Je, Teuzi za Serikali Zizingatie Udini na Ukanda?

Tunapoelekea katika uandishi wa Katiba Mpya, ambao nahisi hauepukiki, yafaa suala la uwakilishi serikalini lizingatiwe ili kuondoa uwezekano wa taifa kupasuka na kugawanyika. 

subscribe to our newsletter!

Kuna mjadala unaendelea kuhusu teuzi zinazofanywa na Rais wa Tanzania kwamba je, teuzi hizi zinapaswa kuzingatia uwiano na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii au ziangaliwe tu sifa stahiki za mtu anayetakiwa kujaza nafasi fulani iwe ya uwaziri, ukatibu mkuu au utumishi wowote ule wa umma?

Ni mjadala mzuri unaopaswa kuendelezwa. Kwa upande wangu, nadhani kuna aina ya uwiano ambao umetajwa na kukubalika katika sera za nchi, ikiwemo uwiano wa kijinsia na rika. Lakini kuna aina za uwiano katika teuzi ambazo hakuna muafaka wa pamoja. Huu ni kama vile uwiano wa kidini na kikanda.

Mjadala kuhusu mamlaka kuzingatia, au kutozingatia, uwiano kidini na kikanda katika teuzi ni muhimu sana kwa sababu malalamiko ya upendeleo yamekuwepo kwa miaka mingi, tangu wakati wa utawala wa awamu ya kwanza,  chini ya Rais Julius Nyerere. 

Kwa msingi huo, ni muhimu taifa lijadili masuala haya kwa uwazi ili kutafuta muafaka wa pamoja na kuondoa hali ya wasiwasi na kutoaminiana. Hivi sasa, suala la uwiano wa kidini na kikanda katika teuzi limebaki katika utashi na busara za viongozi. Lakini, ukweli ni kwamba haya malalamiko yanatengeneza nyufa katika umoja na mshikamano wa taifa.

Kila upande unahisi kuonewa

Nilichojifunza katika masuala haya ni kuwa kila upande unalalamika kutegemeana na dini au kanda atokayo mamlaka ya uteuzi kwa wakati huo. Akitawala Muislamu, Wakristo wanalalamika; na anapotawala Mkristo, Waislamu wanalalamika. Akitawala mtu wa Pwani, wa Bara wananung’unika, na kinyume chake. 

Awamu ya tano na sita ni ushahidi wa haya. Hali hii ya kutoaminiana, ikiachwa ikomae,  inaweza kuzaa changamoto nyingi, ikiwemo dini na ukanda kutumika kama vigezo vya kuchagua viongozi.

Katika tafakuri yangu, naona yapo maelezo ya kimantiki yanayoweza kuchangia kiongozi kujikuta anachagua watu wengi wa dini moja au kutoka kanda moja bila kukusudia kuwa mdini au mkanda. Viongozi huchagua wasaidizi kwa kuzingatia sio tu weledi lakini pia imani kwa mteule yule.

Ni kawaida kwa kiongozi kutokea kuwaamini watu anaowajua binafsi kutoka shule walikosoma wote, kazini walikofanya kazi pamoja. Pia, mtu anaweza kumteua mtu kwa kumjua  kutoka eneo moja walikotokea. 

Kama kiongozi alisoma, alifanya kazi na kuishi maeneo ya Wakristo zaidi, mzunguko wa marafiki huwa wengi wa dini hiyo na kanda husika; na kinyume chake pia kama kiongozi ni Muislamu. Kwa hiyo, viongozi hujikuta lawamani bila kuwa na nia ovu.

Changamoto nyingine ni kuwa wakati mwingine hata akitaka kuleta uwiano mzuri anaweza kukosa watu wenye kiwango cha uwezo na weledi wanaoutarajia. Kwa hiyo, kabla kundi halijadai uwakilishi zaidi katika teuzi, ni muhimu pia kuangalia uwakilishi wao katika taasisi (kwa mfano Bunge) ambayo mamlaka inategemewa ichomoe watu kwa nafasi kama zile za uwaziri

Uwiano utajwe kwenye sera, sheria

Lakini, licha ya changamoto hizo zinazowasukuma viongozi kushindwa kuleta uwiano bila kukusudia, tutawasadia sana viongozi wetu kama kukiwa na maelekezo, ya kisera na kisheria, walau juu ya suala la hili la uwakilishi na uwiano.

Kwa sasa, tunajifariji na kuwadhania vema viongozi waliopita kuwa hawakuwa na nia mbaya, licha ya mapungufu ambayo watu waliyaona. Lakini ipo haja ya kuchukua tahadhari kwani siku moja tunaweza kupata kiongozi muovu, asiyejali. 

Kiongozi huyo ataamua kuchagua wajumbe wote wa baraza la mawaziri au makatibu wakuu kutoka sehemu moja ya nchi na kutoka miongoni mwa watu wa dini moja. Hili si jambo lisilowezekana kabisa kisiasa.

Wasiwasi ndio akili.  Hivyo ni bora kutunga sera na sheria zitakazowasaidia kuteua baraza lenye uwiano unaokubalika, katika mazingira husika. Kuondoa changamoto hii kisheria kutasaidia kuilinda kila jamii dhidi ya kubaguliwa na kiongozi mbaya. Kutegemea busara za Rais pekee haijitoshelezi kwani ni wazi kabisa kuwa viwango vyao vya hekima vinatofautiana. 

Hatutakuwa wa kwanza

Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuweka katika Katiba au sheria nyingine vifungu vitakavyomlazimisha Rais aunde Serikali kwa kuakisi uwiano wa idadi ya makundi ya kijamii walau ya kidini na kikanda. 

Kenya walipoandika Katiba Mpya walikubali uhalisia wao wa Uafrika na wakaweka vifungu vya Katiba ambavyo sio tu vinazuia kijumlajumla ubaguzi kwa misingi ya dini na kabila lakini, wakaenda mbali zaidi kwa kulazimisha uundwaji wa Serikali na hata ajira za kada fulani fulani zizingatie uwiano wa makundi ya kijamii.

Kuanzia mwanzo kabisa kwenye malengo yao ya taifa na kwenye uelekeo wa sera za taifa na utekelezaji wake, Katiba ya Kenya inataja kwa uwazi kuwa uundwaji wa Serikali utaakisi uwakilishi mpana wa kitaifa na utazingatia tofauti za kijamii zilizopo nchini humo. 

Ibara ya  130 ya Katiba ya Kenya kuhusu mhimili wa Serikali (The National Executive) inataja wazi kuwa muundo wa Serikali ya taifa utaakisi tofauti za kimaeneo na makabila ya watu wa Kenya. 

Ibara ya 250 (4) inayohusu miundo ya tume na wakala za Serikali vilevile inataka teuzi za maafisa wa taasisi hizo, kwa ujumla wake, iakisi tofauti za maeneo na makabila ya watu wa Kenya. 

Ibara ya 232 kifungu (h) inataja uwakilishi wa jamii tofauti za Kenya kama moja ya misingi ya Muundo wa Utumishi wa Umma. Msingi mwingine katika kifungu (i) ni uwepo wa fursa sawa na ya kutosha katika uteuzi, mafunzo na kuendeleza (watumishi) katika ngazi zote za utumishi wa umma, hususan kati ya wanawake na wanaume, makabila tofauti na watu wenye ulemavu.

Ibara ya 238 (2) inayozungumzia misingi ya usalama wa taifa inataja kuwa uajiri wa vyombo vya usalama vya dola viakisi utofauti wa watu wa Kenya katika uwiano sawa. Ibara za 241 na 246 zinakazia jambo hilo hilo kwa Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Polisi.

Kinachofurahisha zaidi kuhusu Katiba ya Kenya, Ibara ya 56, ni kwamba inataja wazi pia wajibu wa Serikali kuweka mipango mahsusi ya kusaidia jamii za wachache na watu waliotengwa kushiriki na kuwakilishwa serikalini na nyanja nyingine za maisha, wanapewa fursa maalum za kielimu na uchumi na kupata huduma za kijamii.

Fursa sawa kwa jamii zote

Tunapoelekea katika uandishi wa Katiba Mpya, suala la fursa sawa kwa  jamii zote ni la msingi sana. Ni muhimu, Tanzania, kama wenzetu Wakenya na Waganda, tukubali tu kuwa nchi zetu za Kiafrika zimegawanyika katika kanda, makabila na madhehebu za dini (kutegemeana na taifa na taifa); na kadhia hizi huchonga mitazamo yetu ya kisiasa. 

Kwa Tanzania, uwakilishi wa kikanda na dini ni muhimu sana. 

Sasa, tunapoelekea katika uandishi wa Katiba Mpya, ambao nahisi hauepukiki, yafaa suala la uwakilishi serikalini lizingatiwe ili kuondoa uwezekano wa taifa kupasuka na kugawanyika. 

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts