The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ndugai, Ni Mikopo Kweli au Kampeni Dhidi ya Mkopaji?

Ushahidi unaonesha kwamba Kiongozi huyo wa muhimili wa Bunge hakerwi na ongezeko la deni la taifa kwani kwa kipindi cha miaka mitano ya Rais Magufuli, Ndugai hakuwahi kujitokeza hadharani na kuonesha wasiwasi wake wa nchi kupigwa mnada.

subscribe to our newsletter!

Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha utaratibu mpya wa uwazi katika mikopo. Anaeleza idadi ya fedha zinazokopwa, zitafanya nini kwa kuorodhesha miradi itakayotekelezwa na wapi amezikopa na ni yepi masharti yake. Na kwa uwazi huo, ndio leo watu kama Spika wa Bunge Job Ndugai na wenye mtazamo kama wake wanapata sauti ya kuhoji na kufanya inda na inadi.

Hivi ilikuwa ni kwa faida ya nani Rais John Magufuli na wapambe wake kuficha uwazi na ukweli kuwa miradi ile ya reli, barabara, umeme, ujenzi wa hospitali na mingine mingi aliyoijenga alikuwa akitumia fedha za kukopa? Hivi wananchi tungejua anakopa, tungemzuia? Kikifichwa nini wakati huo? Ndugai na wenzake wanaohoji leo walikuwa wapi kipindi chote hicho?

Miaka mitano ya Magufuli, Rais wa awamu ya tano aliyefariki Machi 17, 2021, wananchi waliaminishwa kwamba Serikali inajenga miundombinu na kufanya shughuli nyengine za maendeleo kwa kutumia fedha za ndani. Kumbe kinyume chake ndio ukweli!

Nani mkopaji mkuu kati ya Samia na Magufuli?

Kwa mujibu wa uchambuzi wangu, ndani ya kipindi cha miaka mitano ya Rais Mafuguli, kiongozi huyo alikopa fedha nyingi kuliko fedha zote alizokopa Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu, kwa miaka 10 aliyokaa madarakani. Pia, Rais Magufuli alikopa fedha nyingi zaidi kwenye miaka yake mitano kuliko fedha alizokopa Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 10 aliyokaa madarakani!

Rais Mkapa alipambana na madeni, akaiingiza nchi katika Mpango wa Kusamehe Madeni Nchi Maskini (HIPC) na mpaka anaondoka madarakani, Tanzania ilikuwa inadaiwa Shilingi trilioni 20. Wakati wa Rais Kikwete, deni la taifa liliongezeka kwa Shilingi trilioni 23, hivyo akatoka madarakani deni la taifa likiwa ni Shilingi trilioni 43 kwa miaka 10. Rais Magufuli, kwa miaka mitano tu, deni la taifa liliongezeka kwa Shilingi trilioni 29 na kufikia Sh trilioni 72.

Kwa kasi hii ya ukopaji ina maana kama Rais Magufuli angekaa madarakani kwa miaka 10 na akaendelea na kasi ya ukopaji wa wastani wa Shilingi trilioni 29 kwa miaka mitano, basi angetoka madarakani mwaka 2025 huku deni la taifa likiwa ni Shilingi trilioni 101.

Akina Ndugai walikuwa wapi?

Cha kujiuliza ni, mbona hatukuwahi kusikia chambuzi kama hizi kuhusu deni la taifa na kasi ya Tanzania kukopa kutoka kwa watu kama Ndugai wanaoonekana kuhofia sana nchi kupigwa mnada? Ndipo hapa unapojiuliza, akina Ndugai wanakerwa na ongezeko la deni la taifa au wanakerwa na mkopaji?

Au ndio kama wasemavyo waswahili, ukipenda chongo huliita kengeza? Maana falsafa zinasema kwamba jicho linaweza kuukana mwanga wa jua kwa sababu ya upofu. Na kinywa kinaweza kukana tamu ya maji kwa sababu ya homa. Na mtu yoyote mwenye kinywa cha homa, hata maji matamu atayaona machungu. Jicho la kupenda nalo halioni kasoro; na jicho la kuchukia halioni sifa.

Job Yustino Ndugai leo anadai kuwa kulingana na mwenendo wa madeni, eti ipo siku nchi itapigwa mnada. Ndugai hana mamlaka wala nguvu ya kimaadili, au moral authority kama wanavyosema Waingereza, ya kuwanyooshea vidole wengine kwa kuwaambiwa wanaongeza madeni ya taifa. Ndugai hana moral authority ya kujifanya shujaa wa kupambana na hilo.

Sote tunakubaliana kwamba kuendesha vita dhidi ya wanaolitia hasara taifa ni jambo la lazima lakini wale wanaopambana ni lazima vile vile wawe watu safi, waadilifu na wasioyumba katika kusimamia haki. Ukweli ni kuwa Ndugai hana sifa hizo.

Ndugai ni wa kulaumu

Yeye ni mmoja wa waliolisababishia taifa deni kubwa kupitia posho mbalimbali na gharama nyengine lukuki. Wananchi siyo wajinga kama kama akina Ndugai wanavyodhani. Wanaelewa mchele ni upi na pumba ni zipi!

Kabla ya kuhoji mikopo ya sasa iliyowekwa wazi na Rais Samia na Serikali yake, tulitegemea Ndugai kwanza angetueleza mikopo ya kibiashara inayoanza kulipwa baada ya miaka mitatu na inayopaswa kulipwa ndani ya miaka minane, ikiwa na riba za kati ya asilimia 6 na 8 aliyochukua Rais Magufuli iliyokuza deni la taifa kwa kasi kutokana na riba lilofikia Shilingi trilioni 78.

Hayo ndio maadili ya misingi ya utawala bora na ustaarabu wa kileo wa kuendesha Serikali yenye kuwajibika, ya uwazi na shirikishi badala ya kuja na mbwembwe nyingi za kujitakatisha hata kama ni kwa gharama ya kulipotosha taifa na wananchi wake. Tuwe na asili na rekodi ya kusema kweli, tena kweli tupu.

Tuamini katika kutenda na kutendewa uadilifu, na kila tunachokisema na kukitenda kiwe na misingi yake na hatimae tuwasaidie wananchi wenzetu kuujua ukweli kamili ambao umejaribiwa kufichwa sana na kwa muda mrefu kwa malengo munayoyajua wenye kufanya hivyo.

Ushauri wangu kwa Spika Ndugai, kanuni ya kuwa mtu wa misimamo ni kuwa na misimamo, siyo kuwa na misimamo nusu nusu. Mtu hawezi kuwa na misimamo kwa msimu. Matendo uliyoya fanya ya kupindishaa Katiba, kupindisha sheria, kupindisha kanuni, kudhulumu haki za wabunge kwa sababu ya itikadi na kwa sababu ya kumfurahisha mtawala yanakutoa kwenye kundi la watu wenye heshima ya kusimamia na kutakasa sheria.

Khaleed Said Suleiman ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayeishi Toronto, Canada. Unaweza kuwasiliana naye kupitia  khaleed_ihaab@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unaweza kuchapisha kwenye safu hii kwa kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *