Unamiliki Gari? Angalia Exhaust Yake, Unawezakuwa Umeshaibiwa

Ni wizi wa masega, au catalytic converter, yanayopatikana kwenye mfumo wa bomba la kutolea moshi (exhaust) katika gari unaodaiwa kushika kasi nchini Tanzania.
Lukelo Francis12 November 20215 min

Dar es Salaam. Je, wewe ni mmiliki wa gari dogo na huna uelewa wa kiufundi utakao kuwezesha kutambua mabadiliko yanayoweza kutokea katika gari yako pindi uhalifu wowote utakapotendeka kwenye gari hilo?

Kama jibu lako ni diyo basi kuna uwezekano mkubwa sana kwamba umeshakumbwa au upo kwenye hatari ya kukumbwa na uhalifu wa wizi wa masega, au catalytic converter kama yanavyojulikana kwa kimombo, yanayopatikana kwenye mfumo wa bomba la kutolea moshi (exhaust) katika gari yako, pasipo wewe mwenyewe kufahamu. 

Kwa mujibu wa uchunguzi wa The Chanzo, uhalifu huu unafanywa na mafundi wa magari ambao sio waaminifu pale wanapopewa kazi ya kutengeneza gari husika.

Mafundi hao hutoa masega hayo na kwenda kuyauza kwa wanunuzi wake katika mazingira ya usiri mkubwa sana, wanunuzi ambao The Chanzo imeshindwa kubaini ni nani haswa.

Unajuaje kama umeibiwa?

Katika mfumo wa ufanyaji kazi wa gari, mafuta yanapoungua kwenye injini pamoja na nguvu ya kuendesha gari kuna gesi ambayo si salama kwa mazingira, hivyo masega hayo yamewekwa ili kusafisha gesi inayotoka nje ya exhaust kuwa na kiwango ambacho hakitaleta madhara kwenye mazingira.

Na endapo masega hayo yakitolewa gari hutumia kiwango kikubwa cha mafuta lakini pia hukutana na changamoto ya kuishiwa nguvu, mlio wa tofauti, hizi ni baadhi tu ya dalili ambazo zinaweza kukuamsha kwamba huenda gari lako linaweza kuwa limeshakuwa muhanga mwengine wa uhalifu huo.

“Kwa sisi mafundi, yaani gari likija kwetu endapo [mwenye gari] amekuja na gari, huwa tunafungua kwenye exhaust,” mmoja kati ya mafundi ambaye anashiriki kwenye uhalifu huo na ambaye jina lake tumelihifadhi ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye eneo lake la kazi hivi karibuni. “Sisi tunakwenda, tunapasua exhaust ndio unakuta kuna unga mle. Tukishapasua [ile exhaust tunakuta] ule unga [halafu] tunauchukua.”

Nini kinachochea uhalifu huu?

The Chanzo ilibaini kwamba kinachowasukuma mafundi wengi kujihusisha na uhalifu huu ni kiwango kikubwa cha pesa wanachokipata baada ya kuuza masega hayo kwa wanunuzi wao.

Bei za ‘bidhaa’ hii hutofautiana kulingana na aina ya gari ambayo masega hayo yametolewa, huku masega kutoka katika magari kama Toyota Crown, Toyota Mark X, na Vogue yakitajwa kuwa na bei nzuri katika soko hilo haramu.

Kwa muujibu wa wauzaji wa vifaa vya magari, biashara hii haramu inachochewa na vitu viwili vikubwa: pesa nzuri inayopatikana kutokana na biashara hiyo na ugumu uliopo katika kukilinda hicho kinachoibiwa kwenye magari, yaani masega.

“Inaonekana biashara ni nzuri,” anasema muuzaji wa vifaa vya magari kutoka Ilala, Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdulrahman. “Ni biashara yenye pesa nyingi. Kwa hiyo, ukipata huo unga, labda ukiiba gari tatu, inaonekana unapata hela nzuri ndio maana ni kitu ambacho hakilindiki.”

Wizi wa masega si kitu kinachofanyika nchini Tanzania pekee, kwani kumekuwa na taarifa kadhaa kutoka nchi mbali mbali zinazohusiana na aina hiyo ya uhalifu.

Madini yaliyopo kwenye masega

Wataalamu wanabainisha kwamba ndani ya masega hayo kuna madini yenye thamani na ambayo huweza ndio lengo haswa la kufanyika kwa uhalifu huo.

“Ndani ya ule mfinyanzi kumechanganywa pia madini ya Platinum, Pladium na Rhodium,” Dk Edgar Mapunda, mtaalamu wa masuala ya kemia kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum.

Dk Mapunda anafafanua: “Sasa kwa vile [hayo madini] hayapatikani kirahisi ndio maana bei zake zipo juu. Nafikiri hawa ambao wanakusanya ule unga wanakwenda na kuchenjua hizo Paladium, Platinum pamoja na Rhodium halafu wanaziuza kama madini.”

Hiyo inaweza ikawa sababu moja inayochochea biashara hii haramu lakini pia zipo taarifa kwamba masega hayo huenda yakawa yanatumika kama madawa ya kulevya.

Madai ya madawa ya kulevya

Kwa mfano, chombo cha habari cha Reuters kimewahi kuripoti kwamba nchini Jamhuri ya Kidemokraia ya Kongo (DRC), masega hayo yanatumika kama moja ya madawa ya kulevya nchini humo.

Hapa nchini Tanzania, kwa mfano, mnamo Mei 2021, Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya (DCEA) Gerald Kusaya alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba mamlaka hiyo inachunguza uhusiano unaodaiwa kuwepo kati ya masega na matumizi ya madawa ya kulevya.

Kwa mujibu wa Dk Mapunda: “[Watumiaji wa madawa ya kulevya] wanachukua hayo masega, wanasaga, wanachanganya na vidonge vingine vya hospitali, vile vya usingizi, halafu mtu anakunywa. Anasema akinywa analewa haraka.”

Ni uhalifu ambao upo kweli

Wizi huu wa masega siyo wa kinadharia na tayari kuna watu ambao wameshawahi kuwa waathirika wa uharima huo. Dk Mapunda mwenyewe, kwa mfano, anasema magari yake mawili yameshaibiwa masega yao.

Juma Abdallah, mkazi wa Dar es Salaam, aliiambia The Chanzo wakati wa kuhoji watu mbali mbali ambao wanaweza kuwa wamekutana na kadhia hiyo kwamba rafiki yake alishawahi kukutwa na mkasa huo.

“Mimi imeshawahi kutokea kwa rafiki yangu, lakini tulirudi mpaka kwa mafundi, ambao baada ya kuwabana walikataa tukaenda polisi ikabidi wanunue muffler nzima,” anasema Abdallah.

Polisi hawana taarifa, waahidi uchunguzi

Ilipotafutwa ili isema kama inafahamu kwamba kuna aina hii ya uhalifu unaotokea jijini Dar es Salaam, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilieleza The Chanzo kwamba haifahamu.

Hata hivyo, afisa wa polisi kutoka kanda hiyo anayehusika na masuala ya habari Inspekta William Muliriye aliwaahidi waandishi wa habari hii kwamba Jeshi la Polisi lingefanyia kazi uchunguzi wa The Chanzo na kuutaarifu umma pale uchunguzi wao utakapokamilika.

“Ushauri wangu kwa watu wenye magari ni kwanza kuwa waangalifu, yaani kuweka, kama wanaweza kuweka, alama kwenye magari yao,” anashauri Abdulrahman, muuza vifaa vya magari kutoka Ilala, Dar es Salaam.

“Pale mtu anapoagiza gari yake mpya na pale anapoenda kuanza labda kumpelekea fundi kwa maana ya kuifanyia huduma kwa mara ya kwanza yaani ile ndio hatua nzuri ya kuangalia,” anasisitiza.

Lukelo Francis na Shafii Hamis ni waandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kuwapata kupitia anuani zao za barua pepe ambazo ni lukelo@thechanzo.com na shafii@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Lukelo Francis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved