The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwaka Mmoja Bila Magufuli: Alipotuacha Na Anapotupeleka Rais Samia

Katika makala hii, Mbunge wa Ubungo (CCM) Profesa Kitila Mkumbo anarejea mchango wa Rais Magufuli katika ujenzi wa Tanzania kwa kuainisha pale Magufuli alipoikuta Tanzania na alipoiacha wakati anafariki, na hivyo kujenga msingi wa kuelewa Tanzania inapoelekea chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

subscribe to our newsletter!

Siku ya Jumatano ya tarehe 17, Machi 2021, itabaki kuwa moja ya siku ngumu na kubwa katika taifa letu. Ni siku ambayo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wakati huo akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, akiwa mkoani Tanga, alilitangazia taifa taarifa ngumu na ya kushtusha: kwamba Mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli, wakati huo akiwa Rais wa Tanzania, alikuwa amefariki dunia! 

Binafsi ninaikumbuka kipekee siku hii kwa kuwa nilikuwa katika msafara wa Makamu wa Rais aliyekuwa katika ziara ya siku tatu mkoani Tanga, wakati huo nikiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji).

Picha wakati wa tangazo la kifo cha Hayati Rais John Pombe Magufuli

Leo hii siku ya Alhamisi, tarehe 17, Machi 2022, ni mwaka mmoja kamili tangu taifa lipate msiba huu mkubwa kuwahi kulikumba taifa letu kwa kuwa Hayati John Magufuli ni Rais wa kwanza kufariki akiwa madarakani.

Katika makala haya ninarejea mchango wa Rais Magufuli katika ujenzi wa taifa letu. Katika kutafakari mchango wa Hayati Rais Magufuli, ninaainisha alipotukuta wakati anaingia madarakani na alipotuacha wakati anafariki, na hivyo kujenga msingi wa kuelewa tunapoelekea chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Katika kujenga msingi wa kuelewa vizuri mafanikio ya uongozi wa Rais Magufuli, andiko hili linaanza kwanza kwa kuangazia pale ambapo Rais wa Nne wa nchi yetu alituacha ili kubaini mafanikio na changamoto ambazo Rais Magufuli alirithi. Ninafanya hivi kwa kutambua kuwa kila awamu ya uongozi hupata mafanikio fulani na wakati huohuo huzalisha changamoto fulani.

Mafanikio ya awamu moja huwa ni mtaji na msingi wa awamu inayofuata; wakati changamoto za awamu moja huwa ni kichocheo cha fikra mpya na mipango mipya ya maendeleo kwa awamu inayofuata ya uongozi.

Alipotuacha Jakaya Mrisho Kikwete

Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa Rais wa Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaweza kumwelezea Rais Kikwete kama mlinzi na muendelezaji wa aina ya uchumi uliojengwa na Rais Benjamin Mkapa. 

Mchango mkubwa wa Rais Mkapa ulikuwa katika kuisimika rasmi sekta binafsi kitaasisi kama mhimili mkuu wa uchumi wa nchi, na kuiacha Serikali na jukumu la msingi la urekebu (pia huitwa ushirika). Hivyo,moja ya mchango mkubwa kabisa wa Hayati Rais Mkapa ni ujenzi wa taasisi za urekebu katika kusimamia uendeshaji wa uchumi chini ya sekta binafsi.

Hivyo, moja ya kazi kubwa aliyofanya Rais Kikwete ilikuwa ni kulinda misingi ya uchumi iliyojengwa na kusimikwa wakati wa uongozi wa Hayati Rais Mkapa. Rais Kikwete anakumbukwa kwa kuimarisha sekta binafsi na kuvutia wawekezaji, mambo yaliyosababisha uchumi kukua kwa kiwango cha kati ya asilimia sita hadi saba takribani katika kipindi chote cha uongozi wake.

Sherehe za uapisho wa Hayati Rais Magufuli, Novemba 5,2020

Uongozi wa Rais Kikwete ulishuhudia mafanikio pia katika ujenzi wa miundo mbinu, hasa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Aidha, uongozi wake ulishuhudia kupanuka kwa huduma za jamii, hususan elimu, afya na umeme vijijini. Ni katika kipindi chake ambapo idadi ya vyuo vikuu iliongezeka sana. 

JK atakumbukwa, kwa mfano, kwa kujenga vyuo vikuu vipya viwili vya umma: Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo mjini Arusha.

Pengine mchango mkubwa na wa kipekee ambao JK atakumbukwa daima ni katika kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini. 

Hata hivyo, ni katika kipindi chake ambapo CCM ilikumbukana na ushindani mkubwa kuliko katika kipindi kingine chochote katika uhai wa mfumo wa vyama vingi nchini. Kwa mfano, ni katika kipindi cha JK ambapo kura za Urais kwa upinzani zilifika asilimia 40 ya kura za Urais na kushinda wabunge wa majimbo 70 katika uchaguzi wa Mwaka 2015.

Kwa wapinzani hii inaweza kuchukuliwa kama mafanikio ya JK kidemokrasia.  Lakini kwa upande wa wana CCM hali hii ni kielelezo kwamba wananchi hawakuridhika na utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha Urais wa JK.

Kikubwa zaidi, Rais Kikwete aliruhusu na kusimamia mchakato wa Katiba Mpya hadi kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa. Hata hivyo, mchakato uliishia njiani kutokana na vyama vya upinzani kususia kwa kile walichodai kutelekezwa kwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Warioba. 

Huu ndio ukawa msingi wa kuanzishwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uliokuja kutoa ushindani mkubwa kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. 

Changamoto kubwa zilizoibuka wakati wa uongozi wa Rais Kikwete ni Serikali ya yake kuandamwa na kashfa za ufisadi na rushwa katika kipindi chote cha urais wake, zikiwepo kashfa kubwa katika sekta ya madini (Buzwagi) na umeme zilizosababisha Waziri Mkuu wake wa kwanza Edward Lowassa na mawaziri kadhaa kujiuzulu. 

Hivyo, moja ya changamoto ambayo Rais Kikwete aliizalisha katika uongozi wake, na ambayo Rais wa tano ilibidi apambane nayo, ni taswira ya rushwa katika Serikali na utumishi wa umma kwa ujumla.

Alipotukuta na kutuacha JPM

Dk Joseph Pombe Joseph Magufuli ni Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Magufuli alipata nafasi hiyo katika mazingira halisi ya Kitanzania: ilikuwa haitarajiwi kwamba angegombea na, zaidi ya yote, kwamba angeweza kupitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake. 

Hii inatokana na ukweli kwamba, ukiacha nafasi ya uwaziri aliyoshikilia kwa takribani miaka 20, Rais Magufuli hakuwa moja ya vigogo katika chama hiki na alikuwa hajafanya harakati nyingi za kugombea kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine waliokuwa na majina makubwa ndani ya chama, kama vile Edward Lowassa na Bernard Membe. 

Hayati Rais Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi akichukua fomu za Urais CCM

Hata hivyo, baada ya kuondolewa Lowassa katika kugombea, na baada ya dalili kujitokeza kuwa angeweza kwenda kugombea urais kupitia upinzani, inaaminika kuwa CCM ililazimika kumpitisha ndugu Magufuli ambaye alionekana ndiye pekee katika CCM aliyekuwa na nguvu ya kutosha kisiasa kuweza kupambana na nguvu ya Lowassa ndani ya upinzani.

Rais Magufuli alichukua uongozi huku nchi ikiwa imara kiuchumi, kwa maana kwamba kiwango cha uchumi (kwa kipimo cha pato la taifa – GDP) kilikuwa kikikuwa kwa asilimia kati ya sita hadi saba kwa kipindi chote cha urais wa Kikwete. Nchi ilikuwa katika mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wa nje na sekta binafsi ilikuwa inashamiri vizuri.

Rais Magufuli alitambua mapema hali imara ya uchumi aliyorithi kutoka kwa uongozi wa Rais Kikwete na katika hotuba yake ya kufungua Bunge aliahidi kulinda mazingira mazuri ili kuhakikisha kuwa uchumi unaendelea kuimarika na kukua katika kipindi chake. 

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli alisema haya kuhusu hali ya uchumi aliyoirithi: “Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa.”

Hali ya ukuaji uchumi toka 2011 mpaka 2021

Pamoja na jitihada zilizofanyika, changamoto kubwa ambayo Rais Kikwete alishindwa kuishughulikia, na ambayo alimrithisha Rais Magufuli, ni taswira ya rushwa na ufisadi katika Serikali. Kipindi chote cha Rais Kikwete kiligubikwa na kashfa nzito za rushwa na ufisadi, ambayo hadi anaondoka madarakani zilionekana kutotatulika, na kwamba rushwa na ufisadi vilianza kuzoeleka kuwa sehemu ya utamaduni wa Tanzania. 

Kutokana na hali hii, Rais Magufuli aliahidi kupambana kwa dhati na mapema na adui rushwa na ufisadi. Akielezea dhamira yake ya kupambana na rushwa na ufisadi, Rais Magufuli alisema: 

“Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri. Wamechoka kabisa. Wamechoka sana. Hawako tayari kuvumilia upuuzi wa Serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi. Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu.”

Tafsiri ya falsafa ya kutumbua majipu ilikuja kujitokeza waziwazi katika utawala wa Rais Magufuli kwa kushamiri kwa kutenguliwa kwa wateule wake pale ambapo walionekana kushindwa kuwajibika au kuhisiwa kufanya vitendo vya rushwa. Ni katika uongozi wa Rais Magufuli ambapo ile dhana ya cheo ni dhamana ilionekana kutekelezeka kiuhalisia kwani hakuna mteule wa Rais aliyejua kwa hakika kesho yake ingekuwaje.

Mchango na aina ya uongozi wa Rais Magufuli tunaweza kuuweka katika maeneo makubwa matatu. Mosi, JPM anajitokeza kama kiongozi aliyekuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi makubwa. Pili, ni kiongozi mwenye kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali yake. Tatu, Rais Magufuli alikuwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuwajibisha watendaji na wasaidizi wake bila woga wala upendeleo.

Mfano mojawapo unaoelezea azma yake ya kupambana na rushwa na ufisadi ni jinsi alivyoshughulikia sakata la IPTL lililoanza kipindi cha uongozi wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (1985-1995). Kashfa ya IPTL ilidumu kwa takribani kipindi cha robo karne hadi ikazaa kashfa zingine za Richmond, Dowans na Tegeta Escrow. 

Kutokana na mtandao mpana wa rushwa katika sakata hili, awamu zote nne zilishindwa kulimaliza sakata hili hadi kusababisha hasara kubwa kwa Serikali, watumiaji wa umeme na Watanzania kwa ujumla. Kwa mujibu wa Brian Cooksey, mtafiti anayejitegemea na ambaye amefuatilia sakata la IPTL tangu mwaka 1997, Watanzania waliendelea kulipa bei kubwa ya umeme kutokana na kashfa za IPTL na watoto wake (Richmond, Dowans na Tegeta ESCROW). 

Aidha, mwezi Oktoba 2014, wafadhili walisitisha misaada ya kibajeti yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni mia tano kama shinikizo kwa Serikali kushughulikia sakata la Tegeta ESCROW.

Ilimchukua Rais Magufuli takribani miezi sita tangu alipochaguliwa kuwa Rais kushughulikia sakata la IPTL na hatimaye vigogo wahusika wakuu wa sakata hili kufikishwa katika vyombo vya sheria mwezi Juni 2017.

Maamuzi mengine ambayo Rais Magufuli amefanya katika kipindi cha uongozi wake ni pamoja na kukamilisha zoezi la kuhamishia shughuli za Serikali makao makuu ya nchi Dodoma, uamuzi ambao umechukua takribani nusu karne kuutekeleza. Aidha, Rais Magufuli alitekeleza takwa la sera ya elimu la kuondoa ada kwa wanafunzi wa sekondari.

Kampeni za ujenzi wa viwanda zilikuwa kubwa katika kipindi cha JPM pengine kuliko kingine chochote. Kampeni hii ilikuwa na pande mbili kubwa. Kwanza ni dhana. Kwamba ni muhimu Watanzania kuwa na fikra na mtazamo wa uzalishaji na kujitegemea. Pili, ni ujenzi wenyewe wa viwanda vidogo na vikubwa.  

Hivyo, muhtasari wa mchango wa Rais Magufuli upo katika maeneo matano aliyotuachia. Mosi, kuanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa ya kati (SGR). Pili, kupanuka kwa huduma za jamii hususani afya, elimu na maji. Tatu, kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma. Nne, kupiga vita ya rushwa na ufisadi ndani ya utumishi wa umma. 

Rais Magufuli alijipambanua kuwa MTEKELEZAJI mahiri wa sera na ilani ya CCM. Aidha, katika miaka ya uongozi wake, Rais Magufuli alifanikiwa KUTIBUA na KUUVURUGA mtandao wa wababaishaji, maarufu kama wapiga dili, au kwa maneno ya JPM mwenyewe waliozoea maisha ya ujanja ujanja, ambayo yalianza kujikita katika jamii na taifa letu kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita kabla ya yeye kuingia madarakani. 

Eneo la tano ni kujenga hali ya kujiamini kama nchi na kama jamii ya Watanzania kwamba TUNAWEZA wenyewe kujitegemea kama taifa na kama mtu mmoja moja.

Alipotukuta na anapotupeleka Rais Samia

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,nafasi ambayo aliipata kikatiba kufuatia kifo cha Rais Magufuli. Ni Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alipoingia madarakani kama Kiongozi Mkuu wa nchi, Rais Samia alikutana na changamoto kubwa tatu, ambazo anazishughulikia hadi sasa na ambazo ndizo zimekuwa msingi wa mafanikio yake katika mwaka mmoja aliokwishakaa madarakani. 

Rais Samia wakati wa kiapo cha Urais, Machi 19,2021

Changamoto ya kwanza ni kushuka kwa ukuaji wa uchumi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi kutoka asilimia zaidi ya sita mwezi Julai Mwaka 2020 hadi kufikia chini ya asilimia nne wakati anaanza uongozi wake mwezi Machi 2021. Pamoja na sababu zingine, kushuka kwa uchumi kulisababishwa na janga la ugonjwa wa UVIKO-19.

Changamoto ya pili ilikuwa ni kuyumba kwa sekta binafsi  kutokana na Serikali kuanza kushiriki  moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo kuchukua kandarasi za ujenzi wa miradi ya maendeleo. Hali hii iliifanya Serikali kuwa mshindani wa sekta binafsi. Kwa vyovyote vile sekta binafsi isingeweza kushindana na Serikali na hivyo kuifanya sekta hiyo kuanza kudorora.

Changamoto ya tatu ni kuanza kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kutokana na malalamiko mengi ya vyama vya siasa vya upinzani dhidi ya chama tawala na Serikali yake. Kimsingi, hakuna mabadiliko makubwa ya kisheria yaliyofanyika wakati wa uongozi wa Rais Magufuli yanayogusa vyama vya siasa.  

Tofauti pekee iliyokuwepo ni aina na mtindo wa uongozi. Inajulikana kuwa Rais Magufuli hakuwa kiongozi aliyependa mtindo wa majadiliano na viongozi wenzake wa kisiasa kutoka vyama vingine. Kwa kuwa kushamiri, au kufifia, kwa vyama vya upinzani nchini kunategemea zaidi haiba ya kiongozi mkuu wa nchi aliyepo madarakani, badala ya mapambano ya kisera na uongozi mbadala, mtindo wa uongozi wa Rais Magufuli haukutoa nafasi kubwa kwa vyama vya upinzani kukua. 

Kuyumba kwa sekta binafsi na malalamiko ya vyama vya upinzani vilianza kufifisha mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara na diplomasia ya uchumi kwa ujumla.

Hivyo, mafanikio makubwa ya Rais Samia katika mwaka wake wa kwanza ni katika kushughulikia changamoto alizozirithi. 

Mazingira ya uwekezaji na biashara yameirimika sana kufuatia hatua za Serikali za kuchukua nafasi yake na sekta binafsi kuanza kushamiri tena. Aidha, kufuatia Rais Samia kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia falsafa yake ya kuifungua nchi, kuimarisha mahusiano na ushirikiano na nchi mbalimbali, wawekezaji kutoka nje ya nchi wameanza kumiminika tena kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Rais Kikwete na Mkapa. 

Pia, Rais Samia ameendelea kuimarisha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya muda mrefu ya upungufu wa madarasa. Aidha, malalamiko ya viongozi wa vyama vya upinzani yameanza kupungua kufuatia uamuzi wa Rais Samia wa kuonana na viongozi wa vyama hivyo, pamoja na kuruhusu na yeye mwenyewe kushiriki majukwaa mbalimbali yanayokutanisha viongozi wa vyama vya siasa kupitia taasisi za TCD na Baraza la Vyama.

Hatua hizi tunatarajia zitachochea uwekezaji na biashara nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na hivyo kujenga uwezo wa Serikali katika kuleta maendeleo ya watu na ustawi wa jamii. Ninawaaga wasomaji wote kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, KAZI IENDELEE!

Profesa Kitila Mkumbo ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Pamoja na nyadhifa nyengine, Kitila alipata kuwa Waziri katika Serikali za Rais Magufuli na Rais Samia. Anapatikana Twitter kama @kitilam. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *