Zanzibar. Wakulima wa mwani visiwani hapa wamelalamikia maslahi duni wanayoyapata kutoka kwenye kilimo cha zao hilo la biashara hali wanayosema inatokana na kulazimika kuuza bidhaa yao kwa bei ndogo isiyolingana na uwekezaji wa kifedha na nguvu kwenye uzalishaji wake.
Wakulima hao kutoka kijiji cha Kisakasaka, mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja walikuwa wakizungumza na The Chanzo iliyofika kijijini hapo hivi karibuni kufahamu maisha ya wakulima wa mwani na kupata mtazamo wao wa namna Serikali inaweza kuboresha maslahi yao.
Wakati wanakiri kwamba bei ya kilo moja ya mwani uliokaushwa imepanda kutoka Sh600 tu hadi Sh2,000, wakulima hao, wengi wao wakiwa ni wanawake, wanasema bado bei hiyo haiakisi juhudi wanazochukua kuendeleza kilimo hicho na maumivu ya kimwili yanayoambatana nazo.
“Maslahi yanayotokana na ukulima wa mwani hayaridhishi kusema ukweli,” anasema Mariam Salum, mama wa watoto watatu ambaye amekuwa akijishughulisha na kilimo hicho kwa kipindi cha miaka mitatu sasa. “Hii ni kwa sababu baada ya kuuuza huo mwani, faida inakuwa ni ndogo sana baada ya kutoa gharama ulizotumia kulima mwani huo.”
Gharama za uzalishaji
Kutokana na mazungumzo kati yake na wakulima hawa, The Chanzo iliweza kubaini mambo kadhaa yanayowapunguzia wakulima wa mwani tija kutoka kwenye kilimo chao.
Jambo la kwanza ni usafirishaji wa mwani kwa kutumia boti kutoka baharini unakolimwa mpaka nchi kavu na kutoka bandarini mpaka sehemu ya ukaushaji ambapo mara nyingi gari za ng’ombe ndiyo hutumika.
Gharama nyingine wanayoingia wakulima hawa ni za zana na vifaa vinavyohitajika ili kufanikisha kilimo chenyewe ikiwemo kamba, miti, taitai, mitaimbo pamoja na vifaa vya kujikinga wao wenyewe dhidi ya athari wanazoweza kuzipata wakiwa kazini.
Hivi vinajumuisha vitu kama vile viatu vinavyoweza kuwakinga dhidi ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali wakati wakitembea baharini wakifanya shughuli zao za kilimo.
“Mwani ni lazima upandishwe bei kama wakulima wanatakiwa wanufaike na kilimo hicho,” anasema Khadija Abdallah Seif, 25, mama wa mtoto mmoja ambaye amekuwa akilima mwani kwa kipindi cha miaka mitatu. “Pia, tusaidiwe kwenye vitendea kazi. Serikali ni lazima itutazame kwa macho yote mawili.”
Suala la maslahi duni yatokanayo na kilimo cha mwani kwa wakulima wa zao hilo ni suala ambalo pia linamsumbua Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi.
Wakati wa mkutano wake wa kila mwezi na waandishi wa habari uliofanyika mnamo Februari 28, 2022, kwa mfano, Rais Mwinyi alieleza dhamira yake ya kuhakikisha wakulima wa zao la mwani wanakuwa na soko la uhakika, kitu ambacho anaamini kitaimarisha maslahi yao.
Ujenzi wa kiwanda cha mwani
“Tunajenga kiwanda kule Pemba, [maeneo ya] Chamanangwe, [mkoa wa Kaskazini] kwa lengo la kuhakikisha kwamba wakulima wa mwani wanapata soko la uhakika,” Dk Mwinyi aliwaeleza waandishi wa habari. “[Kwamba] wakulima wanapata bei nzuri kuliko wanayopata sasa.”
Kiwanda hicho ambacho jiwe lake la msingi liliwekwa na Rais wa awamu ya saba wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein mnamo Septemba 18, 2020, kinajengwa kwenye eneo hilo la viwanda lililopo Chamanangwe, Pemba.
Akijibu swali kuhusu hatua ya ujenzi ambao kiwanda hicho kimefikia kwa sasa, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban alisema kwamba ujenzi wa kiwanda hicho ulikwama kidogo kwani Serikali ilikuwa inafikiria namna bora za kukiendesha ili kiwe na tija kwa uchumi wa Zanzibar.
“Tulikuwa tunaandaa utaratibu mzuri wa kukiendesha hiki kiwanda,” alisema Shaaban wakati wa mahojiano na The Chanzo kwa njia ya simu. “Ila mimi nilipoteuliwa kama Waziri niliamua kusukuma mbele hili jambo. Kwa maana tunataka tukiendeshe hiki kiwanda kibiashara. Tayari utaratibu huo umeanzishwa na hivyo ujenzi utaanza hivi karibuni.”
Utaratibu anaozungumzia Shaaban ni ukamilishwaji wa uundwaji wa kampuni tanzu inayojumuisha mashirika matano ya umma kutoka Zanzibar inayojulikana kama Zanzibar Seaweed Company Limited itakayokuwa na jukumu la kuendesha kiwanda hicho.
Mashirika hayo ni Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Shaaban anasema tayari jumla ya Shilingi bilioni 3.4 zimetengwa kama mtaji uliochangiwa na mashirika hayo ambayo itatumika kugharamia ujenzi wa kiwanda hicho.
“Kampuni tayari imeshaundwa na kila mdau ameshaleta mwakilishi wake,” anaeleza Shaaban.
“Kilichobaki ni kupatikana kwa Mkurugenzi Mtendaji tu ili kazi ianze,” anaongeza. “Sasa, kwa mujibu wa utaratibu ni kwamba Rais ndiyo atamteua Mkurugenzi Mtendaji wa hiyo kampuni. Na tayari nimeshatuma jina la mtu kwa Rais [Mwinyi] wa kuteuliwa kwenye hiyo hiyo.”
Utafiti, sera madhubuti
Said Ali M’barouk ni Mratibu wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo kisiwani Pemba ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Kilimo wa Zanzibar. Licha ya kuamini kwamba kiwanda hicho kinaweza kupunguza baadhi ya matatizo yanayokikabili kilimo cha mwani Zanzibar, M’barouk anaishauri Serikali iende zaidi ya hapo kwa kufanya utafiti wa kina kuhusu kilimo hicho na kuweka sera madhubuti itakayokiongoza.
“Kuna haja ya kufanya utafiti wa kina juu ya uzalishaji wa zao la mwani Zanzibar,” anasema M’barouk. “Utafiti ambao utabainisha ni maeneo yapi sahihi zaidi kwa ajili ya kilimo hiki. Ni aina gani ya mwani inastawi vizuri Zanzibar? Ni mbegu zipi nzuri zinaweza kutupatia mwani nzuri na mbegu hizo zitapatikana wapi na vipi?”
Kwa mujibu wa M’barouk, kwa sasa wakulima wa mwani visiwani Zanzibar ni kama vile wameachwa wapambane wenyewe kwenye kutafuta majibu juu ya maswali haya na hivyo kuishauri Serikali iingilie kati.
Kuhusiana na suala la ujenzi wa kiwanda na matumaini ya kukuza tija ya wakulima wa mwani, M’barouk amesema ni lazima itamkwe wazi kwamba kiwanda hicho kitanunua mwani mbichi na siyo ule uliokaushwa.
“Kununua mwani uliokaushwa ni kumuangamiza mkulima kwani atauza kilo chache sana na hivyo maslahi yake kutokuongezeka,” anabainisha. “Pia, Serikasli isiachie sekta binafsi kwa asilimia 100 kwenye kupanga bei za kununua mwani. Ni muhimu Serikali ikafikiria namna ya kuingilia kati.”
Mikakati ya Serikali
Mbali na bei, wakulima wa mwani Zanzibar pia wanakumbana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo wataalamu wanabainisha kwamba kama hatua stahiki hazitachukuliwa kwa wakati basi uzalishaji wa zao hilo la biashara unaweza kupungua, hali itakayoathiri wakulima na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.
Hili, hata hivyo, tayari limeanza kuripotiwa kutokea visiwani humo. Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji wa mwani kutoka Ofisi ya Takwimu ya Zanzibar, uzalishaji wa zao hilo kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2021 ulishuka kutoka tani 2,382 zilizoripotiwa kwenye robo ya pili ya mwaka 2020 mpaka tani 2,027. Hili ni sawa na anguko la asilimia 15.
Dk Zakaria Ali Khamis ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Rasilimali za Baharini ambaye ameieleza The Chanzo kwamba kwa sasa mamlaka visiwani humo zinafanyia tathmini uwezekano wa kuwawezesha wakulima wa mwani kulima zao kwenye maji makubwa yapatayo mita tatu ili kukabiliana na athari kama hizi.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba athari za mabadiliko ya tabia ya nchi mbali na kupunguza uzalishaji pia zinafanya mwani unaozalishwa Zanzibar kuwa na thamani duni kwani unalimwa kwenye maeneo yenye maji madogo yanayoweza kupata joto na vilevile husababisha mawimbi makubwa ya bahari kukata kamba za zao hilo.
“Joto la maji kuongezeka husababisha mwani kutokuwa vizuri na mwani mwingi unapata maradhi. Kuna maradhi yanayosababisha mwani kufa na inaufanya kukosa ubora unaotakiwa kwani huufanya mwani kudumaa,” anaeleza Dk Khamis. “Tumegundua kwamba kulima kwenye kina cha maji marefu kunaweza kutatua hizi changamoto.”
Salim Khamis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitia salimkombo437@gmail.com.