Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya takwimu Tanzania wamebainisha kwamba ili wanawake nchini humo waweze kufanikisha harakati zao za kujikomboa kutoka kwenye changamoto kadhaa zinazowakabili ni lazima wafuatilie takwimu zinazotolewa pamoja na kuwa na uwezo wa kuzichambua ili wagundue maana iliyonyuma ya takwimu hizo.
Wito huo umetolewa huku wanawake nchini Tanzania wakiwa wameungana na wanawake wenzao ulimwenguni kote kuadhimisha sherehe za Siku ya Kimataifa ya Wanawake inayosherehekewa kila Machi 8 ya kila mwaka.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku hiyo ni Usawa wa Kijinsia Leo kwa Kesho Endelevu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Albina Chuwa anaamini kwamba ni ngumu kuyatenganisha maendeleo ya wanawake na takwimu.
Dk Chuwa alikuwa akizungumza wakati wa warsha maalum iliyoandaliwa na Tanzania Data Lab (dLab) kwa kushirikiana na Women in Data Science (WiDS) – Africa mnamo Machi 8 kama sehemu ya kuadhimisha siku hiyo.
“Kwa mwanamke, bila takwimu, huwezi kujua fursa zipo wapi; takwimu ndio kila kitu, yaani kama damu na moyo,” alisema Dk Chuwa.
“Moyo unasukuma damu kuelekea sehemu mbalimbali za mwili,” aliongeza mtakwimu huyo mkuu wa Tanzania. “Vivyo hivyo, kwa mwanamke, takwimu zinakusukuma ili upate nguvu. Lakini pia ili uweze kuwezeshwa katika kila kitu [ili] mwisho uweze kufanikiwa.”
dLab, kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wengine wa takwimu duniani, kama vile WiDS – Afrika, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kushajihisha ushiriki mkamilifu wa wanawake wa Kitanzania kwenye masuala ya kitakwimu, ikiwemo kuendesha mafunzo pamoja na matukio mengine mbalimbali ya uhamasishaji.
“Takwimu zinahitajika kwa wanawake kwa ajili ya maendeleo,” aliendelea kusisitiza Dk Chuwa. “Kupitia takwimu, tunaweza kufichua ukosefu wa usawa wa kijinsia. Tunaweza kugundua mapungufu yaliyopo katika usawa wa kijinsia. Lakini pia tunaweza kuamua chochote tunachotaka kutoka kwenye usawa wa kijinsia.”
Nuzulack Dausen ni Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Afrika, kampuni ya habari na teknolojia inayojikita kwenye kuzalisha habari za kitakwimu.
Kwenye mahojiano maalum na The Chanzo, Dausen alibainisha kwamba anahofia endapo kama wanawake wengi watashindwa kujihusisha na masuala ya takwimu hali hiyo inaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa changamoto nyingi zinazowakumba kwa sasa kuendelea kubaki hivyo.
“Maana yake ni kwamba [wanawake] watashindwa kubaini vihatarishi vinavyodokezwa na takwimu mbalimbali zinazoteolewa,” anasema Dausen ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Nukta Afrika.
Mshauri huyo wa masuala ya kitakwimu anatolea mfano wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2019/2020 kutoka NBS inayoonesha kwamba kati ya watu waliopata mikopo kwenye sekta ya kilimo na ufugaji wanawake walikuwa ni kama asilimia 26 tu.
“Yaani, kati ya watu wanne waliopata mkopo kwa mwaka huo wa kilimo, mtu mmoja pekee ndiyo alikuwa mwanamke,” anasema Dausen. “Sasa, kama wanawake hawashiriki kupata takwimu kama hizi itawawia vigumu kufaulu katika masuala ya kilimo.”
Zahara Tunda ni Mchambuzi wa Takwimu anayefanya kazi na shirika la Code for Africa lenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini.
Zahara anaona kwamba manufaa makubwa ambayo wanawake wenzake wanaweza kuyapata kwa kujihusisha na takwimu ni kuonekana na kuweza kupata fursa mbalimbali zinazoweza kubadilisha maisha ya mtu.
“Namaanisha, yaani, kupanua wigo wa fursa ambazo mtu anaweza kuzifukuzia,” anasema Zahara ambaye pia ni mwandishi wa habari. “Ukiwa na uwezo wa, kwa mfano, kuchambua takwimu, wigo wako wa fursa utakuwa ni mpana ukilinganisha na ule wa ambaye hana huo ujuzi.”
Zahara anaamini kwamba takwimu pia ni muhimu kwani zinamsaidia mtu kuwa katika nafasi nzuri ya kuwashauri watu wanaotoa maamuzi kwa niaba ya wananchi.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.