Ripoti ya CAG: ACT-Wazalendo Yapendekeza Njia Nne Kudhibiti Ubadhirifu Serikalini

ACT-Wazalendo yataka uwazi uongezeke ndani ya Serikali na Bunge lifanye kazi yake ya kuisimamia Serikali vizuri kama njia ya kuzuia ubadhirifu ndani ya Serikali usitokee.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Chama cha upinzani nchini Tanzania ACT-Wazalendo kimependekeza njia nne kuu ambazo kinaamini, kama zitatekelezwa ipasavyo, zinaweza kusaidia kudhibiti ubadhirifu wa fedha za walipa kodi ndani ya Serikali ambao umekuwa ukiibuliwa kila mwaka na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

ACT-Wazalendo yataka uwazi kwenye namna Serikali inavyofanya kazi uongezwe ili kuepesha mambo mengi kufanyikia gizani. Pia, kinataka Bunge lifanye kazi yake ya kuisimamia Serikali vizuri. 

Chama hicho ambacho ni mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar pia kimevitaka vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujengewa uwezo wa kuwezo kudhibiti ubadhirifu kabla haujatokea.

ACT-Wazalendo pia imemtaka CAG kuweka wazi ubadhirifu wote ambao anaona umetendeka, kikidai kwamba ripoti hiyo inayohusu ukaguzi wa shughuli za Serikali, mifumo ya udhibiti wa ndani na taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021, kuanzia Julai 1, 2020 hadi Juni 30, 2021, kuna taarifa haikuweza kuweka wazi.

Hayo yameibuliwa na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe wakati akiongea na waandishi wa habari jijini hapa wakati wa hafla ya uchambuzi wa ripoti mpya ya CAG iliyofanyika mnamo Aprili 14, 2022.

Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) amesema kwamba CAG anapaswa awe anatoa taarifa kwa TAKUKURU na Mkurugenzi wa Mashtaka punde tu baada ya kubaini ubadhirifu badala ya kusubiri kuripoti ubadhirifu huo kwenye taarifa yake ya mwisho wa mwaka.

“Taarifa kama hizi [za CAG] huko nyuma zilikuwa zinaripotiwa, lakini, mimi kwa uzoefu wangu, na nimekaa bungeni miaka 15, sijawahi huona taarifa yenye wizi wa waziwazi kama hii,” alisema Zitto, akimaanisha kwamba hali isingekuwa hivyo kama ubadhirifu huo ungeripotiwa mapema na hatua stahiki kuchukuliwa. “Kwa sababu ni wizi ambao, mtu yoyote yule, hata ambaye hajui mahesabu, anauona kabisa.”

Taarifa za ubadhirifu

Ripoti hiyo ya CAG ambayo iliwasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Machi 30, 2022, imesheheni taarifa za ubadhirifu wa fedha za walipa kodi na watendaji wa Serikali, ukiwemo ule unaohusisha ngazi za juu za Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi.

Baadhi ya mambo yaliyosheheni kwenye ripoti hiyo ni lile linalohusisha mashine 89 za makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani zinazotumiwa na trafiki ambapo iligundulika kuwa hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo wa malipo wa Serikali.

Mengine yanahusisha gharama ya Shilingi bilioni 478 ambayo Serikali imeingia baada ya kuvunja mikataba kiholela; wizi wa Shilingi bilioni 71 katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA); na Sintofahamu fedha za wananchi takribani Shilingi bilioni 196 kwenye mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.

CAG pia amebainisha uwepo wa wanaume waliopata huduma ya upasuaji au huduma za kawaida za kujifungua kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), huduma ambazo hutolewa kwa wanawake tu. 

CAG pia anabainisha kwamba Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambayo kazi yake ni kusimamia ujenzi wa barabara na madaraja, wamepewa kazi ya kuleta mtambo wa kuzalisha sukari katika kiwanda cha kuzalisha sukari Mkulazi, halafu mtambo wenyewe haujaletwa na fedha zimeshalipwa zote zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 50.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu kivuli wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu, akiongea wakati wa hafla ya uchambuzi wa ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni mnamo Machi 13, 2022, “[ripoti] imeibua hoja nyingi za ukaguzi ambazo tusingeweza kuchambua zote. Ilikuwa wakati mgumu sana kuamua hoja ipi tuichambue na ipi tuache,” alisema Semu, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Tanzania Bara).

Uwajibishwaji

Kwa upande wake, Zitto anaamini ipo haja ya kuongeza uwazi ndani ya Serikali, akibainisha kwamba kile kilichodhihirishwa kwenye ripoti ya CAG ni madhara ya kuendesha nchi gizani.

“Haya ni madhara ya kuendesha Serikali gizani,” Zitto aliwaeleza waandishi wa habari. “Kwa sababu tulikuwa tunaaminishwa kila kitu ni kizuri. [Kwamba] mambo yanakwenda sawa sawa, [kwamba] hakuna ubadhirifu. Lakini kumbe ni kwa sababu vyombo vya habari vilifungwa. Bunge likashughulikiwa, kwanza Bunge lenyewe likawa gizani”. 

Emmanuel Mvula, ambaye ni Waziri kivuli wa Fedha na Mipango wa ACT-Wazalendo, ameitaka Serikali kuwachukulia hatua wale wote ambao wanaweza wakawa wamehusika kwa njia moja ama nyengine na ubadhirifu ulioripotiwa na CAG.

Mvula alisema kwamba watumishi wote walioonekana kuhusika na ubadhirifu huo wachukuliwe hatua, ikiwemo kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa fedha zilizoainishwa kupotea katika kipindi husika. 

“Watu wote walio husika katika ubadhirifu wachukuliwe hatua,” alisema Mvula, akiita hiyo hatua ya muda mfupi. “Mengine haya tumependekeza masuala ya kimfumo yafanyiwe kazi ili kuweza kudhibiti yasijitikeze tena kwa muda mrefu.” 

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts