Dar es Salaam. Kwenye sehemu hii ya pili ya mahojiano na mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo Ismail Jussa, mwanasiasa huyo anasema hakubaliana na pendekezo kwamba mchakato wa kuandika Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, ingawaje anaamini kwamba kutoka sasa mpaka 2025 ni muda mdogo kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mjumbe huyo wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar anasema mchakato wa kudai Katiba Mpya unaweza kwenda sambamba na ule wa kudai mageuzi madogo kwenye mfumo wa usimamizi wa uchaguzi nchini, na kwamba si suala la kipi kitangulie kipi. Jussa anadai hili ndiyo chama chake cha ACT-Wazalendo kinachomaanisha kwa kauli mbiu yao ya Tume Huru Kuelekea Katiba Mpya.
Jussa anasema mkakati huo ni muhimu kwani anaamini kwamba licha kwamba mchakato wa Katiba Mpya unapaswa uanze sasa muda uliobaki mpaka kufikia Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni mdogo sana kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya. Hapa Jussa anaanza kwa kuelezea kwa nini anaamini hivyo. Endelea …
Ismail Jussa: Tuna uzoefu tayari wa mchakato kama huo kutoka mwaka 2011 mpaka mwaka 2014 ambapo lilikuwa ni jaribio la mwanzo la kupata Katiba Mpya. Tumejifunza kwamba kwanza tufahamu kitu kimoja kwamba Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni tofauti mno na Katiba Mpya ya Kenya, na Katiba Mpya ya Afrika Kusini pengine na Katiba Mpya ya Ghana au Katiba Mpya katika nchi ambayo ni nchi moja.
Kwa sababu hapa unazungumzia, ndio maana inaitwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, unazungumzia nchi mbili ambazo zimekuja pamoja na kwa hiyo Katiba yake haizungumzii taasisi za utawala ndani ya nchi tu, unazungumzia pia mahusiano ya nchi hizi mbili ambazo ndio zimeunda Jamuhuri ya Muungano.
Kwa hiyo, panahitajika kazi kubwa sana ya kujenga muafaka wa kitaifa, [kujenga] maelewano juu ya vipi kuuendea huo mchakato wa kupata Katiba ambao utaweza kuzifanya sauti mbalimbali kuweza kupata maelewano na muafaka. Kwa sababu sote tunajua kwamba kazi ya kutengeneza au kuandika Katiba Mpya ni kazi ambayo inahusisha kupata muafaka wa kitaifa kwa sababu hamuwezi nyote katika nchi mkawa na mawazo ya aina moja juu ya vipi nchi yenu iendeshwe.
The Chanzo: Lakini tumeshafanya hivyo.
Ismail Jussa: Hatujafanya Khalifa.
The Chanzo: Tumefanya chini ya Tume ya Jaji Warioba.
Ismail Jussa: Hatujafanya. Hatujafanya na ndio hoja yangu ya msingi. Pengine walifanikiwa Tume ya Jaji Warioba kufika pahala wakaja na rasimu. Lakini Tume ya Warioba imeleta mapendekezo ndio maana inaitwa rasimu, chombo cha kupitisha Katiba ile ni Bunge la Katiba kwa mfumo ambao ulikubaliwa wakati ule.
Bunge la Katiba halikuweza kujenga muafaka wa kitaifa kabla ya kukutana kwa maana washiriki wake na ndio maana utakuta mijadala katika Bunge la Katiba ilikuwa ni ya mivutano mikubwa sana, ilikuwa imejengeka katika sura kama vile ni ya ushindani kama vile mnashindania, katika Bunge la kawaida kuna Serikali na upinzani.
The Chanzo: Lakini hiyo si pengine ni kwa sababu ya uamuzi wa kisiasa uliofanywa wa kupeleka wanasiasa kwenye Bunge la kutunga Katiba, pengine hali ingekuwa tofauti, kwa mfano, kama kungekuwa na busara zaidi ya kupeleka watu wengine kwenye kutunga Katiba.
Ismail Jussa: Kwa sababu kwa asili mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ni wa kisiasa. Lakini pengine namna ya kuwafanya watu gani wapatikane [na] washiriki katika shughuli ile ilipaswa yenyewe kwamba iwe ni muafaka wa kitaifa.
Sasa hayo ndio mambo ambayo hayakufanyika na kwa nini hayakufanyika, ni kwa sababu ukitazama palianza mzozo pale mwanzo katika kutengeneza rasimu ya muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo yenyewe ndio ilipaswa iongoze huo mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Ndio maana nikasema ikiwa wakati ule muda haukutosha sembuse sasa na msipofanya maridhiano mapema mkapata muafaka wa kitaifa mtakwenda kurejea makosa yale yale.
Kwa hiyo, ni sahihi kabisa kwangu mimi ninaamini kwamba tunapaswa kwanza kujenga maelewano na muafaka wa kitaifa na kama nilivyosema hapa kwa asili ya maumbile ya Jamuhuri ya Muungano ilivyo kwanza kuna kazi ya kupata muafaka kitaifa kabla hamjaenda katika Bunge la Katiba baina ya Zanzibar na Tanganyika kuhusiana na mahusiano yao yanasanifiwa vipi katika Katiba Mpya.
Halafu mnapaswa muwe na maelewano ya pamoja juu taasisi za kinchi, iwe ni Tume ya Uchaguzi, iwe ni Mahakama, iwe ni Bunge, iwe ni taasisi za kuichunga Serikali, kwa mfano, pengine wenzetu wana chombo cha kusimamia maadili ya umma, kuna vyombo mbalimbali vinavyopaswa kusimamia teuzi katika nchi, kuna masuala ya kuwajibishana, kuna masuala ya madaraka ya Rais.
Haya msipoelewana mapema na mkawa hakuna mazungumzo yakutosha baina ya hao waokwenda kuingia katika Bunge la Katiba kabla mtakwenda pale mkazozane pale na matokeo yake kila wakati mtakuwa mnapata mkwamo.
The Chanzo: Kwa vile mimi nafahamu, labda utanirekebisha, vile mimi nafahamu ni kwamba wadau wengi ambao wanataka Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wafufue mchakato wa Katiba Mpya ni kwamba wanataka tuanze na rasimu ya Warioba kwa sababu tayari ipo, hawapendi Katiba inayopendekezwa. Kwa hiyo, rasimu ya Warioba ipo tayari na wewe unaibua hoja kwamba maelewano maridhiano, mustakabali wa makubaliano na jinsi ya kupata chombo cha kupitisha yaani kuurejesha huu mchakato kwenye sehemu inayostahili. Unadhani hiyo inaweza ikachukua zaidi ya mwaka? Kwa mfano, kama Serikali ikawa na nia leo ya kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya kwa kutumia rasimu ya Katiba ya Warioba na kutengeneza hiyo mifumo ya kupatikana kwa hao watu, inaweza ikachukua zaidi ya mwaka, kwa sababu tupo ndani ya mwaka 2022, ndio kwanza tupo Aprili?
Ismail Jussa: Kwanza nadhani Khalifa ngoja tuliweke wazi kwamba hata mimi, mimi ni muumini wa Katiba Mpya, chama cha ACT-Wazalendo ni waumini wa Katiba Mpya, sote tunasema kwamba nchi yetu pale ilipofika inahitaji Katiba Mpya. Suala linakuja kwamba vipi kuuendea mchakato ambao utatupa Katiba Mpya.
Sasa tunapozungumza, kwa mfano, suala la kwamba kipi kianze mwanzo haina maana ya kwamba kimoja kinabadilisha kingine, au kinachukua nafasi ya kingine. Sasa kujibu swali lako mahususi kuhusu suala la muda bado mimi ninachosema ni kwamba unaweza kuwa mwaka mmoja labda ni mrefu sana, narudia tena katika hali ambayo tunayo mimi siamini kwamba mwaka mmoja unatosheleza.
The Chanzo: Sio mwaka mmoja, yaani tuna mwaka 2022, 2023, 2024 tuna uchaguzi Oktoba 2025.
Ismail Jussa: Umeuliza swali lako kwamba masuala haya kwamba yanahitaji
zaidi ya mwaka mmoja, ndio maana ninachosema kwamba ni kwa mfano wako wa mwaka mmoja.
Lakini ninachosema mimi ni kwamba unapolichukua suala hili ukalitazama kwa upana wake kwanza ili tufufue kazi ya kuandika Katiba Mpya tunapaswa kwanza kurudi katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu sheria ile imeshapitwa na wakati, sheria ile ilikuwa imetaja tarehe maalumu za kufanya hatua mbalimbali ambazo sasa hivi zote zimeshapitwa na wakati.
Lakini si suala la kubadilisha tarehe tu kwa sababu kuna vitu tumejifunza kama nilivyosema katika mchakato ule wa mwanzo, bila shaka kama tutataka tupate Katiba Mpya, tusifikie kuwa na mgongano na mkwamo mwingine kwa sababu sidhani kama tunahitaji mkwamo mwingine basi tunahitaji pia kuyaondosha na kuyarekebisha yale ambayo yalisababisha mkwamo kwa mara ya mwanzo.
Kwa mfano, litakuja suala la muundo wa Bunge la Katiba liweje. Hilo si suala ambalo pengine tunadhani kwamba linaweza likamalizwa ndani ya muda mfupi kama inavyofikiriwa, kwa sababu binadamu ndio sisi, kila mmoja ana mawazo yake mpaka mfike mahala muelewane.
Na mimi ninashukuru Khalifa, katika uzoefu wangu nimeshiriki katika mazungumzo mengi ya kutafuta miafaka ya kisiasa, si kazi nyepesi kama ambavyo watu wanaweza kufikiria.
Kabla hamjaanza kila mmoja anadhani kwamba ana hoja za kumshawishi mwenzake lakini katika siasa na mambo kama haya unakuta kwamba si suala la hoja tu ni suala la hofu na wasiwasi ambao kila upande unataka ziondolewe ambazo unazo ili kufika pahala muelewane.
The Chanzo: Sasa nini kinakupa imani kwamba tukianza huo mchakato mwaka 2025 baada ya Uchaguzi Mkuu kama hiki kikosi kazi kinavyopendekeza mambo yatakuwa tofauti? Kwa sababu mpaka hivi sasa tuna miaka minne na pale kitakachoongezeka labda ni mwaka mmoja, nini kinakupa matumaini kwamba pengine tukianza huu mchakato wa kuandika Katiba Mpya baada ya Uchaguzi Mkuu hali itakuwa tofauti na sasa? Kwa sababu mimi nadhani kwamba mchakato unapaswa uanze kitakachotokezea hapo kati kitokezee lakini mchakato unaendelea. Wewe unaamini kwamba sasa hivi muda ni mchache sana lakini nini kinakupa matumaini kwamba tukianza huu mchakato mwaka 2025 au baada ya mwaka 2025 huo mchakato unaweza ukafanikiwa? Kwa sababu hata hapo kutakuwa ni miaka michache, una miaka mitano kabla ya uchaguzi mwingine.
Ismail Jussa: Kwanza mimi siamini, wala sisemi kwamba mchakato wa Katiba kwamba usimame au usianze wakati tunashughulukia haya mengine. Hoja ambayo mimi nimekuwa nikiisema na kuisimamia pamoja na ACT-Wazalendo tunaisimamia ni kusema kwamba kunahitajika kile kitu kinachoitwa mabadiliko ya msingi kwanza ambayo yatatupitisha katika chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2024 huku bara na vilevile Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Lakini hiyo haizuii, kwa mfano, haya majadiliano kuanza. Ninachosema mimi ni kujidanganya kuamini kwamba tunaweza kupata muafaka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na tukaingia kwenda kutengeneza Katiba Mpya tukiwa tunamaelewano hayo ya kitaifa na nitakupa mfano.
Chukulia kwa mfano kwamba tunalipataje Bunge jipya la Katiba. Tunarudia katika mfumo ule ule kwamba wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ndio wanaounda sehemu kubwa ya Bunge la Katiba?
Ikiwa ni hivyo, je, hata hao watetezi wa Katiba Mpya sasa wanaridhika kwamba Wabunge waliopo sasa ndani ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano au Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliopo sasa kwamba ndio waunde sehemu kubwa ya Wajumbe wa Bunge la Katiba?
Au ile sehemu iliyobakia ya watu ambao wanawakilisha makundi mbalimbali ambayo yaliingizwa ambao wengi walipendekezwa tulivyoambiwa na zile taasisi lakini wakateuliwa na Rais, tunataka turidhike na mfumo ule ule na kama haturidhiki na mfumo ule tunakuwa na mfumo gani wa kuwapata Wajumbe wa Bunge la Katiba?
Kama watachaguliwa na wananchi, kwa sababu tunayo mifano ya nchi nyingine ambapo ili kuondosha maslahi ya kisiasa basi watu wanaokwenda kutunga Katiba huwa wanachaguliwa kupitia uchaguzi huru na wa haki kwa ajili ya kazi moja tu ya kwenda kutunga Katiba Mpya na katika nchi za wenzetu mara nyingi wameweka hata masharti ili kuondosha maslahi kwamba mtu ambaye anagombea kwenda kuingia katika Bunge la Katiba hataruhusiwa baadae kugombea katika uchaguzi wa kuingia katika vyombo vya kutunga sheria ya nchi.
Sasa kama tunafikiri hiyo ndio njia nyingine mbadala wa hii je, ili kufanya uchaguzi wa hao wajumbe wa Bunge la Katiba huhitaji Tume huru kabla kuipata hiyo Katiba Mpya? Ndio maana nasema watu wamekuwa wakizungumzia hadithi ya yai na kuku lakini hadithi ya yai na kuku haina jibu la mkato kwamba lilianza yai ndio akaja kuku.
Kwa sababu nitakuuliza pia hilo yai alilitaga nani na kama alilitaga kuku huyo kuku alipatikana vipi kwanza. Kwa hiyo, haya mambo si mepesi ambavyo labda yana majibu ya mkato kama ambavyo wengi wanavyofikiria.
The Chanzo: Lakini si kwamba haya mambo yote yangepatiwa ufumbuzi ingekuwa nia tayari ipo? Yaani, kwa mfano, leo Serikali na nyinyi vyama vya upinzani mngekuwa mpo mstari mmoja kwamba Katiba Mpya inahitajika sasa na ni muhimu tukaanza mchakato sasa na kwamba haya maswali yote ambayo umeyaibua hapa ambayo ni ya msingi kusema ukweli pengine yangepatiwa jibu na kikosi kazi ambacho kimeundwa na ambacho kinataka mchakato wa Katiba Mpya uanze baada ya uchaguzi mkuu? Na swali langu jingine ni kwamba, kwa nini ninyi ACT-Wazalendo mnadhani ni muhimu kupigania mageuzi madogo madogo wakati uwezekano wa kupigania mageuzi makubwa upo? Kwa nini mnakwenda kwenye mageuzi madogo madogo wakati mngekuwa na uwezo wa kupigania mageuzi makubwa?
Ismail Jussa: Narejea pale pale Khalifa na wewe unaingia katika mtego ule ule kwamba labda sisi tunapigania mageuzi madogo.
The Chanzo: Hapana, mimi siingii kwenye mtego wowote. Wewe umezungumza hapo kwamba ninyi mnapigania mageuzi madogo, Tume huru na hicho ndio kitu ambacho kipo hadharani watu wanajua. Lakini swali langu mimi ni kwamba kwa nini uende kwenye mageuzi madogo madogo wakati ipo fursa, upo uwezekano, wa wewe kupigania kitu kikubwa hivi vitu vidogo vingejikuta humo humo. Kwa nini inakuwa hivyo?
Ismail Jussa: Unarejea tena pale pale Khalifa, kwamba unaingia katika mtego ule ule wa kudhani kwamba sisi tunapigania mabadiliko madogo madogo dhidi ya mabadiliko makubwa. Sisi tunapigania yote mawili. Tunachosema ni kwamba hatuoni uwezekano wa kufanikiwa katika haya makubwa ndani ya muda huu uliobakia.
Na ndio maana, kwa hiyo, tunaona kwamba tutainga katika uchaguzi mwingine kuanzia uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao upo ndani ya miaka miwili kutokea sasa kwa maana Oktoba 2024 halafu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Sasa tunaona hatari ya kwamba kuingia moja kwa moja katika mabadiliko makubwa ambayo unazungumza kuna uwezekano mkubwa msifanikiwe na pale mwanzo ulisema kwamba kama hamtafanikiwa mtaacha njiani halafu baadae mtarejea.
Sasa suala la mnaendelea na haya ambayo mnayakuta njiani, kwa mfano, chaguzi hizo katika mazingira yapi, na hivyo hivyo tena si vyema kwa Tanzania kwa hivi tunavyopendekeza sisi, watu wanatoa mifano lakini hawataki kuingia ndani katika mifano hiyo.
Chukua mfano wa Afrika Kusini. Afrika Kusini imepata Katiba Mpya imekuja kutungwa mwaka 1996 lakini katika kipindi cha mpito kutoka katika mfumo wa ubaguzi wa ukaburu kuingia katika mfumo wa kidemokrasia palipatikana kitu kilichoitwa Katiba ya muda ambayo ndio iliyotumika katika uchaguzi wa mwaka 1994.
Sasa ni suala la jina tu. Wewe utaita Katiba ya muda, sisi tutasema labda ni mageuzi madogo. Lakini kwa kifupi inakuwekea misingi kwanza ya kufanya chaguzi kwa sababu unajua kazi ya kukubaliana katika mifumo yote ya uendeshaji wa nchi ambayo inakuwa ndani ya Katiba ni kazi ngumu zaidi kuliko pengine kukubaliana kwanza mfumo wa uendeashaji wa siasa za chaguzi katika nchi.
Hiyo ndio mantiki yetu kwamba pengine kupigania kufanya marekebisho ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa inawezekana ikawa si kazi ngumu kama ambavyo kwa mfano kuzungumzia Katiba ambavyo inajumuisha madaraka ya Rais, mgawanyo wa madaraka, nguvu za Bunge, nguvu za mahakama. Kivipi vyombo na viongozi watahakikisha wanapatikana, mifumo ya uwajibishaji, vyombo vya ulinzi na usalama, masuala ya haki za binadamu, rasilimali za nchi na suala la muungano kwa upande wetu sisi.
Haya pengine mazungumzo ya kupata maelewano katika kila nukta, katika kila kifungu chake, yanachukua muda mrefu zaidi pengine zaidi unavyozungumzia sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa. Ndio maana tunachosema sisi, si kama kimoja kinafuta kingine.
Nimesema hapa yote yanaweza yakaanza, tukapata mabadiliko madogo ambayo yatatupeleka katika chaguzi ambazo zitaridhiwa na wengi 2020 hadi 2025, wakati huo huo bila kuzuia, kwa mfano, kuanza kwa majadiliano ya kutupeleka ni vipi kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.
The Chanzo: Kwa nini ACT-Wazalendo msichukue hiyo mbinu ambayo unaizungumza hapa?
Ismail Jussa: Ndio ambayo tumeichukua.
The Chanzo: Nyinyi mnasema Tume Huru kuelekea Katiba Mpya.
Ismail Jussa: Kabisa.
The Chanzo: Na nyinyi ni sehemu ya kikosi kazi ambacho kimesema mchakato wa Katiba Mpya utaanza baada ya Uchaguzi Mkuu. Kwamba sasa hivi tunataka mageuzi ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ambapo Katiba Mpya itakuja baada ya Uchaguzi Mkuu. Kwa nini nyinyi msisukume kwamba hapana mchakato usianze baada ya uchaguzi mkuu, mchakato uanze sasa wakati huku tunapigania Katiba Mpya huku tunapigania mageuzi mengine ya kimfumo ili uchaguzi unafanyika na mchakato wa Katiba unaendelea. Kwa nini hamchagui hiyo mbinu?
Ismail Jussa: Narudia tena, hatuiachi mbinu hiyo Khalifa na ukitusikiliza hata hiyo kauli ambayo umeinukuu hapo unaizungumzia Tume huru kuelekea Katiba Mpya. Sasa ile kuelekea sisi hatujasema tarehe na mimi nadhani hata hoja iliyotolewa na kikosi kazi kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, siamini kwamba pendekezo lile kwamba ndio limefunga mjadala wa suala zima.
The Chanzo: Wewe unakubaliana nacho lakini.
Ismail Jussa: Mimi binafsi sikubaliani nacho.
The Chanzo: Lakini chama chako kinakubaliana nacho.
Ismail Jussa: Nasema tena Khalifa, sisi kama chama hatujawahi kutamka hivyo na kwamba kuwa na mjumbe ndani ya kikosi kazi hakuhalalishi kwamba kile kilicholetwa na kikosi kazi ni kwamba umekiridhia.
Nitakupa mfano mimi haya mambo tusiyafanye labda ni mambo mapya sana, mimi na Mheshimiwa Tundu Lissu tulikuwa wajumbe wa Kamati ya Uandishi wa Kanuni za Bunge la Katiba. Tulivyokwenda wakati ule kulikuwa na mambo mengi sana ambayo tulikuwa tukiyataka, sio peke yetu mimi na yeye na wengine. Lakini kwa sababu ya mchakato wa kupewa na kuchukua haliwezi likafanyika kila jambo.
Ndio hivyo kuna baadhi ya mambo tumefanikiwa kuna baadhi ya mambo hatukufanikiwa. Na ndio maana tulipofika katika Bunge tukaja tukatetea kwa ujumla wake na yale ambayo yalikuwa yamepitishwa na kamati ya uandishi wa kanuni hata kama kuna mengine huko nyuma tulikuwa tunatofautiana nayo.
Kwa hiyo hata hili uzuri wake halijafungwa mjadala wake. Mimi ambacho nakiona bahati mbaya na kwamba hakisaidii katika hili na kumeundwa utaratibu wa kushauriana na umeanzia wapi, katika mkutano ambao ulisimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Dodoma, wengine wakaamua kususia.
Mimi naona mijadala, au mikusanyiko, kama ile ndio inapaswa itupe jukwaa la kubadilishana mawazo juu ya hizo hatua za kupita. Sasa watu wanaweza kuwa na mawazo tofauti lakini ukiyasemea nje ukawa si sehemu ya majadiliano yale unanyima fursa ya mawazo yako pia kuchukuliwa.
Ni kama ambavyo sasa hivi kuna mkutano ndani ya siku chache zijazo wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), mikutano ile si mikutano ya kisheria wala maamuzi yake hayatufungi kikatiba na kisheria ni mawazo. Lakini kwa sababu wanahusika, wananafasi mbalimbali katika taasisi mbalimbali katika nchi wananafasi ya ushawishi pengine kushiriki kwetu katika mikutano kama ile kunatoa nafasi ya kuchanganya na kuchakata mawazo tofauti ili tupate kilicho bora.
Kwa hiyo, mimi hata hilo lililokuwa limeletwa la kwamba pendekezo alilotamaka Profesa Rwekaza Mukandala kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya mimi binafsi siungi mkono. Lakini sio siungi mkono tu, siamini vilevile kwa sababu haijawahi kufikishwa bado ndani ya chama chetu.
Kwa hiyo, bado ni suala ambalo linajadilika, lakini linataka kuwa tayari kwa mazungumzo, mnapokuwa kila mmoja ana msimamo wake mkali katika upande wake hamuwezi kufikia maelewano katika nchi, wala upande mmoja hauna haki zaidi kuliko mwingine.
Hamtapata muafaka kwa kujionesha kila mmoja ni bora ili kulinda hoja, ni suala la kuweka hoja mezani. Na ndio maana hata huyo mjumbe wetu ambayo yupo ndani ya kikosi kazi, kwa maana kiongozi wa chama, ukisoma mijadala amekuwa akisema kwamba watu wamechanganya kwamba mkutano wa TCD unakwenda kueleza lilelile, amesema hapana, kila kitu kipo juu ya meza. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu watu kuendeleza mijadala.
Na siku zote baada ya kuwa mmepita katika kipindi kirefu cha misuguano na hujuma nyingi na uminywaji wa haki hamuwezi kurudi katika hali ya kuaminiana ndani ya muda mfupi. Tunazungumzia mwaka mmoja tu tangu jitihada hizi zimeanza kuwa zikifanyika. Pengine hizi hatua ambazo zinatupeleka katika Katiba Mpya zingeanza kuzungumzwa miezi michache iliyopita.
Kwa hiyo, nasema kwamba unaweza ukiwa nje ukadhani kwamba nitakwenda pale nikajenge hoja, nishawishi na nikubalike. Haifanyi kazi namna hiyo katika siasa, inahitajika mazungumzo mengi, majukwaa mengi watu kubadilishana mawazo. Na katika kusema haya narudia tena Khalifa, nayasema kwa uzoefu kwamba tumeshashiriki mazungumzo ya vyama tukadhani hivyo hivyo kwamba utakwenda pale kwa sababu unahoja mwenzako ataliona hilo. Siasa haiko hivyo. Kila mmoja anakuwa anavutia kwake.
The Chanzo: Mheshimiwa Jussa mimi nakushuru sana kwa muda wako na maoni yako ya ujumla. Lakini tumalizie labda unadhani ni kwa kiasi gani unaona kwamba chama chenu au nyinyi ACT-Wazalendo mpo katika upande sahihi wa historia ya kupigania mageuzi ya kisiasa nchini Tanzania? Nini kinakupa imani kwamba mnaona mnachokifanya ni sahihi?
Ismail Jussa: Mimi naamini tupo sahihi kwa sababu kwanza nichukue mambo mawili makubwa sana. Kuna suala, kwa mfano, Zanzibar tungeweza kuwa kama chama kingine cha siasa tukasema tu kwamba uchaguzi ulivyofanyika haukuwa sahihi, haukuwa uchaguzi, haukuwakilisha matakwa na maamuzi ya Wazanzibar na kwa hivyo sisi tunasusia.
Tulifanya hivyo mwaka 2016 katika uchaguzi wa marudio lakini katika pahala ambapo watawala wasio wastaarabu hilo halimfanyi kubadilisha chochote na tumeona miaka mitano ilikwenda hakuna chochote kilichofanyika, sio hakuna chochote kilichofanyika katika kurekebisha hali, kinyume chake yamefanyika maamuzi ya kuturudisha nyuma zaidi kuliko ambapo tulikuwa tumefika.
Kwa hiyo, katika hilo kwanza naamini tupo sahihi katika kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa upande wa historia kwa sababu bado tuna nafasi ya kuendelea kupaza sauti tukiwa ndani ya Serikali na tukiwa nje ya Serikali.
Na moja ambalo naliona, kwa mfano, kwa hali ilivyokuwa wakati ule tungeendelea kukaa nje tungepelekea ukandamizaji kuendelea dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. Kwa hiyo, kwa kunusuru maisha ya watu, kwa kunusuru ukandamizaji, tunaamini tulikuwa sahihi na hadi leo tunaamini tupo sahihi.
Bado kuna changamoto kama ambavyo tulizungumza mwanzoni mwa mahojiano haya lakini ni jukumu letu kuendelea kuzipazia sauti na mimi ninaamini historia itakuja kutuonesha kwamba tulikuwa pale kwa usahihi.
Na hivyo hivyo katika upande wa Jamuhuri ya Muungano. Tuna njia mbili: kuna njia ya kusema kwamba labda kama wenzetu tususie na tutoe mashinikizo tukiwa nje lakini pia tumeona kwamba tunaishi katika nchi ambayo utamaduni wa kisiasa, haswa upande wa Tanganyika huku, kwamba watu wake si watu ambao labda wako tayari kuingia barabarani kudai haki zao.
Kwa hiyo, mtaishia kupaza sauti katika hali kama hiyo inahitaji upande wa pili uone msingi, mchakato wowote wa mabadiliko inajumuisha kwenda hatua kwa hatua, hasa pale ambapo huna watu ambao wapo tayari kutoka hadharani na kuingia barabarani kuzitetea haki zao.
Na tumeona Watanzania mara ngapi tumeona vyama vya siasa au makundi mengine ya kijamii yamedai halikutokea kwa sababu utamaduni wakisiasa haukujengeka namna hiyo. Kwa hiyo, katika hali kama hiyo, naamini tupo sahihi katika upande wa kihistoria kudai mabadiliko kupitia kushiriki kwetu katika majukwaa mbalimbali na vilevile kushiriki katika mazungumzo na watawala tukiamini hiyo ni njia sahihi.
Na tunaamini kwamba siku wala si nyingi hata wenzetu ambao labda wanaona sisi hatupo sahihi watakuja kuungana nasi kwa sababu hakuna njia nyingine. Tusidanganyane Khalifa. Na hata kutoa matishio. Mimi ni mmoja siamini vyama ambavyo vinasema kwamba bila Katiba Mpya hatushiriki uchaguzi wa mwaka 2025. Tulifanya hivyo hivyo mwaka 2020 tukasema [bila] Tume huru hatushiriki uchaguzi lakini chama chochote cha siasa kinatambua kwamba uhalali wake, uwepo wake, unapimwa kupitia chaguzi.
Kwa hiyo, hata hao wanaosema hivyo kama hakujapatikana Katiba Mpya [hawatashiriki uchaguzi] tutaona hapo ukifika uchaguzi watashiriki katika uchaguzi. Sasa, kwa nini tufike katika hatua hiyo tusiianze sasa kushiriki katika michakato mbalimbali ambayo inaweza ikafanya hali ikawa afadhali wakati huo huo tunatafuta hilo kubwa zaidi ambalo litatujengea mfumo mpya wa uendeashaji wa nchi kupitia Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania?
Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Joseph Kirati amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com.