The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fatma Taufiq: Wanawake Tunahitaji Ukombozi wa Kiuchumi

Mbunge huyo wa Viti Maalum anasema kwamba bila ukombozi madhubuti wa kiuchumi harakati za kumkomboa mwanamke kisiasa unaweza kuchukua muda mwingi zaidi kufanikiwa kuliko inavyotegemewa.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum kwa mkoa wa Dodoma kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Fatma Taufiq amesema kwamba kitendo cha wanawake wengi nchini Tanzania kushidwa kijikwamua kiuchumi ni moja kati ya vikwazo vikubwa vinavyowazuia wanawake hao kutojitokeza kuwania katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Taufik, ambaye amewahi kufanya kazi kama Mkuu wa Wilaya kabla ya kuanza kazi hiyo ya uwakilishi, aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalum aliyofanya na The Chanzo jijini hapa kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake inayoadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.

Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa mwakilishi huyo wa wananchi anaanza kwa kutoa tathmini yake ya namna Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyozingatia suala zima la usawa wa kijinsia kwenye teuzi na masuala kama hayo. Endelea …

Fatma Taufiq: Ninachoweza kusema ni kwamba, kwanza ninampongeza Rais Samia kwa juhudi za kuhakikisha kwamba wanawake wengine wanashiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi na ngazi za uongozi.

Hii ni hatua kubwa. Tunatamani ingefika 50 kwa 50 lakini kwa muda unavyozidi kwenda tunaona juhudi za Serikali zilivyofanywa. Kwa hiyo, ninachoweza kusema kwamba  hatua ni nzuri sana.

The Chanzo: 50 kwa 50 ambayo wanawake wengi wamekuwa wakiihitaji kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo kwenye nafasi mbalimbali, wanawake wenyewe wanatumia vyema nafasi zao kuhakikisha usawa unaendelea kuwepo?

Fatma Taufiq: Haya mambo yanakwenda hatua kwa hatua. Awamu ya kwanza walikuwepo wanawake wachache. Tukaja awamu ya pili wakaongezeka. Tukaja awamu ya tatu wakaongezeka. Ya nne, ya tano, ya sita  wameongeka zaidi.

Kwa hiyo, kwa jinsi muda unavyokwenda mwisho wa siku Mungu akitujalia tunaamini hiyo 2030 inawezekana yasiwe maeneo yote lakini baadhi ya maeneo tutaweza kufika 50 kwa 50. Bado tunasafari ndefu ya kwenda. Kwa sababu bado wanawake tuna vikwazo na vigingi.

The Chanzo: Rais Samia ameonesha mwanga kwa wanawake wengi katika nafasi mbalimbali za uongozi, kwa nini bado kuna muamko mdogo wa wanawake kujitokeza kuwania nafasi hizo?

Fatma Taufiq: Unajua kwenye kuwania nafasi [za ungozi] kuna changamoto nyingi. Pengine wanawake wengine hawaruhusiwi na wenza wao. Pengine kuna wengine hawaruhusiwi na wazazi wao. Lakini kuna wengine pengine [hawana] uwezo wa kifedha.

Unapotaka kwenda kugombea nafasi za uongozi na kutoa maamuzi ina maana kwamba inabidi ni lazima uwe na uwezo wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kama huna uwezo wa kwenda kuwatafuta hao wapiga kura unafafanyaje, mwisho wa siku utashindwa tu.

Kama mwanamke akiweza kujikwamua kichumi, mwisho wa siku akawa na uwezo wake wa kutosha, kama akiamua kugombea nafasi tuseme, nafasi ya udiwani, anaweza akakimbilia vile vijiji ambavyo viko katika kata husika hivyo ataenda kukutana na wapiga kura. Kwenye hizi chaguzi napo kuna gharama zake.

Maana huwezi kutoka hapa  kwenda mahali fulani bila ya kuwa na mafuta. Pengine itabidi uchukue pikipiki maana yake si pesa? Ukitaka kuchukua labda bajaji, gari maana yake ni pesa.

Kwa hiyo, kama wanawake wakiweza kujikwamua kichumi, wakawa  na uwezo kichumi, ina maana watakuwa kwenye nafasi nzuri [na] ni rahisi kugombea. Na sisi sasa hivi tuna hamasishana sana wanawake wengi waingie katika ngazi za maamuzi. Kwa sababu ajenda ya wanawake zifanana.

The Chanzo: Ni vikwazo gani unaona kwamba wanawake wakiepukana navyo vitasaidia kuibua wanawake wengi viongozi?

Fatma Taufiq: Kama nilivyosema kwamba suala zima mtu akijikwamua kiuchumi. Wakishajikwamua kiuchumi hiyo itakuwa ni njia moja wapo. Lakini pia kifikra na zile mila na desturi ambazo zinawakandamiza wanawake. Ambazo zinaona kwamba mwanamke ni daraja fulani na zile nazo tukiziondoa na tukaondoa dhana fulani katika baadhi ya jamii.

kwa sababu kuna baadhi ya jamii bado haziamini kwamba mwanamke anaweza akawa kiongozi. Kwanza katika zile jamii ambazo bado wanamuona mwanamke kama hayuko sawa na wanaume bado kuna makabiliano hayo. Na bado hizo mila na desturi zipo.

Mimi nataka nikupe mfano. Wakati mimi ni Mkuu wa Wilaya nilikwenda kwenye kijiji fulani ambacho sitakitaja. Na nikakutana na jamii ya watu siwezi hata kutaja hili kabila. Unaona sasa, tumefika pale mimi ndio Mkuu wa Wilaya nipo na DSO, OCD na kamati yangu yote ya ulinzi na usalama.

Sasa akatokea bwana mmoja akauliza haya huyo Mkuu wa Wilaya yuko wapi? Kuna huyo mwanaume mmoja akasimama na kusema Mkuu wa Wilaya yupo. Yule mtu akauliza hee, mwanamke ? Yaani baba mtu mzima akashangaa kuona Mkuu wa Wilaya mwanamke.

Kwa hiyo unaona mpaka sasa hivi bado kuna watu wana dhana ya ule mfumo wa kufikiri kwamba bado wanawake hawawezi kuwa viongozi.  Kwa hiyo, inabidi tuitoe hii fikra hasi ya kufikiria kwamba wanawake siyo viongozi. Jamii nzima ikajua hilo. Basi mwanamke apewe nafasi.

The Chanzo: Umekuwa kwenye nafasi ya uongozi kwa muda mrefu, ni kitu gani kimekufanya uendelee kudumu katika nafasi yako?

Fatma Taufiq: Mimi ni kule kujiamini. Lakini pia kwa sababu kwenye nafasi yangu ya ubunge wale wapiga kura wangu ambao walinipigia kura nimeweza kufanya nao kazi kwa pamoja.

Yale malengo, labda mambo, waliyofikiria kwamba ninaweza nikawafanyia nina jitahidi. Siwezi kuyamaliza yote lakini kwa mfano labda kuwaelimisha wanawake kuhusu haki zao, kuelimisha wanawake jinsi ya kujikwamua kiuchumi, kuelimisha wanawake waweze kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi na kuwasaidia fursa mbalimbali vitu kama hivyo vyote hivyo vimenisaidia.

Kwa hiyo, bado wale wanawake wanaona kwamba huyu ni kiongozi wetu. Kwa sababu amekuwa akitushirikisha masuala mengi.

Kwa hiyo, ninachoweza kusema ni kwamba nimekuwa nikishiriki katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa pamoja na hawa wanawake ninao fanya nao kazi. Bahati nzuri na mimi ni muelimishaji.

The Chanzo: Unadhani nini kikifanyika kitasaidia wanawake kuwa na moyo wa kuendelea kujitokeza kuwania katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Fatma Taufiq: Ni hamasa. Lakini pia sisi ambao tumepata fursa mbalimbali tuendelee kukutana na wanawake na kuwaelezea ni kwa jinsi gani tumeweza kufikia nafasi hizi. Yaani mafanikio ,hatua tulizopitia ni zipi na wao waweze kujua kusudi na wao waweze kuhamasika.

Kwa hiyo tukiweza kuwabaini viongozi wanawake ina maana watatokea wengi. Kwa sababu gani?  Kama mwanamke anaweza kuongoza katika ngazi ya familia yake ana uwezo wa kuongoza ile familia yake sijui kuna mume, watoto, baba watoto, sijui mjomba.

Sasa kama kwenye ngazi ya familia tunaweza tukafanya hivyo tunashindwaje kwenye hizi nafasi nyingine? Kwa hiyo, hii kuwatengeneza tu mitazamo yao kifikra kwamba mwanamke anaweza kuongoza. Na kwa kuwa tunaweza kuongoza basi tupewe nafasi.

Jackline kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dodoma anayepatikana kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *