The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tito Magoti: Tukiwa Tunaadhimisha Wiki ya Sheria, Tuwafikirie Wanaoendelea Kusota Gerezani Bila Kutiwa Hatiani

Watu walioko magerezani ambao haki yao haimaanishi kuachiwa tu, bali kusikilizwa, na kupata matokeo kwa wakati, wapewe kipaumbele. Hakuna lugha nyingine ya kuelezea mfumo wetu wa haki jinai zaidi ya kusema tuko njia panda!

subscribe to our newsletter!

Wiki ya Sheria ni jambo la kawaida kwa wadau wa sheria kwa kuwa inachukuliwa kama sehemu ya utamaduni wa kila mwaka.

Ni la kawaida kwa sababu hata huduma za kisheria zinazotolewa katika wiki hii zimeelekea zaidi kutimiza wajibu, na pengine kujinadi baina ya wadau wa sheria, kuliko kufanya tathmini na uvumbuzi wa majibu ya changamoto sugu zinazoikumba tasnia ya sheria chini Tanzania kwa sasa.

Kwa upande mwingine, wiki hii ni muhimu sana kwa mahabusu walioko magerezani. Sikuwahi kufahamu umuhimu wa siku hii kwa mahabusu hadi kipindi kama hiki mwaka 2020 nikiwa gerezani Segerea.

Niliona shauku na matarajio ya mahabusu wenzangu kufahamu kitakachojiri siku ya kilele cha Wiki ya Sheria, na muelekeo wa Mahakama kwa mwaka huo. Waliitazamia sana hotuba ya Jaji Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa matarajio makubwa.

Mwaka huu, Wiki ya Sheria imeadhimishwa tena kuanzia Januari 23 hadi Februari 2, 2022. Nilishiriki kwa kutoa msaada wa kisheria katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, jijini Dar es Salaam. Kama nilivyotangulia kusema, wiki hii kwa wadau inamaanisha kuendeleza utamaduni zaidi wa kutatua changamoto.

Eneo la Kisutu, kwa vyovyote vile, huwezi kutegemea kukutana na umma. Idadi ya watu waliofika kupata huduma iliakisi mtazamo wangu. Ilifaa waandaaji wa Wiki ya Sheria wawafikirie zaidi wanufaika na kuwasogezea huduma kuliko kujificha Kisutu. Hii ni mada ya makala nyengine.

Miaka 12 gerezani bila kutiwa hatiani

Ninafahamu kwamba siku ya kilele cha Wiki ya Sheria, ambapo viongozi watatoa hotuba, mahabusu wataketi kwenye redio na televisheni siku nzima kusikia majibu ya maswali yao.

Moja ya swali sugu ambalo mahabusu wanaishi nalo bila majibu ni upatikanaji wa vikao. Hii ni kwa mahabusu na pia wafungwa, mathalani walioko Gereza la Ukonga, wanaosubiri vikao Mahakama ya Rufani.

Shauku yao kuu ni kusikilizwa. Ukiambiwa mtu amekaa miaka sita hadi 12 gerezani bila kutiwa hatiani utaona ni nadharia. Lakini wapo.

Hizi hapa ni baadhi tu ya kesi za muda mrefu, ambazo mahabusu wake wako Gereza la Segerea:

 

“Mahakama haina fungu la kuendesha vikao,” ni jibu wanalopewa kila wakati watuhumiwa hawa wakihoji kuhusu vikao. Je, hotuba za viongozi katika kilele cha Wiki ya Sheria zitajibu maswali ya mahabusu na wadau wa sheria na haki jinai? Matarajio yangu ni hafifu!

Serikali, Mahakama zitimize wajibu wao

Kwa kuwa uelewa wa mahabusu ni kwamba Mahakama haina fungu la kuendesha vikao, na kwa kuwa ukweli ni kwamba fedha za uendeshaji wa kesi zinatolewa na Serikali, basi Serikali itimize wajibu wake, na Mahakama vivyo hivyo.

Watu walioko magerezani ambao haki yao haimaanishi kuachiwa tu, bali kusikilizwa, na kupata matokeo kwa wakati, wapewe kipaumbele. Hakuna lugha nyingine ya kuelezea mfumo wetu wa haki jinai zaidi ya kusema tuko njia panda!

Pia, sababu nyingine zote za ucheleweshwaji wa kesi zitatuliwe. Kwa mfano, upelelezi usiokoma; mamlaka yaliyopitiliza kwa waendesha mashitaka kiasi cha kuiongoza Mahakama; zuio la dhamana; na changamoto za miundombinu, ikiwemo Mahakama mtandao.

Nashauri, kama nchi, tuwe na mfumo wa dhamana kwa makosa yote ya jinai. Mahakama irejeshewe mamlaka ya kuamua haki ya dhamana kwa kuangalia mazingira ya kesi husika kama ilivyokuwa hapo zamani.

Tutaondokana na kadhia ya kutesa watu magerezani muda mrefu bila hatia kwa kudhibiti upelelezi, kuruhusu dhamana, na kuruhusu Mahakama ifanye kazi yake bila vikwazo kutoka mihimili mingine.

Tito Magoti ni mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe titomagoti@gmail.com au kupitia Twitter kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungepanda kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *