The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kimeua Uandishi wa Habari za Wafanyakazi Tanzania? 

Waandishi wanalo jukumu la kuwasemea wasio na sauti na kuitaka Serikali iwawajibisha wawekezaji wanaodhulumu watu maskini wanaohenyeka kwa kazi ngumu na kulipwa kiduchu. Lakini jukumu hilo linatekelezwa kwa kiwango kidogo sana nchini.

subscribe to our newsletter!

Vyombo vya habari vinatajwa kuwa na jukumu la kuangazia uovu unaotokezea katika jamii na kuwasemea wasio na sauti. Kwa bahati mbaya, vyombo vyetu vya habari Tanzania haviangazii masuala ya wafanyakazi kwa uzito unaotakiwa.

Wataalamu wanasema habari za tahsusi ya wafanyakazi na maslahi yao ni sehemu ya habari za uchumi na biashara isipokuwa habari hizi huandikwa kutoka kwenye mtazamo wa wafanyakazi na sio mabwanyenye, waajiri, wawekezaji na matajiri.

Habari zikiandikwa katika mtazamo wa  matajiri aghlabu zinatetea sera zinazombeba mwekezaji – punguzo la kodi, ulegezaji sheria na masharti yanayowabana, kutweza maslahi ya wafanyakazi. Wakati kwa mwekezaji hayo ni mafanikio, kwa mfanyakazi ni madhila.

Wakati habari za uchumi na biashara zinaandikwa kwa wingi katika vyombo vyetu vya habari, chache sana zinaangalia masuala kutoka katika mtazamo wa wafanyakazi.

Leo ukisoma magazeti mengi utakutana na habari za kampuni zilivyotengeneza faida, uzinduzi wa biashara na bidhaa mpya, miradi mikubwa ya kiuchumi nakadhalika. Lakini siyo hali, nafasi na maslahi ya wafanyakazi.

Kuna mambo kadhaa yanayofanya uandishi wa habari wa masuala ya wafanyakazi ufifie siyo tu Tanzania bali na kwingineko duniani ikiwemo Marekani na bara zima la Amerika ya Kaskazini.

Kwa hapa Tanzania, ambapo zamani kuliwahi kuwa na gazeti lenye ushawishi lililomilikiwa na jumuiya ya wafanyakazi lililoitwa Mfanyakazi na kuangazia masuala yao, pia ishara zinaonesha kudondoka kwa tahsusi hii.

Nikizungumzia hali ya Tanzania, sababu kadhaa zinaweza kuwa zilichangia, au zinachangia mpaka sasa, kutozingatiwa kwa tahsusi hii.

Siasa za kibepari

Kwanza, mhamo kutoka kwenye siasa za ujamaa na uchumi uliomilikiwa na Serikali hadi kwenye siasa za kibepari na uchumi wa soko huria unaopendelea mabwanyenye.  Uwekezaji wa sekta binafsi ndio oksigen ya uchumi wa soko huria ambao Serikali inajiondoa kwenye uzalishaji na badala yake inakusanya kodi tu.

Katika uchumi wa soko huria, wawekezaji wanapewa kipaumbele hadi kiwango cha Serikali kuwabembeleza kwa vivutio mbalimbali, ikiwemo punguzo au misamaha ya kodi.

Serikali zinafanya kila linalowezekana kuwavutia wawekezaji na kuhakikisha wanabaki nchini. Imefikia hatua Serikali hazitaki kuwabana sana wawekezaji juu ya maslahi ya wafanyakazi wao kwa kuhofia wataondoka. Vyombo vya habari navyo vimefuata mkondo huo wa kuimba mapambio ya uwekezaji.

Lakini tukumbuke pia viongozi wa Serikali na waandishi wa habari wetu ni binadamu wa kawaida, tena waishio katika moja ya nchi maskini zaidi duniani na ya kupigiwa mfano katika ufisadi.

Wawekezaji wengi wana uhusiano mzuri sana na viongozi wa Serikali na vyombo vya habari ambao unawaweka wafanyakazi katika nafasi ngumu kunapoibuka migogoro.

Tusisahau pia kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya vyombo vya habari na waandishi wenyewe ni matangazo kutoka kwa makampuni na matajiri. Siku hizi waandishi wanafanywa mabalozi wa kampuni kutangaza bidhaa zao.

Hali hiyo inaviweka vyombo vya habari na waandishi katika mazingira magumu ya kuwakosesha uhuru wa kitaaluma. Hata Waswahili wanasema, Huwezi kung’ata mkono unaokulisha.

Kadhalika, ni haohao matajiri pia ndio wamiliki wa vyombo vya habari vingi vikuu tuviitavyo ’mainstream’ ambao nao pia wananyonya wafanyakazi wao kwenye tasnia ya habari na nje ya tasnia hiyo.

Kwa hiyo, maslahi ya wafanyakazi, kwa vyovyote, hayawezi kuwa ajenda ya kipaumbele kwa vyombo hivi. Na kuseme ukweli, kada yenyewe ya waandishi wa habari, hasa wa ngazi za chini, ni miongoni mwa kundi linalonyonywa zaidi na kudhalilika katika jamii kwa maslahi duni na ndio maana hupewa majina kama ya kejeli kama kanjanja.

Waandishi wengi huishia kuwa vibarua wanaoishi kwa kutegemea posho ndogo na vipesa vya rushwa.

Vuguvugu dhaifu la wafanyakazi

Sababu nyingine inayopelekea kufifia kwa uandishi wa habari wa tahsusi ya wafanyakazi ni kudhoofika kwa vyama vya wafanyakazi na vuguvugu la kudai haki zao.

Kwa hapa Tanzania, kipindi kigumu zaidi kilikuwa ni katika awamu ya tano ya uongozi. Inashangaza sana Tanzania kwamba viongozi wa vyama vya wafanyakazi si watu unaowaona sana kwenye habari, licha ya shida zote zinazokabili watu wao zinazohitaji kusemewa.

Kadhalika, hata mifumo yenyewe ya vyama vya wafanyakazi inaonekana kuwa ni dhaifu.

Kama hakutakuwa na umoja wenye nguvu unaowawakilisha wafanyakazi hawa, changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa kada za chini wasio na ujuzi maalum, wakiwemo wafanyakazi wa usafi, walinzi wa kampuni binafsi, wafanyakazi za ndani na baadhi ya viwanda vya wawekezaji uchwara hazitasikika katika vyombo vya habari.

Hali ya sasa ya uandishi wa habari za wafanyakazi haitii matumaini, huku wanaoumia zaidi wakiwa ni wafanyakazi wa matabaka ya chini wasio na ujuzi maalum kama wale dada zangu.

Wale wa  tabaka la kati na juu walau wanapata kipato ambacho hata kama hakilingani na kazi zao, lakini kinawawezesha kuishi maisha ya heshima kama binadamu lakini pia wamekuwa wana nafasi kubwa ya kupata utetezi, licha ya nafasi ndogo ya habari za wafanyakazi.

Hoja yangu muhimu zaidi ni kuwa kuna sababu nyingi za kufufua tahsusi hii kwa sababu ni kazi ya kiutume. Waandishi wanalo jukumu la kuwasemea wasio na sauti na kuitaka Serikali iwawajibisha wawekezaji wanaodhulumu watu maskini wanaohenyeka kwa kazi ngumu na kulipwa kiduchu.

Tahsusi hii pia inampa mwandishi fursa ya kuchungulia nyuma ya takwimu na athari kwa binadamu katika jamii mbalimbali.

Ni rahisi sana kusema uwekezaji umeongezeka, uchumi umekua, pato la Mtanzania limeongezeka, lakini ni mpaka pale utakapoangalia hali za watu, vipato vyao, mgawanyo wa mapato ndio utapata habari kamili.

Tabaka la watu wa chini

Pia, tahsusi hii inatoa fursa ya kuangazia mafanikio ya harakati za tabaka la watu wa chini waliojiajiri kujikomboa kimaisha.

Uzuri ni kwamba habari hizi hata kivigezo vya soko la habari zina mvuto kwa sababu kuna mnyukano (conflict), kuna majina makubwa yanahusika na ni habari zinagusa hisia.

Miaka miwili ya janga la maradhi ya UVIKO-19 yaliyoisumbua dunia nzima imeacha wengi hoi. Ajira zimepotea kwa sababu ya kudondoka kwa sekta muhimu za kiuchumi kama utalii na usafirishaji.

Sasa dunia imeingia vitani ambapo tunasikia kitisho cha ongezeko la bei za bidhaa muhimu kama mafuta. Haya yote yanafanya uandishi wa tahsusi ya wafanyakazi kuwa muhimu zaidi sasa.

Kwa sababu vyombo vikuu vya habari vinavyokilisha maslahi ya matajiri vitawiwa ugumu kuandika habari hizi, nadhani tunahitaji vyombo vingi zaidi vya aidha wanahabari wenyewe au vile vya kijamii.

Uzoefu unaonesha vyombo vya aina hii vipo huru zaidi kuliko vile vinavyomilikiwa na matajiri. Tunaweza kutaja mifano mingi ya vyombo vya habari vya waandishi ambavyo viliandika habari zilizoitikisa Serikali na kuibua uozo mwingi, hasa upande wa magazeti.

Nalo Shirikisho Huru la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), ambalo linaunganisha vyama vyote  vya kisekta linapaswa kufikiria kuanzisha vyombo vyao vya habari, walau gazeti.

Kama iliwezekana zamani, kwa nini ishindikane sasa wakati mambo mengi yamekuwa rahisi zaidi? Kiukweli, tahsusi ya wafanyakazi ina habari nyingi sana na zenye mvuto hata kihabari.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *