The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Walalamikia Muamko Mdogo wa Kuandika Habari za Haki za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza

Waandishi na wahariri katika vyombo vingi vya habari nchini wanadaiwa kuwa na muamko mdogo kwenye kuandika habari zinazohusiana na haki za kiraia na uhuru wa kujieleza.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) imesema kwamba kuna muamko mdogo sana miongoni mwa waandishi na wahariri katika vyombo vingi vya habari nchini kwenye kuandika habari zinazohusiana na haki za kiraia na uhuru wa kujieleza.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni jijini hapa na Afisa Habari na Utafiti wa shirika hilo Neema Kasabuliro pembezoni mwa mafunzo yaliyolenga kwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ili waweze kuandika habari kuhusu haki za kiraia na uhuru wa kuijeleza.

“Lengo letu hasa ni kuwajengea uwezo  [waandishi wa habari] wa kuweza kutengeneza vipindi vingi ambavyo vitakuwa vinaongelea masuala  ya haki ya kiraia na uhuru wa kujieleza kwenye vituo vyao na maeneo mbalimbali ambapo vituo hivi vinapatikana,” Kasabuliro aliieleza The Chanzo wakati wa mahojiano naye.

Kasabuliro pia amekiri kuwepo kwa mabadiliko chanya kwenye suala zima la uhuru wa vyombo vya habari nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike hatamu za uongozi wa nchi, akisema hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa viwango vya maudhui vya vyombo vya habari husika.

“Miezi ya nyuma maudhui mengi yalikuwa yanafanana; kwenye vyombo vingi vya habari kulikuwa hakuna utofauti wa taarifa,” anasema Kasabuliro. “Kwa mfano, ukichukua gazeti hili unajua kabisa gazeti hili na hili utakuta kila kitu kipo sawa. Lakini sasa hivi angalau kuna utofauti, walau wapo wa kukosoa na kutoa mapendekezo.”

Wakielezea changamoto wanazokutana nazo katika kazi zao, baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo waliieleza The Chanzo kwamba licha ya uwepo wa unafuu katika namna vyombo vya habari na waandishi wa habari wanavyofanya kazi zao nchini, bado kuna changamoto zinazohusiana na uhuru wa kiuhariri.

Kassim Chikwenda, mwandishi wa habari na mtetezi wa haki za binadamu katika masuala ya jinsia kutoka Mtwara, analalamikia uwepo wa hofu iliyopo ndani ya vyombo vingi vya habari, ambayo anadai imesababisha waandishi wa habari kushindwa kufanya  kazi kwa weledi.

 

“Hatujui kesho yetu kwa sababu shughuli zako hufanyi kwa uhuru,” anasema Chikwenda. “Hofu imepelekea kuona mwandishi akifikwa na changamoto tunaona kwamba hazituhusu, hii yote imejengeka na hofu. Nafikiri haya mafunzo yanatujengea uwezo wa kujua kwamba kuna vitu viko hivi na namna ya kuepukana na changamoto hizo.”

Kwa upande wake, Adela Madyane kutoka kituo cha redio Buha kilichopo mkoani Kigoma anasema changamoto kubwa anayokabiliana nayo yeye kama mwandishi wa habari ni kupata taarifa kutoka kwa mamlaka husika pale anapofuatilia habari fulani.

“Mtu unaweza kuandika taarifa yake vizuri, pale unapotaka kwenda kuweka mizania kwa wale ambao ndio wahusika wakuu wanakuwa hawako tayari kutoa taarifa zile ambazo unazihitaji,” anasema Adela. “Unaweza ukaandika mpaka barua ukirudi kufuatilia wanakupiga chenga taarifa yako inakufa na inaishia hapo.”

Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa waandishi wa redio za kijamii yalilenga kuonesha jinsi gani uhuru wa kujieleza una umuhimu katika maendeleo, na jinsi gani uhuru wa kushiriki bila hofu katika masuala ya kiuchumi na kijamii ulivyo muhimu kwa taifa.

Pia, yalilenga kuwaonesha waandishi wa habari ni jinsi gani vyombo vya habari kama vikiwa huru vinaweza kufanya kazi zake na kusaidia maendeleo katika taifa.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma. Anapatikana kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *