The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanasiasa, Wanaharakati Wataka Masheha Wapigiwe Kura Zanzibar

Kumekuwapo na tuhuma kwamba katika utekelezaji wa majukumu yao Masheha wamekuwa wakikipendelea chama cha CCM na wakila njama za kuvidumaza vyama vya upinzani. Tuhuma hizi huibuka zaidi wakati wa michakato ya chaguzi kuu kuanzia utoaji wa kadi za Mzanzibari Mkaazi na usajili wa daftari la wapiga kura.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Tofauti na wenzao upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano, wananchi wa Zanzibar hawana fursa ya kuchagua wenyeviti wao wa Serikali za mitaa, ambao visiwani humo hujulikana kama Masheha, licha ya watu hao wanaopatikana kwa kuteuliwa na wakuu wa mikoa kuwa na nguvu kubwa za kuamua maisha ya kila siku ya Wazanzibari.

Kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya mwaka 2014 ya Tawala za Mikoa kifungu cha 8 (1) ya Zanzibar, Mkuu wa Mkoa anaweza kuteua Masheha wa mkoa husika, huku vigezo vinavyotakiwa ni mtu anayeteuliwa kuwa Mzanzibari; anayeheshimika; mkazi wa eneo husika ambalo linaitwa Shehia; mwenye uadilifu; mwenye umri wa miaka 40 au zaidi; na aweze kusoma na kuandika.

Sheria hiyo inataja majukumu ya Sheha ambayo ni pamoja na kusimamia sheria, sera na maagizo yote ya Serikali kwenye Shehia yake; kutatua migogoro na kufanya usuluhishi; kusajili ndoa, talaka, vifo na vizazi; kutoa vibali vya kusafirisha mazao, mifugo na mkaa; kusimamia uhamiaji; kupokea taarifa za kufanyika kwa mikutano ya hadhara; na kusimamia fedha, rasilimali watu na mali zingine za Serikali kwenye Shehia husika.

Wakati Sheha anategemewa kutimiza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye sheria, Zanzibar siyo mgeni wa malalamiko yanayohusu namna Masheha wanavyotoa huduma zao kwa misingi ya vyama vya siasa, huku wakidaiwa kuwapa vipaumbele watu wanaothibitika kuwa ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kunyima huduma hizo kwa watu wanaoonekana kuwa ni upinzani.

Hali hii hudhihirika zaidi kipindi cha uchaguzi ambapo Zanzibar hukumbwa na myukano mkali wa kisiasa, kwa Masheha kudaiwa kushindwa kuwapa wananchi wanaonekana wa upinzani barua zinazoweza kuwafanya wapate kitambulisho cha uraia cha ZAN ID au cha kile cha mpiga kura.

Kesi za Masheha kuwaambia wananchi kwamba siyo wakazi wa Shehia husika ili wakose fursa ya kushiriki kwenye mchakato wa kidemokrasia kama vile kupiga au kupigiwa kura wakati wa uchaguzi zimekuwa zikiripotiwa kwa kiasi kikubwa visiwani humo, hali inayowasukuma wanaharakati na wanasiasa wa upinzani kudai mageuzi yatakayowawezesha wananchi kuchagua Masheha wao badala ya kuteuliwa.

“Utaratibu huu wa Masheha kuteuliwa ni tatizo kwetu sisi [kama chama cha upinzani],” Juma Duni Haji, mwenyekiti wa taifa wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo anaieleza The Chanzo. “Sheha ana nguvu zaidi kuliko hata diwani ambaye anayechaguliwa. Diwani wetu anachaguliwa lakini hana nguvu. Sheha anayeteuliwa na Mkuu wa Mkoa ana nguvu zaidi. Hili inabidi libadilike.”

Abdallah Abeid ni mdau wa maendeleo ya vijana anayefanya kazi na ​​Shirika la Kupambana na Changamoto Zinazowakabili Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) anayeamini kwamba shutuma nyingi wanazotupiwa Masheha, kama zile za kupendelea wafuasi wa CCM dhidi ya wafuasi wa upinzani, zimeshindwa kutatuliwa kwa sababu wananchi hawana mamlaka yoyote juu ya upatikanaji wa watu hao.

“Wapo Masheha ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwamba wamekuwa hawatoi huduma kama ambavyo inatakiwa,” anasema Abeid wakati akizungumza na The Chanzo. “Kwa hiyo, nadhani wakiwa wanatokana na wananchi ni rahisi pia kuwawajibisha kwa sababu wananchi wenyewe ndio watakuwa na mamlaka ya kuwawajibisha.”

Ni ipi asili ya mfumo wa Masheha Zanzibar?

Wanahistoria wanashindwa kubainisha ni lini haswa mfumo wa kutumia Masheha ulianza kutumika Zanzibar. Hata hivyo, wasomi hao wanakubaliana kwamba mfumo huo ulikuwa mfumo wa utawala hata kabla ya ujio wa Washirazi katika miji ya Tumbatu na Nungwi kisiwani Unguja mnamo karne ya 10.

Inaaminiwa kwamba zama hizo kulikuwa na Mwinyi Mkuu na chini yake walikuwepo mamwinyi wa sehemu mbalimbali. Chini ya mamwinyi walikuwa Masheha. Wanahistoria wanabainisha kwamba wanawake ndiyo waliokuwa watawala asilia wa Zanzibar katika zama hizo ambao walikuwa wakirithiwa na wanawake wenzao. Mfano mzuri ni wa Mwana wa Mwana wa Tumbatu.

Dk Abdulaziz Lodhi, Profesa mstaafu wa Kiswahili na Lughawiya ya Kibantu (Bantu linguistics) katika Chuo Kikuu cha Uppsala, nchini Sweden, aliieleza The Chanzo kwenye mahojiano mafupi kwamba neno Sheha huenda likawa limetokana na lugha ya Kiarabu kwani kwa Kiarabu mkubwa wa mji huitwa Sheikh akiwa mwanamume na Sheikha akiwa ni mwanamke.

“Inawezekana,” alisema Profesa Lodhi, “kwamba Sheikha lilibadilika na kuwa Sheha kulingana na lafudhi ya kikwetu,” akimaanisha Kizanzibari. “Katika Kiswahili kuna neno shaha lenye maana ya mshairi mkuu katika mji na kila mji ukichagua shaha wake. Na kila mwaka akichaguliwa ‘shaha wa mashaha’ aliyekuwa mshairi mkubwa kabisa.”

Naye Abdul Sheriff, Profesa mstaafu wa historia aliyeandika vitabu vingi kuhusu historia ya Zanzibar, ameiambia The Chanzo kwamba Washirazi wa Zanzibar walianza kutawaliwa moja kwa moja na Waomani wakati wa enzi ya Sultani wa pili wa Zanzibar, Seyyid Barghash bin Said bin Sultan (aliyetawala kati ya mwaka 1837 na mwaka 1888).

Kwa mujibu wa Profesa Sheriff, Barghash ndiye aliyeanza kuwateua Masheha kuanzia miaka ya 1870.  Katika enzi hizo za usultani, anaongeza msomi huyo, Sheha alikuwa akiteuliwa kuwa mwakilishi wake sultani katika Shehia yake. Mbele ya nyumba ya sheha kulikuwepo bendera nyekundu, iliyokuwa bendera ya sultani, ikimaanisha kwamba yeye ndiye aliyekuwa mwakilishi wake.

Ahmed Rajab ni mwandishi wa habari wa siku nyingi anayeishi nchini Uingereza ambaye alibahatika kuishi Zanzibar kabla ya uhuru wa Disemba 10, 1963, na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Akiongea na The Chanzo, Rajab anakumbuka kwamba siku hizo kulikuwako na Masheha katika mitaa ya ng’ambo na sehemu za mashamba Unguja lakini Mji Mkongwe haukuwa na Sheha.

Masheha walikuwa wakipendwa, kuheshimika

“Kwa ujumla, zamani Masheha walikuwa wakipendwa na kustahiwa na wanajamii,” anakumbuka Rajab. “Hata baada ya kuanza kwa siasa za ushindani wa vyama vingi katika miaka ya kati ya mwongo wa 1950 Masheha hawakuonekana wakipendelea upande mmoja au mwingine, chama kimoja au kingine.”

Kwa mujibu wa Rajab, baada ya Mapinduzi, Serikali ya Zanzibar ilifuta mfumo wa Masheha na badala yake kazi nyingi za usheha zilikuwa zikifanywa na wenyeviti wa matawi ya chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) pamoja na makatibu wao.  Baadaye, Zanzibar ikaiiga Tanzania Bara kwa kuwa na Balozi wa Nyumba Kumi Kumi, ambao Rajab anasema walikuwa “wakitisha na wakiogopwa.”

Mfumo wa Masheha Zanzibar ulifufuliwa na Serikali ya awamu ya tano chini Rais Dk Salim Amour ulioanza mnamo 1990, hali ambayo Rajab anaamini iliambatana na mabadiliko makubwa ya namna watu hao wanavyofanya kazi.

“Masheha walianza kutumika kama makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama kinachotawala,” anasema. “Kumekuwapo na tuhuma nyingi kwamba katika utekelezaji wa majukumu yao Masheha wamekuwa wakikipendelea chama cha CCM na wakila njama za kuvidumaza vyama vya upinzani.  Tuhuma hizi huibuka zaidi wakati wa michakato ya chaguzi kuu nchini kuanzia utoaji wa kadi za Mzanzibari Mkaazi na usajili wa daftari la wapiga kura.”

Shutuma nyingine zinazoelekezwa kwa Masheha ni kwamba watu hao wamekuwa wakituhumiwa kuwanyima wapinzani haki zao za kiraia na za kikatiba.  Sambamba na yote hayo, Masheha wamekuwa wakishutumiwa kuwanyima Wazanzibari halisi haki zao huku wakiwapa haki hizo wageni waliohamia Zanzibar kutoka sehemu nyingine za Tanzania, kwa mujib wa Rajab anayeishi nchini Uingereza.

CCM yakataa kuhusika na Masheha

Dk Abdulla Juma Mabodi ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) ambaye anakanusha chama chake kupendelewa na Masheha visiwani humo, akisema: “Sisi hatuhusiani na Masheha. Chama Cha Mapinduzi hakihusiani na mambo ya Masheha. Siwezi kuzungumzia madai kwamba Masheha wanalinda maslahi ya CCM. Wazungumze wenyewe.”

The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohamed kufahamu kwamba upo uwezekano wa Serikali kubadilisha utaratibu unaotumika kuwapata Masheha lakini juhudi zetu zilishindwa kuzaa matunda baada ya simu zake kutokupokelewa na ujumbe mfupi aliotumiwa kutokujibiwa.

Thabiti Juma ni wakili anayefanya kazi na Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Kuangalia Chaguzi Tanzania (TACCEO) kutoka Zanzibar ambaye anaiambia The Chanzo kwamba Serikali ya Zanzibar haiwezi kuendelea kulifumbia macho suala na kwamba ni muda muafaka sasa kwa Zanzibar kuiga wenzao wa Tanzania Bara kwa kuruhusu wananchi wachague Masheha wao

“Ikiwa [Masheha] watapigiwa kura, watakuwa wanawajibika moja kwa moja kwa wananchi na siyo kufanya kazi kwa lengo la kukidhi matakwa ya Mkuu wa Mkoa [anayewateua],” anasema Juma. “Mtu kama anapigiwa kura kidogo nadhani ule urasimu wa kila kitu kumkatalia mtu utaondoka.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *