Kila mwaka wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inapotolewa huwa ni kipindi cha kuijua sura halisi ya Tanzania, uozo na aibu zake. Kwa mwaka huu haikuwa tofauti.
Kama lilivyoandika gazeti la Mwananchi: “Ni madudu yaleyale ripoti ya CAG.” Ni mwendo wa ufisadi wa kila aina: wizi, udanganyifu, upigaji, uhujumu uchumi.
Kinachouma ni kuwa wakati wavujajasho wengi wa nchi hii katika kada mbalimbali wakihangaika kuungaunga, kudunduliza vijipesa walau wapate kiasi cha kujikimu kwa mahitaji ya msingi, kuna watu wanadibua mapesa ya umma na kuyachezea.
Sikiza hii: maofisa sita wa Benki Kuu wamepiga Sh3.99 bilioni! Miongoni mwa maeneo yanayovuja sana ni zabuni na manunuzi ya umma. Inaelekea siku hizi watu hawachukui tena asilimiia 10 bali nusu au zaidi ya thamani halisi ya kinachonunuliwa.
Pesa za zabuni zinazotolewa haziendani na thamani halisi ya miradi kiasi kwamba mzabuni anaenda kuuza tena zabuni hiyo kwa kampuni nyingine na kubakia na faida kwa zaidi ya nusu!
Licha ya mijadala mahsusi ya jambo moja moja lililojitokeza katika ripoti ya CAG, kuna haja ya kujadili ufisadi, tatizo ambalo uwepo wake umethibitika hata kupitia taarifa za mashirika ya kimataifa, kwa upana wake.
Ripoti ya Shirika la Transparency International ya mwaka jana inaiweka Tanzania katika nafasi ya 87 kati ya nchi 180, katika viwango vya mafanikio ya kupambana na ufisadi.
Katika nafasi hiyo, Tanzania inaonekana kufanya vema kuliko majirani zake Kenya ambayo ni ya 128, Uganda 144 na Burundi 169, lakini ikipitwa na Rwanda iliyo katika nafasi ya 52.
Hata hivyo, ingawa kiulinganifu dhidi ya majirani zake Tanzania iko vema, ukiangalia alama 39 iliyopata unagundua kuwa tatizo la ufisadi bado ni kubwa. Kwa viwango vya shule zetu, 39 ni alama D (ikimaanisha dhaifu) huku ikitanguliwa na madaraja A (vizuri sana), B (vizuri) na C (wastani).
Tuzingatie pia kuwa Tanzania ilipata alama hiyo wakati nchi, kwa maneno ya Zitto Kabwe, ikiwa gizani ambapo uhuru wa habari ulifinywa, taasisi za kiraia zilikandamizwa, vyama shindani vilikandamizwa, na hata mihimili ya bunge na mahakama haikuwa na nguvu sana.
Katika kipindi hiki ilikuwa ni jambo hatarishi kuzungumzia ufisadi wa Serikali, labda kama uko nje ya nchi; na waliojaribu walikiona cha mtema kuni.
Katika kipindi hicho cha giza, tulikuwa na Rais aliyefanikiwa mno katika siasa za umaarufu (populism) akifanikiwa mno kuwafanya wengi waamini ufisadi umedhibitiwa na kuondoshwa kabisa.
Lakini ripoti hii inatoa taswira tofauti na ni ushahidi kuwa kinyume na imani hiyo, ukweli ni kuwa ufisadi ulitamalaki katika Tanzania ya awamu ya tano.
Udhaifu wa Serikali au tatizo la kijamii?
Wengi wanaangalia ufisadi kama tatizo linalotokana na udhaifu wa Serikali. Wanaamini ufisadi unaweza kudhibitiwa kwa mkono wa chuma. Hawa hawajakosea, ila kuna picha pana zaidi hawajaiona, nayo ni, mchango wa jamii ya Watanzania, au jamii za Kiafrika kwa ujumla, katika kulea ufisadi.
Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu, tutakiri kuwa jamii ya Kitanzania, na huenda ni tatizo la sehemu kubwa ya Afrika, inatukuza ufisadi.
Ushahidi wa hili ni mitazamo inayoakisiwa na mazungumzo yetu katika familia na mitaani, ambapo tunawasema vibaya watu wachache waaminifu na kuwaona wazembe kwa kutoiba na kufanya ubadhirifu.
Utasikia kauli kama: “Anachezea nafasi yule.” “Atajuta uzeeni.” “Unaona wenzake wanavyojenga, yeye amezubaa tu!?” Katika msingi huo, mtu akifanya kazi katika baadhi ya ofisi za Serikali kama vile TRA, Benki Kuu, vitengo vya ugavi na manunuzi, jamii inategemea tu awe tajiri na asipotajirika huyo ni mzembe.
Si hivyo tu, kwa wengi wetu, ufisadi huwa tatizo pale tu tunapokuwa hatufaidiki kwa ufisadi huo. Vinginevyo kama wapigaji ni ndugu, rafiki na jamaa zetu huwa tunaubariki huo ufisadi na hata kuutetea.
Katika mazingira hayo, unajiuliza tunapinga ufisadi kwa kuuchukia au tunawaonea wivu mafisadi na kutamani nafasi zao?
Hili ni swali muhimu kwa sababu wakati inauma kuona mtu akichota mabilioni, ukweli mchungu ni kwamba hata watumishi wa ngazi za chini nao wanafanya udanganyifu ‘katika urefu wa kamba zao.’
Kwa sisi raia, ni kawaida mtu anapotaka huduma, ajira au kitu kingine katika ofisi fulani kuuliza watu wa karibu kama wana mtu pale wanamjua. Maana yake huyu anatafuta mwenyeji atakayemsaidia kwenda kukata kona, kutofuata taratibu, kuruka foleni na kadhalika. Kwa namna hii jamii inafanya ufisadi kuwa jambo la kawaida.
Kwa hiyo, wakati tukinyonyea Serikali zetu kidole, tujiulize nafsi zetu kama kweli tunachukia ufisadi, na pia tujiulize kama sisi wenyewe hatuchangii kukomaza ufisadi kwa kusherekea wapigaji na sisi wenye kukata kona tunapotaka huduma katika maeneo ofisi mbalimbali: uhamiaji, TRA, polisi na kadhalika.
Ni nchi ya wachamungu au wenye dini?
Hali hii ya jamii ufisadi mkubwa kutamalaki na wananchi kutukuza ufisadi inatokea katika nchi ambayo inasemekana ni ya watu wa dini sana. Hii inafikirisha sana na kutupeleka katika swali la nini maana ya dini? Kuna mtazamo finyu na mpana. Mtazamo finyu wa dini ni kwenda msikitini na kanisani na kusali na labda kutoa sadaka.
Lakini kwa mtazamo mpana, ukiacha suala la kujenga mahusiano na Mungu kupitia sala, ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya amri za dini zinahusu mahusiano yetu na watu na viumbe wengine wa Mwenyezi Mungu.
Je, tunawatendea ipasavyo viumbe wa Mungu? Kwa bahati mbaya upande huu wa dini unaohusu miamala yetu na watu wengine umesahaulika.
Katika jambo hili la dini kuna unafiki mkubwa. Laiti tungekuwa watu wa dini kiukweli, tungetekeleza amri kama usiibe, usidhulumu, usinyang’anye, usidanganye, ambazo nina hakika zinatajwa katika Biblia na Qur’an. Na kama tungetekeleza amri hizo, kiwango cha ufisadi kingepungua sana.
Hapa tunagundua kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kuwa mfuasi wa dini na mchamungu. Unaweza kuwa mfuasi mzuri wa dini, unaenda kanisani au msikitini, unatoa sadaka lakini sio mchamungu.
Uchamungu ni dhana pana ambayo inavuka mipaka ya dini. Awe Muislamu, Mkristo, Mhindu, Mpagani mchamungu haibi, hadhulumu. Kwa hiyo, ripoti za CAG zitusaidie kutafakari tena masuala haya ya kiroho.
Nafasi ya elimu
Kwa upande mwingine, ni muhimu tutathmini upya mfumo wetu wa elimu. Tunawezaje kuwa na mitaala inayomuandaa mtu kuwa sio tu mtendaji mzuri lakini pia muadilifu?
Nafahamu kuwa kuna masomo ya maadili katika karibu kila fani za chuo kikuu, lakini kwa nini somo hili limekuwa kama kozi yoyote nyingine ya kujipatia alama tu na si zaidi?
Nikimalizia, jambo la msingi hapa ni kuwa vita dhidi ya ufisadi na rushwa lazima ipiganwe kwa mbinu tofauti. Ni kurahisisha tatizo gumu na kujidanganya kudhani kuwa ukali wa viongozi pekee utaondoa ufisadi.
Tusichoelewa ni kwamba haohao viongozi wa Serikali tunaowategemea kupambana na ufisadi ni sehemu ya jamii hii hii inayobariki ufisadi. Huko katika ngazi za juu za uongozi ndiyo ufisadi mkubwa hutokea. Usishangae hata madaraka yao waliyapata kwa ufisadi! Ufisadi ni tatizo la kijamii na tukigundua hilo mapema ndiyo salama yetu.
Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.
One Response