Dar es Salaam. Ilikuwa ni ngumu kufikiria kwamba mtu aliyekuwa akiongea kama mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyoandaliwa na wanawake wa chama cha upinzani CHADEMA mnamo Machi 8, 2022, mjini Iringa alikuwa ndiyo kwanza ametoka gerezani baada ya kusota humo kwa siku 226 akituhumiwa kwa makosa ya ugaidi na uhujumu uchumi.
Freeman Mbowe, mwenyekiti taifa wa CHADEMA, hakuruhusu, kwa namna yoyote ile, kesi hiyo iliyoisha kwa Mwendesha Mashitaka (DPP) kuindoa mahakamani akisema hana nia ya kuendelea nayo tena ishawishi namna anavyowasiliana na wanachama wenzake wa CHADEMA au Watanzania kwa ujumla kama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Kama ulifuatilia hotuba ya kiongozi huyo ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza tangu arudi uraiani, na baada ya kumsikiliza unashawishika kwamba Mbowe hajabadilika, basi hutakuwa peke yako unayeamini hivyo. Wengi, kama siyo wote, ya wale waliofuatilia kwa shauku kubwa hotuba hiyo waliishia kuwa na hitimisho hilohilo.
Hotuba hiyo ya Mbowe yenye ukubwa wa saa moja na nusu, hata hivyo, ilikuja huku wadadisi wa mambo wakielezea wasiwasi wao juu ya kile wanachokiona kama mtihani unaomkabili kiongozi huyo, ambaye jina lake la kwanza lina maana ya Mtu Huru, wa kusawazisha matakwa ya wafuasi wake na yale ya Serikali ambayo wachambuzi wanabainisha ndiyo iliyomrudishia uhuru wake.
Mbowe yuko huru kiasi gani?
“Je, Mbowe [kwa sasa] anaweza kuzungumzia suala la Katiba Mpya ambalo ndilo alilokuwa akizungumzia mpaka anatiwa korokoroni?” anauliza Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kisheria kwenye andiko lake la hivi karibuni kwa The Chanzo. “Je, Mbowe na wenzake watakuwa na uwezo wa kujadili mambo kwa uhuru kiasi gani katika kipindi hiki cha baada ya ‘kuokolewa’ na Serikali kupitia DPP?”
Mbowe alikamatwa mnamo Julai 2021 katikati ya vuguvugu la kudai Katiba Mpya ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameomba apewe muda kidogo kabla ya kufufua mchakato wa kumalizia kuandika nyaraka hiyo muhimu. Ni maoni ya wengi kwamba kesi dhidi ya Mbowe ilikuwa ni ya kisiasa iliyolenga kuvuruga harakati hizo.
Na wakati wapo watu wanaoamini kwamba kutoka kwa Mbowe ni matokeo ya shinikizo la wananchi ni ukweli pia hatua hiyo ilifikiwa baada ya wadau mbalimbali – wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya upinzani na jumuiya ya kimataifa – kumsihi Rais Samia afikirie kumaliza kesi hiyo kwa mustakabali wa umoja wa kitaifa na maridhiano ya kisiasa.
Mazingira ya kuachiwa kwa Mbowe na washtakiwa wenzake watatu, hata hivyo, yanaibua hofu miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania kwamba Mbowe anaweza kujihisi ana deni la kulipa kwa Rais Samia na hivyo kupunguza kasi ya kudai mabadiliko ya kimsingi yanayotakikana nchini, msimamo ambao unaweza ukakinzana na matakwa ya wanachama wenzake wa CHADEMA ambao wangependa kasi ya kudai mabadiliko hayo iongezwe maradufu.
“Kuna mstari mwembamba sana kati ya [chama cha upinzani] kushirikiana na Serikali kufanya kile kinachoitwa ujenzi wa nchi na chama hicho kuwa katika hatari ya kupoteza hadhi yake kama chama kinachopaswa kuisimamia Serikali kwa kuikosoa na kuuaminisha umma kwamba chenyewe ndiyo mbadala sahihi wa chama kinachotawala,” anasema Dk Muhidin Shangwe ambaye ni Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hofu na mshtuko
Mtihani wa kusawazisha matakwa ya wana-CHADEMA na yale ya Serikali siyo wa kinadharia tu kwani tayari Mbowe alikabiliwa na mtihani huo ndani ya siku ya kuachiwa kwake kutoka Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, alikokuwa akishikiliwa.
Jioni ya siku hiyo Mbowe alikwenda Ikulu kuonana na Rais Samia na kufanya naye mazungumzo. Hata hivyo, inaonekana kwamba hatua hii haikuwafurahisha baadhi ya watu ndani ya CHADEMA na Mbowe alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake hiyo ya Jumanne kutetea uamuzi wake huo.
“Pamekuwepo na mkanganyiko wa hofu, mshtuko, mshangao, furaha na taharuki nyingi tu [zilizotokana na uamuzi wangu wa] kukutana na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, siku hiyo hiyo niliyofutiwa kesi,” Mbowe aliwaeleza wanawake wa CHADEMA waliokuwa wakimsikiliza kwa makini.
Mbowe alisema kwamba kwa siku nyingi alikuwa anataka kukutana na Rais Samia lakini mpaka anafunguliwa mashtaka na kuwekwa kizuizini hilo halikuwa limefanyika licha ya Samia kujibu barua yake. Baada ya kesi yake kufutwa, alipokea ujumbe wa Rais Samia akimtaka wakutane “haraka iwezekanavyo,” ujumbe ambao aliuridhia.
Rais kama Mkuu wa Nchi, Mbowe alisema, ndiye mwenye ufunguo wa vikwazo vingi vinavyosababisha simanzi ya muda mrefu nchini Tanzania. Alisema alitumia fursa ya kukutana na Rais Samia kujadiliana na yeye juu ya umuhimu wa kuanzisha utaratibu utakaoiwezesha Serikali kusimamia haki nchini, kitu ambacho alikiri walikubaliana.
“Naomba kuwauliza Watanzania, nilikosea [kukutana na Rais Samia] ama nilipatia?” Mbowe aliwauliza wanawake wa CHADEMA ambao walimjibu kwa sauti moja kwamba alipatia. “Sasa Watanzania, hususan wana-CHADEMA, wana hofu. Watu wakasema: ‘Mwenyekiti Mbowe, yaani ametoka tu, hata hajatulia, hajakutana hata na sisi, kashaenda Ikulu. Huyu yuko salama kweli huyu?’”
“Mbowe ni yule yule,” kiongozi huyo aliwahakikishia wafuasi wake. “Mbowe ni yule yule.”
Mbowe atimize wajibu wake
Lakini ili wana-CHADEMA na Watanzania kwa ujumla wamuamini Mbowe kwamba kweli ni yule yule ni kitu gani kiongozi huyo anapaswa kufanya?
Kwa mujibu wa Fatma Karume, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mbowe anapaswa kutimiza wajibu wake kama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania na si vyenginevyo.
“Wajibu wake yeye [Mbowe] ni kuendesha chama chake kwa mujibu wa itikadi na katiba ya chama chake,” Karume, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anabainisha.
“Hakuna maana ya kuwa chama cha upinzani kama huna uchu wa madaraka,” aliendelea kueleza mwanaharakati huyo. “Lazima uwe na uchu wa madaraka. Lazima uwe na uchu wa kutaka kuchukua madaraka na kushinda uchaguzi. Kwa hiyo, matakwa ya Serikali, kama yanakinzana na uchu huo, ni lazima [Mbowe] akatae kuyatii.”
Dk Paul Luisulie, Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, ameiambia The Chanzo kwamba mtihani huo unaomkabili Mbowe unaweza kutatulika kwa urahisi endapo tu kama Rais Samia atakuwa tayari kutekeleza kile walichokubaliana na kiongozi huyo wa upinzani.
“Je, Serikali sasa itaondosha zuio lake haramu ililoliweka dhidi ya mikutano ya hadhara ya kisiasa?,” anauliza Dk Luisulie. “Je, Serikali itakuwa tayari kufufua mchakato uliokwama wa kuandika Katiba Mpya? Kama hakuna hatua hizo mantiki inamtaka Mbowe aendelee na mapambano tu.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.