Morogoro. Wakati maandalizi ya sherehe za Siku ya Kimataifa ya Wanawake yakiendelea duniani kote, akina mama ambao ni wakulima wadogo walikutana mjini hapa chini ya mwavuli wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kujadili changamoto kuu wanayokabiliana nayo: mila potofu na mifumo mingine kandamizi inayowazuia kumiliki ardhi.
Wakiwa wametoka sehemu mbali mbali za Tanzania, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakulima hao wadogo walikutana huku wakiamini kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha nguvu kikanda na kimataifa katika kuendeleza mapambano dhidi ya mfume dume ambao wanaamini ndiyo chanzo kikuu cha wao kushindwa kumiliki ardhi kwenye nchi zao husika.
Hoja na maoni yaliyokuwa yanatolewa na akina mama hawa wakati wa mijadala yao ilidhihirisha, pamoja na mambo mengine, uelewa wao mpana wa kero zao na namna ya kuzitatua.
Pia, walidhihirisha weledi wa namna maarifa katika jamii yanavyozalishwa. Hawakupepesa macho katika maelezo yao ya mchango wa taasisi za dini, mila na desturi, familia na jamii, pamoja na shule na vyuo vikuu katika kujenga na kuchochea mgawanyo wa majukumu kati ya mwanamke na mwanaume katika kijamii na imani potofu zitokanazo na mgawanyo huo.
“Tuko mwaka 2022 lakini bado wanawake tunalia na changamoto za umiliki wa ardhi,” anasema Constance Marubini, mkulima mdogo kutoka nchini Afrika Kusini, wakati wa warsha hiyo iliyofanyika Machi 5 na Machi 6, 2022, mjini hapa. “Tumekuwa tukiisihi Serikali iingilie kati kwa niaba yetu lakini imekuwa ngumu kuondokana na utaratibu unaoruhusu machifu kumiliki ardhi.”
Usawa wa kijinsia leo kwa kesho endelevu
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka kwa lengo la kusherehekea mafanikio ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii ambayo wanawake ulimwenguni kote wameweza kuyapata.
Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo Usawa wa Kijinsia Leo kwa Kesho Endelevu.
Pamoja na kwamba siku hiyo yenye asili yake kwenye vuguvugu la wafanyakazi duniani hutumika kusherehekea mafanikio yaliyofikiwa na wanawake kwenye nyanja mbalimbali za maisha yao lakini pia hutoa jukwaa imara la wanawake kuelezea changamoto zinazowazuia kufikia maendeleo wanayoyahitaji.
Kwa wakulima wadogo wengi barani Afrika, suala la umiliki wa ardhi ni changamoto sugu inayotishia ustawi wao kama wanawake na sehemu muhimu ya jamii.
Ni katika muktadha huu ndipo MVIWATA kwa kushirikiana na vuguvugu la kimataifa la wakulima wadogo lijulikanalo kama La Via Campesina iliamua kuwakutanisha wakulima wadogo wanawake kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ili waweze kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto hii.
“Taratibu za kimila zinazozuia wanawake wasimiliki ardhi barani Afrika zinafanana katika nchi zote ambazo ni wanachama,” Lina Andrew, Mratibu wa La Via Campesina kanda ya Afrika Mashariki aliieleza The Chanzo pembezoni mwa warsha hiyo. “Uzoefu kutoka nchi hizi [ikiwemo Tanzania] unaonesha kwamba mwanamke hana haki ya kumiliki ardhi. Na chanzo ni mila. Iko hivyo kwa karibu nchi zote.”
Safari bado ndefu
Wanaharakati wanaopigania haki za umiliki wa ardhi kwa wakulima wadogo wanabainisha kwamba ulimwenguni kote licha ya ukweli kwamba wanawake ni takribani nusu ya watu wote wanaoishi duniani, asilimia zaidi ya 70 ya wanawake hao hawana haki ya kumiliki ardhi.
Kwa upande wa Afrika, tafiti zinasema kwamba kati ya asilimia 70 na 90 ya utajiri wote unaozalishwa barani humo unatokana na ardhi huku asilimia 10 tu ya wanawake barani humo ndiyo wanaripotiwa kumiliki ardhi.
Kwa Tanzania, ripoti ya hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia inaeleza kwamba taifa hilo la Afrika Mashariki linaweza kunufaika zaidi kiuchumi endapo kama litapanua wigo wa fursa za kiuchumi kwa wanawake, hususan kwenye eneo la umiliki wa ardhi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuziba pengo la kijinsia kwenye uzalishaji wa kilimo, ambao unajumuisha kuongeza umiliki wa ardhi kwa wanawake, kunaweza kuwainua Watanzania takriban 80,000 kutoka kwenye umasikini kila mwaka na kuongeza pato la taifa la mwaka kwa asilimia 0.86.
Watafiti hao wanashauri Serikali kuimarisha umiliki wa ardhi miongoni mwa wanawake Tanzania kwa kutoa ruzuku zitakazowasaidia wanawake kupata hatimiliki kwa familia zenye kipato cha chini pamoja na kuwashauri wanandoa kuwa na hatimiliki za pamoja.
Rehabu Sumaye ni mkulima mdogo kutoka mkoani Manyara ambaye anadhani suala la kuwa na hatimiliki ni la muhimu ili kudhibiti uuzwaji holela wa ardhi na wanaume ambao mara nyingi huwa hawawashirikishi wenzao wao kwenye maamuzi hayo.
“Mwanaume akihitaji kuuza shamba hamshirikishi mwanamke,” anasema Rehabu wakati wa warsha hiyo iliyoandaliwa na MVIWATA. “[Mwanaume] anaenda tu anaongea na madalali. Hajui kwamba mwanamke yule ana sehemu kubwa katika familia. Na ukijaribu kumshawishi asiuze hufanikiwi kwani hatakusikiliza.”
Kubadilishana uzoefu wa mapambano
Akielezea kilichoisukuma MVIWATA kuwakutanisha wakulima hao wadogo kutoka maeneo mbali mbali ya Afrika, Mwenyekiti wa mtandao huo Apolo Chamwela aliiambia The Chanzo kwamba ni muhimu wakulima wakabadilishana uzoefu kwenye kukabiliana na tatizo la ukosefu wa umiliki wa ardhi ili kupunguza tatizo hilo.
Anasema Chamwela: “Kama tunavyofahamu, ardhi ndio msingi wa mtu anayeitwa mkulima. Yaani msingi wake wa maisha lazima awe na ardhi. Tukija kwenye upande wa uzalishaji wakulima wanawake wana mchango mkubwa sana. Kazi nyingi sana zinafanywa na wanawake. Lakini hawana umiliki wa hizi ardhi.
“Kwa hiyo, sisi kama taasisi huwa tunawajengea uwezo [hawa wakulima] kwa njia ya mafunzo, matamasha na kadhalika. Na hiyo imekuwa ikiwasaida sana kuweza kusimama wao wenyewe kuhahikisha kwamba wanapambania haki zile ambazo wanaona wanabaguliwa kama wanawake.”
Jackline kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dodoma anayepatikana kupitia jackline@thechanzo.com.