Vodacom: Takribani Robo ya Miamala ya M-Pesa Imepungua

Kampuni hiyo ya simu imehusisha anguko hilo na tozo zinazotozwa kwa Watanzania pale wanapofanya miamala kwa kutumia simu za mkononi.
Na Mwandishi Wetu31 January 202211 min

Dar es Salaam. Kampuni mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania PLC imebainisha kwamba miamala iliyofanyika kupitia huduma ya kutuma pesa kwa kutumia simu ya mkononi ya kampuni hiyo M-Pesa imeshuka kwa asilimia 24.8.

Vodacom imebainisha hilo kwenye taarifa yake ya fedha ya robo ya mwisho wa mwaka 2021 ambapo inaonekana kwamba kampuni hiyo iliwezesha kufanyika kwa miamala yenye thamani ya Shilingi trilioni 14.2 katika robo ya mwisho ya mwaka 2021.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu inayoelezwa kuchochea anguko hilo la miamala ni tozo zinazotozwa kwa Watanzania pale wanapofanya miamala kwa kutumia simu za mkononi.

“Hali hii ya kushuka inadhihirisha athari ya tozo mpya hata baada ya kupunguzwa kwa asilimia 30 Septemba 2021,” Vodacom Tanzania wanasema kwenye taarifa yao hiyo.

Taarifa hiyo pia inaonyesha kwamba kumekuwepo na mdororo wa ukuaji wa watuamiaji wa M-Pesa ambapo wamepungua kwa asilimia 4.4 ukilinganisha na mwaka 2020. Hata hivyo bado Vodacom inabakia kampuni yenye soko kubwa zaidi kuliko kampuni yoyote katika huduma za fedha kwa mitandao ya simu.

Katika bajeti mpya ya Serikali 2021/2022 iliyoanza Julai 2021, Serikali iliweka tozo mpya katika miamala ya simu, ambapo miamala yote ilitozwa kati ya Sh10 mpaka Sh10,000.

Hata hivyo, baaada ya malalamiko ya wadau, Serikali ilipunguza tozo hizo kwa asilimia 30 mnamo Septemba 2021.

“Pamoja na punguzo la tozo, thamani na kiwango cha miamala bado ni kidogo kulinganisha na kipindi kabla ya tozo,” inasema taarifa hiyo ya Vodacom. “Ni kwa sababu ongezeko la tozo bado linachangia gharama kwa mtumiaji wa mwisho.”

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Vodacom ilijikuta katika changamoto mbalimbali zinazotokana na sera.

Changamoto hizo ni pamoja na kukamatwa kwa watendaji wake wakuu kwa makosa ya uhujumu uchumi, pamoja na kupata hasara ya Shilingi bilioni 30 kwa mwaka 2020, huku changamoto za kikodi na kuzuiwa kwa laini milioni 2.9 zikitajwa kama sababu kubwa za hasara za biashara.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Vodacom na makampuni ya mitandao mingine ya simu zinaaendela kufanya mazungumzo na Serikali katika kuangalia athari za tozo katika mitandao ya simu na kwa uchumi kwa ujumla.

Na Mwandishi Wetu

One comment

  • Asanterabi

    2 February 2022 at 5:35 PM

    Serekali ifike mahali itoe hizi tozo maana zinarudisha nyuma mzunguko wa hela unakua mdogo.itafika sehemu watu wanahifadhi fedha majumbani mwao

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved