The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kilichojificha Nyuma ya Kuvuja kwa Video za Utupu Mitandaoni

Kwa mujibu wa wahanga, video nyingi za utupu zinazosambaa mitandaoni zimevujishwa na kikundi cha wahalifu walioamua kuchukua hatua hiyo baada ya mabinti husika kukataa kutoa fedha ambazo wahalifu hao wamekuwa wakiwaomba ili wasivujishe video hizo za kashfa.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kama imetokea kutazama moja kati ya video nyingi za utupu ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni siku za hivi karibuni, hususan zile zinazohusisha chupa za soda, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa umetazama binti ambaye ni muhanga wa vitendo vya ulaghai unaofanywa na baadhi ya wahalifu wa kimtandao unaowalenga mabinti kwa ajili ya kujipatia fedha.

Kwa mujibu wa wahanga, ambao wengi ni mabinti walio na umri kati ya miaka 18 na 20, video nyingi za utupu zinazosambaa mitandaoni zimevujishwa na kikundi cha wahalifu walioamua kuchukua hatua hiyo baada ya mabinti husika kukataa kutoa fedha ambazo wahalifu hao wamekuwa wakiwaomba ili wasivujishe video hizo za kashfa.

Video hizi za utupu hufikia kwenye mikono ya wahalifu hawa pia kwa kupitia njia za kilaghai, kitapeli na kihalifu, lakini kikubwa ni kile kinachoweza kuelezewa pia kama tamaa za fedha na kuishi maisha ya kifahari ambazo mabinti wengi wanadaiwa kuwa nazo. Kwa mujibu wa maelezo ya wahanga na watu waliokaribu na wahanga hao, mchakato mzima wa upatikanaji wa video hizo unakuwa kama hivi:

Sh700,000 kwa video moja

Mhalifu mmoja wa kimtandao alifanikiwa kumlaghai binti mmoja kwa njia za kimtandao, sana sana kupitia mtandao wa Instagram, kwa kumwambia kwamba anaweza kupata Sh700,000 kama anaweza kujirekodi akiwa mtupu na kuituma video hiyo kwa mhalifu huyo. Mhalifu huyo hudai kwamba kuna mtu mwengine – kuna siku anataja mzungu, mhindi, au mwarabu – na ndiye atakayelipa fedha hizo.

Baada ya binti husika kutuma video hiyo, mhalifu huyo humuomba binti huyo anuani yake ya barua pepe na neno la siri, akidai kwamba vitu hivyo ni muhimu ili aweze kufanya malipo husika. Lakini baada ya binti kufanya hivyo, anakuwa ni yeye sasa anayedaiwa kutuma pesa vinginevyo video zake za utupu zitavujishwa mitandaoni.

Haishii hapa. Kwa sababu tayari mhalifu huyu ana umiliki wa akaunti ya Instagram ya muhanga wake, anaanza kuwaendea baadhi ya marafiki wa muhanga wake kwenye mtandao huo wa kijamii na kuwarubuni wafanye vile vile alivyomtaka muhanga wake wa kwanza kufanya.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wahanga wa vitendo hivi, mabinti hao walishtuka kwanza wanapoambiwa kwamba wanaweza kujipatia Sh700,000 kwa kutuma video za utupu. Lakini mwisho wa siku hushawishika kufanya hivyo baada ya kuona ni rafiki yao wanayemfahamu ndiye anayewaambia kufanya hivyo; rafiki ambaye huwahakikishia kwamba hata yeye amefanya na kuwatumia video zake kama uthibitisho.

Baada ya kukubali, rafiki huyo huwapa mabinti hao namba ya simu, ambayo siyo ya Kitanzania, akiwaambia hiyo ndiyo namba ya mtu anayehitaji hiyo video na ndiye atakayetoa hizo pesa baada ya video kutumwa. Binti huyo akifanya hivyo tu, na yeye anaanza kudaiwa kutuma pesa ili video zake zisivujishwe.

Walengwa wa uhalifu huu

Jessica Maleko* ni mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam ambaye baada ya kukutana na mabinti wengi ambao ni wahanga wa matukio haya aliamua kuitafuta The Chanzo ili aeleze kinachotokea ili kuwapa tahadhari mabinti wengine lakini pia kuvitaka vyombo vya dola kuingilia kati na kukomesha vitendo hivi.

“Tunazungumzia [mabinti] kuanzia miaka 17, 18 na 19,” anasema Jessica, ambaye anadai kufahamu mabinti takriban 40 ambao wamekuwa wahanga wa uhalifu huu. “Tunazungumzia wasichana ambao wametoka shule ambao wanaingia kidato cha tano, kidato sita na chuo mwaka wa kwanza, ni wasichana kama wawili [au] watatu ambao labda wapo chuo mwaka wa mwisho.”

Jessica anadhani uchaguzi wa kundi hili la wasichana umefanyika kwa makusudi. Anafafanua: “Kwa sababu [hawa] ni watoto hata uwezo wao wa kuchanganua mambo sio kama wa watu wazima. Kwamba ni mtoto mdogo ambaye ukimfuata ukimwambia kwamba nina kiasi cha [Shilingi] laki saba nataka nikupe naomba ufanye moja, mbili, tatu ni rahisi kwake kurubunika.”

Kwa mujibu wa uchunguzi ambao Jessica na timu wameufanya, ilibainika kwamba kijana aliyenyuma ya uhalifu huu anajulikana kwa jina moja la Victor. Amesomea Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Kigoma kwa miaka miwili, akisomea teknolojia ya habari kabla ya kufukuzwa kwa madai ya wizi.

Polisi yalaumiwa

Mabinti wengi waliojikuta kwenye kadhia ya aina hii walichukua uamuzi kama ambao raia mwema mwengine yoyote angeuchukua pale anapogundua kuna aina fulani ya uhalifu unafanyika katika jamii: kuripoti polisi. Lakini wahanga wengi wa uhalifu huu wamelalamikia kukosa msaada kutoka kwa chombo hicho cha kusimamia sheria za nchi.

Polisi wanadaiwa kuwaomba wahanga wa matukio haya Sh500,000 ili kesi zao zichunguzwe. Muhanga mmoja aliyeripoti polisi baada ya video zake kuvuja aliwekwa ndani badala ya kusaidiwa. Wahanga wengine waliambiwa na polisi wapotezee tu, kwamba baada ya wiki mbili watu watakuwa wamesahau.

Kituo kikubwa kilicholalamikiwa ni Kituo cha Polisi Oysterbay. The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Kituo hicho kwa nini polisi wake wanashindwa kuwasaidia watu wanaoripoti uhalifu na badala yake wana wahukumu. Alikataa kujibu, akisema atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhani Kingai ambaye naye pia aligoma kujibu maswali yetu.

“Nashindwa kuelewa hiyo [Shilingi] laki tano ni ya kazi gani,” analalamika Jessica, “kwa sababu mimi nafikiri ni kazi ya Jeshi la Polisi kutusaidia kama vitu kama hivi vinatokea.”

Hali hii imewafanya baadhi ya mabinti walioangukia kwenye kadhia hii kushindwa kuripoti kesi zao polisi na kutafuta njia nyengine za kutatua tatizo hilo, ikiwemo kufikiria kujinyonga.

Hawa ni pamoja na Miriam Hamis*, binti wa miaka 19 anayesoma kidato cha sita ambaye mpaka muda wa kuzungumza na The Chanzo alikuwa anaendelea kutishwa kwamba video zake za utupu zitawekwa mitandaoni endapo kama hatatuma kiwango cha fedha anachoambiwa atume.

“Binafsi sijaripoti polisi kwa sababu nilikuwa na wasiwasi,” anasema Miriam aliyeshawishika kujirekodi video za utupu baada ya kuahidiwa kulipwa Sh700,000. “Kuna huyo mwenzetu alikuwa ameenda kuripoti polisi akaonekana yeye ndio anakosa kwa sababu yeye ndio alirekodi hizo video.”

Wito

Asha Abinallah ni mmoja kati ya viongozi wa Women at Web, mradi unaohamasisha matumizi salama na sahihi ya mitandao ya kijamii, anayesema kwamba uhalifu wa aina hii unawakumbusha watumiaji na wadau wengine wa mitandao ya kijamii kuhusu kutokuchukulia kwa wepesi kwamba kila mtu anajua kipi ni sahihi cha kufanya anapotumia mitandao ya kijamii.

“Leo hii mtu anaona kawaida kutoa barua pepe yake na kutoa codes zake kwa sababu labda alipopewa smartphone ni mtu wa bandani hajajitengenezea barua pepe kwa hiyo hajui kwamba hiyo ni ya kwake tu anaona kwamba unaweza ukamshirikisha na mtu mwingine,” anasema Asha.

Kwa mujibu wa Jessica, ambaye ametumia muda mwingi kukaa na wahanga wa uhalifu huu, vitu hivi ni muhimu kufanyika ili kudhibiti aina hiyo ya uhalifu kuendelea kutokea:

“Kwanza ni kuongea na wadogo zetu, ama kuongea sisi wenyewe kwa sababu sio kitu ambacho ni watoto tu wanakifanya hadi watu wazima wanafanya, kwamba tuache kuwa na tamaa, kwamba wasichana waitambue thamani yao.

“Lakini pia ni wazazi kuongea na watoto wao kuhusu uhalisia wa maisha kwa sababu wasichana wengi wanarubunika kutokana na maisha wanayoyaona Instagram wenzao wamezaa, wametoka, wamefanya hiki na kile. Kwa hiyo, ni kumwelewesha mtoto kutoka mwanzo kwamba uhalisia wa maisha upo moja, mbili, tatu.

“Kwa upande wa Serikali, tunaomba nguvu yao zaidi. Ndio ni kosa [kujirekodi video za utupu] lakini wasiwe kama wanatulaani, wanatulaumu ama kutusumbua kwamba tumekosea. Mwisho wa siku inakuwa hamna msaada ambao tunakuwa tunaupokea kutoka kwao.”

*Siyo majina yao halisi.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusu habari hii unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *