The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vitali Maembe: Sijawahi Kuogopa Kusema Ukweli

Msanii huyo anasema kwamba hana mawazo ya kukimbilia uhamishoni kuepukana na usumbufu anaoupata kutoka kwa vyombo vya dola vya Tanzania ambavyo anadai vimemfanyia kila aina ya masaibu yanayolenga kumfanya aache aina ya mziki anaoufanya.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Vitali Maembe ni moja kati ya wasanii wachache sana nchini Tanzania ambao unaweza kusema muziki wao unaakisi moja kwa moja kile wanachokifanya kwenye jamii zao husika kama wanachama wa jamii hizo. Ni msanii anayeonekana kukerwa na aina zote za dhuluma lakini sana sana dhuluma zinazofanywa na wale waliopewa dhamana ya uongozi wa nchi kwa wananchi wa nchi hiyo. 

Hili linaonekana wazi wazi kwenye nyimbo na kazi nyingine za sanaa za msanii huyo kama vile uchoraji. Nyimbo yake ya hivi karibuni kabisa Kaizari, kwa mfano, ilimuingiza Vitali Maembe matatizoni na mamlaka za nchi baada ya polisi kufika nyumbani kwake, kuendesha msako, kumkamata “kama jambazi” kwa maneno yake mwenyewe na hata kumuweka ndani kwa muda kwa kile walichodai kwamba wimbo huo unawachonganisha wananchi na Serikali yao. Wimbo huo unahusu masaibu ya kimaisha ambayo Mtanzania wa kawaida anakabiliana nayo bila kupata msaada kutoka kwa Serikali.

Hii bila ya shaka haikuwa mara ya kwanza kwa msanii huyo kujikuta matatizoni na vyombo vya dola kutokana na kazi zake za kimziki na wala hadhani kwamba itakuwa ni mara ya mwisho. Lakini katika mahojiano haya maalum aliyofanya na The Chanzo hivi karibuni, Vitali Maembe anasema kwamba kamwe hawezi kuacha kuzungumza ukweli pale atakopohisi hitaji la kufanya hivyo. Anadai hakuna kitu ambacho Serikali haijafanya dhidi yake mpaka sasa labda kumuua tu na wala hali hiyo haimshawishi kukimbilia uhamishoni.  

Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Bagamoyo, mnamo Novemba 20, 2021. Endelea … 

The Chanzo: Karibu sana The Chanzo.

Vitali Maembe: Asante sana, nashukuru pia kwa kufika kwenu kwa sababu sio bahati tu, ni baraka pia. Kwa hiyo, karibuni sana.

The Chanzo: Tunashukuru sana. Labda kwa kuanza, kuna vitu vingi sana vinaambatanishwa kwenye majina ya watu. Wengine wanapenda kuitwa waheshimiwa, wengine masheikh, wengine wachungaji, wengine ndugu, wengine comrade [kamaradi]. Wewe unapenda kiambatanisho gani kwenye jina lako? 

Vitali Maembe: Mimi unaweza kuniita vyovyote kwa jinsi unavyojisikia, isipokuwa usinitukane au kuniita kwako kusimdhalilishe mwingine. Kwa hiyo, mimi ukiniita ndugu nitafurahi zaidi. Sitafurahi ukiniita muheshimiwa kwa sababu wote tunatakiwa kuheshimiwa. 

Lakini mimi sasa ni mkubwa, ni mtu mzima na familia nyingi. Kuna familia za karibu na familia za mbali. Kwa hiyo, wale watakao jisikia kuniita mjomba, baba, babu, kaka, wawe huru tu hawatakuwa wamekosea. Hawajanitukana wajisikie huru tu kuniita vyovyote. Au kama ni kwenye kuandika aniite tu ndugu au comrade.

The Chanzo: Mimi nitakuwa nakuita comrade maana mimi pia ni comrade.

Vitali Maembe: Nashukuru sana [kicheko]

The Chanzo: Wakati unapiga hiki kifaa [gitaa], nikawa nawaza hiki kifaa kwako kina maana zaidi ya kuwa gitaa, au sivyo?

Vitali Maembe: Ndivyo, kwangu mimi ni rafiki zaidi kwa sababu wakati mwingine, napenda sana kuwa karibu na watu wengi  ila  ninapo kuwa peke yangu nakuwa na gitaa hili. Kwa sababu ninapo kuwa nalipiga kuna vitu huwa tunashiriki katika hali ya kawaida huwezi ukavijua lakini najiamini zaidi ninapo shika gitaa. 

Hata ninavyo ongea na wewe kama nisingelikumbatia hivi, kuna wasiwasi fulani ungeuona, mchecheto fulani, lakini kwa sababu nipo na gita hapa, nahisi nina company fulani. Kwa hiyo, ndio hivyo. Lakini pia katika utunzi wangu zaidi, gitaa huwa linanisaidia katika kutunga, unaona, hata kulinda sauti yangu sababu gitaa lenyewe lipo kwenye mpangilio fulani linasaidia kutengeneza sauti yangu.

The Chanzo: Moja kati ya vitu vingi sana ambavyo mimi nimevigundua nikiwa natazama nyimbo zako, lakini pia nikikutazama uki-perform live, unavyotumia hiki kifaa chako [gitaa] huwa unatabasamu, na wakati mwingine ukitabasamu huku umefumba macho kabisa. Ni kwa sababu gani?

Vitali Maembe: Najaribu kuzama kwenye yale ambayo nayaimba, kwa hiyo wakati mwingine huwa nafumba macho, yaani najaribu kuzama kwa yale ninayoyaimba. Lakini ninavyo fumbua macho kama wewe ni mtazamaji mbele utaona nimekutazama, mara nyingi watu wengi ninavyo tumbuiza hata kama mimi sijakusudia kumtazama lakini nahakikisha kwamba ajihisi kama kuna wakati tumekutana naye macho kwa macho, naye ajihisi yupo. 

Pia, inanisaidia mimi kuwepo katika lile eneo kwa sababu napata mawasiliano na yule mtu aliyekuwa mbele yangu. Lakini kutabasamu ni maneno ninayoimba. Wakati mwingine naimba maneno yanaweza kuwa makali sana, yanakemea sana kwa hiyo tabasamu ni kwa ajili ya kupooza tu, kwa sababu mtu asifanye kuona naimba sababu namchukia, hapana. 

Wengine nikiwa naimba wananionea huruma, wanaona  aah, huyu jamaa akitoka hapa ataweza kufanya hivi. Kwa hiyo, nikiwa natabasamu nawaondoa mashaka kwamba mi naimba kitu cha kawaida, maisha yetu haya ya kawaida. 

The Chanzo: Na kwa sababu ya maudhui ya nyimbo zako maana yake?

Vitali Maembe: Eeeh, maudhui ya nyimbo. Kama wimbo wa hasira au uchungu kama mimi nalia, kwa hiyo hata watazamaji wangu wote wataanza kulia. Lakini pia inasaidia ku-take home, yaani mtu anapotoka pale [kwenye hafla ya kutumbuiza] akirudi nyumbani ndio anaanza kutafakari yale maneno. Kwa hiyo, utumbuizaji unakuwa haumalizikii jukwaani.

Kwa hiyo, hata katika maisha yangu pamoja na vuguvugu za kukamatwa au kuzuiwa sijawahi kukamatiwa jukwaani. Yaani mtu anarudi nyumbani ndio anakumbuka huyu jamaa alitutukana pale, unaona eeh, kwamba akitafakari zaidi anasema hapa hakunitukana. Kwa hiyo, inakuwa ni yeye mwenyewe na mawazo yake wakipambana mpaka anapata jibu la uhakika. 

The Chanzo: Kwa hiyo, unatumia kutabasamu kama silaha yako pia?

Vitali Maembe: Ni kinga.

The Chanzo: Huwa inatokezea mtu akawa na jina la kipekee sana, mara nyingi si majina mawili. Unakuta mtu ana majina mawili ya kipekee kabisa. Mfano kwa kesi yako Vitali Maembe, nilitaka kufahamu kuhusu asili ya hili jina, ni wazazi wako walikupa au ni jina la kisanii au ilikuaje ukafikia kujiita Vitali Maembe? Kuna hadithi yoyote ipo nyuma ya jina lako labda?

Vitali Maembe: Mimi niliitwa Vitali na ndio jina nililokuwa nalo toka utotoni nikiitwa Vitali. Lakini mimi niliwahi kubatizwa, nikaitwa Vitalis. Lakini nilibatizwa majina mawili Vitalis Mathias, yaani jina moja ukipenda Mathias Vitalis. Lakini wazazi wangu hawakuwahi kuniita Vitalis, yaani kuniita tu Vitalis au waseme huyu mwanangu anaitwa Vitalis au mwanangu anaitwa Mathias. Wao walizoea [kusema] mwanangu anaitwa Vitali. Lakini Vitali kwetu sisi, mimi ni Mmambwe kikabila.

The Chanzo: Wamambwe ni watu wa wapi hao?

Vitali Maembe: Watu wa Sumbawanga huko ambao pia ni sehemu ya Wafipa. Kwa hiyo, sisi Vitali maana yake ni virefu eeh, kutali maana yake ni mbali unaona eeh. Sasa Vitali ni virefu, kwa hiyo jina hilo kwangu lina maana hiyo.  Sasa hizo maana nyingine Vitalis sijui. Kwanza mimi ni mkristo wa kurithi, siishi maisha yale ya Kikristo kama Wakristo wengine wanavyoishi ila mimi ni Mkristo wa kurithi sababu wazazi wangu ni Wakristo. 

Mimi nina imani yangu nyingine kabisa,  imani yangu ni ya Kijamaa [kicheko]. Ndio naamini, ndio itikadi yangu. Naamini katika Ujamaa, tutatendeana haki,  tutapeana haki zetu na tutashiriki katika maendeleo yetu na maendeleo ya watu wengine, hatuta shiriki katika harakati zozote za kumuharibia mtu mwingine maisha. Kwa hiyo, mimi katika imani yangu naamini kabisa pamoja na kwamba siendi huko ila pepo inanihusu [kicheko]. Lakini hata hivyo, [mshairi] Shaaban Robert aliwahi kutuambia kuwa ipo pepo ya wapigania haki. 

Kwa hiyo, nikiikosa ile kule sababu sio muumini kivile nitapata nafasi ya pepo ya wapigania haki. Kwa hiyo, Vitali ipo kwa namna hiyo. Lakini pia nilijarbu  kutafuta maana zaidi ya Vitali, na ndio nikawa nakwepa watu kuniandika Vitalis tena, umeona eeh?  Kwa sababu wazazi wangu wameniita Vitali, na sehemu zote naitwa Vitali, nimekua nikiitwa Vitali nikasema basi ngoja nitafute maana ya Vitali. Kuja ndio nakuja kugundua Vitali maana yake ndio hiyo. 

Ukisikia Vitali mpee, maana yake virefu sana, yaani vimekuwa virefu sana. Lakini pia nikasema hebu ngoja nitafute maana nyingine. Maana nyingine ya Vitali nikaenda kwenye kamusi za lugha mbalimbali nikakuta Vitali maana yake maisha, uhai.

The Chanzo: Maisha, uhai?

Vitalis Maembe: Eeh, umeona. Kwa hiyo, vitu muhimu kwa uhai, umeona. Halafu nikaona sasa basi nichukue nafasi hii sasa kuweza kuikuza maana hii, yaani niwepo, uwepo wangu duniani uwe ni wa kuwafanya watu waweze kuishi zaidi kuliko kuwafanya watu wapunguze nanii [siku] zao za maisha. Lakini pia Vitali, mimi nikapata hitimisho kwanza,  ni someone who see from afar.  

The Chanzo: Mtu ambaye anaona mbali.

Vitali Maembe: Eeh unaona. Kwa hiyo, kabla jambo halijatokea. Kwa hiyo, matukio yote unayoyaona yamenitokea leo mi nimesha yaimba umeona?  Kwa hiyo, kuna mambo fulani nakuwa naona. Mi nilikuja kuona mbona naweza nikaona kitu fulani. Halafu mbona nikinyamaza kinatokea kitu kibaya, mbona nikisema kinakuwa watu wanakiangalia [na] wanakijadili? Kwa hiyo, najaribu kutumia nafasi ile mimi ninayo au niliyopewa na Mwenyezi Mungu kuweza tu kuwafanya watu wafurahie maisha.

The Chanzo: Ungeamua kuanzisha kanisa kama ungekuwa practising Christian.

Vitali Maembe: Eeh! Ningekuwa labda ni yule Mkristo kabisa  ambaye yupo vizuri kwenye masuala ya Kikristo ningeweza kuanzisha au labda ningekuwa Muislam hata ningeweza kuhangaika walau nipate hata msikiti wangu nifanye nanii zangu. Lakini pia nimebahatika kuwa na majina mengi, unaona eeh. Pangani mimi naitwa Abdul.

The Chanzo: Pangani, Tanga?

Vitali Maembe: Eeh, Tanga. Kuna miji mitatu ambayo imekuwa kama nyumbani: Pangani, Bagamoyo na Dar es Salaam, Mtoni kule Temeke.  Kwa hiyo, nimekuwa mwenyeji hata nikienda kwa Mwenyekiti [wa Serikali ya Mtaa] anajua huyu jamaa ni mkazi wa hapa. Katika miji hiyo yote najulikana kwa majina tofauti. Bagamoyo ndio Vitali. Mikienda Dar es Salaam pia Vitali. Pangani nitaitwa Abdu.

The Chanzo: Walikupa wao hilo?

Vitali Maembe: Walinipa na kuna hadith ambayo iliyofanya mpaka iwe namna hiyo. Waliwahi kuwa na mtoto zamani sana ambaye waliamini nilivyo kwenda mimi wakasema ndio huyu huyu, yule mtoto na wanamjua kabisa anaitwa Abdul Maembe. 

The Chanzo: Wao?

Vitali Maembe: Eeh! Lakini kipindi wanachokisema mimi sikuwepo.

The Chanzo: Ni zamani?

Vitali Maembe: Ni zamani miaka hiyo ya sabini na nane, sabini na tisa [1978, 1979]. Umeona. Alikuwa ni mtoto mdogo. Kwa hiyo, mimi nilivyokwenda nilivyojitambulisha tu Maembe wakasema ndio huyu huyu mtoto wa Maembe huyu Abdul. Kwa hiyo, huwezi kuwakatila, mnaheshimiana basi nikalichukua. 

The Chanzo: Na Maembe je?

Vitali Maembe: Maembe ni jina la familia. Sisi ukoo wetu ni wa kina Sichilima, lakini babu yetu aliwahi kuwa anaitwa Maembe, babu yetu wa babu yetu. Kwa hiyo, jina limekuwa tunaliendeleza. Maembe mpaka leo. Kwa hiyo, unaweza ukawakuta kina Maembe wengi, wengine unaweza kuwakuta Maembe lakini sio wa kwetu [kiukoo]. Sichilima sasa ndio wa kwetu. 

The Chanzo: Wewe ni mwanaharakati na mwanamuziki. Kipi kilianza mwanzo, kipi kilitangulia?

Vitali Maembe: Kilichotangulia nafikiri ni harakati kwa sababu mimi sikuanza kama mwanamuziki. Nilianza kama mchoraji. Nilikuwa nachora. Kwa hiyo, nachora.  Nilikuwa nachora pia maisha ya watu. Nilipenda sana kupigania haki za watoto wa mitaani. Na ilinipelekea kuingia kwenye matatizo mengi sana. Nilibahatika kufukuzwa shule nikiwa darasa la saba. 

Sababu mi nilianza kupambana nikiwa mdogo yaani. Kwa hiyo, ilionekana hii ni bughuza shuleni, huyu jamaa mbona anasumbua, mbona anazungumza mambo ambayo hayamuhusu, katumwa. Watu wengi wakiona umri mdogo halafu wakiona mambo unayozungumza watasema huyu katumwa, ngoja tumtoe tuone hao waliomtuma. 

The Chanzo: Harakati ulianzia shule ya msingi?

Vitali Maembe: Eeh, Mbagala.

The Chanzo: Ilikuaje mpaka ukafukuzwa shule?

Vitali Maembe: Kuna watu walikuwa wanarudia shule za msingi wanapo feli sababu kupata nafasi za sekondari zilikuwa chache kipindi hicho. Kwa hiyo, mtu akianguka darasa la saba anarudi nyuma anabadilisha jina anakuja kurudia tena shule. Sasa Serikali ilikuwa hairuhusu ile kitu, umeona? Sasa pale kuna dhulma fulani zilitumika kuna baadhi ya watu walifukuzwa ingawa hawakufanya hivyo mradi kuwalinda wale watu wengine. 

Kwa hiyo, ndipo mimi nilipoanza ku-experience rushwa. Kwa hiyo, mimi nikaanza kusema kuhusu rushwa, kuchora kuhusu rushwa, nikaonekana mimi ni tatizo pia. Kwa hiyo, hayo yakatokea na kuna wakati tutazungumza zaidi kuhusiana na masuala ya  shule kwa sababu shule peke yake kwangu mimi imekuwa ni funzo kubwa sana, na shule kwangu mimi imetengeneza nyimbo nyingi sana.  

Kwa sababu sio hapo tu, mimi nimefukuzwa shule ya msingi nikahangaika nikarudi shule sababu nilipata maana ya shule na mzee wangu alikuwa anapenda elimu umeona? Kaka zangu, dada zangu [wote] wanajua maana ya elimu. Kwa hiyo, kitendo cha kutokuwepo shule mimi nikawa sina raha. Nikalazimisha nikarudi shule kama mcheza mpira, umeona? Nikarudi  shule, kurudi tena shule nikafukuzwa tena sekondari. 

The Chanzo: Sekondari, kidato cha ngapi?

Vitali Maembe: Kidato cha pili nilifukuzwa, unaona eeh? Baadaye nikaja nikahangaika nikarudi tena kusoma shule nikaenda chuo sasa. Chuo napo nikaja nikafukuzwa tena. Kwa sababu ya kidomo domo tu.

The Chanzo: Chuo gani?

Vitali Maembe: Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Kuongea, yaani mimi siwezi kuficha, siri yangu tu mwenyewe siwezi [kuificha].

The Chanzo: Hiyo ilikuwa mwaka gani?

Vitali Maembe: Ilikuwa mwaka, mara ya mwisho kufukuzwa ilikuwa mwaka 2000 nilifukuzwa TASUBA, Chuo cha Sanaa. Lakini nilimwambia Mkuu wa Chuo, mimi hapa siondoki. Nikachukua mabegi yangu, nikamwachia, nikamwambia mimi naenda lakini nitarudi nitasoma tena hapa. Kama wanaruhusu kurudia nitasoma hapa mpaka nitamaliza.

The Chanzo: Hiyo ilikuwa ni ngazi gani, Diploma au Shahada?

Vitali Maembe: Ilikuwa Diploma [Stashahada]. Kwa hiyo, nilirudi nikawa nasoma nikafaulu lakini ndio chuo ambacho nimesoma miaka mingi. Nimesoma miaka tisa kwa diploma niliyotakiwa nisome miaka mitatu. Kwa hiyo, nilipomaliza pale nikaona  mambo ya kusoma soma sasa haya katika mipangilio ile kwangu mimi itanipotezea muda wa kwenda kwenye kazi kama kazi. 

Kwa hiyo, basi nikawa nawawezesha watu wengine kusoma mimi nikawa nasoma kwa namna nyingine. Kwa hiyo, nimesoma kwa namna nyingine. Nimepata elimu nyingine mbalimbali. Nilibahatika  pia kwenda kufundisha Chuo Kikuu cha Agder, Agder University Norway. Walikuwa wana vitengo mbalimbali vya elimu, elimu ya watoto, mimi nimefundisha watoto muda mrefu sana.  Kwa hiyo, wao waliona kabisa huyu jamaa anaweza kutusaidia kwenye nanii zetu. Kwa hiyo…

The Chanzo: Hapo hujaanza muziki?

Vitali Maembe: Aah, muziki nimeanza, muziki hata sikumbuki nimeanza lini kwa sababu uliingia tu ndani ya life [maisha].  Kwa hiyo, muziki nilikuwa nimeanza, kufukuzwa chuo cha sanaa muziki ulichangia napo. Kwa vile nilivyokuwa nikiviimba, vile nilivyokuwa nikiviongea. Kwa hiyo, kulikuwa hamna namna nyingine mtu anaweza kunizuia zaidi ya kunitoa pale kukaa mbali na lile eneo. Lakini kwa kunizuia, hapana. Sijawahi kuogopa kusema ukweli, pale panapokuwa ni suala linahusu  ukweli au haki yangu mimi au haki ya mtu mwingine sijawahi kuogopa.  

The Chanzo: Kusema ukweli nitatumia mwanaharakati na mwanamuziki kwa wakati mmoja, kwa sababu ninavyoona, utanisahihisha, sababu nikisikiliza muziki wako ni wa harakati fulani, mambo ambayo unayazungumza unaweza ukawa unayafanyia harakati kwenye jamii. Labda kama msanii na mwanaharakati ni masuala gani haswaa ya kijamii ambayo yanakugusa wewe na ambayo yanachukua sehemu kubwa sana kwenye kazi zako za kiharakati na kimuziki pia?

Vitali Maembe: Mimi kikubwa zaidi ni elimu. Unajua katika vitu vinavyoniuma ni elimu.  Elimu inaniuma sana kwa sababu sisi hatuna sababu ya kutokuwa na nafasi ya kupata elimu. Unapokutana na mtoto mdogo, au kijana, unamwangalia  unaona kipaji chake labda cha ufundi, au unaona kipaji chake cha kilimo, halafu unamuuliza wewe umesoma mpaka darasa la ngapi anakwambia mimi sijasoma.

[Ukimuuliza] kwa sababu gani anakutajia kitu ambacho kimesababishwa tu na mtu fulani, umeona? Kwa hiyo, inakuwa inaniuma sana na mimi ninachokifanya najaribu tu kuangalia tusiwe wengi ambao tumekosa elimu kwa sababu ya kitu kama hicho. 

Lakini pia kingine ni afya. Umeona hivyo vitu viwili vinanisumbua sana. Afya, kwa nchi kama Tanzania umeona, kwa mtu kusema kwamba anakua na matatizo ya lishe unaona eeh, kwamba mtu anaambiwa wewe una tatizo fulani kwa sababu una upungufu wa chakula fulani.

The Chanzo: Matatizo ya udumavu, utapiamlo

Vitali Maembe: Eeeh, umeona! Kwa hiyo, kwangu mimi inanisumbua  kusema ule ukweli kwa sababu ni kitu ambacho unaona kinawezekana [wananchi kuwa na lishe]. Ingekuwepo labda vita kwamba mtu kapoteza mguu ndio amekuwa mlemavu tunasema hiyo ipo nje ya uwezo wake au nje ya uwezo wa jamii ni kwamba suala limetokea  tu. Lakini sasa unakuta vile vitu vipo.

Kwa hiyo, mimi ninapo angalia nagundua kabisa kuna tatizo kwenye masuala ya uongozi, umeona? Kwa hiyo, na  hatupaswi kuwachukia viongozi isipokuwa kuwakumbusha. Bahati mbaya kwenye nchi yetu hii ukimkumbusha mtu majukumu yake inakuwa ni kosa.  Lakini pia ninavyo zungumza uongozi nazungumza kwenye ngazi mbalimbali, kutokea kwenye ngazi ya familia, unajua. 

Watu wengine mtoto hawezi kufanya jambo fulani mpaka baba yake au mama yake awe amemuongoza kulifanya. Sio lazima afanye naye lakini ukimpa muongozo tu anafanya lakini sasa unakuta kila mtu yupo busy  na maisha yake, baadaye mtu akipata tatizo ndio watu wote wanamwangalia daah! 

Sasa mtu fulani anaumwa au sasa mtu fulani kashafikia umri fulani na kusoma hajasoma. Kwa hiyo, inakuwa tatizo kubwa ambalo hata kutibika inakuwa ngumu. Lakini muziki wangu mimi kusema ukweli hauimbi tu, yaani kutunga tu, unatunga from nowhere, hapana. Kutoka kwenye jamii kule kule na mawazo mengine tunapata kutoka kwa watu kwa sababu watu..

The Chanzo: Na hilo ndilo lilikuwa swali langu jingine kwamba mawazo yako ya kuandika nyimbo, ya kuimba nyimbo fulani, unayatolea wapi? Kwa mfano,  kama hapa tumesikia tu [unaimba huu wimbo], huo utakuwa ni mpya tu, haujautoa?

Vitali Maembe: Eeeh bado, huu wa kwanza. 

The Chanzo: Kwa hiyo ni maalum kwa The Chanzo? Kwa maana huo sijauona kwenye accounts zako za muziki. Mawazo yako kama msanii yanatoka wapi?

Vitali Maembe: Yanatoka kwenye jamii. Kwa sababu kwanza, kuwa na sanaa unajua ni kama  kuwa, yaani kuwa msanii ni kama kuwa na kiwanda,  umeona eeh? Kwa hiyo, ukiwa kiwandani tu unataka kutengenezea kitu kiwandani unaweza kutengeneza product ambayo haifai kwenye jamii ila sasa unatoka nje kwenda kutafuta zile malighafi. Ndio unakwenda kuwasikiliza watu wana tatizo gani. Watu wana raha gani. 

Zipo nyimbo ambazo naimba raha, burudani, umeona eeh? Kwa sababu nakutana na watu wenye furaha. Kwa hiyo, natengeneza inaakisi yale maisha. Kwa hiyo, natengeneza, na ukishamaliza kutengeneza narudisha tena kwenye jamii. Kwa hiyo, jamii sasa ikiona umeigusa  ina-react. Kwa hiyo, yule ambaye umemfurahisha atafurahi na yule ambaye umemkera atakereka. 

Kwa hiyo, hiyo ni sehemu tu ya nanii. Lakini hivi vitu mimi navitoa kwenye jamii moja kwa moja na muda mwingi natumia muda wangu kukaa na jamii, kuwasikiliza watu, kuongea na watu masuala lakini pia hao hao watu kuwapa nafasi ya kuniuliza maswali. Kwa hiyo, badae ndio tunapata hiko kitu tukikirudisha kwenye jamii matokeo ndio unayaona hapo.  

Kuna mwingine atafurahi, atakwambia niuzie huo wimbo. Mwingine atakwambia bwana umenifurahisha sana shika hiki. Mwingine atasema umenikera sana njoo, anakufunga pingu anakupeleka huko. Kwa hiyo, kila mtu ana namna yake.  Nakuwa najua, mimi sikushitushwa kukamatwa [na polisi hivi karibuni]. 

Naona kama wamechelewa sana kwa sababu najua kuna vitu fulani ukiviimba na kwa hulka yao na tabia zao zilivyo [watawala] watakukamata, wakutishe, wakufanyaje, wakufanye wanavyoweza kufanya ikiwezekana wakupoteze, umeona? 

The Chanzo: Kwenye suala la kukamatwa tutakuja. Nilikuwa nataka kufahamu, mimi naangalia sana live performance zako, samahani nashindwa kutafsiri kwa Kiswahili ‘live performances’ Kwa hiyo, mimi napenda sana kukuangalia kwenye  live performances, na vile unaimba unakuwa umetulia  unanielewa? Hivyo nikawa nawaza mchakato wako ya kupata wimbo ukoje, ni kwamba unaandika, unakaa chini kabisa na kitabu na kalamu unaandika kuwa huu ndio wimbo wangu au unaingia tu studio na gitaa lako, unajua umekutana na wakulima wa korosho hapo kona wanalalamika, vitu vinakuja akilini unaimba. Mchakato ni upi? 

Vitali Maembe: Mchakato ni kama hivyo nilivyokwambia unaingia kwenye jamii, ukishapata sasa ule ujumbe huulazimishi kwenye kuimba, lazima uzame kwenye uhusika wa yule mtu. Kwa hiyo, sasa wewe uwe sehemu ya yule mtu, sehemu ya lile tatizo  umeona eeh? Ukishamaliza unaingia sasa kwenye suala la kutengeneza muziki. 

Ninavyo tengeneza mimi muziki naingia moja kwa moja kwa watu. Kwa hiyo, naweza kwenda kijiweni nikapiga muziki najua wapo ambao huo muziki unawahusu. Kwa hiyo, napiga. Watu wanaweza wakafurahi, wengine wakasema aaah hapo mbona kama kazingua, sijui kafanyaje. Kwa hiyo, nawe unarekebisha kulingana na vile. Ila kama ukiwagusa zaidi nao wanakupa mawazo. 

Kwa hiyo, mimi sianzi kuutengenezea muziki studio. Mimi muziki wangu mpaka ukue kwanza, yaani unazaliwa, unakua, ukishabalehe ule muziki ndio naupeleka kwa watu.  Kuna wakati mwingine muziki unadumaa. Zipo nyimbo ambazo nimezitengeneza zamani kabisa zina miaka zaidi ya kumi lakini sija-record kwa sababu sioni kama zimefikia hatua stahiki. 

Kwa hiyo, ni kama hivyo. Lakini zipo improvisation [maboresho] ambazo unaweza ukakaa una improvise na mtu anaweza akaichukua ukaikuta kwenye mtandao kazi imetoka. Lakini baadae, baada ya mwaka mmoja au miwili, ukasikia sasa wimbo halisi umebadilika kidogo. Kwa hiyo, ni vitu kama hivyo. 

The Chanzo: Tunafahamu kuwa uliingia matatizoni hizi siku za karibuni kama nilivyotangulia kusema kwenye utangulizi wetu, hali kama hii ya kujikuta matatani na vyombo vya dola vya Tanzania kutokana na kazi unazozifanya imekuwa ikitokezea kwa kiasi gani au mara ngapi? Ni kitu ambacho ni cha  kipekee au ni kitu ambacho umekizoea pengine hii sio mara ya kwanza kujikuta ukihojiwa kutokana na kazi uloifanya, ama ni vipi?

Vitali Maembe: Hii sio mara ya kwanza kutokea. Hii inatokea mara kwa mara. Na [polisi] wakijisikia tu, bwana tunataka kumsumbua huyu bwana, basi. Yaani, kitu ambacho watendaji wa Serikali yetu walichobakisha mimi ni kuniua tu, umeona. Walishanifanyia vitu vingi sana.

The Chanzo: Vitu vingi sana ukimaanisha nini?

Vitali Maembe: Kama nisingalikuwa na uzalendo au mapenzi na hii nchi ningekuwa nimeshakimbia. Lakini, mimi muziki, watu nilioanza kupiga nao muziki wameshaacha sahizi, unaona, wengine. Mimi recording ya kwanza nimefanya mwaka 1999 na Band ya Manyani nani, lakini baada ya hapo mimi mwenyewe nikawa naendelea kupiga muziki kama mimi. 

Lakini ndugu yangu nina albums tano  lakini muziki wangu haupigwi redioni. Ukisikia umepigwa wamepiga Sumu ya Teja.  Kujikosha tu. Lakini miziki yote we unayoijua mizuri ambayo mi nikipiga sehemu nyingine yoyote nikikaa na watu mpaka wenyewe watangazaji wa redio wanakuambia miziki yako tunaipenda sana lakini hatuwezi kupiga kwa sababu gani, wamekatazwa. 

Yaani wanafanya ile kampeni ya siri siri yaani kwamba miziki yangu wasiipige kwa sababu ikipigwa mimi nitapata chakula, nikipata chakula maana yake nitakuwa na kiburi. Kwa hiyo, wao mimi ninavyokuwa na njaa yaani ndio  burudani kabisa kuwa huyu atakuja kuacha kwa njaa.

The Chanzo: Wao ukimaanisha?

Vitali Maembe: Watendaji wa serikalini. Sizungumzii Serikali, nazungumzia watendaji wa Serikali ambao wanabadilika. Leo anakuja huyu, kesho huyu, wanarithishana chuki zile, umeona? Serikali kama Serikali ni Serikali tukufu, ila watendaji wa Serikali sio watukufu hata kidogo. 

The Chanzo: Ni watukutu?

Vitali Maembe: Eeeh! Wapo baadhi yao [watendaji wa Serikali] ni wazuri lakini wanapokuwepo wazuri wawili wabaya kumi. Hata ikipigwa kura wenyewe wanakwambia mkataa wengi mchawi. Kwa hiyo, sisi tunaendelea kuteseka mpaka siku ambayo watatokea wazuri sita, wabaya wanne. Labda hapo ndio kura itasimama. Lakini bado mimi sijakata tamaa hata kidogo. 

The Chanzo: Ukiacha hii ya nyimbo zako kutokupigwa redioni na kwenye TVs, labda kuna kitu kingine kinachokukumba au changamoto yoyote inakukumba, ambayo unadhani ina uhusiano wa moja kwa moja na hao watendaji wa Serikali?

Vitali Maembe: Ujue mimi nikipiga muziki, unajua unaweza kukuta watu wanapiga piga muziki barabarani, mimi pia huwa naenda kutoa burudani barabarani unapiga unajitangaza watu wanaangalia, umeona? Mimi nikienda kupiga, sijawahi kwenda kupiga muziki barabarani haija-park defender [gari ya polisi] pembeni. Kwa hiyo, watakuja watatafuta kosa, wapi nitakapokosea, umeona?

Sasa watu kama Watanzania wataogopa, watu kama polisi sio watu wabaya, polisi ni muhimu kwenye jamii yetu kwa sababu wanafanya angalau hata ukipata tatizo lolote ukimbilie kwao. Ni chombo ambacho kipo pale lakini kutokana na baadhi ya utendaji wao mwingine akishaona tu polisi anaondoka. Wananifukuzia watu wangu ambao wangeweza kutazama ule muziki, umeona? Lakini  usitegemee mimi nikaitwa kwenye [tamasha la muziki la] Fiesta. 

Usitegemee mimi nikaitwa kwenye matamasha makubwa wala usitegemee kama nitakuja kupata tunzo  fulani hivi kwa sababu tunzo zote za muziki wa Tanzania ni tunzo za kutengeneza, kwamba huyu atakuja kutusaidia badae tumuweke hapa.  Kwa hiyo, mimi ambaye nawasaidia wananchi ni wananchi pekee ndio wanaweza kunisaidia mimi. Lakini hakuna mtu mwingine yoyote  anaweza kunisaidia mimi. Lakini hilo suala kila unapopiga muziki askari anakaa pembeni, kwa sababu mimi lazima nikaombe kibaali, mimi sipigi ovyo ovyo kama wanavyofanya jamaa wengine mimi lazima niombe kibali cha kufanya maonesho. 

Wakati napata hiko kibali kuna maneno kibao pia naambiwa lakini unavumilia kwa sababu unajua mimi sivunji sheria ya nchi na hiki ninacho kifanya ndicho kinatakiwa. Kwa hiyo, nitakwenda watazuia kwa namna hiyo. Lakini  wakati mwingine unaweza ukawa umeelewana na mtu, eeh, bwana kuna kazi hii hapa ya milioni mbili, mnaelewana vizuri siku zinakwenda zikikaribia anakuambia bwana tumehairisha ule mkutano. 

Lakini ule mkutano baadaye unafanyika, ukimwambia bwana vipi? Anakuambia wenye nchi ndio wameamua hivi. Kwa hiyo, mimi maisha yangu yamekuwa namna hiyo. Kwa kifupi, mimi nikifanya majumuisho, naona Serikali yangu inataka mimi nife na njaa. Serikali yangu haitaki ione watu wengine waone mfano wangu wa kuimba mambo ya maendeleo ya nchi yetu. Bado sijaimba chochote kile cha kuipinga Serikali, na kama nitapata wazimu huo wa kuipinga Serikali basi watu watanifuata, lakini ya nini? Kwa nini niipinge Serikali yangu? 

Mimi naamini katika mfumo wa demokrasia na Serikali imewekwa kwa mfumo wa demokrasia siamini katika namna yoyote. Kwa hiyo, basi mimi nitakaa, wakijisikia kuniua wataniua.   Labda kinachoweza kufanyika, labda nizungumze kama alivyozungumza mzee wangu mshairi Abdulatifu Abdallah, alikuwa akizungumza na kaka yake, kaka yake akamwambia unazungumza maneno mazuri, unazungumza jambo zuri kabisa kwenye jamii lakini hiyo lugha unayotumia na hao watu unaowaambia unajua madhara yake? 

[Abdulatifu Abdallah] akasema mimi nayajua madhara yake. Akamwambia madhara yake ni nini? Akamwambia madhara yake ni kwamba watanifunga wakinionea huruma sana,  lakini kama huruma watakuwa hawana wataniua. Kwa hiyo, katika hayo mambo mawili siwezi kuyakosa kwa hatua niliyofikia. Wataniua, wakinionea huruma sana, watanifunga. 

The Chanzo: Lakini unadhani ni kwa nini wanafanya vitu kama hivyo hapo?

Vitali Maembe: Kwa sababu sisi tunaamini kwamba mzalendo ni kiongozi, anapotokea mtu mwingine akaonesha uzalendo ambao ni bora zaidi na ukamzidi kiongozi, basi kiongozi anaona uwepo wako wewe ni tatizo. Eidha uiache kazi inayokufanya uonekane mzalendo, au ukimbie nchi yako au ufe au utafutiwe kosa lolote lile ufungwe kwa sababu waswahili wenyewe wanasema mpeni mbwa jina baya mumuue. Mbwa wa mtu ukimuua bila kumpa jina baya basi wewe utaonekana una tatizo. Unamtafutia tu sababu, huyu jamaa hivi, huyu jamaa hivi, umeona.

The Chanzo: Lakini ndio umesema hapo mwanzo kabla ya mimi  kukukatisha kwamba hivi vitu sio kwamba vinakutisha uweze kuacha kazi zako unazozifanya? 

Vitali Maembe: Mimi kwangu muziki ni imani. Naamini sio kwamba wazazi wangu walikuwa bora sana mimi kuweza kupata malezi hayo kuliko wazazi wengine. Siamini kwamba mtaa wangu niliokulia ulikuwa mtaa bora kuliko mitaa yote Tanzania. Siamini kwamba wale watoto waliobadilika badae kuwa mateja kwamba Mungu hawapendi kama anavyonipenda mimi, hapana. 

Haya ni majukumu tu ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu, kwa hiyo mimi nafanya majukumu yangu na ninaamini kabisa nitaondoka na watakuja wengine. Mimi siwezi kuacha kufanya kitu ambacho ni bora, mimi siachi na sitaacha. Anasema mshairi mmoja ‘Siwati,  nshishero.’ Yaani, siachi nililolishika hata uning’ate meno siutoi mkono wangu kwa sababu hilo ninalolifanya najua ni jambo zuri. Ningekuwa nafanya jambo baya kwa hizi adhabu nilizozipata ningekuwa nimeshabadilika kufanya zuri. 

Lakini zuri kwao ndio baya na baya kwao ndio zuri. Kwa faida ya nchi yangu nimepewa jukumu hili ili niweke sawa na ndio maana sitaki wao waonekane wabaya. Sitaki Serikali waonekane wabaya. Sitaki polisi waonekane wabaya. Sababu mwisho wa siku ukipata tatizo utakimbilia serikalini, utakimbilia polisi. Kwa hiyo, ukiharibu jina la hawa watu, ndio maana sisemi Serikali. Nasema watendaji wa Serikali sabau wakija watendaji wengine wazuri maisha yatakuwa mazuri. Lakini siachi [muziki], sitegemei kuacha.

The Chanzo: Sawa sawa. Mwaka 2020 uliamua kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea ubunge, nadhani ni jimbo la Bagamoyo si ndio?  

Vitali Maembe: Naam, ndio.

The Chanzo: Kwa kupitia chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo. Nilitaka kufahamu ni nini kilikusukuma mpaka uone jukwaa la muziki na harakati zako hazitoshi kutumikia jamii yako mpaka ukaamua labda niingie bungeni labda sauti yako inahitajika huko na vitu kama hivyo. Nataka kusikia kutoka kwako msukumo ulikuwa ni nini?

Vitali Maembe: Kwanza, yapo mambo mengi yaliyonisukuma. Kila wakati tunasukumwa lakini unapoona misukumo imekuwa mingi kiasi cha kutosha unasema sasa ngoja niende. Mimi sikuwa najaribu na sikushindwa. Mimi sikushindwa [kwenye uchaguzi wa ubunge] ila watu wa Bagamoyo ndio walishindwa kunichagua mimi. Mimi nilishinda kwa sababu nilimaliza kampeni, nilikwenda kila sehemu na niliwafikia watu. Hakuna mgombea yoyote aliyefika sehemu nilizofika mimi. 

Kwa hiyo, ilibakia kazi kwa jamii yenyewe, jamii ndio imeshindwa uchaguzi, umeona, na ninawaonea huruma. Kwa sababu mimi sio mwanasiasa, nilikuja kufanya kazi ya kijamii kama ningepata fursa ya kufanya kazi ya uwakilishi. Kilichonisukuma kwanza, mwaka 2020 ulikuwa mwaka ambao demokrasia ilinajisiwa sasa katika hali ile ndio nikasema huu ndio mwaka wa kugombea kwa sababu  mwaka huu kama utawania tayari utajaribu kuwaonesha watu kuwa demokrasia bado iko hai. 

Mimi nilikuwa nataka kuweka picha nzuri kwa taifa langu. Kwa sababu watu walijiweka pembeni. Watu wengine walikuwa wanasema sisi hatupigi kura, sisi hatuendi kwenye uchaguzi. Kwa hiyo, nikasema ikiwa kwenye jamii kiongozi wetu tunampata kwa njia ya kidemokrasia ya kupiga kura lakini jamii  ikianza kurudi nyuma ikisema haifanyi namna hiyo ujue sasa taifa linakoelekea sio kuzuri. Kwa hiyo, jambo la kwanza nilikuwa nataka niwarudishe watu kwenye mstari kwamba, iwe isiwe njia yetu ya kumpata kiongozi wetu lazima iwe ya kidemokrasia. 

Nani atasimama mstari wa mbele kuwaonesha watu kuwa demokrasia inatakiwa isimame? Nikaona ngoja nichukue hii nafasi. Nilichukua hii nafasi nikiwa na uchungu pia kwa sababu hatukuwa na hali ambayo inaweza  kutupa uhuru wa kushiriki kwenye uchaguzi kwa uhuru bila mashaka. Katiba tulokuwa nayo ni Katiba chonganishi kulingana na wakati, kuna vipengele vinakuruhusu kuandamana na kuna vipengele kuzuia maandamano. Yaani maana yake kukitokea chochote kile watu watapigana tu. 

Lakini sasa unasema ngoja tuingie. Kingine kuwa mmoja katika vyombo vya maamuzi, maamuzi ya kidemokrasia, maana maamuzi unaweza ukaamua tu mtaani ukawakusanya watu mkaenda hivi lakini bado haitakuwa  njia nzuri ya maendeleo. Kubishana mnaweza mpaka mkapigana mapanga lakini mkibishania bungeni mtabishana kwa hoja na kwa kidemokrasia. Nikasema  kwa nini nisitafute fursa ya kwenda kufika kule  na kuweza kutoa hoja zangu kwa sababu nimetoa hoja miaka mingi sana zimekuwa zikipuuziwa.  

Nasema zinapuuziwa kwa sababu wabunge, mawaziri na Serikali wanasikiliza nyimbo zangu lakini wanapuuzia. Unakuta robo ya yaliyomo kwenye wimbo wangu akisema mbunge yanafanyiwa kazi.  Nikasema labda tukizungumza huko tunaweza isaidia nchi yetu kwenye maendeleo. Yaani huku kutapa tapa kote huku ni tunatafuta namna ya kuwasaidia wananchi kweli. Kwa sababu sisi tunaishi kwenye yale maisha ya kweli ya huku kwenye jamii. Mimi nipo kati kati unajua, nayajua maisha mazuri kwa sababu nimeshayaishi, nayajua maisha mabovu sababu nimeyaishi. 

Kwa hiyo, najua nikiwakilisha watu nitawakilisha kwenye njia nzuri. Lakini pia niliona huu ndio wakati wangu kufahamu huku ndani ya siasa kuna nini? Haya mambo ya uchaguzi wanayosema yana nini?  Na mimi sikufichi nimeyagundua mambo mengi kweli kweli. Kwa hiyo, sasa nchi naifahamu kijiografia. Nimefika sehemu zote katika nchi hii. Sehemu ambazo inawezekana hata Rais wetu hajafika lakini [mimi] nimefika.

The Chanzo: Sehemu zote?

Vitali Maembe: Sehemu zote kasoro kisiwa cha Ukerewe. 

The Chanzo: Hata nyumbani kwetu unaweza ukawa hujafika.

Vitali Maembe: Wapi?

The Chanzo: Chake Chake, Pemba.

Vitali Maembe: Pemba sijafika [kicheko]. Sehemu mbili sijafika, sijafika kisiwani Pemba na sijafika Ukerewe. Kwa sababu nilifika wakati nikitangaza kuhusu chanjo ya rushwa, nilifika sehemu nyingi kuhusiana na chanjo ya rushwa, nilifika mwenyewe mimi kama mimi. Nilifanya maonesho 550 ndani ya miaka mitano. Hawaandiki waandishi wetu kwa sababu hamna kinachotakiwa kuandikwa kizuri, wanaandika vitu vibaya. Kwa hiyo, hizo ndio sababu zangu mimi kuweza kushiriki [kwenye] uchaguzi. 

Ningefurahi sana kama kungekuwa na mgombea binafsi. Ingekuwepo hiyo ningeifurahia zaidi kwa sababu naona pia hawa viongozi wetu wanavyopata shida kwenye kuongoza anapokuwa yupo chini ya chama. Kwa hiyo, kuna vitu fulani vinavyoturudisha sana nyuma kwenye siasa yetu. Kwa mfano, tuchukulie wewe ni muumini wa dini fulani, wewe ni kabila fulani, wewe ni mtu wa chama fulani, halafu wewe ndio kiongozi wa Serikali. 

Kiserikali wewe Katiba inakuvuta, inakutaka uongoze vile ambavyo yenyewe imekuweka madarakani maana umewekwa pale kwa mujibu wa Katiba. Lakini ukirudi nyumbani una familia yako, sasa kuna mtu kwa sababu wewe ni baba yake au mama yake anataka ufanye vitu vile yeye anataka. Lakini pale una mtu ambaye wewe ni kabila lake naye ataanza kuzungumza mambo mengi ya kikabila, [atasema:] tangu awe kiongozi imekuwa hivi na hivi. Yaani watu wanavutia kwao. 

Lakini kuna  mtu wa dini sasa, huyu ni muumini mwenzetu, tunaingia naye kwenye ibada. Kwa  hiyo, kuna vitu fulani vinakuvuta vingi sana. Kuna chama sasa. Chama kinakuambia wewe umeingia pale kwa tiketi yetu, kwa hiyo, lazima ufanye hivi. Ukikuta bahati mbaya sasa mwenyekiti sio wewe wa hicho chama, kwa hiyo maana yake wewe zile fikra za menyekiti ziendelee kudumu.   Kwamba mwenyekiti anaweza kuamua uzungumze nini hata useme nini kwenye hotuba. 

Kwa hiyo, pia mfumo wetu wa siasa unamfanya mtu ambaye amepewa mamlaka ya kufanya jambo fulani hana uhuru wa kulifanya lile kwa upeo wake. Lazima pia asukumwe na mambo mengine. Kwa hiyo, bado uongozi ni kitu kigumu sana. Na nashauri sana tuwasiaidie viongozi, wanahabari tuwasaidie viongozi kwa sababu tusipowaambia tunakuwa hatuwasiaidii. Tuwasaidie ili waweze kuwa viongozi bora kwetu. 

The Chanzo: Kama kuna mafunzo yoyote ya msingi umeyapata katika kushiriki kwako kwenye siasa za kuomba kura kabisa, mafunzo ya haraka haraka uliyoyapata kutoka kwenye mchakato huu unaweza kuwa umepata mafunzo gani?

Vitali Maembe: Kufundishwa maalumu kutoka kwa watoa mafunzo au kujifunza kwenye jamii?

The Chanzo: Mafunzo ambayo mchakato umekufunza wewe?

Vitali Maembe: Aha! Mchakato umenifunza vitu vingi aise! Kutoka kwenye jamii moja kwa moja, sehemu nyingi ukiondoa sehemu za mjini huku ukiingia kijijini wewe ukifika pale kama mgombea kuna mawili, wewe  ni mfadhili, yaani wao wanataka uwafadhili kwenye mambo yao yote, kilimo na nini na nini. Lakini wewe pia sijui nikuite, nisikuite mlalamikiwa maana mlalamikiwa ukirudi kwenye sheria inakuwa mtu mwingine. Lakini malalamiko yao yote mambo ambayo wamefanyiwa, machungu yao yote..  

The Chanzo: Mtatuzi wa matatizo.

Vitali Maembe: Eeh! Machungu yao yote utamwagiwa wewe, umeona eeh? Kwa hiyo, kuna namna hiyo. Watu wanategemea, wamezoeshwa, wanategemea wewe utawapa rushwa au utawapa chochote ili wao waweze kutatua matatizo yao. Lakini pia wanakuelezea kila kitu ambacho wao kinawakabili hasa ukiwapa nafasi. Na mimi kampeni yangu ilikuwa lazima niwape watu nafasi ya kuzungumza. Watu wazungumze ya kwao, sio kwamba ile kutoa hotuba na kuondoka, hapana.  

Nafikiri kampeni zangu zilikuwa bora kuliko nyingine kwa sababu wagombea wenzangu walikuwa wanaogopa sana kumpa mtu nafasi ya kuzungumza kwa sababu alishakuwepo kafanya makosa. Mimi sikuwahi kuwepo kule. Nilikuwa nawapa watu nafasi ya kuzungumza na walizungumza sana, hiko nimejifunza. 

Kingine nilichojifunza ni kwamba tunahitaji kuimarisha mfumo wa kitaifa kama taifa, yaani endapo watakutana mtu wa chama hiki na chama hiki  kuwe na kitu ambacho kinawakutanisha kama taifa, endapo wakutane mtu wa dini hii na dini hii hata wagombane lazima kuwe na kitu kinawakutanisha kama taifa na kuwaweka pamoja, umeona? Hiko ni kitu muhimu kweli kweli kwa sababu tunapokosa kitu kama hicho ndipo tunapopata chuki. 

Unajua ndugu wanaweza wakagombana, wakakorofishana, wakagombania mali lakini udugu unabakia pale pale.  Sasa tukitafute kitu kinachoitwa udugu katika taifa letu, tukishakipata kile sasa watu hata tugombane vipi unasema aah lakini ni ndugu yangu. Kwa hiyo, sasa hiko kikipotea inakuwa ngumu, sasa hiko mimi nimekiona. Nimekwenda nimekutana na watu wa familia mbili wako vyama tofauti na ni maadui kweli kweli. Kwa hiyo, vitu kama hivyo hawatakiwi wawe maadui, viwe ni njia tu ya kuifikia nafasi ya kuweza kuwakilisha ila isiwe uadui. Kitu ambacho tukikifanyia masihara nchi inaweza ikawa nzito hii baadaye. 

The Chanzo: Sasa nataka kukuuliza, ujue kumekuwa na mazungumzo mengi ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa waandishi wa habari lakini ni mara chache sana tumesikia watu wakipigia kampeni uhuru wa kisanii au uhuru wa wasanii kuweza kuandika vile wao wanataka ifanyike. Una tathmini vipi uhuru wa kisanii au artistic freedom kwa Tanzania, wasanii kwa kiwango gani mna uhuru wa kuweza kuandika mashairi ya kile kinatoka moyoni mwenu bila ya hofu ya kuishia kituo cha polisi au nyimbo yako kutopigwa redioni na vitu kama hivyo? Una tathmini vipi uhuru wenu?

Vitali Maembe: Uhuru wa wasanii Tanzania unaweza ukaununua kwa bei rahisi kwa kuiona  lakini kubwa sana kwa kuiishi. Ndio maana mimi ninaweza nikaimba leo Kaizari kwa maneno ya kuficha, kwa maneno ya heshima lakini mwingine akaimba kwa maneno ya kutukana kabisa uongozi, kwa kukashifu kabisa uongozi na asifanyiwe chochote. Kwa mfano, mimi kwenye wimbo wangu [wa Kaizari] nimetaja tozo nimekamatwa kama jambazi unajua? Wamekuja wamekagua humu ndani [kwangu], wamekuja na gari yao sio defender waliogopa kuniumiza kwa sababu mimi nimekamatwa yaani kama mtu akamatwe akiwa hai. 

Eeh nimekamatwa namna ile. Nimewekwa kati, nimewekwa hivi, watu kwenye gari na silaha zao lakini nakwenda naendeshwa. Yaani ni vitu fulani ambavyo kwamba tumekamata jambazi fulani hivi ambaye tunatakiwa tukapate maelezo yake. Lakini kuna watu wanaimba maneno mazito, makali, wazi kabisa na kila mtu anajua, unaona, lakini je huyu mtu ni nani? Huyu mtu ni wa kwetu, yaani wa kwetu maana yake tumemuandaa sisi  awe upande huu halafu badae aje kwetu ili aweze kuja na watu wengi. 

Kwa hiyo, mimi kama mimi, kwa sababu sijatumwa na mtu kuimba nimeimba mwenyewe hiyo ni tatizo. Lakini yule ambaye ametumwa kuimba, kwa hiyo atalindwa kwa nyimbo zake zote anazoimba. Akikashifu mwanamke, akikashifu Serikali, akikashifu wakulima, akitukana watoto, akidhalilisha watoto umeona, unaona, safi tu sababu ni mtu wetu.  Kwa hiyo, kuna watu wana kibali cha kuvunja sheria kwenye nchi yetu na sisi wengine hatuna kibali cha kuvunja sheria na hatuna kibali cha kuwa huru. 

Kwa hiyo, ndivyo namna tunavyoishi na uhuru huo ni mgumu zaidi. Wewe unaweza  ukawa na chombo chako cha habari na ukaambiwa kwamba upo huru lakini wanakuvizia wewe ili kuwa mfano,  na wakikukosa kwenye mambo yako ya habari au sanaa watakutafutia hata kosa lingine. Kwa sababu wao ndio waendesha mashitaka, wewe ndio utakaye andika  na anaweza akaandika yeye wewe ukasaini kitu ambacho sio cha kwako. Watakuja watasema jambo hili au watakuzushia. 

Kwa hiyo, uhuru kusema ukweli upo, lakini upo kwa baadhi  ya watu ambao wanatumika kuweza kuilaghai jamii. Kwenye hilo Serikali inabidi ijirekebishe kwa hilo. Kwa sababu leo wapo serikalini kesho watatoka serikalini watakuwa wazee ambao wanahitaji msaada.  Kwa hiyo, leo tunavyopigania wazee wapewe huduma za afya kwa sababu walilipa kodi. Lakini wakiona kwamba hawatazeeka, waendelee tu kutunyanyasa.

The Chanzo: Labda tukiwa tunaenda kumalizia kwenye hilo hilo eneo la uhuru, unajua tunakwenda  Disemba 9 mwaka huu ambapo Tanganyika itakuwa inafikisha miaka sitini ya uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Kama mtu ambaye umekuwa ukifanya kazi karibu na wananchi kupitia harakati, siasa na muziki nilikuwa nataka kupata pia tathmini yako. Kwa mfano, unadhani kwa kiwango gani leo hii 2021 Watanzania wako huru kwenye kujiamlia mambo yao wenyewe kama wananchi? Kwa sababu  kitu tulichokilenga wakati tukipigania uhuru kuhakikisha wananchi wanakuwa na nafasi ya kujiamulia wenyewe, una tathmini vipi tukiwa tukielekea kuamisha miaka sitini ya uhuru?  

Vitali Maembe: Mimi nafikiri nizungumze hilo katika eneo moja, waswahili wanasema uhuru usio na mipaka ni utumwa. Mimi nafikiri wasanii wamepewa uhuru kupitiliza, lakini huo uhuru waliopewa ni wamepewa kwenye kuharibu, sasa mimi sitaki wasanii wabanwe. Mimi nataka wasanii wapewe uhuru  na wapate pia maelekezo ili waweze kuwa huru kutengeneza kitu chenye faida. 

Kwa sababu leo sisi wasanii na wanahabari ndio chombo cha kupata taarifa. Kwa hiyo, taarifa inapofika kwenye jamii kama itakuwa nzuri basi mambo yatakuwa mazuri, ikiwa taarifa mbaya basi mambo yatakuwa mabaya. Kwa hiyo, sisi uhuru tunao ila tumewapa watu nafasi kuharibu. Hivi unavyoona mtu anakwenda kuimba jukwaani maneno yanayomkashifu mama yake, sio kwamba anapenda, yule ana njaa.  Anajua akiimba hivi atapata pesa. 

Lakini nayo Serikali imemuacha afanye hivyo. Lakini Serikali ingemtengenezea njia nzuri apate pesa sio lazima avunje sheria, sio lazima akashifu. Basi hivyo tungeweza kuwa na jamii nzuri. Lakini sasa watu wote, wewe mwenyewe utaniambia, Serikali itanambia wasanii wote wanaamini tukitukana ndio tunapata pesa. Hiyo ndio hali halisi, wanibishie, wasibishe hiyo ndio hali halisi. Lakini kwa nini tutukane mbele ya watoto wetu? Kwa nini tutukane mbele ya wazee wetu? 

Kama sanaa ni jambo zuri kwa nini tusitengeneze mfumo mtu akapata chochote bila kutukana? Inawezekana. Kwa hiyo, basi tuufanye uhuru wetu uwe wa kufanya kazi iliyo halali. Sio kitu rahisi maana ni mifumo imeshatengenezwa, unaona? Mfumo ulishatengenezwa na waharibifu fulani ambao wengine wamesha ondoka zao  lakini inatuumiza sisi. 

Kwa hiyo, sisi tuliokuwepo hapa tusiangalie nani aliyeondoka amefanya kosa, tuangalie tuna rekebisha vipi lile kosa  kwa sababu tulikuwepo wakati yeye yupo. Kingine naweza kusema Watanzania wengi hawako huru kufanya shughuli zao za kiuchumi, za kuweza kujipatia kipato chao cha kila siku. Haya tunaingia mwaka wa sitini na moja huu sasa, Watanzania wengi hawana uhuru wa kufanya kazi zao walizoamua kuzifanya.

The Chanzo: Kivipi?

Vitali Maembe: Kwa mfano, mkulima sasa hivi, yeye atakuwa anafanya kazi anamtumikia mtu mwingine kuja kupanga [bei]. Lakini hata kwenye michezo, tunalalamika kila siku kuhusu timu zetu za taifa. Lakini hebu angalia hao wachezaji wetu wana uhuru? Mchezaji amesaini analipwa Sh5,000,000 kwa mwezi, Sh4,000,000 inakwenda kwa mtu aliyepiga blah blah ili asajiliwe pale lakini yeye anakula Sh1,000,000 moja tu. Utasema huyo ni mchezaji huru? Hakuna uhuru hapo. 

Sio hivyo tu, hawa wamachinga wewe unaona wanahangaika, wanataka kufanya biashara lakini hawana uhuru wa kufanya biashara. Wanaambiwa waende wanapotakiwa. Sawa, tunaweka mipango miji, tumemuandalia mazingira gani?  Haya tumempa uhuru wakujitafutia, anapofanya shughuli zake tunamtoa, basi tumjengee mazingira mazuri.  Unajua unapomhudumia machinga kwa kumtengeneza mazingira mazuri ya kibiashara unajihudumia pia wewe kwenye kupata eneo zuri la kununua bidhaa zako. Unapo mtupa mbali kule basi jua na wanajamii unawatupa mbali, kwa hiyo ule uhuru haupo. 

Daktari je? Anayeletewa mgonjwa hospitali, mgonjwa anafika ana hali mbaya na yeye anataka kumuhudumia   lakini hakuna vifaa tiba, unafikiri daktari atakuwa huru kweli kumuhudumia? Kwanza atatukanwa kwa kosa lisilo la kwake, manesi wanatukanwa kila siku, nesi anapokwambia ukalete ndoo, ukalete gloves, ukalete nini sijui sio kwamba anapenda. Sisi [wananchi] tunalalmika tunaona kama anatudhulumu kumbe kweli pale vile vifaa havipo. 

Kwa hiyo, wataishia kupata matusi, hawapo huru kazini, hawapo huru nyumbani hasa kina mama. Nyumbani ni mtumwa, kazini ni mtumwa. Afadhali ya baba yeye akirudi nyumbani anakuwa mbabe akiwa kazini anakuwa mtumwa na yeye hasira zake anazirudishia huku [nyumbani kwa familia yake]. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *