Dar es Salaam. Wakiwasilisha mada yao waliyoipa jina la Mabadiliko ya Tabia ya Nchi na Haki ya Mazingira wakati wa Mkutano Mkuu wa 26 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) uliofanyika mjini Morogoro kati ya Disemba 6 na Disemba 7 mwaka huu wa 2021, wasomi katika eneo hilo Theodora Pius na Sabrina Nafisa walibainisha kwamba wakulima wadogo duniani wameendelea kutumika kama mawakala wa masulihisho potofu kwenye mapambano yanayoendelea dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Theodora Pius anafanya kazi na MVIWATA na Sabrina Nafisa ni mtafiti kutoka shirika la African Centre for Biodiversity (ABC), shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utafiti kwenye masuala ya usalama wa chakula na ikolojia ya kilimo barani Afrika.
“Wakulima wadogo kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi ni kama wapo wenyewe au wapo peke yao,” wanasema wasomi hao kwenye mada yao hiyo ambayo The Chanzo inaichapisha hapa kwa urefu wake. “Hivyo katika kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo hili, ni lazima [wakulima wadogo] wawe na mfumo wa uwakilishi kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabia ya nchi.”
Lifuatalo ni wasilisho hilo lililotolewa na Theodora Pius na Sabrina Nafisa kwenye mkutano huo wa MVIWATA:
Jambo moja wapo ambalo linatishia na linasikitisha ni habari za mabadiliko ya tabia ya nchi, na nyinyi [wawakilishi wa vikundi vya wakulima na ushirika] mnayafahamu mabadiliko ya tabia ya nchi, kweli ama si kweli? Mnakumbana na mabadiliko ya tabia ya nchi? Mnakumbana nayo vipi au mmoja atuelezee kwake yeye mabadiliko ya tabia ya nchi yanajitokeza katika sura gani au ni kipi ambacho kimetokea huko anapotokea kinachomfanya aseme kwamba hapa na mimi nakumbana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Yoyote yule ambaye yupo tayari?
“Naitwa Tobias Zakia, natoka kata ya Kinoli, tarafa ya Mkuyuni, wilaya hii ya Morogoro. Kule ninakotoka dalili za mabadiliko ya nchi ni ukame wa mda mrefu, mvua ambazo za vuli kutokuja kwa wakati na kuwezesha wakulima kupanda mazao yao. Miche au mimea ambayo imezoea kupata maji kwa muda wa miezi sita nayo imekauka. Hivyo ndivyo ninavyo jua katika mabadiliko ya tabia ya nchi kule ninakotoka tarafa ya mkuyuni wilaya hii.”
Unaona hichi ambacho amekitaja? [Hiki] ndicho ambacho na sisi wengine tunakishuhudia, hata kama kuna utofauti hakuna tofauti sana katika namna ambavyo tunapitia. Haya ambayo yanaleta mabadiliko ya tabia ya nchi tumesikia kwamba yanaletwa na kitu gani au yanasababishwa na nini? Nani ambae anajua mabadiliko ya tabia ya nchi yanasababishwa na nini kutokana na mapokeo ama kutokana na yeye anavyofahamu?
“Kwa jina naitwa Mendrad Shemziku, natokea Njombe. Mabadiliko ya tabia ya nchi yanatokana na sababu kama mbili au tatu ninazo zifahamu. [Hizi ni pamoja na] wingi wa viwanda, kwa maana [ya] uzalishaji wa hewa ya ukaa kutokana na kuwa na viwanda vingi. Lakini pia ukataji wa misitu, kwa maana ukataji wa miti asili inapotea hivyo inasababisha hiyo changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi.”
Hapo hapo Shemziku, kina nani wanakata misitu?
“Sisi wenyewe wakulima. Ninavyo zungumzia kukata misitu nasema wakulima, lakini tuna wakulima aina mbili. Tuna wakulima wadogo kwa kiasi kidogo akini wakulima wakubwa kwa kiasi kikubwa ndio wanaokata zaidi miti. Nizungumzie mfano sisi wakulima wadogo, hususani mkoa ninao toka mimi [wa] Njombe, ukiona mtu anakata misitu lakini atahakikisha amepanda misitu mara mbili ya ule aliokata. Lakini kuna wawekezaji ambao wanakuja kwenye maeneo yetu wao ni kukata misitu tu bila kupanda. Hao ndio wanatuletea madhara makubwa sana.”
Kwa hiyo, kumbe tunafikiri hakuna wasilisho ambalo litakuwa rahisi kama hili. Ni kwa sababu vingi vipo kwenu [wakulima wadogo] na vingi vinatokea kwenu kama uzoefu. Kwa hiyo, amezungumza pale baba kutoka Kinole na nafikiri ni kitu ambacho kila mtu anakumbana nacho kwamba kwenu nyie mabadiliko ya tabia ya nchi au kwa wakulima wadogo mabadiliko ya tabia ya nchi yanajitokeza kutokana na kubadilika kwa misimu ya mvua, kuna joto limeongezeka sana, unapeleka mbegu shambani hazioti au muda mwingine mazao yanaweza yakaota, yakifikia muda fulani kutokana na kwamba joto limeongezeka sana mazao yanakosa maji kwa muda mrefu na vyanzo vya maji vinakauka. Kwa hiyo, unakosa hata maji ya kwenda kumwagilia au kama umezoea mvua itanyesha, ukizingatia kilimo chetu ni cha kutegemea mvua, mvua inakuwa hainyeshi.
Lakini moja kubwa pia katika namna ambavyo tunaelewa mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na athari zake siku hizi tunashuhudia kwamba mzigo wa kazi, katika kile tulichotoka kuzungumziwa hapo nyuma kwa wanawake umeongezeka zaidi. Kina mama sahizi mnatembea umbali mrefu kutafuta kuni, sindivyo? Maji hayapatikani na mnahitaji maji kufulia, mnahitaji maji kuoshea vyombo, [na] mnahitaji maji kupikia.
Kwa hiyo, tunaona namna ambavyo hiki kinachoitwa mabadiliko ya tabia ya nchi kina jitafsiri katika maisha yetu sisi wakulima wadogo wala hata hatuhitaji mtu kuja kukaa chini kuanza kutuelezea hapa ni hivi au hapa unapitia hatua gani.
Sasa nimeuliza swali lingine ambalo Ziku alijaribu kutuelezea kwamba tunavyosikia sisi mabadiliko ya tabia ya nchi yanasababishwa na mtu gani au na kitu gani? Shemziku amesema ukuwaji wa viwanda. Ndivyo wote ambavyo tuna amini. Jamani, sio kwamba kilimo chetu cha kuchoma choma na kuhama hama kina sababisha mabadiliko ya tabia ya nchi? Hapana au kweli? Kinachangia sawa sasa tukirudi katika misingi hichi ambacho tunakiita mabadiliko ya tabia ya nchi kwa sababu mabadiliko ya tabia ya nchi ni matokeo ya vitu ambavyo vimefanya joto kuongezeka katika uso wa dunia, mvua kuchelewa au kuwa chache ni matokeo ya visababishi fulani, sindivyo? Yaani kuna kitu ambacho kimefanywa matokeo yake ndio haya ambayo sisi tunakumbana nayo.
Dhana ya mabadiliko ya tabia ya nchi
Sasa kimsingi na kiufupi tu suala zima au tunapozungumzia mabadiliko ya tabia ya nchi tunazungumzia mabadiliko ya muda mrefu, yaani yanayopatikana ndani ya muda mrefu au baada ya muda mrefu kutokana na kubadilika katika vitu mbalimbali ambavyo vinapatikana katika mifumo inayotengeneza kitu kinachoitwa tabia ya nchi.
Kwa hiyo, maswala ya mvua, maswala ya joto na vitu vingine vya namna hiyo na kadri ambavyo wengine wanazungumza kwamba wakulima wadogo ni kisababishi kikubwa sana kinachosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi lakini kiuhalisia wakulima wadogo ni wachangiaji wadogo sana wa hayo yanayoitwa mabadiliko ya tabia ya nchi ilihali wao ndio wanaopitia athari kubwa za mabadilio ya tabia ya nchi.
Leo hii mimi ninaeishi mjini mvua ikichelewa kunyesha mimi sijali, nitakacho umia ni joto na joto likizidi kama nina mshahara naenda kutafuta feni, kweli si kweli ? Lakini wewe mvua ikichelewa kunyesha utashindwa kupanda kwa wakati. Mimi mvua ikinyesha nyingi ntatafuta makoti yangu makubwa makubwa nitavaa, nitabadilisha gari kama nilikuwa natembelea magari flani nitatafuta nyingine usafiri nitabadilisha illa wewe mazao yanaondoshwa [na maji].
Hiyo inakuonyesha kwamba sisi kama wakulima wadogo tunaathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kuliko mtu mwingine yoyote wala hakuna mtu ambae anaweza akazungumzia swala la mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake na kuzungumza maumivu au machungu yake kutushinda sisi au sisi tunavyopaswa kufanya.
Sasa mabadiliko ya tabia ya nchi ukiyatazama na yenyewe hayaondoshwi nje na kilichotoka kuzungumzwa hapa au tangia jana. Limezungumzwa swala la mfumo ambao tunao, unahamasisha alichokizungumza Shemziku.
Matumizi ya nishati za mafuta katika viwanda ndio chagizo kubwa la mabadiliko ya tabia ya nchi tunayoyapata kwa sababu unachangia kwa kiasi kikubwa utolewaji wa hewa ya ukaa. Kinachotokea ni kitu kimoja, zinapotoka gesi ya aina tofauti tofauti ambazo zina dondokea katika hilo kundi ambazo zinazuia joto linalotolewa na jua kutoka mwisho wa siku joto katika uso wa dunia linaongezeka, tunaanza kupata misimu ya mvua ambayo haieleweki na vitu vya namna hiyo.
Hapa kuna kitu kimoja ambacho tunapaswa kukiangalia pia kwa kadri ambavyo aina ya mfumo wa uchumi ambao nchi na ulimwengu unachukua ndivyo ambavyo pia mabadiliko ya tabia ya nchi na yenyewe yanachukua kasi kuendana na mfumo huo.
Tunashuhudia uzalishaji umepungua na nyinyi mnasema kila siku zamani ardhi niliyokuwa nalima hekari moja ninapata gunia tano sasa hivi mpaka upate hizo gunia tano unatumia nguvu ya ziada. Lakini pia hatuna maji vijijini, hata katika maeneo kama Kinole ambapo maji yalikuwa yanatiririka muda wote lakini sasa hivi hakuna. Milima ambayo muda wote ilikuwa inatiririsha maji sasa hivi hakuna.
Habari mbaya kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi
Lakini pia tuna mafuriko, tuna vimbunga ambavyo kila siku tunaendelea kushuhudia leo vipo huku, kesho vipo kule. Kuna habari mbaya nyingine ni kwamba tuna mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo hakuna mvua, joto limezidi lakini kuna nguvu kubwa ya soko ambayo inazungumzwa kuwa yenyewe ndio inaweza kuleta suluhu.
Leo hii wakulima wa Njombe wanaambiwa wapande miti ili kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi. Wakulima wa Njombe wanapelekewa mipango ya kwamba panda miti halafu mimi ninae miliki kiwanda kutoka Uingereza nitakuwa nakulipa kwa sababu kwa kukulipa mimi naruhusiwa kuendelea kuzalisha na kutoa gesi ukaa na wewe utaendelea kunipandia mti.
Lakini pia habari nyingine mbaya ni kwamba kuna siasa kubwa katika swala zima la mabadiliko ya tabia ya nchi ambazo hazilengi kuleta suluhu. Juzi tulisikia kulikuwa na mkutano unafanyika sijui wa maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi na Rais [Samia Suluhu Hassan] alienda kuhudhuria tulisikia? Tulifatilia? Lakini ulikuwa hautuhusu kwa sababu ni sehemu ya hizo siasa ambazo hazileti suluhu.
Habari nyingine mbaya katika haya yanayoendelea ya mabadiliko ya tabia ya nchi kwa wakulima, na hususani wanawake, [ni kwamba] wameendelea kutumika sana kama mawakala wa masulihisho potofu. Kwa hiyo, kwa nguvu yao kubwa na kwa kuwa ni wengi katika uzalishaji wanatengeneza muwe mawakala [wa] masuluhisho potofu.
Kwa upande wa habari njema ni kwamba wakulima wadogo wa Tanzania na wa ulimwengu mzima wana masuluhisho yao ya kweli dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi lakini masuluhisho yao. Sasa waliopo katika mifumo ya kutengeneza sera wanayaelewa au wanawasikiliza wakulima wadogo?
Suala la mabadiliko ya tabia ya nchi ni suala la kimfumo
Ukitaka kufahamu suala hili la mabadiliko ya tabia ya nchi ni suala la kimfumo, angalia mfano ufuatao. Wakulima tumesema ni kama asilimia 75-80 ya nguvu kazi ya taifa, si ndivyo? Kuna utafiti mmoja ulifanywa na La Via Campesina [ambalo ni vuguvugu la wakulima wadogo la kimataifa] katika nchi ambazo zinatengeneza Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika. Utafiti ulikuwa unajaribu kuangalia namna gani hizi nchi, ikiwemo Tanzania, zina sera au zimejipanga katika maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika matokeo ya utafiti huo ilionekana kwamba wakulima wadogo ni takribani asilimia 80 ya nguvu kazi katika hizi nchi zote.
Juu ya hilo ni kwamba wakulima wadogo, ambao wengi wao wanaishi vijijini, wanatengeneza takribani asilimia 90 ya masikini wote wa hizi nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika, ikiwemo Tanzania, Kenya , Uganda , Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini. Kwa hiyo, wakulima wadogo ndio wengi na ndio masikini. Asilimia 90 ya masikini wa hii sehemu wanatokea vijijini na ni wakulima wadogo.
Utafiti huo ulibaini kwamba hawa wakulima wadogo wanakumbana na athari kubwa za mabadiliko ya tabia ya nchi ila si Serikali zao au mipango ya kidunia ina njia ilioziweka kuwezesha wao wakabiliane na hayo mabadiliko ya tabia ya nchi. Katika hizi nchi zote hakuna nchi yenye sera ambayo inatazama maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoathiri hawa wazalishaji wadogo.
Kwa hiyo, kwa ufupi tu, kwa kusema hivyo kwamba wakulima wadogo kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi ni kama wapo wenyewe au wapo peke yao. Hivyo katika kuhakikisha kwamba ni lazima wawe na mfumo wa uwakilishi kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabia ya nchi ndio ikaibuka au iliibuka dhana ya haki mazingira kama ilivyoelezewa jana.
Dhana ya haki mazingira
Dhana ya haki mazingira kimsingi ni dhana ambayo inajaribu kuzungumza na kuwaelezea watu kwamba kuna mabadiliko ya tabia ya nchi, wala sio siri wala si kitu cha kuficha, sio kwa wakulima wadogo sio kisababishi kikubwa cha mabadiliko ya hali ya nchi.
Dhana hii inazungumzia kwamba wakulima wadogo wana masuluhishi ya kweli ya mabadiliko ya tabia ya nchi na katika mapambano ya tabia ya nchi ni mapambano ya kimfumo, sio tu mapambano ya kuja na kuwekeana kampeni za tupande miti tuache kuhama hama, tuache kuchoma na kuondoka , tuache sijui kufanya nini. La hasha! Bali tunavyozungumzia haki mazingira tunahakikisha kwamba yule au wale ambao ni kisababishi cha kwanza cha mabadiliko ya tabia ya nchi wanachukua hatua kubwa kuhakikisha kwamba hawawi sehemu ya kupelekea mabadiliko ya tabia ya nchi.
Sisi ni sehemu ndogo sana ya shida ambayo tunayo. Leo hii joto linaloongezeka, mvua zinazopungua, sisi sio sehemu ya usababishi huo mkubwa. Sisi wakulima wadogo, wachungaji na majina mengine tuliyopewa eti kwamba hatuelewi kilimo lakini ndio tunasaidia kuipoza hii dunia kwa kutumia mifumo yetu kama kilimo ikologia, kwa kutumia mbegu zetu na kadhalika. Tunatumia hizo kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi tofauti na wale ambao wanachangia na kuongeza hiyo athari kubwa ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
Hapo juu tumesema kwa uchache kuhusu mazungumzo ya mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo viongozi wetu walihudhuria. Nafikiri ni vizuri tukaelewa mifumo ambayo ni kandamizi, mifumo nyonyaji na tunapaswa tuelewe kwamba mabadiliko ya tabia ya nchi yamejikita katika mifumo ambayo ni nyonyaji, ambayo inasababisha mmomonyoko sayari yetu dunia, watu na tamaduni.
Mifumo ya ukandamizaji
Muendelezo wa mifumo ya ukandamizaji tunaweza kuona katika mijadala hiyo ya kimataifa ambapo kuna maamuzi mengi ambayo yanafanyika katika ngazi za kimataifa ambazo sisi tunazichukua moja kwa moja kutokana na mipango au mikakati ambayo inaaamuliwa kule juu na Marais tofauti na nchi mbalimbali lakini unakuta maamuzi haya yanaturudisha nyuma sana sana kwenye maswala ya usawa, kwenye maswala ya kupunguza umasikini na pia hata kwenye maswala ya haki ya mazingira.
Unakuta kwamba kwenye hii mikutano ambayo inafanyika kuna makubaliano ambayo yanatekwa na nchi tajiri zilizoendelea. Maamuzi ambayo yamejikita zaidi kwenye kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa lakini bila ya kutoa fidia kwa nchi zinazoendelea. Wao kwa muda mrefu wamekuwa na mfumo wa viwanda na wanaendeleza mfumo huo wa viwanda na wanazalisha zaidi hewa ukaa tofauti na nchi ambazo zinaendelea kama Tanzania na nchi nyingine.
Unakuta sasa makubaliano yanayoafikiwa katika mazungumzo hayo hayaleti suluhu moja kwa moja juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi au mmomonyoko wa mazingira. Hapa tatizo kubwa ni kwamba nchi zinazoendelea kama sisi Tanzania na wengine tumeonyesha au wameonyesha kuvunjwa moyo kwa kushindwa kufikiwa kwa kiasi cha pesa kilicholengwa kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi zao na kinacho sikitisha ni kwamba tunagawana majukumu.
Kwa hiyo, nchi ambazo zinaendelea, na nchi ambazo zimeshaendelea tunagawana majukumu katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa. Utakuta nchi ambazo ni tajiri wamekuwa wakizalisha hewa ukaa kwa muda mrefu sana na nchi ambazo zinaendelea, ikiwemo Tanzania, ambazo tunazalisha kiasi kidogo sana cha hewa ya ukaa, tunaishia kugawana majukumu sawa sawa ya kupunguza hewa ya ukaa. Kitu ambacho sio sawa na pia hii inafanyika bila kujali majukumu ya kihistoria ya nchi ambazo zilizoendelea na matumizi yao ya anga tangia zama za kabla ya uvumbuzi wa viwanda.
Kwa kufanya hivyo wanaepuka kupunguza uzalishaji huu wa gesi ya ukaa na unakuta wanahamasisha katika makubaliano au maridhiano kuwa wao wataendelea kuzalisha hewa ya ukaa na kuahidi wataihamisha hiyo hewa ya ukaa kwenda kwenye maeneo mengine kwenye misitu au kwenye bahari kupitia biashara ya hewa ukaa.
Sasa changamoto ya kuhamisha hewa ukaa ni kwamba wao waendelee kuchafua hewa lakini kwa nchi ambazo zinaendelea, kwa sababu bado tuna maeneo, tuna mazingira salama, tuna misitu, tuna bahari, ile hewa ije ihamishiwe huku kwenye yale maeneo ambayo unakuta miradi kama ya kupanda miti au miradi ambayo watu wanalipwa kutokana na kupanda miti.
Mkataba wa kimataifa unaozungumzia maswala ya mabadiliko ya tabia ya nchi unaeleza kuwa uchafuzi mkubwa unafanywa na nchi tajiri, au unazalishwa na nchi tajiri, lakini nchi hizo wanapinga hii kauli na hawataki kauli kama hii itokee kwenye majadiliano yoyote yale. Kwa nchi ambazo zinaendelea, maswala ya tabia ya nchi sio tu kuhusu tabia ya nchi lakini ni kuhusu maisha ya watu kwa sababu sisi, wakulima wadogo, ndio tunaishi yale maisha halisi.
Mabadiliko ya tabia ya nchi ni kuhusu maendeleo endelevu
Kwetu sisi mabadiliko ya tabia ya nchi ni kuhusu maendeleo endelevu na kupunguza umasikini. Sisi kama nchi ambazo zinaendelea hatupaswi kukubali kurubuniwa na mifumo ya kikoloni au ukandamizaji inayotoa suluhu ya mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia mambo kama biashara ya hewa ukaa.
Nasema hivi kwa sababu nchi ambazo zinaendelea wanaweka masharti, wanakuwa na masharti ikiwemo masharti yaliyo jikita kwenye misaada ya kifedha na teknolojia. Kwa hiyo, unakuta suluhu zao ni kwamba tutaendelea kutoa hela, tutakuja na mbinu za teknolojia ambapo inapelekea mazingira ya utegemezi.
Kwa hiyo, mwisho wa siku wewe utapanda miti ili kuweza kunyonya ile hewa ukaa ukitegemea nchi tajiri, au kampuni kutoka nchi tajiri, ije ikulipe. Mwisho wa siku tunaendeleza utegemezi. Sasa tusipokuwa na suluhu za uhakika mwisho wa siku tutajikuta tunaendeleza utegemezi kuanzia kwenye mbegu na mbolea za viwandani.
Ndio maana katika hili la utegemezi tuliona suluhu ni kuhakikisha wakulima wajengewe uwezo wazalishe mbegu wenyewe, wazalishe mbolea pia. Kama tusipofanya hivyo tutaendelea kuwa tegemezi mpaka lini?
Kwa hiyo, suluhu kama kuhamisha hewa ya ukaa kwenda maeneo mengine katika mazingira, ikiwemo misitu na bahari, nafikiri inapaswa kuwe na angalizo kubwa hasa kwa jamii za asili ambazo wao wanategemea hayo maeneo kwa ajili maisha yao.
Kwenye suala la vuguvugu la haki mazingira ambalo tumelitaja huko juu ambalo linahimiza kujitoa kimaadili hizi nchi ambazo zimeendelea, vuguvugu hili pia linadai suluhu ambazo ni za ukweli na uhakika za mabadiliko ya tabia ya nchi ambazo sio za kinyonyaji wala kikandamizaji.
Suluhu ambazo zinaendelea kulinda haki na maslahi ya wananchi na wale ambao wanaathirika zaidi na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Ni muhimu sana tusiache kujadili haya kama MVIWATA ili kuhakikisha suluhu za uhakika za mabadiliko ya tabia ya nchi zinafikiwa na sio suluhu ambazo zitaendelea kutukandamiza au kukandamiza wakulima wadogo kwenye nchi zetu.