The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hivi Ndivyo Tanzania Ilivyong’ara Kimataifa 2021

Wapo watafiti, wanasayansi, wasanii na wapiga picha pia ambao kwa umoja wao waliifanya Tanzania ing’are kimataifa.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Ni masaa machache yamebakia ili tuuage mwaka 2021 na kuukuaribisha mwaka 2022 – kwa wale watakaojaaliwa kuikamilisha safari hiyo – na bila shaka kila mmoja anatafakari namna 2021 ulivyokuwa kwake binafsi huku akijiwekea mipango ya kile anachokusudia kufanya hapo 2022.

Tanzania nayo, kama nchi, imepitia mambo mengi ndani ya mwaka 2021. Kuna yale yaliyowakwaza, kuwagawa, kuwakera na hata kuwaliza watu; lakini pia kuna yale yaliyowafurahisha, yaliyowaunganisha, na yaliyowafanya watu wajivunie utaifa wao.

Angalau viongozi watatu wamepanga kulihutubia taifa leo kabla ya kufunga mwaka, hawa ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na Makamo Mwenyekiti (Tanzania Bara) wa CHADEMA Tundu Lissu. Ni wazi kwamba kila mmoja atatoa tafakuri yake namna mambo yalivyoenda nchini kwa mwaka 2021.

Hata hivyo, ni wazi kwamba yako mambo yatakayowaunganisha Watanzania kwenye tathmini zao za 2021, na moja wapo kati ya hayo ni watu, taasisi, na mashirika waliosaidia kupeperusha bendera ya Tanzania katika medani za kimataifa na kuliletea heshima taifa lao.

Hawa ni pamoja na Mtanzania anayeishi nchini Uingereza Abdulrazak Gurnah ambaye ameibuka mshindi wa tuzo ya Nobel Prize kwenye kipengele cha fasihi, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya kifahari, na Mwafrika wa pili kushinda tuzo hiyo baada ya mwanariwaya wa Nigeria Wole Sonyinka aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 1994.

Kwenye orodha hiyo pia yupo mwanamama Joyce Singano ambaye ameweza kutwaa moja kati ya tuzo kubwa za heshima ulimwenguni ya Brady Medal. Tuzo hiyo hutolewa kwa wataalam watafiti wa miamba. Mama Joyce ni mwanamke wa kwanza kutoka bara la Afrika kupokea tuzo hiyo. Joyce ni mtaalam wa ukadiriaji wa miamba akifanya kazi katika sekta ya petroli na gesi.

Naye Joyce Shebe, Mhariri Mkuu wa Clouds Media Group, kampuni inayoendesha vituo vya redio na television vya Clouds FM na Clouds TV, aliibuka mshindi wa tuzo ya International Women Peace Poem Writing Competition. Tuzo hiyo ni sehemu ya michakato ya kushajihisha amani ulimwenguni inayofanywa na Umoja wa Mataifa (UN). Shebe pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Taasisi ya Ubongo nayo, inayotumia mbinu za kidijitali katika kutengeza programu elimishi kwa watoto, walijishindia tuzo ya jumla ya Shiling milioni 18 kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali la nchini Canada liitwalo Grand Challenges.

Kuna Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, iliyoibuka kidedea kama hifadhi bora kabisa katika bara la Afrika kwenye mashindano yaliyoendeshwa na  World Travel Awards (WTA). Hii ilikuwa ni mara ya tatu hifadhi hiyo inajichukulia tuzo hiyo.

Mtanzania Salum Faki Hamad, ambaye ni mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI), ametunukiwa tuzo ya Plant Mutation Breeding Award kwa mchango wake katika kufanya utafiti wa kutumia teknolojia ya nyuklia katika kuboresha mbegu.

Kijana Imani Nsamila, mpiga picha za mazingira ameibuka mshindi wa Tuzo za Vijana za EU GCCA+ zinazolenga kuwasaidia wanahabari wachanga, waandishi na wapiga picha kusimulia taarifa au simulizi zenye nguvu za tabianchi.

Pia kuna Regina Kihwele, maarufu kama, Gynah, ambaye ni mwanamziki wa Kitanzania aliyeibuka mshindi wa muigizaji bora wa kike kwenye tuzo  za Lake International Pan African Film Festival(LIPFF). Gynah pia ni mwandishi, muigizaji na mwanamitindo.

Tukiwa tunaenda kufunga mwaka wa 2021, tuungane na Watanzania wengine kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuwapongeza Watanzania hawa walioin’garisha nchi katika medani za kimataifa huku tukijiwekea malengo ya kuing’arisha Tanzania zaidi kimataifa kwa mwaka 2022.

Heri ya Mwaka Mpya!

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *