NACTE Ingilieni Kati Uonevu Chuo cha Afya Mvumi Dhidi ya Wanafunzi Wake

Baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa na wanafunzi chuoni hapa ni pamoja na uwepo wa tozo nyingi zisizokuwa na maelezo ya kueleweka pamoja na wanafunzi kupokea vitisho kutoka kwa walimu wanapoibua hoja zinazohusu ustawi wao chuoni hapo.
Na Mwandishi Wetu7 April 202285 min

Ndugu mhariri, kwa majina naitwa Stanslaus Baraka*, ni mwanafunzi katika Chuo cha Afya Mvumi, kilichopo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma. Nikupe pole kwa majukumu makubwa na mazito uliyonayo na nikupongeze pia.

Ningeomba kutumia jukwaa la The Chanzo kuwasilisha kwa umma wa Watanzania madukuduku tuliyonayo wanafunzi wa chuo ambayo yameshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu licha ya kuyawasilisha zaidi ya mara moja kwa uongozi wa chuo.

Ni matumaini yetu kwamba kupitia The Chanzo, mamlaka zinazohusika na usimamizi wa elimu Tanzania, hususan Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTVET), zitafahamu kilio chetu na kuchukua hatua za haraka iwezekanavyo kurekebisha hali ya mambo chuoni hapa.

Utitiri wa tozo holela

Ndugu mhariri, moja kati ya vilio vikubwa vya wanafunzi chuoni hapa ni uwepo wa utitiri wa tozo za reja reja kwa wanafunzi zinazoanzishwa na uongozi wa chuo bila kujali zitawaathiri namna gani wanafunzi kiuchumi au kitaaluma.

Ndani ya miezi saba zimeanzishwa tozo jumla ya tozo nne ambazo ziko nje ya mpangilio wa tozo za chuo, au fees structure. Tozo hizi ni pamoja na tozo ya Sh80,000 iliyoanzishwa mnamo Oktoba 2021 wakati tunaripoti kwa kuanza mwaka wa masomo 2021/2022.

Msingi wa kuanzishwa kwa tozo hii ulijengwa kwenye hoja ya kwamba wanafunzi wote walioondoka bila kujaza clearance form wanapaswa kupewa adhabu kulipa fedha kiasi cha Sh80,000 ili wasirudie tena.

Ndugu mhariri, chuo chetu ni chuo cha kanisa na ni miongoni mwa vyuo vyenye ada kubwa hapa nchini. Mpaka mwanafunzi akamilishe ada ya muhula mmoja anapaswa kua na fedha kiasi cha Sh1,500,000 au inayokaribiana sana na hiyo.

Kutokana na utofauti wa hali za kiuchumi na maisha magumu, siyo wanafunzi wote wanaweza kulipa fedha hizo kwa wakati. Ukweli huo ndiyo uliotumiwa na uongozi wa chuo kuanzisha tozo nyingine ya Sh50,000.

Tukiwa katikati ya mhula wa kwanza wa masomo kwa mwaka 2021/2022, wanafunzi walitakiwa kufanya continuous assessents two (CAT2) kama utaratibu ulivyo. Hata hivyo, kwa bahati mbaya wanafunzi wengine walifanya na wengine walizuiliwa kufanya mpaka wamalizie kulipa ada.

Lakini licha ya kukamilisha ada waliyokuwa wakidaiwa, wanafunzi hao walitakiwa walipe faini ya Sh50,000 ili waweze kufanya mitihani hiyo. Wanafunzi walilipa faini hii kwani hakukuwa na namna nyengine ambayo ingewawezesha kufanya mtihani bila kulipa faini hiyo.

Tozo nyingine ambayo imekuwa ikiwaumiza wanafunzi chuoni hapa ni ile ya Sh200,000. Ndugu mhariri, tozo hii iliibuliwa katikati ya mwezi Machi 2022 huu ikijengewa hoja ya kwamba wanafunzi waliopata supplementary wanapaswa kulipia Sh200,000 ili wafanye mitihani yao ya supplementary.

Tozo hiyo iliyopewa jina la ‘ada ya mitihani ya supplementary’ ambayo hapo awali ilikua ni Sh30,000  tu inatakiwa kulipwa na mwanafunzi yeyote bila kujali idadi ya supplementary anazotakiwa kufanya.

Ndugu mhariri, pia kuna tozo ya Sh50,000 iliyowafikia wanafunzi kupitia tangazo la kufunga chuo la Machi 4, 2022, ambapo ilitangazwa kua kwa mwanafunzi atakaeshindwa kukamilisha ada na usajili kuanzia Machi 21, 2022, atapaswa kulipa faini ya Sh50,000 ili asajiliwe. Vinginevyo, hakuna mwanafunzi atakae sajiliwa nje ya huo muda.

Lakini tozo ya muda mrefu kidogo kuliko hizi zote ni ile ya Sh350,000 ambayo juhudi zetu za kuushawishi uongozi wa chuo uipunguze mpaka sasa zimeshindwa kuzaa matunda.

Ndugu mhariri, tozo hii hutozwa kwa wanafunzi wanaopata supplementary kwenye mitihani yao ya kumaliza mwaka ambayo kimsingi huwa ipo chini ya Wizara ya Afya. Hii nayo hutozwa bila kujali idadi ya supplentary alizo nazo mwanafunzi.

Uchakavu wa miundombinu

Ndugu mhariri, kilio kingine cha wanafunzi wa Chuo cha Afya Mvumi, ukiachana na tozo, ni uchakavu wa miundombinu kwenye baadhi ya mabweni ya chuo.

Kuna mabweni ni ya muda mrefu sana hivyo yamechakaa vya kutosha. Kwa mfano, nyavu za madishani na vioo hamna. Hii imepelekea wanafunzi kuibiwa vitu vyao na vibaka wanaoingia chuoni usiku kwa kuruka ukuta.

Kuna mabweni pia kutokana na ujenzi wa kizamani hayana milango hivyo wanafunzi wanatumia mapazia tu basi.

Tunalipia sare lakini hatupewi

Ndugu mhariri, maelezo ya kujiunga na chuo, joining instruction, yanamtaka kila mwanafunzi anapokuja kujiunga na masomo Chuo cha Afya Mvumi alipe Sh135,000 kama ni binti na Sh115,000 kama ni mvulana.

Fedha hizi hulipwa kwa lengo la kuwashonea wanafunzi sare za chuo kama ifuatavyo: binti anapaswa kushonewa gauni mbili na koti jeupe moja na mvulana anapaswa kushonewa suruali mbili, shati mbili na koti jeupe moja.

Ndugu mhariri, huu utaratibu umekua changamoto kwa wanafunzi kwani sare zimekua zikiletwa nusu nusu, yaani mwanafunzi anapata baadhi ya sare na baadhi hapati.  Kwa mfano, kuna wanafunzi mpaka muda huu wako mwaka wa tatu hawajapewa shati la pili na wengine wako mwaka wa kwanza hawajawahi kupewa sare yoyote ya chuo ingawaje wamelipia.

Jambo jingine hapa ni aina ya vitambaa vinavyotumika kushonea nguo hizo pamoja ushonaji  mbovu. Mafundi wanatumia vitambaa vya hadhi ya ubora wa chini kiasi kwamba nguo, hususan gauni za mabinti zinapitisha mwanga hivyo kusababisha kuonekana kwa maungo ya ndani ya wavaaji.

Ndugu mhariri, gauni za mabinti haziwekewi lining, mifuko wala zipu jambo ambalo si zuri hata kidogo. Aidha, kutokana na ushonaji mbovu, wanafunzi wamekua wakiingia gharama za ziada kufanya marekebisho ya nguo wanazopewa.

Ukosefu wa sare kwa baadhi ya wanafunzi baadhi umepelekea wanafunzi hao kushindwa kuhudhuria vipindi kwani hata wakihudhuria kuna walimu wanawatoa darasani kwa kuwa hawajavaa sare za chuo.

Ukosefu wa uwajibikaji kwa upande wa chuo 

Ndugu mhariri, menejimenti ya chuo imekua na uzito mkubwa sana katika kutekeleza majukumu yao kwa wanafunzi, hususan yale yanayohitaji wao kutoa fedha. Hapa nitaandika mambo makuu mawili yanayoashiria kua menejimenti haiwajibki ipasavyo kwa wanafunzi.

Mosi, ni kushindwa kufanya ukarabati kwa muda pindi hitilafu za miundombinu zinapotokea. Kwa mfano, tuna darasa haliwaki taa wala soketi hazifanyi kazi toka Januari mwaka huu wa 2022 na mpaka sasa halijafanyiwa kazi licha ya kupeleka taarifa mara kwa mara kwa wahusika. Darasa hilo lina hitilafu ya mifumo ya umeme.

Pili, kuna hosteli socket breaker iliungua toka Februari 8, 2022, imekuja kubadilishwa Machi 28. Hii inamaanisha kipindi chote hiki wanafunzi walikua wanakaa giza.

Tatu, menejimenti haina utaratibu wa kununua taa au socket ili kubadilisha vifaa hivyo vinapopata hitilafu kwenye vyumba vya wanafunzi. Taa au socket ikiungua mwanafunzi anaambiwa anunue yeye, na wakati mwingine akiripoti chuoni anapewa chumba hakina taa halafu bado atatakiwa kunua kwa fedha zake mwenyewe.

Kuna wanafunzi pia wanapewa vyumba havina vitasa na wanalazimika kununua vitasa kwa ajili ya usalama wa vitu vyao kwani kushindwa kufanya hivyo hupelekea upotevu wa vitu vya wanafunzi ikiwemo computer (iliwahi kutokea hivyo).

Nne, menejimenti haina utaratibu wa kuitisha vikao na wanafunzi kinyume na katiba ya chuo inayoelekeza kwamba kutakua na College Baraza mbili kwa kila muhula wa masomo, lakini mpaka sasa ni mihula mitatu mfululizo menejimenti haijawahi kufanya kikao na wanafunzi.

Zimefanyika jitihada mbalimbali za kuomba vikao, ikiwemo kwa kumuandikia Mkuu wa Chuo barua lakini hazijazaa matunda. Tumepeleka pia mihutasari ya vikao vya wanafunzi lakini hatujawahi kupewa mrejesho juu ya mambo ambayo tuliyaainisha.

Mengineyo

Ndugu mhariri, mbali na vilio hivyo, wanafunzi hapa pia wanalalamikia kulipishwa Sh50,000 kwa ajili ya Wi-Fi lakini hawanufaiki nayo. Wanafunzi pia wanalipia hela ya stationary Sh20,000 na ream moja kila muhula wa masomo lakini wakienda kutoa photocopy wanalipia Sh100 kwa kila ukurasa.

Wanafunzi ambao hawaridhiki na mazingira ya kukaa ndani ya chuo, au wale wasioweza kumuda gharama za hosteli, ambayo ni Sh300,000, wakiomba kukaa nje ya chuo wananyimwa ruhusa hiyo.

Pia, wanafunzi pia wanakabiliana na kauli za vitisho kutoka kwa baadhi ya walimu pale wanafunzi hao wanaojaribu kuhoji/kuuliza masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wao.

Ndugu mhariri, nimeandika maelezo haya kwa lengo la kuomba msaada wa kupaza sauti kwa mamlaka zinazohusika na vyuo vya kati vinavyotoa mafunzo ya afya hasa Wizara ya Afya na NACTVET.

Uamuzi wangu unatokana na imani yangu kwamba masuala yote niliyowasilisha hapa yatapata mwarobaini ikiwa tu taarifa zitafika kwa wahusika. Nitashukuru sana kama The Chanzo itasaidia kufanikisha hilo kwa kuchapisha andiko langu hili kwenye jukwaa lake.

*Siyo jina lake halisi.

Na Mwandishi Wetu

8 comments

 • Moses kinyaroto

  7 April 2022 at 9:05 PM

  Binafsi niwape Pole wahanga wote, mimi pia nimesoma vyuo hivyo vya kati tena vya kanisa jina kapuni,ni ukweli usiopingika vinamanyanyaso sana kwa wanafunzi hasa swala la tozo, miundombinu, chakula na wingi wa sheria usiokuwa wa maana hii yote kumfunga mwanafunzi mdomo ili aogope kusema! Na Mara nyingi vyuo hivi vinatabia ya kutoa mlungura kwa baadhi ya wahusika wanaoratibu vyuo hivi vya kati hali ambayo inazidi kumuweka mwanafunzi njia panda zaidi hasa linapokuja swala kama hili la Mvumi!
  Mm niombe kama ilivyo kwnye mashule yote nchini bodi huwa na mixture ya wazaz na wengneo na huku pia bodi iwe na wazaz pia na kama ilivyo kwenye mashule ya upili huwa kuna mikutano ya wazaz,wanafunz na waalimu kusudi ni kujadil changamoto pia ningependa kwenye hivi vyuo vya kati kuwe na utaratibu kama huo!. Trust me Vyuo vya serikali ni mara Mia kuliko hivi vya private, private vinatesa sana watoto wa watu hasa walio na hali za chini. Na kila kukicha vinazid kufungulie kwa sabab elimu ya sasa umeishakuwa biashara na sio kutengeza watu watakaofaa kwa ajili ya kazi fulani hapo baadae.

  Reply

 • Naftal shemshashu

  8 April 2022 at 3:25 PM

  Changamoto nyingne kijana wangu amefeli somo moja tu alifu amembiwa arufi nyumbn arudie mwaka mwingn na wakatumi mtihan alifel na wa muhula wa kwanzaa …tena wametoa matokeo baada yakudai kilipwa ada ya muhula wa pili

  Reply

 • Anonymous

  8 April 2022 at 8:59 PM

  Haya yote ni kweli kabisa pia kuna suala la kutokufuatilia vyeti vya wanafunzi kwa wakati mana kuna wanafunzi wamemaliza tangu mwaka 2020 mpaka leo hii hawajapata vyeti vyao kisa uzembe wa chuo kutowajibika katika majukumu yao Chuo ndio msimamizi wa mwanafunzi na ni kiungo kati ya mwanafunzi na wizara ambayo ndio hutoa vyeti lakini ufuatiliaji ni mbovu kupitiliza Mvumi kwa kusema kweli hakifai kabisa hata kua na usajili hakikidhi vigezo

  Reply

 • Kwanga Njamasi

  9 April 2022 at 8:17 AM

  Aliyoyasema ndiyo yanayotendeka,,
  Serikali kupitia mamlaka zake zinazohusika itusaidie katika haya. ✍️🌍🙏🇹🇿

  Reply

 • Joram j sweya

  9 April 2022 at 10:23 AM

  Ningeshauri nacte watusaidie mikopo angarau kidogo maana wanafunzi wa vyuo vyakati tunaishi maisha magumu sana ,pamoja na ada kuwa juu! ,Masomo magumu ukichanganya na mawazo yani diproma unajikuta unasoma miaka Saba , hasa vyuo vya afya.

  Reply

 • Joseph

  18 April 2022 at 4:52 PM

  Hilo tatizo sio la chuo hicho tu vyuo vingi vya afya , vina hili tatizo la tozo ambazo azipo kwenye join instructions wala nacte,

  Reply

 • Joseph

  18 April 2022 at 4:53 PM

  Hivi vyuo vinavyo funguliwa kila siku kama
  Shule za kata ndo tatizo

  Reply

 • Thomas John Lima

  19 April 2022 at 10:35 AM

  Hiyo kitu ipo pia hapa PIHAS peramiho institute of health and allied science. Ukiondoa tozo nyingi ada kwa mwaka 2000000 mochango ndo usiseme. Mkuu wa chuo sidhani hata kama ana sifa unakisilani na wanafunzi wake na kuwaambai kuwa atawashika na kuwafukuza chuo disco ni nyingi. Kabla kulikua na mkuu wa chuo ambae alijua matatizo ya wazazi na wanafunzi. Mimi mwanangu amedisco lakini inaonekana tatizo ni mahusiano mabaya na mkuu mpya. Hakuna haki kwa wanafunzi. Wizara ya Afya na NACTE Tunaomba patient na huku PIHAS utadhani wanaoskma hapo sio Watanzania.

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved