The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

NEMC Kufanyia Kazi Madai ya Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Kiwanda cha Wachina

Ni kiwanda cha Guoyang Biotech Company Limited kilichopo kata ya Msongola, Dar es Salaam, kinachojishughulisha na uzalishaji wa dizeli kwa ajili ya matumizi ya viwandani.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) Samuel Mafwenga amesema kwamba ofisi yake itachunguza madai yaliyoibuliwa na wananchi wa kijiji cha Kiboga, kata ya Msongola, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam kuhusiana na kiwanda cha Guoyang Biotech Company Limited wanachodai shughuli zake zinaharibu mazingira na kuathiri afya zao pia.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wenye asili ya Kichina kilichopo kwenye kijiji cha Kiboga kinazalisha dizeli kwa ajili ya matumizi ya viwandani. Wakiongea na The Chanzo iliyofika kijijini hapo mnamo Novemba 8, 2021, kufuatilia kadhia hiyo, wananchi wa kijiji hicho walilamika kwamba kiwanda hicho kinatoa moshi mkali na harufu kali, vitu vinavyowafanya kukohoa sana, kutokwa na damu puani, kuzimia, na kutapika pia. 

Hata hivyo, mmoja kati ya watu wanaohusika na usimamizi wa kiwanda hicho Liu Xi Shung amesema moshi na harufu inayotoka kwenye kiwanda hicho ni ya kawaida, akitolea mfano kitendo cha wafanyakazi wake kutokuvaa barakoa kama ushahidi wa anachokisema. Shung anasema kwamba kuna siku moja tu kulitokea kasoro kwenye kiwanda hicho na kuzalisha moshi mwingi lakini hali hiyo haijajirudia tena.

Akizungumza na The Chanzo kuhusiana na malalamiko ya wanakijiji wa Kiboga, Mafwenga alisema: “Mimi sina taarifa za malalamiko ya wanakijiji hao. Lakini kama taarifa hizo zimeshafikishwa hapa [NEMC], basi tutazifanyia kazi, tutazifuatilia.”

Juhudi za wananchi zagonga mwamba

Kwa mujibu wa maelezo ya wanakijiji wa Kiboga, kadhia hiyo inayoambatana na kitendo cha utupaji taka holela unaofanywa na kiwanda hicho umeendelea kwa siku nyingi. Licha ya kuchukua jitihada kadhaa za kuhakikisha kadhia hiyo inakomeshwa, ikiwemo kuzilalamikia mamlaka za Serikali ya wilaya na mkoa, bado wananchi hao wameendelea kukumbwa na usumbufu unaotokana na uwepo wa kiwanda hicho.

“Mimi nalia na watu wa NEMC kwa sababu wao ndiyo wanaohusika na kutoa leseni kwa hivi viwanda,” anasema Devic Maico, mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kiboga. “Inakuwaje wanaweza kutoa leseni kwa kiwanda kama hiki halafu hakuna ufuatiliaji wa kujua nini kinafanyika hapa?”

Kwa mujibu wa wanakijiji wa hapa, madhara ya kiafya yatokanayo na shughuli zinazofanywa na kiwanda hiki ni makubwa sana, kwao wao na kwa watoto wao. Rehema Mringo ni mama wa watoto wawili aliyehamia kijijini hapa siku za hivi karibuni. Anasema tangu ahamie hapo, mtoto wake mmoja mwenye umri wa miezi nane amekuwa akipata hali ambayo haijawahi kumtokea kabla ya kuhamia hapo. 

“Mtoto wangu ameshikwa na mafua tangu siku ya kwanza nihamie hapa,” anasema Mringo. “Ningekuja naye hata hapa [kwenye mahojiano] lakini kwa bahati mbaya amelala kwa sasa. Ana mafua na kifua kisichokuwa cha kawaida. Nimeshampeleka kituo cha afya takriban mara tatu kutokana na hali hiyo.”

Saleh Abdulkarim ni  mfanyabiashara ambaye duka lake lipo mita chache tu kutoka kwenye kiwanda hicho. Akieleza namna anavyoathiriwa na uwepo wa kiwanda hicho hapo kijijini, Abdulkarim anasema: “Kuna wakati harufu inayotoka humo [kwenye kiwanda] inakuwa kali sana kiasi ya kwamba muda mwengine napata kizunguzungu. Hii imeshawahi kunitokea siyo mara moja wala mara mbili.” 

Mitandao ya kijamii yatumika

Juhudi za wanakijiji hawa za kupaza sauti zao ili tatizo hili liweze kushughulikiwa hazijaishia kwenye ofisi za umma tu. Hatua pia zimechukuliwa kupigia kelele kadhia hii kwenye mitandao ya kijamii, hususan mtandao wa Twitter, ambako video na picha zinazoonesha kiwanda hicho kikitoa moshi pamoja na wananchi wakielezea namna hali hiyo inavyoathiri afya zao. Unaweza kuangali video na picha hizo hapa, hapa, na hapa.

Benedict Mpanduji, kijana anaendesha kampeni hiyo mitandaoni dhidi ya kiwanda hicho, ameieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalum kwamba aliamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu anaamini mitandao ya kijamii ikitumika vizuri inaweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.

Ni baada ya Mpanduji kuandika Twitter ndipo The Chanzo ilipoamua kuifuatilia habari hii. Pia, kampeni hiyo pia ilimfikia Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliomba apewe anuani ya kiwanda kilipo na kuahidi kufuatilia.

“Kwanza naiiamini nguvu ya mitandao,” anasema Mpanduji. “Sasa hivi hilo halipingiki kwa sababu mpaka hao wakubwa zetu sasa hivi wanaiogopa. Kwa hiyo, nguvu ya mitandao ni kubwa kwa hilo nina imani kwamba kile nilichokifanya na ndio matokeo yake ndio haya yanaonekana sasa.”

Akieleza hatua zinazochukuliwa na kiwanda chake kuhakikisha kwamba uwepo wake hauathiri afya za wanakijiji, Shung anasema: “[Wafanyakazi] wakifanya vizuri moshi hautoki, wakifanya vibaya moshi unatoka kidogo. Mimi nawafundisha kila siku wafanye vizuri na kwa siku makosa yanaweza fanyika mara tatu mpaka mara tano.  Mimi napeleka nje oili chafu sio mafuta wala haina shida. Mimi siwezi kutupa mafuta.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni lukelo@thechanzo.com. Kama una swali lolote kuhusiana na habari hii, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts