Dar es Salaam. Makamu wa Rais Philip Mpango ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Tanzania kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba Tanzania inarudi katika hali ya amani, akisema kwamba yeye binafsi na Rais Samia Suluhu Hassan wamechoka kusikia habari za mauaji kila siku, na kwamba Serikali haiwezi kuongoza nchi yenye mauaji kila kona.
Kauli ya Dk Mpango inakuwa kauli ya kwanza ya kiongozi mkuu wa kitaifa iliyowahi kutolewa kufuatia wimbi la mauaji holela lililoikumba Tanzania kwa siku za hivi karibuni na kuacha watu wengi na maswali juu ya nini kinaweza kuwa kinachochea mauaji haya ya kikatili na kutisha.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa The Chanzo, kati ya Septemba 2021 na Januari 2022, jumla ya matukio 37 ya mauaji yaliripotiwa kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara. Matukio haya ni yale tu yaliyothibitishwa na Jeshi la Polisi na orodha hii haijumuishi matukio ambayo hayakuripotiwa.
Kwa mujibu wa tathmini hii, jumla ya watu 52 waliripotiwa kuawawa kwenye matukio hayo, ambapo wanawake walikua 26 na wanaume walikua 26. Kati yao, watoto walikua kumi na moja. Uchambuzi wa The Chanzo pia umebaini kwamba mtu mwenye umri mdogo kabisa katika matukio haya alikua ni mtoto wa miaka mitatu, huku mtu mwenye umri mkubwa kabisa alikua na umri wa miaka 75. (kielelezo cha picha chini)
Uchambuzi wa sababu zilizotolewa kama kichocheo cha mauaji haya unaonesha kwamba wivu wa mapenzi unaongoza kwa asilimia 31. Sababu inayofuatia ni uchawi na migogoro ya ardhi ambayo kila moja inachukua asilimia 14.
Uhalifu na kupata mali inafuata na kuchukua asilimia 11 huku ugomvi ukichukua asilimia 11 ya matukio yote. Matatizo ya akili na msongo wa mawazo kwa sababu ya ugumu wa maisha yakichua asilimia nane ya matukio yote, huku asilimia 11 sababu zikiwa hazijatajwa au kufahamika.
Ukatili unapofanywa kawaida
Wakati wadau wakiendelea kuumiza vichwa wakitafakari ni namna gani bora ya kukabiliana na janga hili, utafiti mdogo wa The Chanzo umebaini uwepo wa uhusiano kati ya matukio haya na masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo husika.
Kwa mfano, tafiti za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kwamba ukatili wa kijinsia uko juu mkoani Shinyanga, ambapo asilimia 78 ya wanawake walio katika ndoa mkoani humo wanapitia ukatili wa kijinsia.
Shinyanga inafuatiwa na Tabora (asilimia 71), Kagera (asilimia 67) na Simiyu (asilimia 62). Kwa mujibu wa uchambuzi wa The Chanzo, maeneo yote haya yamerekodi kisa cha mume kuua mke, pengine na watoto kati ya matukio 37 yaliyoripotiwa.
Kwa mfano, huko mkoani Simiyu, Golani Nh’umbu, 35, alimuua mke wake, Pili Masonga kwa kumkata mapanga wivu wa mapenzi ukitajwa. Mkoani Shinyanga, Lima Kulwa, 30, aliuliwa na mume wake kwa kushukiwa kuwa ni mchawi. Mkoani Kagera nako, Odilia Rukasi, 47, aliuwawa na mume wake Clemence Mdende, 51, sababu ikiwa ni wivu wa mapenzi.
Afya ya Akili
Katika hali ya kushangaza, uchambuzi wa The Chanzo wa visa vyote 37 vya mauaji umebaini kwamba nusu ya visa hivyo hutekelezwa na ndugu wa karibu au mwanafamilia. (kielelezo cha picha chini)
Moja kati ya visa hivi ni kile kinachomuhusu askari wa Jeshi la Wananchi (TPDF) Mussa Edward Ndonde, 31, aliyemuua baba yake mnamo Januari 12, 2022, huko mkoani Mbeya.
Au huko Njombe ambapo Vaileth Chaula, 30, aliamua kumuua mtoto wake wa miaka mitatu kwa kumkata na shoka. Visa kama hivi vinavyohusisha wanafamilia ni vingi kwenye matukio yanayoripotiwa.
Wimbi hili la mauaji limepelekea watu tofauti kuibuka na nadhari mbalimbali ili kujaribu kuelewa msingi wa mauaji haya. Kati ya nadharia hizi ziko zile za kisomi na zile ambazo tunazoweza kusema ni za mtaani, au kimazoea.
Kwa mfano, majirani wengi ambao The Chanzo iliongea nao baada ya kijana Musa Ndonde kumuua baba yake huko Mbeya walimuelezea kijana huyo kama kijana mzuri aliyeponzwa na pombe, bangi na imani za kishirikina.
“Pombe na bangi ndivyo vilikuwa vinamponza [Ndonde] na baba [yake] anakaa anasema kila wakati kwamba jitahidi mwanangu pombe hizo acha,” anaeleza Winfred Paul Mgaya, jirani wa Mussa. “Na chanzo alikuwa anasema baba mchawi, anashindwa kupanda cheo kwa sababu ya uchawi.”
Nadharia nyengine inayotajwa ni ile inayohusisha ugumu wa maisha ambapo baada ya mtu kuishiwa na suluhisho la namna bora za kutatua changamoto zake za kimaisha huamua kuchukua uhai wao na wale wa wapendwa wao.
Angalau huu ndiyo utetezi uliotolewa na Veronica Gabriel, 30, mkazi wa Kijiji cha Mwabagaru, Kata ya Buseresere, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, aliyewaua watoto wake wawili kwa kuwanywesha sumu na halafu na yeye kunywa.
“Wakati mwingine mnalala nje, mnashinda njaa, unapiga vibarua hadi nachoka, hata nguvu zinaisha, nikasema heri nife nikapumzike,” Veronika alinukuliwa akieleza sababu zake za kufanya kitendo hicho cha kikatili. “Hata nikiacha watoto ndugu washanitenga, nina kaka watatu washanitenga, baba naye ameshakamatwa nikaona hata nikiwaacha watateseka tu.”
Lakini kwa Beturina Mwamboneke, mtaalamu wa saikolojia na magonjwa ya akili kutoka Mbeya, hivi vinaweza kuwa ni visingizio tu na kwamba tatizo kubwa linaweza kuwa ni tatizo la afya ya akili ambalo linaweza likawa linamsumbua mtu kwa muda mrefu bila kupata msaada stahiki.
Wakati wa mahojiano na The Chanzo hivi karibuni, Mwamboneke anasema: “Msongo wa mawazo uliopitiliza unampelekea mtu kukata tamaa ya kufanya mambo yake. Hukata tamaa ya kutatua matatizo yake. Hasira tunaichukulia kama ni dalili kubwa sana ya magonjwa ya akili. Ndiyo maana watu wengi wakiwa na msongo tu wa mawazo ukimuongeleshe kitu analipuka.”
Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni saba wenye matatizo yanayohusiana na afya ya akili, kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni kutoka serikalini. Kwenye taarifa yake ya mwaka 2017/2018, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliripoti kwamba kati ya kila Watanzania laki moja, 2,727 wana matatizo ya akili.
Bado katika ngazi ya familia utatuzi matatizo ya akili hasa msongo hayapewi nafasi inayostahili,wengi husubiria mpaka hali ikishakuwa mbaya ndipo hapo huanza kuhangaika. Ufahamu wa afya ya akili bado ni mdogo, huku wengi wakiangalia matatizo hayo kwa sura moja tu, ukichaa.
Kukosekana kwa uwajibikaji
Tanzania inaweza ikawa ni moja kati ya nchi ambazo wananchi wake inawachukua muda mwingi zaidi kuliko ilivyo kawaida kupata utatuzi wa kero fulani inayomsumbua kutoka kwenye mamlaka za Serikali.
Kwa mfano, kwenye eneo la migogoro ya ardhi ambayo ni maarufu Tanzania, inaweza kumchukua mtu takribani umri wa mtu mzima mpaka kuja kupata ufumbuzi wa mgogoro husika.
Ndiyo maana haishangazi basi unaposikia kesi kama za Juma Katinda, 58, huko mkoani Morogoro aliyeamua kuichoma moto nyumba ya jirani yake aliyedai kupitiliza na kujenga kwenye hifadhi ya kiwanja chake.
Hata majirani nao, ambao walijaribu kumzuia Katinda kufanya uhalifu huo, pale waliposhindwa waliamua kumvamia kwa silaha za jadi na kuuchoma mwili wake.
Bado kuna sintofahamu juu ya tukio la watu waliomuua mtendaji wa mtaa wa Mbezi Msumi, Kevin Costa Cowo, ambapo alichinjwa katikati ya kusikiliza mgogoro wa ardhi. Kwa mujibu wa taarifa za Polisi moja ya watu waliokuwa upande mmoja wa mgogoro huo wa ardhi, waliamua kumkata mapanga mtendaji huyo.
Migogoro ya ardhi inatajwa kama chanzo kikubwa cha mauaji nchini Tanzania, mifumo ya kutatua migogoro inafanya kazi kiasi gani, inachukua muda kiasi gani, je watu wanaona mifumo rasmi kama njia sahihi za kuzikimbilia?
Pengine hakuna mamlaka inayolalamikiwa zaidi kwa ukosefu wa uwajibikaji na tabia za kutojali kama Jeshi la Polisi.
Ni hivi karibuni tu, kwa mfano, ziliibuka taarifa kwamba maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, walidaiwa kutokufanyia kazi taarifa za wadada wahanga wa uhalifu wa kimtandao ambao video zao za utupu zilikuwa zikivujishwa kwa kushindwa kutoa kiwango fulani cha pesa walizoombwa.
Wadada hao waliokimbilia polisi kama njia ya mwisho ya kupata msaada waliambiwa “wapotezee” tu, kwamba baada ya wiki watu watasahau kuhusu video zao hizo. Wengine walidai kudaiwa hongo ya Sh500,000 ili kesi zao ziweze kufuatilia. Mmoja wa muhanga wa kesi hizi alifikiria hata kuchukua uhai wake mwenyewe.
Tabia hii ya kutojali kwa upande wa Jeshi la Polisi iliweza kusababisha maafa sehemu nyingine kama ilivyokuwa huko jijini Mwanza ambapo kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Issa Simba, 14, aliuliwa kwa kukatwa mapanga mnamo Disema 24, 2021, baada ya polisi kushindwa kufanyia kazi taarifa za uwepo wa makundi ya kihalifu jijini hapo.
“Kila tukipeleka malalamiko kule [polisi] hayafanyiwi kazi, unashangaa tu vijana wamepelekwa mle polisi wanarudishwa,” Geoffrey Tilya, mkazi wa Mabatini ambapo Simba aliuwawa, aliieleza The Chanzo.
“Sisi tunapambana sana kuwakamata hawa waalifu lakini Jeshi la Polisi linaturudisha nyuma,” Samson Peter John, kiongozi wa ulinzi shirikishi Mabatini, aliiambia The Chanzo.
“Unapomshika mhalifu ametenda [kosa] unampeleka na silaha kabisa kituoni lakini inatokea vitu vingine mtuhumiwa anaachiwa,” anaongeza John. “Wakishaawachia wakija mtaani wanakutafta wanakufanyia vurugu. Mimi walinikata kwenye bega na mkononi.”
Kasumba ya Kutojali
Miaka ya hivi karibuni kulitokea hali ya kushangaza katika jamii yetu. Kuliibuka matukio mengi ya watu kupotea, watu kutekwa, watu kuuwawa bila kuwepo kwa ufafanuzi au majibu ya kina, mara nyingi iliishia kuwa ni watu wasiojulikana.
Kupuuziwa kwa matukio hayo ya kutisha na yasiyo ya kawaida kulijenga kasumba ya kutojali na kufikia mahali ikawa kama kawaida isiyo kawaida katika jamii yetu.
Haikushangaza sana pale moja ya Mbunge alipochangia hoja Bungeni kutaka Mbunge mwenzake auwawe. Ilikuwa ni siku ya kawaida tu hata pale ‘mtu asiyejulikana’ alipomtolea Waziri wa Serikali bastola hadharani mbele ya vyombo vya habari kumtishia, majibu rasmi yalikua rahisi tu, tunamsaka na baadae majibu yakawa mtu huyo hakua Polisi.
Tunaona mrejesho wa hali hii kwenye baadhi ya matukio, katika matukio 37 tuliyoaangalia walau matukio matatu watu walilipwa fedha kwa ajili ya kufanya mauaji. Halikua jambo la kawaida katika jamii yetu kuwa na watu wanaojipatia fedha kwa kufanya mauaji.
Tumeshuhudia tukio la hivi karibuni la Polisi Mtwara kumuua kwa sumu Ndugu Mussa Hamisi (25) na kumtupa baada ya kumuibia fedha zake. Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa yule yule mtu aliyemtolea Waziri bastola na kumtishia hadharani, mbele ya vyombo vya habari naye anatajwa kuwa mmoja wa watu wanaotuhumiwa kufanya unyama huo. Hakuna anayejua mtu huyo kafanya matukio mangapi kama hayo, ila wote tunajua ilitakiwa ile siku ametoa bastola kumtishia Waziri angetakiwa kuwajibishwa kisheria na kuachishwa Upolisi.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanabainisha kwamba hali hii iliweka msingi wa watu kutothamini maisha ya watu wengine na hata kushajihisha wengine kufanya matukio hayo wakijua kwamba hakutakuwa na uwajibikaji wowote.
The Chanzo ilimuuliza Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, ni nini kinapaswa kufanyika katika mazingira kama haya kukomesha wimbi hili la mauwaji ya Watanzania. Yeye ameshauri kuundwa kwa tume maalum ya kuchunguza mauaji hayo, itakayokuja na sababu zinazopelekea kuibuka kwake na nini kinaweza kuwa ni suluhisho.
Wakati tukisubiri kuona kwamba Serikali inaweza kulichukua wazo la Sheikh Ponda na kulitekeleza, ni maoni ya Watanzania wengi kwamba hali haiwezi kuendelea kama ilivyo sasa.
Wito umetolewa kwa wananchi kurudi kwenye msingi wa jamii inayojali utu, huku vyombo vinavyohusika na ulinzi na usalama wa wananchi vikitakiwa viwajibike, na kukataa kasumba ya ukatili na kutokujali.