Mijadala mingi inayohusu haki na maslahi ya wafanyakazi imejikita zaidi kuzungumzia watumishi wa umma na kundi la watu wanaofanya kazi za uzalishaji wa bidhaa au huduma ambazo huzalisha faida ya kifedha moja kwa moja.
Tunasahau kuwajumuisha na wale watu wanaotumia nguvu na muda wao kufanya shughuli ambazo hazizalishi faida ya kifedha moja kwa moja, kama vile uangalizi wa watoto, uangalizi wa nyumba, upishi na usafi katika kaya zetu.
Nitakieleza kisa kimoja nilichokutana nacho hivi karibuni wakati nikifanya mazungumzo na rafiki yangu mmoja aliyekuwa anafanya utafiti wa kukamilisha shahada yake ya uzamili uliolenga kuangalia hali za wafanyakazi kwenye baadhi ya viwanda jijini Dar es Salaam.
Mapambano ya kitabaka
Wakati wa mazungumzo hayo, rafiki yangu aliniambia: “Hivi karibuni nimeanza kukubaliana na dhana ya mapambano ya kitabaka kwa sababu ya uzoefu wangu wakati nafanya utafiti kuhusu haki za wafanyakazi. Nimeonana na baadhi ya vibarua na wafanyakazi pale Ubungo External [Eneo maalum la viwanda] wananiambia wanaingia kazini saa moja na nusu alafu wanatoka saa kumi na mbili jioni. Hii ni kinyume na haki za kumfanyisha kazi mtu zaidi ya masaa ya kisheria bila kumlipa malipo ya ziada.”
Baada ya maongezi kuendelea mjadala ulipanuka na kuzidi kufana, nikamwambia pamoja na kwamba tunajadili dhana nzima ya haki na maslahi ya wafanyakazi si vibaya kama hatojali tuendelee kuzungumza kupitia mifano binafsi.
Nikamuuliza yule dada wa nyumbani kwako anaanza kufanya kazi saa ngapi? “Huwa anaamka saa 11 kufanya usafi na kumwandaa mtoto kwenda shule,” akajibu kiungwana kabisa.
Swali lilofuata nikamuuliza huwa anamaliza kazi saa ngapi kila siku? Rafiki yangu akanijibu kwa shauku kubwa kwamba, “Kwa kweli yule dada wa kazi nimepata mchapa kazi. Mara nyingi huwa anakwenda kulala mida ya saa tatu akisha hakikisha amewabembeleza watoto hadi wamelala.”
Maongezi yetu yaliendelea kujadili malipo anayomlipa huyo dada wa kazi na vigezo anavyotumia. Lakini katika muendelezo wa mazungumzo hayo nilichokiona ni kwamba rafiki yangu anaamini pamoja na kwamba binti huyo anafanya kazi zaidi ya masaa 11 kwa siku, bado Sh30,000 anayomlipa kwa mwezi anaona inamtosha sana kwa madai kwamba ni kama anamsadia tu kwa kuwa kijijini alikotoka walikuwa wana maisha magumu sana.
Sasa hoja hapa ikawa sio tena haki ya malipo ya ziada baada ya masaa ya kisheria ya kazi kama tulivyokuwa tukijadili mwanzo kuhusu uzoefu wake wakati wa utafiti aliokuwa anaufanya kuhusu hali za wafanyakazi wa viwandani.
Kwa viwandani alikokuwa anatafiti aliona ni haki wafanyakazi kupata ujira kulingana na kazi waliyoifanya ila ilipokuja nyumbani kwake hiyo hoja haikuwa na maana tena bali hoja kwake ikawa ni historia ya nyuma ya binti huyo wa kazi na huruma yake.
Sasa ukiangalia hoja kama hizo ndio waajiri wengi hata wa viwandani au kwenye kampuni za huduma huitumia kuhalalisha maslahi au malipo kiduchu ya wafanyakazi wao kwa kuamini kitendo cha kuwapa ajira au nafasi ya kibarua ni msaada licha ya kwamba mtu huyo hutumia nguvu na muda wake.
Huu umekuwa mtazamo wa watu wengi walio na wafanyakazi wa majumbani.
Hiyo nguvu kazi na muda anaotumia mfanyakazi wa nyumbani haionekani kama ndio kipimo halisi cha ujira wa kazi anaostaili sio kama hisani bali haki ya msingi kama binadamu.
Hali ya wafanyakazi wa ndani Tanzania
Taarifa nyingi kuhusiana na idadi ya wafanyakazi wa nyumbani katika kaya hazipatikani kirahisi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo utayari wa waajiri wenyewe kuweka wazi taarifa za wafanyakazi wa majumbani.
Baadhi ya tafiti zilizofanyika kwenye baadhi ya wilaya hapa Tanzania, kama vile Nyamagana, Magu na Ilemela zinaonesha kuwa kati ya kaya kumi maeneo ya mijini, kaya saba hadi nane zina wafanyakazi wa nyumbani wanaofanya kazi zinazo husiana na kupika, kufua, uangalizi wa nyumba, uangalizi wa watoto, utunzaji wa bustani, ufugaji,kilimo cha mjini na kadhalika.
Taarifa nyingine kama ile iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya haki za binadamu inayopiga vita utumwa ikifahamika kama Anti-slavery International inabainisha kuwa zaidi ya asimilimia tatu ya wakazi wa mijini ni watu waofanya kazi za majumbani.
Hapa Tanzania, asilimia kubwa ya wafanyakazi wa majumbani ni wasichana wenye umri wa miaka chini ya kumi na nane ambao wengi hufahamika kama ‘wadada wa kazi’ au ’wasichana wa kazi.’
Wadada hawa wengi wao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi licha ya kwamba nafasi yao kama wafanyakazi kwenye jamii bado haijapewa uzito unaostahili.
Pengine ni kwa sababu wanufaika wakubwa wa nguvu nguvu kazi yao sio tu watu wa tabaka la juu bali hata tabaka la kati na hasa wafanyakazi wengi wa sekta rasmi kama walimu, wahudumu wa afya, makarani, wajasiriamali, maofisa katika mashirika binafsi na umma, wafanyakazi wa viwandani nakadhalika.
Wafanyakazi wa nyumbani licha ya kwamba wanatambulika kisheria, asilimia kubwa wanafanya kazi bila ya kuwa na mkataba wa maandishi unaoelezea majukumu yao na ujira wanaostaili kupata.
Tafiti zinaoonesha wanafanya kazi zaidi ya masaa 48 ya kazi ya kawaida kwa wiki bila ya malipo ya ziada, huku wengi wakikosa muda wa kupumzika na kufanya shughuli nyingine kama vile nafasi ya kwenda kuabudu au kujumuika na mambo mbalimbali ya kijamii.
Wafanyakazi wa ndani wengi ni wahanga wa unyanyasaji wa aina mbalimbali, kwani zaidi ya asilimia 65 ya wadada wa kazi hukiri kuwa wanapitia unyanyasaji wa kingono, kudhihakiwa, kufanyiwa mashambulio ya aibu, kutokulipwa kwa wakati au kulipwa tofauti na makubaliano au kutokulipwa kabisa.
Wafayakazi wengi wa ndani wanatoka katika familia au maeneo yenye umasikini hususani vijijini ambako zaidi ya asilimia 31.3 ya wakazi wanaishi katika umaskini na asilimia 9.7 wanaishi kwenye umasikini wa kupindukia.
Kwa hiyo, wasichana na wavulana wengi hulazimika kufanya kazi za majumbani licha ya kuwa na umri mdogo kwa sababu ya msukumo wa kiuchumi unaochagizwa hasa na ahadi mbalimbali za waajiri wao kama ahadi ya kusomeshwa watakapokuwa wanafanya kazi.
Wazazi wa wasichana na wavulana wanaoenda kufanya kazi za ndani nao huwaruhusu watoto wao wakafanye kazi sio tu kwa sababu wanaamini ndio mustakbali wa maisha ya watoto wao, bali hufanya hivyo kwa matarajio watapata usaidizi wa kifedha kutoka kwenye malipo ya kazi wanazofanya hao watoto.
Nafasi ya Serikali
Kwa upande wa Serikali, jitihada za kuhakikisha maslahi ya kundi hili la wafanyakazi linaboreshwa, ambapo mwaka 2013 Serikali ilitoa mwongozo wa mishahara ya wafanyakazi uliowajumuisha kundi la wafanyakazi za ndani kwa mara ya kwanza.
Mwongozo huu pamoja na kwamba ulionekana ni moja ya hatua ya mafanikio katika mapambano ya wafanyakazi wa ndani kupigania maslahi yao, bado ulikuwa na mapungufu na unapaswa kubadilishwa kwa kuwa umebeba dhana mbovu kuhusu ujira wa mfanyakazi wa ndani kutegemea uwezo au nafasi ya mwajiri na sio ukubwa wa kazi au muda wa kazi anaoutumia mfanyakazi kwa mwajiri wake.
Mathalani, mwongozo huo unaeleza kuwa mfanyakazi wa ndani wa mtu mwenye hadhi kama ya wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa kima cha chini cha mshahara ni Sh150,000. Kwa maofisa wa Serikali ni Sh130,000, Sh80,000 kwa watu wengine wa kawaida ambao hawaishi na mfanyakazi, na Sh40,000 kwa wale wanaoishi na wafanyakazi.
Changamoto ya muongozo huu sio tu kwamba unahitaji kurekebishwa kwa sababu ni muda mrefu umepita tangu utungwe, lakini pia hoja ya msingi ya kurekebishwa itokane na swali fikirishi ni kwa nini mfanyakazi wa nyumbani alipwe kulingana na hadhi, hali au uwezo wa mwajiri na sio muda anaoutumia kutoa nguvu kazi yake kwa ajili ya kazi za nyumbani alizofanya?
Katiba ya Tanzania haisemi mtu anastahili kupata ujira wake kulingana na hali au uwezo wa mwajiri, bali mtu anapaswa kupata ujira wake kutokana na kazi aliyoifanya, na huu ndio msisitizo unaotakiwa katika mwongozo wa malipo ya wafanyakazi.
Changamoto hizi kiujumla zina pelekea umuhimu wa sauti na mapambano ya hawa wafanyakazi wa majumbani kunganishwa na mapambano ya wafanyakazi na wavujajasho wengine kiujumla.
Japo kiuhalisia tofauti na wafanyakazi wa kada nyingine, imekuwa ngumu kwa wafanyakazi wa majumbani kujikusanya na kuungana kwa pamoja kupigania maslahi yao.
Hali hii ya kutokuwepo kwa mshikamano miongoni mwao kumeacha ombwe ambapo hivi sasa limetoa nafasi kwa baadhi ya NGOs kuendesha harakati za kudai maslahi ya wafanyakazi wa nyumbani kama sehemu ya miradi yao yenye lengo la awali la kutimiza malengo ya kitaaisi.
Sio jambo baya kwa NGOs kufanya jukumu hilo ila ni muhimu sana kwa mavuguvugu, vyama au mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi kuona ipo haja ya kuunganisha mapambano yao na mapambano ya wafanyakazi wa ndani ili kuweza kuwa na sauti ya pamoja itakayotikisa mahusiano yasiyo ya haki kati ya mwajiri na wafanyakazi.
Ni mshikamano pekee wa wafanyakazi na wavujajasho kwa ujumla ndio utakaoweza kuleta mbadiliko hata yale madogo kama vile mabadiliko ya kisheria yatakayoleta auheni kwa wafanyakazi.
Joel Ntile ni Mwanamajumuhi wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @NtileJoel. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.