwenye, umekuwa kiongozi wa Asasi za Kiraia, kama kiongozi anaonekana anapata shida kwa sababu ya kutumia akili yake, unafikiri kwamba mtu anayemtazama atapata wapi ujasiri wa kwenda mbele kama aliyeko mbele mwenye maarifa, mwenye taarifa anashambuliwa, hana msaada, hana chochote na hatimaye labda atapotea, atauawa, atafilisiwa. Katika haya ambayo hofu inajiunda na imekaa katika mfumo unafikiri kwamba tunaweza kurudi pamoja kama wananchi tukaliangalia taifa letu upya? Karibu.

Dk Ananilea Nkya: Sehemu kubwa ya haya yanayotokea hapa Tanzania nadhani wananchi wenyewe tuna nafasi, tuna mchango [wa kuyasababisha]. Lakini nikisema kwamba mchango wetu unatokana tulivyojengwa kielimu ndio inatufikisha hapa tulipofika. Kwamba tuna mchango kwa sababu kama unajua watawala wetu wanajua kwamba sehemu kubwa ya wananchi wetu, tena wananchi wetu ambao wengi ni vijana wenye nguvu tu, ndio wengi ambao mambo mengi hawaelewi kwa sababu wamesha tengenezwa hivyo, kuwa kundi ambalo sio la kuweza kusimama. 

Kwa hiyo, cha kwanza hicho cha kuogopesha kwa sababu ni wachache wanatoka wanamoyo wamebahatika kupata elimu yao vizuri au kujiendeleza wenyewe kufanya wajibu kwamba nina wajibu wamejua elimu ya uraia, kwa mfano, sisi na kina kaka Jenerali [Ulimwengu] zama zetu tulikuwa tunafundishwa yaani TANU ni nini, kitu gani ni nini. Yaani unaipenda nchi yako kuliko kitu chochote, si ndio? Unaiheshimu Jamuhuri kuliko kitu chochote. Kwa hiyo huogopi mtu, unaogopa hivi Jamuhuri yangu hapa nimeifanyia nini? Hapa nitakuwa nimefanya nini? 

Kwa hiyo, unakuwa na ule moyo kwamba hiki nikikifanya sio kwa ajili yangu ni kwa ajili ya sisi wote, ni kwa ajili ya Watanzania wote. Zama hizi zimekuwa ni zama tofauti. Vijana wametengenezwa zaidi kiakili [na] kielimu wametengenezwa kuangalia maslahi yao binafsi. Kwamba wanajua elimu ni yeye aweze kupata mshahara wake mzuri aweze kuishi maisha yake mazuri. Lakini hajui kwamba, yaani hajali kwamba yeye akipata na mwingine hana kwamba kuna tatizo la kijamii. 

Kwa hiyo, kwa sababu watu wamejengwa namna hiyo ni lazima kuwe na hilo tatizo kwamba akitoka mmoja, wawili, watatu wanatokea kuzungumza habari za wananchi wenye dola wakiwakamata wale watu waliowengi watasema hawa nao si mkate wao wanatafuta si anaongea labda anataka ubunge. 

Mimi nitoe mfano wangu mwenyewe, mimi wakati nimeamua kujitolea kuijenga taasisi yetu ambayo ni [Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania] TAMWA kwamba niliamua kwamba kuna vitu niliona hata haviendi inavyotakiwa, ile sauti tuliyotaka kuona ya wanawake ya pamoja sijaona ikisikika, ile kwamba tunajenga wanawake waandishi wa habari waweze kukua vizuri kitaaluma sijaiona nafikiri ngoja niingie nifanye kitu ambacho naamini. 

 

Yaani hata ndani ya TAMWA yenyewe walikuwa wanasema huyu nae sijui ndio kamekuwa-, siku zile chama kikubwa kilikuwa NCCR-Mageuzi wakati inaanza ndio kilikuwa chama kikubwa cha upinzani, baadae ikaja ya Zanzibar [Chama cha Wananchi] CUF, baadae ndio imekuja CHADEMA, imekuja juzi juzi. Yaani kila chama cha upinzani mimi nimehusishwa nacho, umeelewa? Sijui kama unanielewa. Yaani nikizungumza kwamba ukeketaji ni suala la kisiasa watu wanashangaa inakuaje ukeketaji ni suala la kisiasa. Watu wanafikiria ni suala la watu la kijamii. [Lakini] ni la kisiasa sana, si ndio? Kwa sababu, kama utawala katika ngazi za chini unafanya kazi ya kuelimisha na kuhamasisha ya kufanya wajibu wake kuweka rasilimali za kuhakikisha kwamba watu wanaelewa madhara ya ukeketaji, na kuna uwajibikaji wa uongozi, ukeketaji utakuwa haupo, sijui kama unanielewa? 

Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba yaani kazi hizi, kutetea haki za watu kuleta mabadiliko haitaweza kutokea ikiwa kama watu wanafikiri vile vile, wanatenda vile vile, wanasimamia ubinafsi wao kila wakati. Ni lazima watu wabadilike, ni lazima watu wajitoe, ni lazima ukubali kupewa majina mengi. Kaka yangu Jenerali aliwahi kuambiwa kabisa kwamba sio Mtanzania. Hajasema hilo hapa. Mimi wakati nafanya hizo harakati zangu kila wakati mfumo ulikuwa unanitumia watu wa kwenda kuniuliza sasa ukiteuliwa [kuwa afisa wa Serikali] utakubali? 

Nimepewa teuzi mara chungu nzima, nikasema sio wito nilioitiwa wa kwenda kuwa mbunge. Kama nilikuwa nataka kuwa mbunge ningechagua chama chochote cha siasa kwa sababu lengo la kupata ubunge si labda kwenda kuzungumza kwa niaba ya wananchi bungeni na kupata hela nzuri? Kikubwa ni pesa nzuri. Watu wanaendea kule, samahani kwa kulisema hili, lakini wengi wanaingia kwa sababu ya maslahi, kwa sababu ukiwa mbunge wewe tena una pesa, unaweza kuwa yaani katika mda wa miaka mitano lazima utatoka milionea fulani hivi. 

Kwa hiyo, watu wanakuja kuniuliza kwani ni kitu gani unataka? Kwa sababu miaka ile ya kwanza ndio ulikuwa uchaguzi alipoingia [Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin] Mkapa, wananisukuma [nigombee ubunge]. Sasa awamu ya pili [watu wakataka] niweze kupata uteuzi wa mbunge wa viti maalumu. Nikasema, mbona mimi sisemi haya mambo kwa sababu nataka kuwa mbunge. Sisemi haya mambo kwa sababu nataka kuwa mkuu wa mkoa. Sisemi haya mambo kwa sababu nataka kuteuliwa.

Nasema haya mambo kwa sababu yanagusa Watanzania wengi na hata kama mimi nitapata nini, kama Watanzania wenzangu hawana hicho kitu, [kwamba] maisha yao yapo pale pale, mimi hainisaidi kitu. Kwa hiyo, hata leo hii nadhani nikiongea chochote wanasubiri sijui kahamia chama gani? Kuna miaka hii ya karibuni wananiita CHADEMA. 

Lakini naomba samahani kusema mimi sina chama chochote cha siasa. Nilikuwa [Chama cha Mapinduzi] CCM na nikwambieni mimi niliondoka CCM kwa sababu gani? Cha kwanza nilivoingia TAMWA nikajua hapa kutakuwa na mgogoro wa kimaslahi. Mimi ni mwanachama wa CCM halafu chama changu [cha TAMWA] kinapaswa kuikosoa Serikali iliyoko madarakani, si ndio? Kwa hiyo, itakuwa ni mgogoro wa kimaslahi. Siwezi kuishambulia Serikali ya chama ambacho mimi ni mwanachama hata kama sio kiongozi. 

Lakini la pili kabisa lililoniondoa [CCM na] nikarudisha kadi siku hiyo hiyo [na] hapo hapo kwa mkuu wa wilaya, kulitoka kesi hapo mtaani kwangu [ambapo] viongozi wa Serikali ya mtaa wakauza jengo la Serikali ya mtaa tulilojenga sisi na matofali yangu kama mwananchi wa pale, wakamuuzia mwarabu mmoja ajenge kituo cha mafuta. Tukapambana kumbe walishagawa pesa hawa viongozi wa Serikali ya mtaa wakaenda kununua mashamba, wakanunua viwanja, wakaanza kujenga. 

Nikapambana ile kesi, nikanusurika kuuawa na huyo mwarabu mwenyewe maana yake walitoa mapesa mengi nilikuwa naambiwa nimetengewa Shilingi milioni 120 lakini kunifikia sasa hawanifikii niipokee. Kila wanaemuuliza anawaambia huyo hata maji ya kunywa mbona hanywi maji ya mtu, yupo radhi asinywe maji. Kwa hiyo, huyo hatapokea hiyo hela. Kwa hiyo, akawa anauhakika sipokei hela yoyote. Lakini tukapambana ile kesi na watu wachache kwa sababu wengi walirudi nyuma walihongwa tukabaki wachache. 

Sasa ninachotaka kusema lilipofika mkoani kumbe ni kesi ambayo ipo mpaka mkoani wanahusika katika kutoa hilo jengo, si unajua haikutoa hicho kiwanja na kumbe Rais ameshafanya nini, ameshaitia saini. [Hilo eneo] likabadilishwa kwamba sio kiwanja, kilikuwa cha Serikali ya mtaa, tulipewa na Shirika la Nyumba la Taifa [NHC] ndio waliokuwa wamepewa hivyo viwanja kwa hiyo tuliwaomba wakatupa kiwanja kimoja. Kumbe huyo wale viongozi wa mtaa wameshakiuza, yule mwarabu ameshakwenda kubadilisha kuwa cha kiwanda sasa mafuta si mambo ya viwanda? 

Tukaenda mpaka Dodoma. Kila mtu kwa pesa yake. Na mimi nikatoa pesa yangu na wengine tukafika. Waziri yule akasema hapa hii habari ya kiwanja haipo tena mikononi mwa waziri. Kiwanja hiki kipo mikononi mwa Rais kwa sababu Rais ndio anatia saini hivi viwanja kuwa vya uwekezaji. Sasa hapo kikaniuma nikajua kweli tushafeli sasa hapa wataniacha? Ilivyofika wilayani, mkuu wa wilaya jina sitamtaja lakini aihamishwa baadae na Rais baada ya hii kesi, kufika hapa ananiambia Ananilea nitakuhamisha wilaya. 

Yaani mimi nitahamishwa wilaya kwa sababu mimi ndio mpinzani mkuu peke yake, yaani mpinzani, sijui kama unaelewa, yaani ndio niko chama kikuu cha upinzani, nikasema jamani mimi sina chama na ninaomba na hii kadi ya CCM niiache hapa nilikuwa CCM lakini sina chama chochote naungana nacho sawa. Sasa baadae nikaona hii kesi ikiishia hapa itakuwaje? 

Uandishi ulivyo wa maana nimekesha siku hiyo akili inapiga nasema Mungu wangu, yaani kweli mimi niliweka tofali pale na wananchi wenzangu tuliweka matofali pale, kwa hiyo hili jengo letu la Serikali ya mtaa linachukuliwa kuwa kituo cha mafuta kweli? Nikafikiria kitu gani kitakuwa habari hapa na kama ipo, unajua Mkapa alikuwa anasoma magazeti ya kila siku. Nikaandika habari ya maelezo mafupi. 

Nikamwita rafiki yangu anaitwa Leah Simike nikamwambia Leah nakuomba piga picha, kwa sababu lile jengo letu tulikuwa tunaweka na bendera inapepea kila wakati, siku hizi hawaweki bendera za Jamuhuri kwenye Ofisi za Serikali ya mtaa sijajua kwa nini. Ilikuwa inapepea. Nikamwambia Leah nipigie picha kwenye hii bendera na hakikisha unapata hili jengo. 

Nikaandika habari ya maelezo mafupi inasema hivi, Muda si mrefu bendera hii ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayopepea katika jengo hili lililojengwa katika kiwanja fulani — unataja na namba, si ndio? — kama Ofisi ya Serikali ya mtaa huu itashushwa, itapandishwa bendera ya muuza mafuta, sikuandika jina maana yake ni defamation lazima uandike kwa akili. Hii itakuwa si aibu na fedhea kwa wananchi 10,000 wa mtaa wa Kimanga Darajani bali kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania nzima nikafunga habari imeisha. 

Nakwambia, si unajua Rais [Mkapa] alikuwa anasoma magazeti na maana yake nilihakikisha nimesambaza magazeti yote na vyombo vya habari niliwahusisha kwa sababu niliwaambia jamani kiwanja chetu kinaondoka Serikali yetu ya mtaa, Ofisi yetu ya Serikali ya mtaa imeshauzwa. Kwa hiyo, walitoa huo msaada wakachapisha. Nasema nguvu ya vyombo vya habari. Wanahabari tunadharau kazi yetu lakini nakwambieni ina nguvu sana kama utakuwa unania thabiti ya kupigania masuala ya Watanzania wote. 

Nakwambia kile kiwanja kilifutwa, umeelewa? Kilifutwa! Hati ilifutwa mpaka leo ile Serikali yetu ya mtaa iko pale, bendera yetu kama inapepea sasa hivi lakini hawaipandishi maana ndio ilileta huo mzaha? Maana yake mimi nilichokitumia pale ni bendera, maana yake nilifikiria ni jinsi gani hii itakuwa habari, niliwaza habari hapa ni nini jamani? Maana yake nilikuwa nimeandika makala kibao bado wameuza lakini nikajua hii bendera hii ndio habari. Yaani habari kubwa [ikawa] ni bendera ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kweli watu wanaosema kuhusu mabadiliko ni wachache. Mabadiliko sio lazima yaletwe na watu wengi. Lakini nataka kusema hata ukiwa peke yako ukileta mabadiliko kidogo na mwingine akaleta kidogo na mwingine akaleta kidogo na mwingine akaleta kidogo Jamuhuri inabadilika. Leo hii tunazungumza kwamba kuna hitaji la kubadilisha misingi yetu ya utawala kuweka misingi ya kikatiba inaweza kuwa kwamba LHRC imekuwa ikisimamia hili jambo toka mwanzoni wa miaka ya tisini, imesimamia masula ya Katiba na umuhimu wa Katiba Mpya ya wananchi, inaweza kuwa ikachukua mda mrefu lakini nakwambieni kwamba kama LHRC mtaendelea na huu utaratibu wa kujihusisha namna hii utashangaa mabadiliko yanaanza kuja hata kwa haraka kwa nguvu ya watu wachache si lazima wakawa watu wengi. 

Mabadiliko kuna wakati yanakuja kwa hoja tu. Sijui kama mmesikiliza hoja za Jenerali. Ni hoja ambazo watu wengi pengine walikuwa hawajazijua lakini ni hoja. Fikiria kwamba kuna mtu tumemuweka ni Rais anaweza kutoa uteuzi wa watu hawa wengi ambao hawajui na yeye pengine hata hajui kama hiyo ina madhara kwa maendeleo ya Watanzania. 

Lakini akifahamu kama vyombo vya habari tutatumia vyombo vyetu vya habari kuwafahamisha watu kumfahamisha na huyo Rais kuna siku anaweza kusema hapana Tanzania yangu na Watanzania waliowengi ni muhimu kuliko mimi pengine na chama changu kwa sababu jambo kubwa limekuwa tatizo kwetu sisi sasa hivi sio tu Watanzania ambao hawaelewi lakini pia tuna tatizo kubwa kwamba tatizo la vyama kwamba ni chama basi mtu anapenda vyama vyao kuliko nchi yao, wanathamini vyama vyao vya siasa kuliko taifa lao kinyume kabisa na [Rais wa kwanza wa Tanzania Julius] Nyerere.

Nyerere kabla hajafa alisema: “Chama hiki kinaitwa CCM si baba yangu, si mama yangu kama kinakuwa kinakiuka matakwa ya Watanzania, kile ambacho Watanzania wanakitaka, hicho chama siko nacho.” Nyerere aliwahi kusema sijui kama ninamsingizia lakini ndivyo nilivyomuelewa alivyozungumza. Kwa hiyo, ninachotaka kusema mabadiliko ya kuwa na Tanzania iliyobora zaidi pamoja na matatizo yote tuliyonayo sasa hivi kwamba Watanzania wengi wako radhi kutafuta mkate wao kwa sababu ya shida zao lakini wale ambao tumeamua kusimama tusimame mpaka mwisho wa maisha yetu hata kama tunaishi miaka 3000. 

Hiyo miaka yako 3000 hakikisha umesimamia masuala ya Tanzania kwa sababu kuna sababu gani ya kuogopa? Mradi usiongee kwa matusi. Usiongee lugha mbaya. Usitukane mtu. Ongea hoja. Toa hoja. Songa mbele. Huyo ambaye atakufanyia kibaya yuko pia Mungu wa mbinguni, yuko aliye juu kuliko yote ambaye anaijua Tanzania na Watanzania.

Tito Magoti: Wakati unatoa ile shuhuda yako mwanzoni nilitaka nikupe pole nikafikiri ulikwama kumbe ilikuwa ni mapema, hongera kwa uthubutu na kwa kutufundisha kwa vitendo kwamba tunaweza, tunaweza na inawezekana. Umezungumza suala la kujifunza kujielimisha kutafuta taarifa na kuzitumia. 

[Lakini] katika mazingira ambayo sasa hivi tumekuwa na ongezeko la sheria nyingi sana zinazobana upatikanaji wa taarifa. Jana [Novemba 8, 2021], nilikuwa nazungumza na waandishi wa habari mahali fulani, tunajadiliana kuhusiana na sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari. Kwenye mazingira kama haya ambayo tuna sheria nyingi sana zinafanya waandishi wajihariri na kujihariri na kujihariri kabla hata ya kuhaririwa na sheria na katika mazingira ambayo tuna Serikali ambayo mlengwa wake ni kuhodhi taarifa. 

Tumekuwa na Sheria ya Takwimu ambayo ilidhibiti ushirikishanaji wa takwimu kielektroniki hata kufanya takwimu rasmi na kadhalika na kadhalika. Tumekuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo imekuja kuzuia, imekuja pia kufanya jinai kupokea taarifa ambayo kwa maoni yao kwenu ninyi ni kero. Tumekuwa na Sheria ya Huduma za Habari na kanuni zake za maudhui ya mitandaoni ambazo zote zinakuja kuweka utando katika upashanaji wa habari na mimi naamini kwamba ni kupitia upashanaji wa habari tunaweza kujifunza.

Tunaondokaje kwenye mazingira haya ili kuelekea kujifunza kupata elimu stahiki kwa sababu hata elimu tunayoipata sasa hivi kupitia vyombo vya habari ni elimu ambayo imehaririwa na kuhaririwa na kuhaririwa. Mimi nimeacha, niwe mkweli, nimeacha kwenda kufanya vipindi vya TV vya kurekodi. Kwa nini? Kwa sababu kitahaririwa, kitahaririwa, kitahaririwa. Ukiwa na kipindi, tufanye mubashara, tuzungumze mubashara kwa sababu gani? Kwa sababu ninajua mazingira yao. Kuna vipindi vyangu vingine havirushwi. Vingine vinakatwa katwa. Nikasema hii sio sahihi. 

Sasa tunaondokaje hapa, na wewe ni mtaalamu wa masuala ya habari, mimi kutokana na mtazamo wa haki za binadamu, naamini kwamba hizi sheria zinakiuka haki za binadamu, zinakiuka Katiba [na] zinakiuka pia mikataba ya kimataifa ambayo tumejiwekea kama taifa na ninaamini kwamba tunatakiwa kuondoka hapa kwa sasa. Ushauri wako kama mkongwe, kama mwanahabari mkongwe, kama mwananchi, ni upi ili kuelekea kuilinda Katiba na kuitengeneza misingi katika Katiba ambayo itahakikisha kwamba tunajifunza kwa usahihi, tunapata elimu sahihi na tunapata maarifa yatakayo tusaidia kulisaidia taifa letu?

Dk Ananilea Nkya: Asante sana. Kama ulisikia kaka Jenerali alizungumza kwamba wakati Tanganyika ilipata uhuru, ile mifumo yote ambayo wakoloni waliokuwa wanatumia kuongoza nchi ndio utawala wa wazalendo wenzetu, Watanzania wenzetu, Watanganyika wenzetu waliichukua kama misingi yao ya kuongoza Watanzania wenzao. 

Siwezi kulaumu sana zama hizo, pengine kwa sababu wanasiasa, unajua ukiingia kwenye siasa, sijawahi kuwa mwanasiasa wa jukwaani, mimi ni mwanasiasa kama binadamu ambaye najua siasa ndio sehemu nzima ya maisha yangu. Lakini ninajiuliza hata mimi mwenyewe kwamba ni kwa nini ile mifumo na sheria ambazo walikuwa wanatumia wakoloni zama hizo tumezirithi. 

Na kwa kweli katika utafiti wangu wa masuala haya niliyofanyia [Shahada ya Uzamivu] PhD yangu niliangalia sheria ambazo walikuwa nazo wakoloni. [Kipindi cha] Wajerumani kulikuwa sheria moja ya vyombo vya habari, kwa mfano. Wakaja Waingereza zikawepo lakini sio nyingi zilikuwa kama tano, tatu, nne. Sasa wakati wa Nyerere zikawepo kiasi lakini leo zimeongezeka sheria za kudhibiti vyombo vya habari tunazokaribu ishirini na ishirini na zaidi. Tafsiri yake [ni kwamba] tunazidi kuwa na ukoloni mkali zaidi, sijui kama naeleweka nikisema hiyo sentensi?

Yaani kwamba kama tulikuwa na ukoloni wa kiasi fulani wakati wa Ujerumani, tukaingia wa Uingereza ukawa mkali zaidi, tulipokuja tukapata uhuru sheria zile si zinazidi kuongezeka kuwa nyingi zaidi kwa wakati zinazidi, maana yake yaani ukoloni unazidi kuwa mkali zaidi, sijui kama tunaelewana? Na [huo ukoloni] unakuwa mkali kwa kujua pengine na kutokujua kwa sababu nasema kwa kujua [au] kutokujua kwa sababu ninaamini kabisa, kabisa, kabisa kwamba wengi wa viongozi wetu wanaotuongoza wanaoingia kwenye dola ni Watanzania wa kawaida ambao wanakuwa wamepita kwenye mfumo wetu wa kawaida wa elimu ambao hauangalii kwamba hapo nyuma wakoloni walikuwa wanatuongozaje na sasa tunajiongoza vile vile au tunajiongoza tofauti zaidi.

Kwa sababu, wakoloni walikuwa wanatuongoza kwa maslahi yao waweze kuchukua mali, rasilimali zetu hapa wapeleke kwao, si ndio? Haya, kama viongozi wetu wenyewe wazalendo wenzetu, Watanzania wenzetu, wanatuongoza wanatumia sheria zilezile kama sheria zile zilikuwa ni kwa ajili ya kuwezesha wakoloni wachukue rasilimali je, na hizo sheria wanaziweka ili wao kama kikundi cha waongozi wachukue rasilimali zetu? Ni swali nauliza majibu siyajui, si ndio? 

Kama sio kwa lengo la kuwezesha hicho kikundi kidogo kinachoongoza dola kiweze kufanya vitu ambavyo ni vya kukinufaisha chenyewe ni kwa nini tuendelee na sheria alizotumia mkoloni Mwingereza, mkoloni Mjerumani ambazo hazina maslahi kwa Watanzania? Ni kwa nini Mtanzania ambaye tumesema nchi yake imepata uhuru unamwekea sheria ya kuzuia kusema hapa mtaani kwangu ilikuja shilingi kutoka halmashauri, ilitoka shilingi, labda milioni tano kutoka halmashauri ikafika hapa kwa ajili ya kufanyia hiki lakini hiyo hela haikufanya hicho ilifanya shughuli nyingine, mmeelewa? Sijui kama mnanielewa. 

Ninatoa huo huo mfano wangu mwenyewe kwamba mimi nilipaza sauti na wenzangu wachache pale mtaani kwetu kwamba kiwanja chetu cha wananchi kimechukuliwa na utawala wa mtaa, likawa zogo, nikawaambiwa mimi ni mpinzani wakati sina chama chochote mpaka leo cha siasa wala kilichopo wapi, wapi. Mimi ni Mtanzania [niko] na nchi yangu tu basi. Sasa kama hali ni hiyo, tuna hizo sheria ambazo zinazuia wananchi kujiongoza, kusimamia rasilimali zao, kuhoji rasilimali zao zimetumikaje, waandishi wa habari kuhoji kufuatilia na kuandika hivyo vitu akiandika utaambiwa kwa nini umechapisha habari inachafua Serikali? 

Tunataka Tanzania iende mbele na Watanzania wanufaike na nchi yao. Kama watawala hawataki hivyo,  je, tupo kwenye ukoloni au tupo kwenye uhuru? Ni masuala ambayo lazima tuweze kujiuliza, si ndio? Sijui kama tunaelewana mpaka hapo. Kwa hiyo, kuna suluhisho lake tufanyaje? Kwangu mimi suala la Katiba Mpya ya wananchi ni suala ambalo halihitaji mjadala mkubwa kwamba liwepo [au] lisiwepo. Ni suala tu la kujadili kama hivi kwamba umuhimu wake wananchi wa kawaida waelewe kwa sababu wananchi wengi hawajaelewa kwa sababu hatujawafikishia taarifa za kutosha waweze kufungamanisha maisha yao yalivyo sasa na suala la ukosefu wa Katiba Mpya. 

Kwa hiyo, kwangu mimi ukiniuliza kuna kazi kama hii LHRC inayofanya ya kuhakikisha kunakuwa na mijadala kila mahali. Kunakuwa na mijadala ambayo itawasaidia wananchi kuhusisha umuhimu wa Katiba Mpya na hali zao za sasa za maisha. Kwa mfano, namna Katiba inavyoweza kuweka mambo sawa sawa, kama vile kwamba hatuhitaji mtu wa kuteuliwa, tunahitaji mtu wa kumchagua ili tumuulize, si ndio? Tumuulize wewe ile mali yetu iliyokuja hapa imefanya nini? Ile pesa iliyotoka halmashauri kwa ajili ya kufanya kitu fulani, ile iko wapi? 

Yaani uongozi ambao wananchi watasema sisi kabla hatujaletewa hela yoyote tunataka tujadili kipaumbele chetu ni nini katika eneo letu la huu mtaa hapa, hivi kipaumbele chetu ni nini? Tunataka kwa mfano tuulize vile viwanja vyetu vyote vya wazi vilivyokuwa hapa ndani viko wapi? Mbona wamepewa watu hata watoto hawana pa kutokea? Leo hii watu wakiuliza katika hali kama hiyo yaani unaingia katika mtego mkubwa kwa sababu elimu haijatoka sana kuhusiana na Katiba. [Wanananchi] wengi hawawezi kuunganisha maisha yao na Katiba.

Tito Magoti: Asante sana kwa hitimisho zuri na kabla sijahama kwako niende kwa washiriki wengine, umezungumzia mwelekeo kwamba tunahitaji kujielemisha [ili kuweza] kung’amua mambo ya kimsingi ambayo yanafaa kupewa kipaumbele, kutengenezea taasisi chini ya Katiba, kuilinda na kuiheshimu Katiba yenyewe na kadhalika na kadhalika. 

Lakini kumekuwa na jitihada ambazo nasema ni za makusudi za kutengeneza mgawanyiko kwenye masuala yenye maslahi ya pamoja, kwa mfano, kuna upotoshaji unaoendelea kwamba Katiba Mpya ni ajenda ya vyama vya siasa. Hiyo moja. Lakini pili, kuna upotoshaji mwingine unaoendelea ambao naona ni upotoshaji wa makusudi kwamba inafaa kuendelea kwanza kama taifa tuwe na maendeleo ya kiuchumi kwanza ndio tuwe na Katiba. Mimi naona ni upotoshaji na sikubaliani nao. 

Na sauti za namna hii zinatoka wakati mwingine kwa viongozi. Kuna mtu mmoja amezungumza hivi karibuni, tena alikuwa huko kaskazini, ni waziri mmoja akawa anawatolea mfano wananchi akasema hawa wananchi hawahitaji Katiba [Mpya], ni wananchi fulani ambao kwa picha walikuwa wanaonekana wanaishi maisha duni, kwa hiyo akawa anatumia maisha yao yale kuonesha kwamba vipaumbele vyao ni tofauti na vipaumbele vya watu wengine.

Wewe umetuambia hapa kwamba kwenda mbele [kama nchi] tunahitaji kujitawala vizuri [na] kuwa na mifumo na kadhalika. Sasa huu upotoshaji ambao wakati mwingine tunausikia kutoka kwa viongozi unaathiri kiasi gani uelewa wa wananchi wa kawaida [juu ya umuhimu wa hivi vitu unasema]? Kwa sababu wakati huo kiongozi amezungumza kuwa hivi wewe unaenda pale na taasisi yako ya kuelimisha watu kuhusu mazingira, utasikilizwa kweli kwa aina ya wananchi tulionao? 

Na je, tufanye nini ili kuondokana na huu mgawanyiko unaotengenezwa na ni mgawanyiko ambao naona ni wa makusudi wa kuwapotosha wananchi wasione njia na kama wananchi hawataona njia kwa wakati, unafikiri nini kifanyike ili kuelekea lengo hili unalolihubiri? Karibu.

Dk Ananilea Nkya: Jambo la kwanza kabisa naamini katika vyombo vya habari na wanahabari wenzangu hata kama ni mmoja mmoja, wale wanaoamini kwamba wameingia kwenye tasnia kuchochea mabadiliko kwenye jamii zao husika. Mimi naamini sana katika vyombo vya habari kuwa vina nguvu na ninaamini zaidi katika mwanahabari mmoja mmoja ama ameingia kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuleta mabadiliko fulani ya wananchi na kama ameingia kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kusaidia Tanzania itoke hapa ilipo kwenda pazuri zaidi. 

Nilikuwa nadhani kwamba ni muhimu sana, sana, sana wanahabari wenyewe wakawa wanaelewa hili suala zima la Katiba, mahusiano [kati] ya Katiba na uongozi bora. Kwa mfano, ni muhimu wananchi wakaelewa kwamba uongozi bora wenyewe ni rasilimali na uongozi bora hauwezi kupatikana kama hamna Katiba ambapo sauti ya wananchi ndio inasikika [na] ndio inakuwa ya mwisho. 

Yaani wananchi wakiamua tunamchagua fulani na iwe hivyo kwamba ni huyu aliyechaguliwa na sio vinginevyo. Kwamba ameshachaguliwa lakini kutakuwa na uvurugaji na vitu kama hivyo. Kwamba kama uongozi katika ngazi zote kuanzia ngazi ya mtaa mpaka kule juu kwenye taifa kama hakuna uongozi bora, kama hakuna mtu ambaye ameonekana na wananchi kwamba kweli anasifa za uongozi, nadhani itakuwa ngumu kama nchi kupiga hatua. 

Kwa hiyo, la kwanza naiona nafasi hiyo ya kuweza kuleta mabadiliko. Embu tusaidie vyombo vyetu vya habari viweze kuwa na maudhui na viweze kuwasilisha maudhui katika namna ambayo itasaidia wananchi kuelewa mambo yanayowahusu. Na ninafikiri pia wanahabari na vyombo vya habari tumekuwa na woga ambao si wa lazima. Kuna ule woga kwamba Rais akishazungumza jambo basi waandishi wanaona hawawezi tena kuandika kuhusu hilo jambo. Kuna wakati nafikiria kuwa vyombo vya habari havikumuelewa Rais Samia [Suluhu Hassan pale] aliposema kwamba hebu suala la Katiba lisubiri kwanza.

Yaani kwake yeye sio kipaumbele lakini hakusema sio kipaumbele cha wananchi. Hii haimaanishi kwamba vyombo vya habari viache kuelimisha wananchi uhusiano kati ya Katiba nzuri na maendeleo yao [na] maendeleo ya nchi yao, si ndio? Kwa mfano, hata kama hukutaja kabisa Katiba, mwandishi wa habari unafanya kazi sijui redio gani hapa Arusha, ukiandika habari yako hata bila kutaja Katiba, ukafuatilia kwenye ngazi ya kijiji tu habari yako uliza wananchi mwaka huu kumefanyika mikutano mingapi ya Serikali ya mtaa hapa? Watakwambia. 

Umekwenda kuuliza ni masula gani waliyojadili watakueleza ni suala gani lilikuwa likienda vipi? Ninavyoamini mimi, hakuna kijiji chochote ambacho angalau kina changamoto fulani ambayo inahitaji shughuli za uongozi yaani kwamba uwajibikaji wa viongozi halafu kukawa hakuna habari. Hiyo ni habari kubwa sana. Lakini sisi wanahabari tunaandika hizo habari? Na je, tunajua kuandika habari? 

Maana yake mimi katika [kufanya Shahada ya Uzamivu] PhD yangu kitu kimoja nilikigundua kabisa katika utafiti wangu ni kwamba hatuandiki habari za wananchi. Tunaandika habari za viongozi. Kwa hiyo, kama Tanzania kuna matatizo, sisi wanahabari ndio tumechangia namba moja kuifikisha Tanzania hapa tulipo. Ndio tumeifikisha Tanzania hapa tulipo. Kwa mfano, habari ambazo nilizifanyia utafiti zaidi ya 10,300, kipengele cha kwanza niliangalia tu kwamba nukuu, habari imetoka wamenukuliwa watu gani? Ni wangapi? Je, ni wanawake [au] ni wanaume? 

Utakuta habari imemnukuu mtu huyu mmoja, kwa mfano, mkuu wa wilaya kasema hivi kasema hivi na hivi na hivi. Hata kama ni jambo la hovyo kabisa ambalo tena liko nje ya kikatiba na ambalo hata katika hali ya kawaida ni uongo, mwandishi anaripoti hivyo hivyo na anapata nafasi kwenye gazeti na inapata nafasi redioni. Kwa hiyo, kuna nakisi kubwa, kubwa katika kuipeleka Tanzania kwingine. Tunanakisi kubwa sana kwenye uandishi wa habari na ninadhani waandishi wengi wa habari pia wameondoka kwenye taaluma kutokana na hivyo vitisho vya sheria na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo, waliobaki wanakazi kubwa. Sisemi kwamba hawafanyi kazi nzuri. Lakini nasema kama ni kazi ya kuleta mabadiliko ya kweli Tanzania, waandishi wa habari inabidi tuanze sasa na ninawaomba kwenye suala la Katiba, LHRC embu jaribuni kuhusisha waandishi kwa namna mbalimbali. Jaribuni kuwapa elimu ya jinsi ya kutumia mbinu kuandaa habari zinazohusiana na masuala ya Katiba na utawala bora kwa namna ambayo sio hii ya kwamba tunataka Katiba

Hapana, ni muhimu waandishi wenyewe waweze kuona mahusiano kati ya Katiba [Mpya] na maisha yao pale mtaani yalivyo na jinsi wenyewe ambapo wamekaa hawafanyi wajibu wao, si ndio? Kwa sababu Watanzania ili waweze kwenda mbele na Tanzania iende mbele ni lazima katika ngazi ya chini wananchi wa kawaida kabisa waweze kujisimamia na kusimamia viongozi wao. 

[Wananchi] wakishajielewa hivyo na vyombo vya habari vitafanya kazi yake kwa sababu kama waandishi wa habari tutaamua kwenda katika maeneo mbalimbali hata kama sio vijijini huwezi kufika hapa Arusha unaweza ukafika mitaa mbalimbali na ukatimiza wajibu wako. Kuna viwanja vingapi hapa Arusha, kwa mfano, vya michezo ambavyo vimeuzwa na viongozi wenyewe sijui, kama tuko pamoja, si vipo vingi? 

Inahitaji moyo kama umeingia kwenye uandishi wa habari kwa sababu ili uandike habari zenye kuchochea mabadiliko inahitaji kujitoa wewe binafsi, sio usubiri kwamba sijui utapewa gari [na ofisi yako]. Hizo ni shughuli za kuleta mabadiliko katika nchi yako inakuhitaji wewe zaidi ya chochote. Na kuna hatari ya kuhongwa pia. Mimi niliwahi kutaka kuhongwa na mwarabu mamilioni ya shilingi ambayo nadhani ingeniua. Ningekuwa nimekufa.

Unajua kuna watu wengi wamekufa, si ndio jamani? Lakini wanatembea kabisa. Yaani unakufa lakini unatembea kwa sababu unapokuwa wewe unaweza, unastahili, unawajibu wa kufanya jambo fulani lakini hulifanyi kwa sababu kuna wakati ulichukua rushwa wewe unakuwa sawa na umekufa tu. Leo unathubutu kuzungumza mahali useme kile na kile, tutasema wewe si ulichukua shilingi milioni kadhaa wewe si ulifanya hivi? Wewe si ulifanya hivi? 

Kama katika maisha yangu yote ya harakati niliwahi kuchukua hata senti tano ya mtu hata kunywa soda, wangenichukua hata mimi mfano waseme huwezi kuongea popote. Lakini leo nazungumza popote kwa sababu najua katika kazi zangu nimezifanya kwa uadilifu wa kiwango ambacho Mungu amenijalia. Na ninadhani nitafanya hivyo kwa sababu ndio wajibu wangu kwa sababu kama ni ugali wangu mbona nikiuza maandazi napata? Ugali wa kawaida, sio? Lakini sidhani kama tumeumbiwa kutafuta ugali wetu tu wa siku, tuna kazi kubwa ya kufanya hapa duniani zaidi ya kutafuta ugali wa siku.

One Response

  1. Elimu na historia kama hii ingekuwa inatumika vizuri ingeleta mabadiliko chanya ambayo sio tu kuamsha uwajibikaji bali pia maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts