Simulizi ya Kijana Mlemavu Mwenye Ndoto za Kuwa Rubani

Augustino Ilomo hana uwezo wa kuongea na baadhi ya viungo vyake vya mwili havifanyi kazi. Amehitimu kidato cha nne mwaka huu akiwa na matumaini ya kufaulu kwenda kidato cha sita.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Pamoja na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha kwamba wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum wanawafichua watoto hao na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao za msingi kama vile elimu, uhalisia kwenye jamii unaonesha bado muamko wa kufanya hivyo ni mdogo sana miongoni mwa wazazi.

Wadau wamekuwa wakiwahimiza wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum wawatoe watoto hao, wakisema kwamba ulemavu siyo kikwazo cha mtoto kushindwa kujiendeleza kimasomo na kufanikisha ndoto zake za kimaisha. Wakati wako wazazi ambao wanaendelea kuwaficha watoto wao, wapo pia wale ambao somo hilo limewaingia na kuchukua juhudi za kuhakikisha kwamba watoto wao wenye mahitaji maalum wanapata fursa ya masomo.

Moja kati ya familia hizi ni familia ya Faraja Kambanyuma na  Godlove Ilomo inayopatikana Tabata, Dar es Salaam, ambayo imepambana kumpatia kijana wao mwenye mahitaji maalum Augustino Ilomo elimu mpaka kufikia kuhitimu kidato cha nne mwaka huu wa 2021 kutoka Shule ya Sekondari ya Kimanga.

Augustino ni kijana mwenye mahitaji maalumu ambaye hana uwezo wa kuongea lakini pia viungo vyake vya mwili havina uwezo wa kufanya kazi. Augustino, 22, alizaliwa na hali hii lakini kwa kipindi chote cha uhai wake hali hiyo haijamkatisha tamaa ya kuendelea kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani. 

Changamoto wakati wa uzazi

Faraja Kambanyuma ni mama mzazi wa Agustino Ilomo aliyeieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalum  kwamba mwanae huyo ambaye ni wa kwanza katika uzao wake wa watoto watatu alipata changamoto wakati wa kuzaliwa kutokana na uchungu uliochukua muda mrefu hali iliyomuathiri viungo vyake vya mwili. Kambanyuma anaeleza kwamba aligundua kwamba kijana wake hayuko sawa katika hatua za mwanzo za ukuaji wake kwani alikuwa tofauti na watoto wengine wa rika lake. 

Kwa mfano, Kambanyuma anaeleza kwamba kulikuwa na baadhi ya vitu ambavyo Agustino alikuwa hawezi kuvifanya. “Kwa kipindi hicho tulihisi labda kwa sababu ya umbo la unene alilokuwa nalo,” anasema mama huyo. “Ukimbeba mtoto shingo inakaa upande, ukimkalisha hawezi kukaa, ukimpa kitu ashike hawezi. Jambo lililotufanya tutambue kuwa mtoto wangu anachangamoto ya ulemavu.”

Pamoja na hali ya kuwa ni mtoto mwenye mahitaji maalumu, familia yake ilihakikisha Augustino anapata moja kati ya haki yake ya msingi ambayo ni elimu. Licha ya kuchelewa kidogo kuanza shule kutokana na changamoto mbalimbali, Augustino alifanikiwa kuanza shule katika ngazi ya awali na mpaka kufikia mwaka huu wa 2021 amefanikiwa kuhitimu elimu ya kidato cha nne huku akiwa na matumaini makubwa ya kufaulu na kuendelea na kidato cha tano. 

Akiongea na The Chanzo hapo hapo nyumbani kwa wazazi wa Augustino, Sylvia Ruambo ambaye ni mwalimu wa elimu maalumu kwa ajili ya watu wenye changamoto mbalimbali anaeleza kwamba kwa kipindi chote cha elimu ya sekondari amekuwa ndio mtu wa karibu akimsaidia Augustino katika masuala mbalimbali ya kielimu ikiwemo kusoma pamoja kufanya mitihani yake ya ndani na ya kitaifa.

“Haki ya msingi ya mtoto kupata elimu kwanza halafu mengine ndio yafuate,” anasema Ruambo. “Kwa hiyo, mimi kwanza naisimamia haki yake ya huyu mtoto kupata elimu.” 

‘Siwezi kumwacha mwanangu’

Katika familia nyingi zenye watoto wenye mahitaji maalumu mara nyingi huonekana baba kutoroka au kumwachia mama majukumu yote ya malezi na kutunza familia. Lakini kwa upande wa baba mzazi wa Augustino Godlove Ilomo hali na mtazamo wake umekuwa tofauti. Ilomo anakiri kuwa katika vituo vingi walivyokwenda kupata huduma wengi anaokutana nao ni wanawake ndio walioambatana na watoto wao wenye mahitaji maalumu. 

“Jambo kubwa ni mwanangu wa kwanza, siwezi kusema nitachukua jukumu la kumwacha nikamkimbia mke wangu kwa sababu ya mtoto [kuwa na ulemavu],” anasema Ilomo wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika nyumbani kwake Tabata, mnamo Disemba 9, 2021. 

Kwa sasa Augustino anaandika kitabu chake alichokipa jina la The Real Love ambapo ndani yake kinabeba maudhui mbalimbali yanayoihusu jamii zetu. Baadhi ya mambo aliyoieleza The Chanzo kuwa ameyaangazia katika kitabu chake ni suala zima la walemavu kukataliwa katika jamii zetu lakini pia suala la watoto yatima pamoja na changamoto wanazokumbana nazo. Kitabu hicho kinatarajiwa kutoka Januari 2022.

Katika harakati zake za kujipatia elimu, Augustino amekuwa akitumia kifaa maalumu kinachojulikana kama Head Pointer ambacho hukivaa kichwani ili kumwezesha kutumia laptop. Vifaa hivyo vinachangamoto kwani si vya kisasa hivyo kutumia nguvu kubwa wakati wa ufanyaji kazi. 

Faraja Kambanyuma, mama mzazi wa Augustino anatoa wito kwamba ni vyema ifike mahali kila mtu kwenye jamii alichukulie suala la ulemavu kuwa ni la mtu binafsi, kwamba hata ungekuwa ni wewe ungefanyaje, na kuhakikisha kwamba watu wenye mahitaji maalum wanasaidiwa kupata haki zao za msingi na kuishi maisha ya staha.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusu habari hii unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts