Mara kadhaa tumekuwa tukipata taarifa za kuuwawa kwa askari polisi wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa kupambana na uhalifu. Hata hivyo, ni mara chache sana kusikia askari wa cheo cha juu akiwa ameuwawa kwani mara nyingi askari hawa huwa hawaendi mstari wa mbele wa mapambano na badala yake huandaa mpango kazi na kutoa maelekezo kwa askari wa ngazi za chini jinsi ya kuendesha zoezi la ukamataji.
Hali ilikuwa ni tofauti siku ya Jumapili, Oktoba 14, jijini Mwanza ambapo nchi ilitikiswa kufuatia habari za kuuwawa kwa Kamanda wa Polisi wa Mwanza Liberatus Barlow Lyimo.
Mazingira ya kifo chake yaliibua mjadala mpana baada ya kusemekana kwamba Lyimo aliuwawa usiku wa manane huku wengi wakihoji iliwezekana vipi kamanda mkubwa wa polisi anaranda mitaani usiku wakati ana askari wa chini ambao ndio walipaswa kuwa kwenye doria?
Mtazamo wangu ni kwamba watu waliojenga hoja hii hawakuwa wakimjua vizuri Kamanda Lyimo kwani alikuwa na desturi ya kupiga doria peke yake usiku kuhakikisha usalama wa raia wa Mwanza na mali zao unaimarishwa.
Minong’ono juu ya wanaowezekana kuhusika na tukio hili ilikuwa mingi. Wengine walijaribu kugusia kuhusu mfanano wa tukio hili na tukio la kushambuliwa kwa risasi (hakuuwawa) wa Afisa Uhamiaji mmoja wiki chache kabla ya tukio hili, na wengine walikumbushia jinsi mkuu wa kituo Mwanza alivyoshambuliwa na kuuwawa kwa risasi jijini humo.
Lawama zamwangukia mwalimu wa shule
Wengine walianza kumnyooshea vidole mwanamke mwalimu wa shule ya msingi aitwaye Dorcas Moses ambaye ndiye aliyedaiwa kuwa na Kamanda Lyimo usiku ule wa tukio. Pia gazeti la Mwananchi liliwahi kuripoti kunaswa kwa ujumbe mfupi kutoka kwenye simu ya Dorcas ukimweka karibu na waliokuwa nyuma ya utekelezaji wa mauaji haya.
Makala haya hayatajikita katika kujadili mambo ya minong’ono bali itajielekeza moja kwa moja kuelezea jinsi Jeshi la Polisi lilivyotegua kitendawili hiki.
Evarist Ndikilo, akiwa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati tukio linatokea, alitoa taarifa kwamba Kamanda Lyimo aliondoka nyumbani kwake siku ya Jumamosi na kwenda kenye kikao cha mtoto wa dada yake aitwaye Sembeli Mareto, kilichofanyika katika hoteli ya Florida, maeneo ya Kitangiri, jijini Mwanza.
Kikao kilimalizika kati ya saa tano au sita usiku wa Oktoba 13, 2012. Inadaiwa kwamba Lyimo aliondoka baada ya kikao kumalizika akiendesha gari lake Toyota Hilux Double Cabin na alipofika kituo cha kona ya Bwiru, alikutana na mwalimu Dorcas Moses na kumpa lift na kumpekeka mpaka nyumbani kwake.
Wakati Lyimo akimpatia Dorcas lift, upande mwingine wa jiji la Mwanza, walikutana vijana sita maeneo ya Nyanshana, Jeshini (watatu baina yao walikutana Gereza la Butimba ambako walifungwa kwa makosa kadhaa na kutoka, wengine kwa kumaliza vifungo na wengine kwa kushinda rufaa zao).
Siku hiyo hiyo usiku saa mbili wakakutana Shule ya Msingi Mbugani, Nyakabungo huku wale watatu waliokutana Gereza la Butimba wakiwa na bunduki aina ya Shotgun Greener iliyokatwa yenye namba 13006 waliyokuwa wameipora mpaka wa Sirali. Wakakubaliana kwenda kupora maeneo ya Kihesa, Kilimahewa na Nyamanoro.
Uporaji
Wakiwa wameanza kazi yao ya uporaji, wakapita grocery moja eneo la Lumala ambako walipora simu tisa na pesa. Maeneo ya Kiseke wakampora simu moja mwanamke aliyeshuka kwenye daladala na maeneo ya Nyamanoro, maarufu kwa jina la “kwa mama mzungu mhaya” wakapora simu nne na pesa. Kisha wakakubaliana kwenda Kitangiri Makaburini kuona wameingiza kiasi gani.
Baada ya kufanya mahesabu, vijana hawa walijikuta na simu 14 na kiasi cha Shilingi 50,000. Vijana hawa wakakubaliana wapite tena Kitangiri mpaka Isamilo. Muda wote huu baadhi ya waporaji hawa walikuwa wamevaa nguo zinazowatambulisha kama Polisi Jamii.
Wakati haya yakitokea, mida ya kama saa saba au nane usiku huo huo, Kamanda Lyimo alishamfikisha mwalimu Dorcas nje ya uzio wa geti lake na alishapiga honi ili afunguliwe geti. Ni muhimu tukakumbuka kwamba lift ilitolewa majira ya saa kabla au baada ya saa tano. Muda ambao Dorcas alikuwa anasubiri geti lifunguliwe ndio muda huo huo ambao wale vijana waporaji walikuwa wanapita njia hiyo na walipoona gari imewasha mwanga mkali kuwamulika wakaliwashia tochi kumpa dereva ishara azime taa za gari zisiwamulike. Bahati mbaya dereva hakuzima taa. Wakaamua kumfata.
Wale vijana wakamvaa dereva wa gari ile, ambaye alikuwa ni Kamanda Lyimo, na kumuuliza kwa nini anawamulika ambapo afisa huyo wa Jeshi la Polisi aliwauliza wale vijana ni kina nani, hasa baada ya kuona wamevaa nguo za Polisi Jamii.
Kamanda Lyimo alipotaka kuwasha radio yake ya upepo ndipo mmoja wa vijana wale aliyejulikana kama Peter Muganyizi akampiga risasi ya bega Kamanda Lyimo ikatokea shingoni na kumuua pale pale, mauaji yaliyoshuhudiwa na mtoto wa dada yake Dorcas aitwaye Keny Rogers, 17, ambaye alishakwenda kufungua geti.
Vijana wale wakaanza kulaumiana kwa nini mwenzao kafanya vile lakini wakaishia kuiba radio call aliyokuwanayo Kamanda Lyimo na kuondoka mpaka kesho yake walipokuja kubaini kuwa waliyemuua ni Kamanda wa Polisi wa Mwanza.
Upelelezi wa polisi
Makachero wa polisi walimshikilia mwalimu Dorcas kwa ajili ya maelezo. Pia, mwenye grocery ya Lumala alienda kuripoti juu ya kuvamiwa jana yake na kuporwa fedha na simu ambapo mmoja wa wateja walioporwa simu alikuwa ni mfanyakazi wa kampuni ya simu ya Vodacom na akawahakikishia polisi kuwa ataibani mahali simu yake ilipo hata ikibadiliswa line. Dada wa mfanyakazi huyu wa Vodacom alifanya mahojiano na mimi na kuthibitisha.
Yule mfanyakazi wa Vodacom, alibaini simu yake inatumiwa kwa namba ya Tigo ikisoma maeneo ya Tabata, Dar es Salaam. Polisi Mwanza wakawasiliana na wenzao wa Dar es Salaam na kumpata mtumiaji wa simu ile ambaye alikuwa ni mpenzi wa jambazi Chacha Waikena ambaye alikuwepo siku ya tukio la mauaji ya Kamanda Lyimo na ndiye alikuwa wa kwanza kukimbilia Dar es Salaam akifatiwa na wenzake kina Peter Muganyizi na Magige Mwita. Wote walifikia eneo la Gongo la Mboto na baadaye Muganyizi akahamia Vingunguti na kukaa nyumba ya wageni ya Kaloreti akipanga chumba namba tano.
Ili kujikimu, na kwa kuwa walikimbilia Dar es Salaam wakiwa na bunduki yao ya Shotgun Greener, wakaamua kufanya tena tukio la ujambazi ili waweze kupora silaha nyingine itakayowasaidia kwenye harakati zao za kijambazi. Chacha aliwaunganisha Muganyizi na Magige kwa jamaa aitwaye Bunganzi Edward ambaye aliwaelekeza waende sehemu kulikokuwa na mlinzi mwenye bunduki ili waende wakaipore, akidai yeye hakuweza kwenda kwani alikuwa akijulikana maeneo yale.
Kwa upande mwingine, duru za kikachero zilizofanikisha kupatikana kwa yule dada aliyekuwa na simu iliyoibiwa Mwanza, zilizaa matunda kwani polisi kwa kumtumia yule dada walifanikiwa kwenda Gongo la Mboto na kumnasa Chacha ambaye waliambatana naye mpaka nyumba ya wageni aliyofikia Muganyizi kisha wakaweka mtego kumsubiri. Wakina Muganyizi nao walishafanikisha tukio lao na wakiwa hajui lolote wakarudi pale nyumba ya wageni. Polisi wakawanasa.
Mashtaka, hukumu
Baada ya kuhojiwa, wale vijana waliwataja wenzao waliopo Mwanza ambao ni Abdulhaman Ismail, mkazi wa Mjimwema na Abdallah Petro Ndayi mkazi wa Mkundi, Kilimahewa ambao nao kwenye maelezo yao ya ungamo walieleza hadi walipotupa Radio Call na funguo za gari la Kamanda Lyimo kwenye shimo la choo huko Nyanshana.
Tukio hili lilizaa kesi namba 192/2014 ambapo watu saba walifikishwa mahakamani wakituhumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mwanza Liberatus Barlow Lyimo. Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza kwenye Mahakama ya Mkoa wa Mwanza chini ya Hakimu Mfawidhi Angelo Rumisha.
Kesi ilipigwa danadana nyingi za ‘upelelezi unaendelea’ hadi ilipofikia hatua ya kusikizwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Sirilius Matupa. Upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili Robert Kidando, Ajuaye Bilishanga na Revina Tibilengwa.
Washtakiwa walitetewa na mawakili Cosmas Tuthuru na Maduhu Ngasa. Upande wa mashataka ulikuwa na mashaidi 36 lakini ni 25 tu waliojitokeza kutoa ushahidi. Watuhimiwa waliokuwa Dar es Salaam walipelekwa Mwanza kwa ndege kwa ‘sababu za kiusalama.’ Kuna kipindi kesi hii ilisimama kusikilizwa kwa mwaka mzima.
Hukumu ilitolewa Novemba 13, 2019, na kuwatia hatiani watuhumiwa wanne ambao ni Peter Mchael Muganyizi, Abddulahan Ismail, Abdallah Petro na Mgige Mwita. Wengine watatu waliachiwa huru kwani mashtaka dhidi yao yalishindwa kuthibitika akiwemo Chacha.
Fortunatus Buyobe ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa habari za uchunguzi katika siasa na jinai. Anapatikana kupitia +255 768 916 060 au kupitia ukurasa wake wa Twitter kupitia @fbuyobe
2 responses
Hongera sana kwa makala elimishi; kifo cha afande Barlow kilitusikitisha wengi.
Very informative and well articulated , good work.