The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukimya Siyo Suluhu ya Manyanyaso Katika Ndoa

Wanawake wanapaswa kusimama wao kama wao bila kuwa tegemezi kwa wenza wao. Hiyo itasaidia kupunguza manyanyaso. Na pale wanapokumbana na manyanyaso, watoke mbele waongee, wasikae kimya. 

subscribe to our newsletter!

Kwa jina naitwa Christine Peter.* Ni mzaliwa wa Dodoma lakini nyumbani kabisa ni Singida. Hivi sasa nina umri wa miaka 25 na ni mama wa watoto watatu. Kazi yangu ni mwalimu wa shule ya msingi iliyopo hapa Dodoma.  Shule ya msingi nimesoma katika Shule ya Martin Luther na shule ya  sekondari nimesoma Marian Girls.

Mwaka 2015 nilihitimu elimu ya sekondari na nilifanikiwa kufaulu vizuri kwenda kidato cha tano na cha sita. Kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, sikuweza kuendelea na masomo. Sio kwamba familia ilishindwa kunisomesha, ni kwa sababu mimi nilitamani kusoma kitu kingine ambacho familia hawakukubaliana na mimi.

Nilipenda sana kwenda kusomea famasia lakini nyumbani walitaka niende kitato cha tano na sita na nikisha maliza niende kusomea sheria. Kwa kweli sikutaka kufanya vile. Nilikuwa nataka baada ya kumaliza kidato cha nne nisome chuo cha kati kwa kile kitu ambacho mimi nilikuwa nakipenda.

Lakini ilishindakana. Niliumia sana lakini sikuwa na jinsi. Kwa sababu familia ndivyo ilikuwa imeamua vile. Baada ya kushindwa kuendelea kusoma niliamua kufundisha watu wazima Kiingereza. Nilikuwa na uwezo wa kuongea na kukiandika vizuri. Mbali na kuwa nilikuwa nikipenda sana kusomea famasia ualimu nao nilikuwa nikiupenda.

Kuingia kwenye mahusiano

Wakati naendelea na harakati zangu za kufundisha Kiingereza mwaka 2016 nilikutana na kijana mwenzangu ambaye nilianzisha mahusiano naye. Alikuwa akinipenda sana. Na mimi nilimpenda sana.  Wakati naanzisha mahusiano naye nilikuwa na umri wa miaka 20 tu. Ilikuwa ni mwezi kama wa saba hivi unaenda wa nane mwaka 2016. Alikuwa ni mwanaume ambaye anaangalia mbele  sana na alikuwa akifanya kazi kwenye shirika fulani.

Kipindi hicho cha mahusiano tulibahatika kufanya maendeleo tukiwa pamoja. Tulinunua kiwanja kwa pamoja, tukajenga na nyumba. Ilipokamilika tulianza kuishi pamoja kama mke na mume. Kwa upande wa mwanaume walikuwa wakinitambua ila kwa upande wangu hakuwa anajulikana. Japo myumbani walikuwa wakisikia tu naishi na mtu. Maisha yaliendelea kama kawaida na mwisho wa siku nikapata ujauzito.

Kabla sijajifungua nilianza kupitia wakati mgumu. Alianza kuninyanyasa. Kunipiga na matusi juu. Nakumbuka kipindi hicho wakati napitia manyanyaso hayo mimba yangu ilikuwa ina miezi saba. Anaanza kunitukana na vinafuata vipigo. Alikuwa akinipiga ananipiga haswa. Alikuwa akinipiga na kunisababishia majereha. Ananichukua mwenyewe ananipelekea hospitali kwa ajili ya matibabu. Baada ya hapo ananiomba msamaha  na ninamsamehe maisha yanaendelea kama kawaida.

Msamaha ule nilikuwa nautoa sikuwa naelewa ni akili ilikuwa ya kitoto au ni vipi. Maana nilikuwa najikuta tu namsamehe. Na haikuwa rahisi kwa mimi kumshitaki popote na nyumbani nilikuwa tayari nimeshaharibu. Niliendelea kuvumilia huku vipigo vikiwa vinaendelea na manyanyaso yalizidi.

Juhudi za kujinusuru

Ilipofika wakati wa kujifungua nilijua huenda vipigo havitaendelea lakini vilizidi. Baada ya kuona tena vipigo vinazidi niliamua kutafuta mawasiliano ya ndugu zake kuwaeleza hali ninayoipitia. Kwa hiyo, nikawasiliana nao. Nilivyowasiliana nao wakanitumia nauli nikaenda Dar es Salaam, kuishi ukweni kwa muda. Nilikaa ukweni kwa zaidi ya nusu mwaka baadaye nikasema huenda atakuwa amebadilika. Kwa upande wa  wakwe zangu hawakutaka mimi nirudi lakini mimi nilihimiza ngoja nirudu nyumbani nikaishi na mwenzangu.

Kabla ya kurudi nyumbani walimuita akaja wakamkalisha kikao akawaomba msamaha ndugu zake  na mimi akaniomba msamaha kuwa hatofanya hivyo tena. Lakini aliniahidi kuwa akirudi huku Dodoma atakwenda nyumbani kwetu kutambulika na mimi nikakubali. Lakini haikutokea kama ilavyoahidi.

Unajua ukimpenda mtu uko radhi kufanya chochote kwa ajili yake. Alikuwa ndiye mwanaume wangu wa kwanza kumpenda maishani mwangu. Nilivyoshika mimba ya pili vipigo viliendelea kama kawaida.  Na hapo mimba, ilikuwa na miezi mitatu, ilikuwa ni mwaka 2018. Alinipiga sana na ile mimba ilitoka na kuniacha na maumivu makali sana.

Nilivyokwenda  hospitali wakaniambia kuwa nimepata maambukizi kwenye kizazi. Ikanibidi tena nianze kutibiwa, hiyo ilikuwa ni Juni 2018.  Hivyo nilitumia mwaka mzima kujitibu. Ilipofika mwaka 2019 mwezi wa kwanza baada ya kupona nikaona sasa hii imetosha. Maana kipigo kilikuwa kimezidi na sio kwamba kilikuwa kinapungua kilikuwa kinaongezeka kila siku na vitisho pia.  Kuna siku nilikaa na kuwaza heri nusu shari kuliko shari kamili. Nikabeba vitu vyangu na mwanangu nikaondoka.

Nakumbuka kipindi niko naye nilianza kusoma mtandaoni. Kwa gharama zangu mimi mwenyewe. Bahati nzuri nilibahatika kuhitimu mwezi wa 12 mwaka 2018. Ilikuwa ni stashahada ya ualimu. Kwa hiyo, ilinibidi niende Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua cheti. Kilichosababisha mimi niondoke kwake, nilimuambia kuwa mimi ninataka kwenda Dar es Salaam kwenda kuchukua vyetu vyangu, yeye akanikatilia.

Hapo sasa ndipo nilipofunguka akili kwamba huyu mtu sina muendelezo naye tena wowote huko mbeleni tena. Ni bora niondoke haijalishi sina sehemu ya kukaa maisha ni yale yale. Nilijua kuwa nitapata urahisi wa kila jambo.

Hivyo niliondoka na nilibahatika kukutana na mtu ambaye alinisaidia na kunipatia nauli nikaenda Dar es Salaama kuchukua vyeti vyangu. Na nilivyorudi Dodoma kuna mtu akaniunganishia sehemu nikapata kazi. Nakumbuka nilianza kazi Aprili 2019. Nikaajiriwa kwa muda wa miaka miwili na baada ya hapo nikaweza kumlea mwanangu wa kwanza.

Mwaka huo huo tena nilibeba mimba nyingine. Hiyo ilikuwa ni ya mtu mwingine. Nilijikuta namlea tena mwanangu wa pili kupitia kipato changu kile kile. Maana kwa yule mtoto wa kwanza baba yake alikataa kumleta mtoto wangu akidai ya kwamba atakuwa anamtunza huyu mtoto wa pili niliyezaa na mtu mwingine. Sikutaka kubishana naye kwa sababu sisi sote ni watu wazima.

Sababu za vipigo

Sababu ya yeye kunipiga kwa kweli ni sababu ambazo hazina mashiko hata kidogo. Nakumbuka kuna siku alinipiga sana, alirarua nguo zangu na kunitoa nje na kunidhalilisha mbele ya watu. Sababu ya kufanya hivyo ilikuwa nimemuomba  pesa ya sukari asubuhi. Kisingizio chake alikuwa akisema kwamba kwa nini sikumpa taarifa mapema? Na wakati nilikuwa nimeshampa taarifa wiki mbili kabla.

Kiujumla sababu zake za kunipiga zikuwa hazieleweki. Nakumbuka kuna kipindi nilikuwa nimejifungua nikiwa na wiki mbili alinipiga na sababu ilikuwa hivi. Alimfokea dada wa kazi, nikamuambia huyu ni mtoto mdogo hutakiwi kumfokea kwa namna hiyo. Wakati tunaendelea kubishana nilimnyoonyoshea tu mkono nikamuambia basi baba yaishe. Hapo tulikuwa chumbani tunajiandaa kulala.

Nikashangaa ghafla kama kakumbwa na nini sijui. Akaanza kusema unaninyooshea kidole mimi, unanitukana mimi? Nikamuambia naomba yaishe mimi nilale. Wee, yaani ilikuwa kama vile nimewasha moto alinipiga sana. Mpaka majirani wakasikia kile kilio nilichokuwa nalia. Waliamua kuja kujua kinaendelea nini kwa kilio ambacho walikuwa wakikisikia.

Baada  ya majirani zangu kuja walinikuta nimepigwa sana. Wakamuambia wewe mbona unafanya hivi na huyu ni mzazi wa wiki mbili? Umempiga hivi kwa bahati mbaya akakufia utafanya nini? Hana sababu ya kujibu. Anaulizwa amefanya nini anasema ameninyooshea kidole. Wakamuuliza, amekunyoonyeshea kidole? Ndio sababu ya kumpiga mtu kiasi hiki?

Wakati mwingine anatoka kazini akiwa na stress zake. Ukimuuliza tu ni kosa anaanza kukupiga. Watu wakija kuamulia anasema ana wanaume huyu. Wanamuambia wanatoka wapi na muda wote tunashinda naye hapa. Maana alikuwa haniruhusu hata kwenda dukani. Nikienda saluni anafanya kunifata nyuma.  Na kama nimeamua kwenda mjini saluni  anafanya kunipeleka na sio kwenda mimi mwenyewe.  Na nikimpigia na kumuambia pesa ya kula anafanya kuniletea . Yaani alikuwa ni kama vile ana matatizo ya akili.

Matatizo ya akili

Kwa hiyo, baada ya kuachana naye nimekuja kugundua kwamba alikuwa na matatizo ya akili. Kwa babu nakumbuka wakati nina mimba ya mtoto wa pili alikutana na mimi hapo Nyerere Square nilikuwa nakula mgahawani na mtoto wangu wa kwanza. Alikuja kunisalimia vizuri tu. Baada ya kumaliza kula nikajilipia mwenyewe na hakuwa najua kama ninafanya kazi. Akatuaga anaondoka, kumbe alienda kujificha mahali.

Maana nilimpigia bodaboda anifuate. Baada ya dereva bodaboda kuja akasema aise mama kijacho umechoka kweli nikusaidie pochi. Kwa akili yake moja kwa moja alijua mimi yule ndiye mwanaume ninayeishi naye. Alitoka alipojificha akaanza kumpiga dereva bodaboda. Akanigeukia na mimi akaanza kunipiga. Watu waliokuwepo pale wakaniona na hali ile ya ujauzito wakasema hivi kaka unaakili? Akasema huyu anatembea na mke wangu.

Kitendo kile kiliniumiza sana, ikanibidi niende kumshitaki polisi lakini mwisho wa siku familia yake iliniomba msamaha hivyo nikaachana naye.

Kiukweli manyanyaso yale ambavyo nilikuwa nayapata kutoka kwa mwanaume yule yaliniumiza sana. Na hata kuathirika kisaikolojia. Kimwili niliumia kwa sababu niliachiwa makovu ambayo yalichukua muda mrefu sana kupotea.

Manyanyaso yale pia yaliniumiza kiakili kwa kiasi kikubwa sana. Kitu hicho kimeniathiri hadi leo. Kuna muda nafikiri kabisa ninahitaji msaada wa kisaikolojia aweze kukaa na mimi ili anirudishe kwenye hali yangu ya kawaida. Maana mpaka sasa siamini kitu kinachoitwa ndoa nikiwa na maana ya kwamba wapo wanaume wasiopiga wake zao naona wote ni sawa.

Kwangu mimi naona kila mwanaume yuko hivyo. Haijalishi nimekutana naye leo kwa mara ya kwanza . Yaani mwanaume yeyote anayeonesha hisia kwangu picha inayonijia akilini mwangu ni kwamba hana nia njema na mimi. Hawezi kunipenda kama nilivyo na akanishemu.

Fundisho kwa wengine

Nimeamua kuongea ili iwe fundisho kwa wasichana wa umri wangu wanaopitia changamoto kama zangu na hawawezi kuzisema. Si kila mwanamke ameandikiwa kuolewa na kuishi kwenye ndoa. Kuna wengine tunalazimisha kuolewa kuingia katika ndoa kwamba ndio chaguo lako. Yaani bila huyo huwezi kuishi.

Tukichukulia mimi kwa mfano nimeishi katika maisha ya ndoa lakini sasa hivi naishi mwenyewe na watoto wangu na nina furaha tu. Kwa hiyo,  ile ya kusema kwamba siwezi labda kula, kunywa bila mwanaume hilo jambo halipo kila kitu nafanya mwenyewe.  Wanawake waondoe hiyo dhana, mwanaume si mteremko wako. Siyo njia ya wewe kufanikiwa hapana.

Kwangu mimi sidhani kwamba ukimya ndio suluhisho la kutatua matatizo hasa manyanyaso kwenye mahusiano. Suluhisho ni wewe mwenyewe kuvunja ukimya. Mimi wakati napitia manyanyaso yale sikuwahi kutoa taarifa popote zaidi ya baadhi ya majirani wachache kujua shida yangu. Serikali yangu ya mtaa ilikuwa haijui. Ustawi wa Jamii sikwenda na wala Dawati la Jinsia halikuwa na taarifa zangu.

Wale watu wangu wa karibu ambao walikuwa wanafahamu changamoto yangu, walikuwa wakiniambia vumilia tu yataisha. Hivyo, ukimya siyo suluhisho la matatizo yako. Nilivyoamua kuinuka mimi mwenyewe ndicho kilichokuja kunisaidia.

Kwanza wanapaswa kusimama wao kama wao, wanapaswa kujua wanataka nini katika maisha yao. Utakapo ona huyu mtu siyo chaguo sahihi katika maisha yako basi ni rahisi sana kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi.

*Siyo jina lake halisi.

Kisa hiki amesimuliwa mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma Jackline Kuwanda. Unaweza kumfikia Jackline kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *