The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rostam Aziz Adaiwa Kushikilia Zaidi ya Bilioni Tatu za Mafao ya Wafanyakazi Wake wa Zamani 

Wafanyakazi hao wanamlalamikia Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo wakati wafanyakazi hao kutoka idara mbalimbali na maeneo mbalimbali ya nchi walikuwa wakiitumikia kampuni hiyo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Jumla ya wafanyakazi 200 wa zamani wa kampuni ya habari ya New Habari (2006) Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz wamejitokeza hadharani na kumshutumu bilionea huyo kushikilia jumla ya Shilingi bilioni 3.4 baada ya kushindwa kupeleka fedha hizo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kipindi cha miaka 10.

Wakiongea na waandishi wa habari mnamo Februari 3, 2022, wafanyakazi hao ambao waliachishwa kazi mnamo Mei 31, 2019, pia wanamlalamikia Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo wakati wafanyakazi hao kutoka idara mbalimbali na maeneo mbalimbali ya nchi walikuwa wakiitumikia kampuni hiyo inayozalisha magazeti ya Mtanzania, The African, Rai, Dimba na Bingwa.

Baadhi ya wafanyakazi hawa tayari wameshafariki kabla ya kupata mafao yaliyopaswa kutolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni wa PPF ambao kwa sasa unajulikana kama Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Kati ya hawa wamo Elia Mbonea, aliyekuwa Mhariri wa Kanda ya Kaskazini; Mwalimu Kresesto Rweyemamu, Mhariri wa maudhui ya habari; na Inocent Mnyuku, Mhariri wa habari wa gazeti la Rai. Juhudi za kupigania mafao ya hawa kwa sasa zinaendelezwa na familia zao husika.

“Ukandamizaji huu wa haki zetu na ukiukwaji wa sheria za nchi, ni kinyume kabisa na msimamo wa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan iliyojipambanua kuwa mstari wa mbele katika kutetea na kulinda haki za watu wake, hususan wananchi wanyonge wakiwemo sisi,” alisema Arodia Peter, Katibu wa umoja wa wafanyakazi hao, wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari.

“Tunampa Rostam siku 11 kuanzia leo Februari 3, 2022, awe amepeleka fedha zetu za mafao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii huskia,” aliongeza Arodia. “Asipotekeleza hilo, tutafanya maandamano ya amani yasiyokuwa na ukomo nyumbani kwake pamoja na ofisini kwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe na kwenye ofisi za mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSSSF hata kama hatua hiyo itagharimu maisha yetu.”

The Chanzo ilimtafuta Bashe kwa simu kumuuliza aliwezaji kuruhusu mafao ya wafanyakazi hawa 200 kutokupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kipindi cha miaka kumi yeye akiwa Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo. Lakini tulishindwa kumpata baada ya simu yake kuita bila kupokelewa na kushindwa kujibu ujumbe mfupi wa simu alitumiwa.

Tulimtafuta Rostam Azizi pia kumuuliza kama anafahamu madai ya wafanyakazi hawa na kama yalikuwa na ukweli wowote lakini hatukumpata baada ya simu yake kutokupatikana hewani.

NSSF, PSSSF zatupiwa lawama

Sababu ya wafanyakazi hao kupanga kufanya maandamano kwenye ofisi za NSSF na PSSSF ni kutokana na mtazamo wao kwamba mamlaka hizo za Serikali zimeshindwa kuwa na msaada kwao, huku wakijiuliza inawezekana vipi mamlaka hizo zilishindwa kumchukulia hatua yoyote mwajiri ambaye ameshindwa kulipa mafao ya wafanyakazi wake kwa kipindi cha miaka 10.

Pia, wafanyakazi hao wamedai kumepeleka malalamiko yao sehemu mbalimbali za Serikali ambazo walidhani wangelipatiwa ufumbuzi wa tatizo lao, ikiwemo kwenye mifuko yenyewe kama NSSF na PSSSF, bila kupata msaada wowote.

“Hapa tulipofikia tumechoka,” alisema Arodia kwa niaba ya wafanyakazi wenzake. “Na tunasema kwamba hatuna imani na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa wameshindwa kuwajibika kwa kuwabana aliyekuwa mwajiri wetu na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni Hussein Bashe na Rostam Aziz.”

The Chanzo ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Profesa Godius Kahyarara kumuuliza kama anafahamu malalamiko ya wafanyakazi hawa na kama ofisi yake ina mpango wowote wa kuyafanyia kazi lakini simu yake iliitia bila kupokelewa na ujumbe aliotumiwa kwenye WhatsApp kutokujibiwa.

Wafanyakazi hawa wanaamini kwamba mwajiri wao huyo wa zamani ana uwezo wa kuwalipa mafao yao hayo siyo kwa sababu tu ni bilionea anayetambulika ndani na nje ya nchi.

Bali pia kwa sababu Serikali ilichukua hatua mahususi na za makusudi kuwasaidia waajiri kama yeye wanaodaiwa malimbikizo makubwa ya madeni ya mafao na wafanyakazi wao kwa kutangaza msamaha wa asilimia 100 wa riba kwenye ulipaji wa madeni hayo.

Msamaha huo ambao ulianza Oktoba 1, 2021, hadi Januari 31, 2022, ili waondolea waajiri wa sekta binafsi tozo zote zitokanazo na ucheleweshwaji wa michango husika kwa kiwango cha asilimia 100.

“Hata hivyo, mpaka muda huu tunapozungumza nanyi waandishi wa habari,” alibainisha Arodia. “Mwajiri [wetu wa zamani] bado hajafanya chochote licha ya kwamba aliyekuwa Afisa Mtendeji Mkuu wa kampuni Hussein Bashe ni waziri katika Serikali hii [ya awamu ya sita].”

Ni sehemu tu ya tatizo kubwa

Tatizo la waajiri katika sekta binafsi ya habari kukabiliwa na shutuma za kuchelewesha au kutokulipa kabisa stahiki za wafanyakazi wao wa zamani au wanaoendelea na kazi ni kubwa sana nchini Tanzania na wakati mwengine waandishi wa habari huibua malalamiko hata sehemu ambayo usingeweza kuyatarajia.

Kwa mfano, mnamo Januari 12, 2022, waandishi wa habari waliokuwa wameshiriki hafla ya kuaga miili ya wenzao watano waliofariki katika ajali ya gari walitumia nafasi hiyo kumuomba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari nchini.

Nape, ambaye alikuwa ni mmoja kati ya waombolezaji katika msiba huo, alielezwa kwamba wengi wa waandishi wa habari nchini, wakiwemo baadhi ya marehemu waliokuwa wanaagwa, hawajalipwa mishahara na stahiki zao kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Nape alitoa siku saba kwa waajiri wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali hiyo kulipa stahiki zao, na kuongeza: “Yawezekana kuna hali ngumu ya kiuchumi, lakini nasema stahiki zote za marehemu hawa zilipwe ndani ya siku saba. Hayo ya hali ngumu tutayazungumza huko mbeleni kwa waandishi ambao wako hai ila kwa hawa marehemu lazima walipwe.”

Kwa Arodia na wafanyakazi wenzake 199 wanaodai stahiki zao kutoka kwa mwajiri wao wa zamani Rostam Aziz, kauli hii ya Nape, japo ilihusu waandishi waliotangulia mbele ya haki, ilikuwa ya faraja na matumaini kwamba na wao siku moja watapata stahiki zao.

“Kwa kauli na msimamo huu wa Serikali, tunaamini kilio chetu hiki kitapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Arodia. “Tunawaomba pia washiriki wa mfanyabiashara Rostam Aziz, wa nje na ndani ya nchi, wamshauri bilionea huyu kufuata sheria za nchi na haki za binadamu kwa kulipa mafao halali ya wafanyakazi.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *