The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Baba wa Rubani Aliyepotea Anasema Kijana Wake Bado Yuko Hai, Atapatikana

Familia ya rubani huyo inasema uamuzi wa kusitisha juhudu za utafutaji wa kijana wao si uamuzi sahihi.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Balina Bernard Gibuyi, baba mzazi wa rubani Samweli Balina Gibuyi ambaye amepotea na kutoonekana mpaka sasa, amesema kwamba anaamini kijana wake huyo bado yuko hai na atapatikana, akiziomba mamlaka za Serikali pamoja na waajiri wa Samweli kuongeza nguvu kwenye juhudi za kumtafuta.

Mzee huyo aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika nyumbani kwake Buswelu, wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, mnamo Novemba 22, 2021, ikiwa ni takribani siku nne tangu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) itangaze kusitisha zoezi la utafutaji na uokoaji wa rubani huyo mpaka pale taarifa sahihi zitakazo saidia kupatikana kwake zitakapowasilishwa kwa mamlaka hiyo.

Samweli Balina Gibuyu alikuwa rubani wa ndege aina ya BatHawk (5H-WXO) inayomilikiwa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya uhifadhi wa maliasili la PAMS Foundation. Alipotea tangu Octoba 18, 2021, huku juhudi za kumtafuta mpaka sasa zikigoma kuzaa matunda.

“[Atapatikana, yupo tu,” anasema Balina Bernard Gibuyi, baba wa rubani aliyepotea. “Yupo. Inawezekana anakula matunda na miti [huko aliko]. Unanielewa [mwandishi wa habari]? [Mwanangu] yuko hai. Yuko hai. Sasa ni namna gani ya kumsaidia hapo ndo kuna shida.”

Familia ya rubani huyo inasema uamuzi wa kusitisha juhudu za utafutaji wa kijana wao si uamuzi sahihi.

Kwa mujibu wa TCAA, utafutaji wa rubani huyo unakoma na sasa mamlaka zitaanza kuchunguza tukio hilo kama ajali. Lakini baba mzazi wa rubani huyo anasema kwamba uchunguzi wa ajali ulipaswa kufanywa tangu tukio hilo limetokea na ulipaswa uende sambamba na jitihada za kumtafuta kijana wake.

“Mimi naiamini Serikali kwamba inafanya kazi,” anasema baba huyo. “Na hii kusitishwa [kwa juhudi za utafutaji] ambako kumesemwa, mimi sijakubaliana na hatua hiyo sana. Mimi naamini kwamba wangesogeza muda wa kuendeleza kutafuta.”

Balina Bernard Gibuyi anaamini kwamba uchunguzi wa kina juu ya kupotea kwa kijana wake unahitajika kwani kuna taarifa kadhaa kinzani kuhusiana na tukio hilo ambazo yeye zinampa wasiwasi kwamba kunaweza kukawa na nia ovu imetendeka mahala fulani.

Jambo moja ambalo linamtia wasiwasi sana baba huyu ni lile linalohusiana na kifaa kinachujulikana kama Spidertrack kinachotumika kufuatilia ndege inapokuwa angani. Ugumu wa kumtafuta rubani huyo unatokana, pamoja na mambo mengine, na kutokuwepo kwa kifaa hicho muhimu kwenye ndege aliyoirusha siku hiyo. 

        Kifaa cha Spidertrack kilichokuwa kinatumika katika ndege hiyo

Kwa mujibu wa maelezo ya baba wa rubani huyo, mara ya kwanza watu walipokwenda kutafuta kifaa hicho kwenye hema la kijana wake, kifaa hicho hakikuwepo. Lakini wao familia walipoenda kufanya upekuzi kwa mara nyengine walikikuta kifaa hicho kikiwa juu ya meza, wakijiuliza ni nani ambaye atakuwa amekiweka hapo.

“Hapo ndipo hoja ikaibuka kwamba hiki kifaa, lazima kitakuwa kilikuwa kwa mtu mwengine,” anasema baba huyo. “Na kwamba, pale [kwenye hema] kitakuwa kililetwa lini sasa kwa sababu wale waliopita [kufanya upekuzi mara ya kwanza] hawakukiona? 

Ni katika mazingira haya ambapo Samson Balina Gibuyi, mdogo wake na rubani aliyepotea, anaamini kwamba kuna hujuma imefanyika kwenye sakata zima la kupotea kwa kaka yake. 

“Mimi kwa mtazamo wa haraka haraka tu na bila ya kupepesa macho, naona kama vile kuna hujuma pale [kwenye kupotea kwa kaka yangu] imefanyika,” anasema Samson kwenye mahojiano maalum na The Chanzo. “Kwa sababu ukiangalia, watu walioenda kwanza kufanya upekuzi hawakukiona hicho kifaa, sisi tukaenda tukakifikia tu mezani, peupe kinaonekana kabisa. Wito wangu ni kwamba hili suala lifanyiwe uchunguzi wa kina. Nahisi kuna namna.”

Jofrey Cosmas ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni cosmasjofrey54@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts