Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

DPP, kama mfumo wa utoaji haki Tanzania ungekuwa mzuri, angeweza kusema kwamba katika kupitia upya ushahidi uliokusanywa kuhusu shauri husika, anaona, pasipo shaka yoyote, kuwa watuhumiwa hawawezi kutiwa hatiani na hivyo anaona kuwa ni kupoteza muda wa Jamhuri na watuhumiwa kuendelea na shauri husika.

subscribe to our newsletter!

Asubuhi ya Machi 4, 2022, ilianza kwa mlipuko wa mchanganyiko wa machozi ya huzuni, mshangao na furaha kwa wakati mmoja. 

Uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP) kutotaka kuendelea na kesi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu ulipokelewa kwa hisia miongoni mwa Watanzania na wageni bila kujali itikadi zao za kisiasa au za kidini. 

Kubwa na muhimu zaidi, watu wengi walijawa – na bado wanayo – furaha kubwa kwamba Mbowe na wenzake kwa sasa wako huru.

Kwa bahati mbaya, katika mazingira kama haya ya furaha au huzuni iliyopitiliza, mjadala juu ya lolote jengine linalohusiana na jambo husika unakuwa umeminywa na mazingira ya hali halisi ya matukio na hisia. 

Kwa mfano, haiko kabisa katika mjadala kuhusu uhuru wa hasa Mbowe kwa sasa na siku za usoni. 

Je, Mbowe anao uhuru wa aina gani na wa kiasi gani? Je, mwanasiasa huyo anaweza kuzungumzia yaliyojiri katika mwenendo wa shauri lililokuwa likimkabili yeye na wenzake kwa kiasi gani? Na je, anaruhusiwa kisheria na kisiasa? 

Au je, Mbowe anaweza kuzungumzia suala la Katiba Mpya ambalo ndilo alilokuwa akizungumzia mpaka anatiwa korokoroni? Au je, ni sababu zipi zimepelekea kuachiwa kwao wakati huu? 

Wako wanaokwenda mbali zaidi na kuuliza mtu unawezaje kukaa mahabusu, au jela, au kizuizini, kwa miezi nane na ikatokea anayekushtaki anasema hana nia tena ya kuendelea na kesi na mambo yote yakaishia hapo? 

Vijijini zaidi, watu wananiuliza, eti sheria imekaaje sasa kwa mtu ambaye ametuhumiwa na kukaa rumande kwa muda mrefu kiasi hicho na baadaye anayemshitaki akapoteza hamu ya kuendelea na kesi? 

Kumalizwa kwa sakata la Mbowe kunatuambia nini?

Haya na mengine mengi yanatosha kutuambia mambo mawili kwa ufupi. Kwanza, kwamba ipo haja kubwa ya elimu ya sheria kwa Watanzania, bila kujali taaluma na tasnia zao, kwa vile sheria ni msumeno na hukata kote kote. Pili, kwamba mfumo wetu wa utoaji haki bado una mapungufu makubwa.

Mbowe na wenzake watatu walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kupanga kutenda makosa ya uhujumu uchumi na ugaidi. 

Miezi nane tangu kukamatwa kwake, DPP amepeleka mahakamani kitu kinachojulikana kisheria kama nolle prosequi, ambayo kwa lugha ya kilatini inamaanisha kuwa DPP, kwa niaba ya Jamhuri, hana mpango wa kuendelea na shauri husika. 

Kwa maneno mengine, kitendo hicho kinamaanisha kuwa Serikali imeamua kuachana na shauri husika na kwa sababu hiyo Mahakama inapaswa kufanya utaratibu wa kufuta kesi nzima kama ilivyoelekezwa na kusudio la DPP. 

Katika hali isiyofanana na shauri linalozungumziwa sasa, DPP angeweza kuweka bayana kuwa nolle prosequi yake inahusu baadhi ya tuhuma tu. 

Katika hali hiyo, Mahakama ingeendelea na tuhuma zinazosalia na ambazo hazijaguswa na kusudio la DPP. Kwa bahati nzuri, katika sakata hili la akina Mbowe, DPP ameeleza kuwa tuhuma zote walizokuwa wakikabiliwa nazo zinahusika na nolle prosequi aliyoipeleka mahakamani. 

Pamoja na hayo yote, watu wengi wasio magwiji wa sheria wanajiuliza: Je, vipi kama watuhumiwa hawa walikuwa na tuhuma nyingine nje ya hizi zinazohusika na kusudio la sasa la DPP? 

Kwa wanasheria, inajulikana wazi kuwa DPP anazungumzia tuhuma zilizomo katika shauri hili husika na si mashauri mengine yoyote kabla au hata baada ya sasa.

Kisiasa, jambo hilo linaleta hofu kubwa kwa Watanzania wapenda haki bila kujali kiwango chao cha ugwiji wa sheria. Kwa mfano, je, Mbowe na wenzake watakuwa na uwezo wa kujadili mambo kwa uhuru kiasi gani katika kipindi hiki cha baada ya ‘kuokolewa’ na Serikali kupitia DPP? 

Hawa wote, kwa mtazamo wangu, wanazo hoja kwa kuzingatia kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura 20 kitendo cha DPP kuweka kusudio la kutoendelea na kesi hakizuii uwezekano wa wahusika kushitakiwa tena kwa tuhuma hizo. 

Natamani Mbowe angeshinda kesi mahakamani

Kwa hakika, hii inafanya watu wengi, hata mimi, kutamani Mbowe na wenzake wangeshinda kesi mahakamani ili ijulikane kuwa hawana hatia kuliko kuachiwa kwa mlango huu wa DPP ambao unaacha utata juu ya uhuru wao wa maoni, pamoja na kisiasa katika mapana yake.

Haishangazi kuona kuwa wanaoachiwa kwa nolle prosequi ya DPP mara nyingi huwa wanaishia kuwa makini mno katika kuongea chochote kuhusu kesi iliyokuwa ikiwakabili, au hata kuhusu lolote jingine nje ya kesi hiyo, kwa kuhofia kesi hiyo isije ikalipuka mithili ya volcano iliyokuwa imelala kwa muda.

Na kuhusu uwezekano wa watu kama hawa kufidiwa kutokana na kadhia waliyoipata wakati kesi yao ikiendelea, hili nalo ni suala la uelewa zaidi. 

Dhana ya kufikishwa mahakamani ni ili ukweli wa tuhuma uweze kujulikana, na kama tusemavyo katika lugha ya kisheria, ukweli huo ujulikane pasipo shaka yoyote. 

Katika mazingira ya nolle prosequi, mtu anao uhalali wa kujiuliza, je, ukweli umejulikana na umejulikana pasipo shaka yoyote? Jingine ni, je, kama kesi imefutwa kwa tamko la DPP kabla ya ukweli kujulikana, jamii ielewe nini kuhusu tuhuma za watuhumiwa? 

Kwa kuwa kama kesi ingekamilika wangeweza, ama kutiwa hatiani, na kuadhibiwa au kuachiwa huru na kusafishwa. 

Je, katika mazingira ambayo DPP ameingilia kati shauri, ama kwa mujibu wa kifungu cha 21 au kile cha 98 cha sheria, watu hawa tuhuma zao zimethibitika au zimebatilishwa? 

Kwa Mtanzania wa kawaida, swali jingine ni, je, watu kama Mbowe na wenzake wanastahili haki yoyote au fidia baada ya yote haya? Kidini, lugha inayotumika ni kwamba tuwe watu wa kusamehe na kusameheana. 

Lakini kusameheana hakumalizi utata juu ya ukweli, haswa kuhusu kwamba watuhumiwa walitenda au kupanga kutenda jinai au la.

Utata au wingu linaloachwa bila majibu linaweza kuleta sintofahamu kubwa miongoni mwa jamii.

Tunahitaji kuboresha sheria zetu

Kama sehemu ya ukuaji wa tasnia na taaluma ya sheria, ninayo mapendekezo mawili. 

Kwanza, ni lile ambalo linashauri maboresho katika sheria ili kuwe na uwezekano wa mtu kuhoji maamuzi ya DPP inapotokea, kwa mfano, kuwa shauri ambalo DPP amelitolea nolle prosequi linagusa masilahi kadhaa ya jamii au watu binafsi. 

Fikiria, kwa mfano, inapotokea mtuhumiwa wa kesi kama ya ubakaji anapata ahueni ya kuachiwa huru kutokana na kusudio la DPP. 

Ukweli mzima kuhusu kosa linalotuhumiwa kutendwa unapotea na kwa namna hiyo kunakuwa na hisia za haki kupotea kutokana na kwamba upande wa mlalamikaji angetamani shauri lifike mwisho ili adhabu ijulikane inakwenda wapi na fidia nayo inakwenda upande gani! 

Ushauri wa pili ni kuhusu haja ya DPP kutoa sababu za kwa nini amepoteza hamu ya kuendelea na kesi. 

Katika jamii iliyostaarabika, DPP angeweza kusema, kwa mfano, kwamba katika kupitia upya ushahidi uliokusanywa kuhusu shauri husika, anaona, pasipo shaka yoyote, kuwa watuhumiwa hawawezi kutiwa hatiani na hivyo labda anaona kuwa ni kupoteza muda wa Jamhuri na watuhumiwa kuendelea na shauri husika.

Inapotokea hivyo, Mahakama ingepaswa wakati wa kutangaza kusudio la DPP kutafsiri pia juu ya hatma ya watuhumiwa katika kesi hiyo. 

Natamani, kwa mfano, ingekuwa inawezekana Jaji Joachim Tingatinga akasema bayana kuwa kusudio la DPP kutoendelea na shauri la akina Mbowe linaleta tafsiri kuwa watuhumiwa hawana hatia na kuwa wako huru dhidi na tuhuma hizi zote, sasa na siku zijazo. 

Kutamka kuwa wako huru pasipo kuweka bayana kuwa wamefikia kuwa huru kwa sababu imeshindikana kuthibitisha tuhuma zao pasipo shaka ni kuleta utata mkubwa wa kisheria mahakamani na utata wa kitaswira nje ya Mahakama. 

Aidha, kuficha ficha mambo kunakinzana na maono ya Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016, ambayo Watanzania waliipokea kwa bashasha kufuatia kampeni ya takribani miaka 10 ya wadau wa haki ya kupata habari chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) hadi kuipata.

Masuala mengine yanayostahili mjadala kuhusu shauri hili la Mbowe na wenzake na jinsi lilivyomalizwa na DPP yataendelea kukujia katika safu hii.

Mungu ibariki Tanzania na watu wake!

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi jamii aliyebobea katika maeneo ya uhusiano wa kimataifa, Katiba na sheria za kimataifa. Anapatikana kwa nambari +255 713 644357 na barua pepe dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

 

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts