The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Marekani Yadaiwa Kukwepesha Mashtaka Dhidi ya Afisa Wake Aliyeua Mtanzania Kwenye Ajali ya Barabarani

Ni John Peterson, Afisa wa US Peace Corps anayedaiwa kumuua raia wa Tanzania Rabia Issa kwenye ajali ya barabarani Msasani, Dar es Salaam, mwaka 2019 na kukimbizwa nchini Marekani na Serikali yake ili kukwepa mashtaka dhidi yake nchini Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania unadaiwa kukwepesha mashtaka dhidi ya raia wa Marekani John Peterson, 67, anayedaiwa kuhusika na mauaji ya raia mmoja wa Tanzania Rabia Issa na kujeruhi Watanzania wengine wawili katika mfululizo wa ajali za barabarani ambazo Peterson alisababisha mnamo mwaka 2019 katika maeneo ya Msasani, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Marekani la USA Today, Peterson, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi kama Mkurugenzi wa Usimamizi na Operesheni wa Shirika la Marekani la kutoa misaada ya matibabu US Peace Corps, alisababisha ajali hizo mnamo majira ya saa 11 alfajiri, Agosti 24, 2019.

Inadaiwa kwamba Peterson, akiwa anaendesha gari aina ya Toyota RAV4 yenye plate namba za ubalozi, alikuwa akimrejesha dada anayefanya biashara ya ngono, maarufu kama dada poa, eneo alilomchukulia majira ya saa 11 alfajiri ambapo alimgonga mtu aliyekuwa amesimama mbembezoni mwa barabara. Ingawaje mtu huyo alipata majeraha mengi lakini hayakuwa yenye kuhatarisha maisha yake.

Baada ya Peterson kusababisha ajali hiyo, hakusimama na kuamua kuendelea na safari yake, kitu kilichoibua hasira kwa watu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo, wakiwemo madereva wa bodaboda, ambao waliamua kumfukuzia kwa nyuma. Katika kukimbizana huko, ndipo Peterson alipokunja kona na kumgonga Rabia Issa, 47, anayefanya biashara ya kuuza mihogo ya kukaanga, aliyekuwa akiandaa eneo lake la biashara.

Hata baada ya kumgonga Rabia, mama wa watoto watatu, Peterson hakusimama na aliendelea kuendesha gari lake, akimjeruhi mpita njia mwengine, mpaka pale gari lake lilipogonga nguzo na polisi kuja kumkamata. Wakati polisi wanakwenda kwenye eneo la tukio alipogongwa Rabia, mama huyo tayari alikuwa ameshafariki dunia.

“Tulipofika kwenye eneo la tukio, tulikuta kundi kubwa la watu likiangalia mwili wa dada yetu akiwa tayari amepoteza maisha, huku mwili wake ukiwa umezungushiwa kitambaa na ukiwa umelazwa nchini,” Hadija Issa, dada yake Rabia, amenukuliwa na USA Today akisema.

Lakini ndani ya masaa machache ya tukio hilo kutokea, maafisa kutoka Ubalozi wa Marekani nchini na ofisi za US Peace Corps wanadaiwa kumkimbiza Peterson uwanja wa ndege, ambapo alichukua ndege na kukimbilia Marekani, uchunguzi wa USA Today umebaini.

Mamlaka za Tanzania, kwa hiyo, zilishindwa kumfungulia mashtaka Peterson huku na mamlaka za Marekani pia zikigoma kufanya hivyo kwa kisingizio cha “kukosa jurisdiction [mamlaka ya kisheria]” ya kufanya hivyo.

Peterson aliendelea kuwa mfanyakazi wa US Peace Corps kwa zaidi ya miezi 18 mpaka alipoamua kujiuzulu mnamo Februari 2020. Kwa mujibu wa uchunguzi wa USA Today, mshahara wa Peterson pia uliongezeka kufikia $155,000 kwa mwaka, ongezeko la takriban $20,000 ukilinganisha na mshahara aliokuwa akipokea alipokuwa Tanzania ambao ni $135,000.

Familia ya Rabia Issa imeiambia USA Today kwamba ilipokea Shilingi milioni 20 baada ya kifo cha mpendwa wao, pesa ambazo zilitoka kwenye kampuni ya bima iliyokuwa ikimuhudumia Peterson.

Carol Spahn ni Mkurugenzi Mtendaji wa US Peace Corps ambaye licha ya kukataa kujibu maswali mahususi kutoka kwa USA Today aliliambia gazeti hilo kwamba “kifo cha Rabia kilivunja moyo wangu na kunishtua.”

Spahn aliongeza kwa kusema: “Vitendo vya mtu huyu [Peterson] vinaenda kinyume kabisa na tunu za US Peace Corps, na tunalaani vikali [vitendo hivyo].”

Scott Anderson, mwanadiplomasia mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ameieleza USA Today kwamba Peterson bado anaweza kuwajibishwa kwa uhalifu alioufanya nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Anderson, mamlaka za Tanzania zinaweza kumshitaki Peterson bila ya yeye mwenyewe kuwepo na kutoa agizo la kukamatwa kwake kwa kushirikiana na Interpol. Wakati Marekani inaweza kukataa ombi la kumsafirisha Peterson kuja Tanzania kukabiliana na mashtaka dhidi yake, Peterson anaweza kuzuiliwa kusafiri kimataifa kwa kuhofia kukamatwa.

Peace Corps wanahistoria ndefu nchini Tanzania, huku taifa hilo la Afrika Mashariki likiwa moja kati ya nchi mbili za kwanza kushiriki kwenye programu hiyo ilipoanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy mnamo mwaka 1961.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *