Malalamiko Zaidi ya 7,000 ya Wananchi Yamfikia Mwinyi Kupitia App ya Sema na Rais

Mfumo huo ambao ulizunduliwa rasmi mnamo Februari 27, 2021, ulilenga kumsogeza Rais Mwinyi karibu zaidi kwa wananchi ili aweze kusikia moja kwa moja kutoka kwao kero zinazowasumbua na hivyo kuzitafutia ufumbuzi wake.
Salim Khamis Kombo3 February 20223 min

Zanzibar. Jumla ya malalamiko 7,089 yamewasilishwa na wananchi wa Zanzibar kwa Rais wa nchi hiyo Dk Hussein Mwinyi kupitia mfumo mpya wa kieletroniki ujulikanao kama Sema na Rais Mwinyi, huku migogoro ya ardhi na kero za maji na umeme zikiripotiwa kuchukua sehemu kubwa ya malalamiko hayo.

Mfumo huo ambao ulizunduliwa rasmi mnamo Februari 27, 2021, ulilenga kumsogeza Rais Mwinyi karibu zaidi kwa wananchi ili aweze kusikia moja kwa moja kutoka kwao kero zinazowasumbua na hivyo kuzitafutia ufumbuzi wake.

Wazo la kuja na mfumo huo lilitokana na imani ya Rais Mwinyi kwamba matatizo mengi yanayowasumbua wananchi wa Zanzibar yanakosa ufumbuzi kwa sababu yeye binafsi hafahamu uwepo wake, na wasaidizi wake wanashindwa kumueleza kwani hiyo itaonesha kwamba hawafanyi kazi.

“Wakati wa kampeni [za uchaguzi mkuu 2020], wananchi walitueleza kwamba watu wa Serikali hawatufikii,” alisema Dk Mwinyi wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo. “Malamiko yetu hatujui tuyapeleke wapi. Kwa hiyo, wakaniomba, wakisema kwamba safari hii ukifanikiwa [kuwa Rais], basi hakikisha unatafuta njia nzuri ya sisi kuweza kufikisha malalamiko yetu [kwako].”

Hata baada ya kuwa Rais, Dk Mwinyi alisema kwamba kila alikokuwa anakwenda kukagua kazi ambazo Serikali inafanya visiwani humo, watu walikuwa wakinyoosha mikono wakitaka kuwasilisha malalamiko yao kwake.

“Siyo rahisi kwa yeyote katika sisi watendaji wa Serikali kusema kwamba utamfata kila mtu alipo,” alisema Dk Mwinyi. “Lakini ni rahisi kutafuta njia ya wao [wananchi] kutufikia. Moja ikiwa ni [huu mfumo].”

Mratibu wa Sema na Rais Mwinyi kutoka Ikulu ya Zanzibar Haji Khamis Makame aliieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake mnamo Februari 1, 2022, kwamba kati ya malalamiko 7,089 ambao Ofisi ya Rais Mwinyi imepokea, asilimia 74.3 yamepatiwa ufumbuzi huku mengine yakiendelea kutafutiwa ufumbuzi.

“Mfumo umepokea malalamiko 7,089 ambayo yametumwa na wananchi,” alibainisha Makame. “Utatuzi kwa asilimia fulani ni mkubwa ambao umefanyika kwa sababu mpaka leo hii tunapozungumza [Feb 1] ni asilimia 74.3 ya utatuzi.”

Makame alieleza kwamba kuna njia mbili ambazo mwananchi anaweza kuzitumia kupitia mfumo huo wa kieletroniki na kuweza kuwasilisha kero yake kwa Rais Mwinyi. Ya kwanza ni ya kutumia App maalum; hii ni kwa wale wanaotumia simu janja. Hawa wanaweza kwenda kwenye Google Play au App Store na kupakuwa App hiyo.

Njia nyengine inayotumika ni kupitia simu ndogo ambapo mwananchi anaweza kupiga simu bure kwenda 0772 444 449 na kufuata maelekezo ya namna ya kuwasilisha kero yake.

“Wale wanaosema labda kuna taarifa zinachujwa wawe na imani kwamba hizo taarifa zinamfikia mwenyewe [Rais Mwinyi],” alibainisha Makame baada ya The Chanzo kumuuliza kama kuna uchujaji wowote wa malalamiko yanayowasilishwa na wananchi.

Licha ya mfumo huu kuonekana mzuri katika mchakato mzima wa kuwaweka viongozi karibu na wananchi wao, jitihada zitahitajika zaidi kuwaelimisha wananchi juu ya uwepo wake kwani wengi ya wananchi walioulizwa na The Chanzo kama wanafahamu uwepo wa mfumo huo walijibu hapana.

“Mimi binafsi sielewi njia yoyote, ama utaratibu ambao naweza kutumia, nikaweza kufikisha taarifa zangu ama malalamiko kwa Mheshimiwa Raisi ama wale ambao wanaweza kuhusika katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali,” anasema Abdalla Kombo Ali, dereva wa bodaboda.

“Hapana sijawahi kuisikia na ndio kwanza nakusikieni nyinyi kuhusu mfumo huo,” Sabrina Khalifa, mkazi wa Chuini kisiwani hapa, ameiambia The Chanzo.

Wakati Dk Mwinyi anaamini kwamba mfumo huu hauwezi kuwa na ufanisi wa asilimia 100 katika juhudi za Serikali kutatua kero za wananchi, Rais huyo wa nane wa Zanzibar anaamini kwamba hatua hiyo ni mwanzo mzuri kuelekea uboreshaji wa uwajibikaji serikalini.

“Mfumo huu utatuonesha, ni nani [ndani ya Serikali] ambaye hatimizi wajibu wake,” alisema Dk Mwinyi wakati wa uzinduzi wa mfumo huo. “Mfumo huu utatuonesha, ni nani analalamikiwa zaidi. Kwa hiyo, mimi kama kiongozi wa Serikali, nitakuwa natambua kwamba matatizo mengi yako wapi na tufanye nini.”

Salim Khamis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe alimkombo437@gmail.com.

Salim Khamis Kombo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved