The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Barua ya Wazi kwa Waziri Bashe Juu ya Mradi wa ‘Ujenzi wa Kesho Njema’

Kabla ya kujishughulisha na kesho ya wakulima, tumetafakari leo yao watu hao inatoa matumaini na hamasa kwa kuwapa nyenzo na huduma, kama ardhi, huduma za kifedha, masoko na teknolojia zenye kuridhisha hivyo na hivyo tunapaswa kuhama kwenda kwenye kundi lingine ambalo ni vijana?

subscribe to our newsletter!

Ndugu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kwanza nikupongeze kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa na kuaminiwa katika kuwatumikia Watanzania kupitia wizara ambayo inasimamia shughuli ya kiuchumi inayotegemewa na zaidi ya asilimia sitini ya wananchi.

Ni matumaini yangu kwamba kutokana na ukweli kwamba historia ya maisha yako imejijenga katika sekta hii ya  kilimo na ufugaji, ukiongezea na hulka yako ya udadisi uliyonayo, ni dhahiri kwamba wizara hii imepata mtu sahihi.

Lakini kilichonisukuma nikuandikie leo ni kuhusu mradi wa Ujenzi wa Kesho Njema ambao kwa kimombo umeuita Building a Better Tomorrow Project ambao hivi karibuni ulitueleza kwamba utawagusa vijana kwa kutengewa maeneo ya kilimo, au kwa kimombo agriculture parks na tayari Serikali imetenga takribani Shilingi bilioni tano kama kianzio na kuwaalika wadau mbalimbali watakaoguswa na mradi huu.

Ndugu Waziri, jitihada hii naomba tuitazame kwa jicho pevu la kihistoria, kitabaka na kuzingatia muktadha tulionao kama jamii ambapo kundi la wakulima ndio kubwa, kwani Watanzania takribani milioni 40 wanajishughulisha na kilimo.

Tunalenga kesho, leo tumeiweka sawa?

Kutokana na ukweli kwamba wakulima ndiyo kundi linaloongoza Tanzania, binafsi baada ya kusoma mpango wa Serikali kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Kesho Njema, nilijiuliza: Je, leo ya wakulima, ambao kwa sehemu kubwa wapo chini ya wizara yako, ipoje? Je, wengi wao kilimo kinawapa hamasa na motisha? Kwa nini tuangazie kesho na sio leo yao?

Ukiangalia kundi kubwa la wakulima leo hii ni wakulima wadogo kwa tija. Sasa tujiulize, ni kwamba leo yao watu hao inatoa matumaini na hamasa ya kutosha kwa kuwa na nyenzo na huduma muhimu kama ardhi, huduma za kifedha, masoko na teknolojia kiasi ya kwamba sasa tunapaswa kuhama kwenda kwenye kundi lingine ambalo ni vijana?

Kama tungefanikiwa kwenye kundi hili la wakulima wadogo kungekuwa na haja ya kuweka nguvu ya mradi wa kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo? Mheshimiwa Waziri, huoni kama msemo wa Waswahili usemao, Kizuri chajiuza kibaya chajitemebeza ungalifaa katika hili?

Kumekuwepo na taarifa nyingi za migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji au wakulima/wafugaji dhidi ya mamlaka za usimamizi wa maeneo yaliyo hifadhiwa, au migogoro baina ya wakulima dhidi ya taasisi za umma na binafsi. 

Je, hii ardhi tunayoiahidi kwa vijana iko wapi, mbona hatuioni ikijitokeza katika kuokoa damu zinazomwagika dhidi ya ndugu zetu wanaouana wakigombania ardhi kwa ajili ya uzalishaji katika kilimo na ufugaji? 

Inawezekanaje wakulima na wafugaji waliopo wakawa na changamoto za ardhi mpaka kufikia hatua ya kutoana uhai lakini tukawa na ardhi maalum kwa ajili ya kundi la vijana?

Mradi wa vijana ulivyofukarisha kaya 50 Morogoro

Mheshimiwa Waziri, labda nikushirikishe kisa kimoja kilichotokea kata ya Msowero, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro mwaka 2019 ukiwahusisha vijana wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kupitia uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa wakati huo Stephen Kebwe ambapo mwisho wa siku mradi huo ulikufa na kufukarisha kaya zaidi ya 50 ambazo ardhi yao ilichukuliwa na mradi huo kimabavu. 

Wakulima walipohoji ni kwa nini wanatendewa vile waliambiwa eneo hilo ni pori ambalo limetengwa kwa ajili ya vijana wasomi wa chuo kikuu. 

Walipohoji mbona kiuhalisia eneo lilikuwa na maotea ya mpunga kuashiria linatumiwa na wakulima na lilikuwa limefyekwa na kubakizwa miti michache kwa ajili ya kutunza bionuai, na pia kama ni suala la vijana, mbona katika kaya zinazolima eneo hilo kuna vijana pia ambao maisha yao yanategemea ardhi hiyo kwa miaka yote?

Maswali hayo katika nyakati zote yalipokuwa yakiulizwa, yalijibiwa kwa vijana kubambikiwa kesi na kuswekwa mahabusu, huku akina mama na wazee wakiogopa kwenda mashambani kutokana na nguvu ya dola na hivyo vijana walioletwa kwa uratibu wa Serikali wakaendelea na uzalishaji. 

Mapambano ya wakulima hayakufua dafu dhidi ya nguvu ya dola na hatimaye vijana wasiozidi watano wakazifukarisha kaya zaidi ya 50, huku vijana wenzao wakazi wa Msowero wakiishia mahabusu kwa kujaribu kutetea maeneo waliyopokonywa. 

Mnamo Julai 2019, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wako, akiwa na viongozi wa mkoa na wilaya, walishiriki katika tukio la kufurahia matunda (mavuno) ya uwekezaji wa vijana kutoka SUA, kama vile wakulima wazawa waliopokonywa maeneo hayo hawakuwahi kuzalisha au hawakuwa wamewekeza katika kilimo!

Ziara ya Mavunde ilikiwa chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya dola, inawezekana ni hali ya kawaida kwa viongozi wa kitaifa, lakini kwa wahanga hiyo ni ishara ya kuonywa kutosogea katika mashamba waliyopokonywa. 

Hii ni kwa sababu kwa utamaduni wa Kitanzania, hakuna anayekwenda shambani kuvuna mazao yake halali katika eneo lake halali akiwa na wadau wake muhimu huku wakilindwa na dola kwa mitutu ya bunduki. 

Tukio hilo lilifana kwenye vyombo vya habari likipambwa kwa makala ndefu na picha za mnato za kuvutia huku ujumbe wake ukipotosha kwa kiasi kisichomithilika.

Wakati huo huo wakulima walikiwa na ukiwa usiomithilika kwa kupoteza ardhi ambayo ni uhai katika maisha yao. Taarifa hii ni kwa muktadha wa wakulima wadogo wakazi na waathirika wa eneo husika. 

Je, aina hii ya miradi ndio mwelekeo tunaotakiwa kuutazamia kutoka kwako, Mheshimiwa Waziri? Kama ekari 50 tu ziliweza kuleta simanzi na ufukara kwa kaya zaidi ya 50, je, hizo agricultural parks zitaleta kimbunga cha kadhia ya aina gani kwa wakulima?

Je, taswira ya kilimo inawavuta vijana katika kilimo?

Kwa upande mwingine, huduma za kifedha na mfumo wa masoko utakuwa mikononi mwa nani? Ni juu ya mabenki haya haya ya kibiashara yanayowabagua wakulima wadogo kwa misingi kwamba hawakopesheki na hawazalishi kwa tija? 

Katika teknolojia, je, vyuo vyetu vya ufundi vimekuwa na mchango gani katika kutengeneza zana zenye kukidhi mahitaji na uhalisia wa maisha yetu? Au mradi unategemea kutumia teknolojia zisizoshabihiana na mahitaji wala uhalisia wa wakulima wa Tanzania kwa sababu tu anayetupatia anafanya hivyo kwa kutoa msaada? 

Ikiwa teknolojia haitakuwa mikononi mwetu, uendelevu wake utakuaje, athari zake kiuchumi, kimazingira na kijamii zikoje?

Tukumbuke pia vijana ni kundi linalohama hama na lenye kutega sikio na kukimbilia kwenye kila fursa, sijui tumejipangaje kwenye hili. 

Kwa hakika ni kwamba wale vijana waliopora ardhi za wakulima pale Msowero hawaendelei tena na kilimo na kampuni zilizowadhamini kwa pembejeo haziendelei kufanya hivyo mpaka sasa. 

Mheshimiwa Waziri, Waingereza wanasema, People respond to incentives. Je, taswira ya kilimo na wakulima inawavuta vijana katika kilimo?

Nisikuchoshe ndugu Waziri, natumai andiko la mradi linaweza kuwa na maelezo mengi yenye majibu kuhusu maswali yangu. Lakini kwa ulichokieleza kwenye ujumbe wako, huu ndio mchango wangu mdogo kwako kama ulivyoomba. 

Asante na nakutakiwa kila la kheri kwenye utekelezaji wa majukumu yako!

Michael Neligwa ni mdau wa maendeleo vijijini na haki za wazalishaji wadogo. Anapatikana kwa barua pepe yake neligwamichael@yahoo.com au kupitia Twitter @MichaelNeligwa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *