The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kutweza Kiswahili ni Ishara ya Kujidharau, Kutojiamini

Kiswahili kinakidhi mahitaji kama lugha ya kufundishia iwapo tukiachana na kasumba ya kujidharau  na kukosa kujiamini.

subscribe to our newsletter!

Nimekulia katika jamii ambayo kila kitu kinachofanyika kwa umahiri, uzuri, usafi, weledi, ufanisi kinanasibishwa na Uzungu. Mzungu ndiyo mtaalamu, Mzungu ndiyo kaelimika, Mzungu ndiyo kastaarabika, Mzungu ndiyo mjanja, Mzungu ndiyo mweledi. Kila kitu kinachohusika na uzungu kimebarikiwa.

Ni katika mtiririko huo ndiyo hata Kiingereza, alama kubwa ya uzungu hapa Tanzania, ndiyo lugha inayoonekana ya usomi yenye uwezo wa kubeba dhana ngumu za kiuanagenzi na kiuanazuoni, na kinyume chake lugha zetu hazina uwezo huo.

Hivi majuzi nilihudhuria mafunzo ya sarafu za kidigitali, yaani cryptocurrency. Muhudhirishaji mada alikuwa Mtanzania na hadhira yake pia ilikuwa ni Watanzania lakini akawasilisha mada kwa Kiingereza.

Nikauliza, kwa nini msifundishe kwa Kiswahili ili watu wengi wapate fursa ya kujiunga kujiongezea maarifa? Nikajibiwa kuna maneno mengi ya kiufundi ambayo hayana fasili ya Kiswahili!

Nikajiuliza, hivi Kiswahili ni maskini kiasi hicho hadi kikose maneno ya kuelezea dhana kama hizi? Au sisi ndiyo maskini wa akili tunaoshindwa kukitumia Kiswahili? Elimu gani hii isiyowezekana kufikishwa kwa wengine kwa lugha zetu za  asili, hususani Kiswahili, lugha iliyoenea nchi nzima na inajulikana kwa utajiri wake mkubwa wa misamiati iwe ya asili au ya kukopa?

Tunaweza pia kuuliza maswali mengi pia kuhusu wasomi wenyewe wasioweza kuhudhurisha mada kwa Kiswahili. Kuna faida gani ya kuandaa mhadhara wa wazi Tanzania halafu uishie kutumia Kiingrereza?

Yaani baada ya kuchimbua elimu  vyuoni mabuku kwa mabuku, msomi hawezi kuielezea jamii yake ya watu wasiojua Kiingereza kile anachokijua? Je, hii ina maana kuwa ili wanajamii wapate maarifa hayo lazima kwanza wajifunze Kiingereza?

Wote tunajichubua kwa namna tofauti

Aghlabu huwa tunawatukana dada zetu kwa kupenda kujichubua ngozi ili wafanane na Wazungu. Lakini kiuhalisia wote tunajichubua kwa namna tofauti, mojawapo ni kuwa na hizi kasumba za kuabudu uzungu.

Kwa maana nyingine, wasomi wanajichubua kwa kutaka kuwa na vijitabia vya  kizungu, bila ulazima wowote.

Tuwe wakweli, mathalan, hii tabia ya wasomi kutukuza Kiingereza hadi inafikia hatua ya kukitumia katika mazingira ambayo nyote mliopo mna lugha moja inayowaunganisha na ambayo mnaweza kuelewana kirahisi zaidi ina tofauti gani na tabia za wadada za kujichubua ngozi na kuvaa nywele za watu wengine?

Hoja ya maneno ya kitaalamu ni dhaifu mno. Kwani ukifundisha kwa Kiingereza maneno hayawi tena ya kitaalamu bali ghafla tu yanakuwa rahisi? Ukweli ni kuwa maneno hayo ya kitaalamu bado hulazimika kupewa tafsiri kwa hichohicho Kiingereza. Sasa kwa nini ishindikane kupewa tafsiri kwa Kiswahili?

Ni Kiingereza hiki ndio kinahusika na uduni wa elimu yetu kwa sababu kinalazimisha watoto kukariri kwa ajili ya kufaulu mitihani na siyo kuelewa. Siku moja nilikuwa nazungumza na wanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo kikuu, nikiwaelezea dhana ya mihimili ya dola na mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge, Mahakama na Serikali.

Niliwasisitizia kuwa hii haipaswi kuwa elimu mpya kwao kwani nina hakika washasoma katika somo la uraia. Hawakunielewa.  Baadae nikataja ‘branches of government’, ‘separation of powers’, ‘executive’, legislature’, na judiciary’ wakang’aka, “Aah kweli hivyo tulivisoma. Ungesema hivyo tungekuelewa!.”

Hawa ni wasomi wasiojua dhana muhimu za kiutawala kwa lugha yao wala kuelewa zina maana gani hasa katika muktadha wa nchi yao!

Kuvunjavunja hali ya kujiamini

Ni hiki Kiingereza pia ndiyo kimehusika na kuvunjavunja hali ya kujiamini ya Watanzania wengi maana ukikosea katika  kuzungumza Kiingereza tafsiri yake wewe hujasoma, wewe kihiyo na tena ni mbumbumbu.

Kwa msingi huo, imefika wakati mambumbumbu wanaojua Kiingereza wana hadhi kuliko wataalamu weledi wenye udhaifu katika Kiingereza, hasa cha kuzungumza.

Kwa kigezo hiki cha kupimana usomi kwa Kiingereza imefika wakati Watanzania wengi wameathirika kwa kuingiwa na hali ya kutojiamini. Mtu anakwenda kwenye usaili wa kazi anawaza aibu ya kuonekana hajui Kiingereza kuliko maudhui ya utaalamu unaohitahitajika.

Kwa nini iwe sharti mtu ajue Kiingereza, lugha ya kigeni, ndio atambuliwe kasoma? Kwa nini Watanzania tujibebeshe mizigo mizito namna hii?

Katika mazingira haya ndio baadhi yetu tunashangaa kwamba watu wanatetea Kiingereza kiendelee kutumika kama lugha ya kufundishia bila kuzingatia kuwa kwa kufanya hivyo tunajifunga zaidi katika mahusiano ya kikoloni na wale waliotutawala na hivyo kujiweka katika hatari ya kuwa chini ya kivuli chao daima.

Lakini hii haishangazi sana kwa sababu kwa bahati mbaya tumekuwa watu wa kuiga wakoloni na umagharibi katika kila nyanja. Waliturithisha mifumo yao kiutawala, wakatufundisha itikadi zao za siasa na wakatuachia hata sheria zao.

Tumejenga utegemezi kiasi kwamba tunawategemea wao hata kwa majibu ya changamoto zetu!

Matokeo ya hali hiyo ni kujidharau na kuwa na jamii inayoamini kwa dhati kabisa kuwa sisi ni dhaifu mbele ya Wazungu na kitu pekee tunachoweza kufanya ni kuiga na kufuata nyendo zao na kuwa nakala yao bora.

Anayewahi kwenye miadi ana tabia za  mzungu

Kujidharau kumepenya hadi kwenye jamii pana. Jamii inaitakidi kuwa anayewahi kwenye miadi ana tabia za  Mzungu, na mchelewaji au mtu mbeambea ana Uswahili, ambapo kwa huku kwetu ni neno linalowakilisha Waafrika wote.

Katika kilele cha  kujidharau, wasanii wetu waliwahi kuimba bora wangezaliwa mbwa majuu huko kuliko kuwa binadamu Tanzania.  Hata mazao, matunda, bidhaa yale yanayoonekana bora ni ya  kizungu.

Ukiacha tabia ya wakinadada kujihariri miili yao kwa kujichubua na kuvaa nywele za watu wa mataifa mengine ili aidha wafanane na Wazungu  au wakidhi vigezo vya Wazungu vya mwanamke mzuri, imekuwa ni fahari na jambo la kupandisha heshima kwa dada zetu, na hata wakaka, kutoka kimapenzi na Mzungu, kwa sababu tu ya rangi. Ni jambo la fahari hadi muhusika anaandikwa magazetini.

Kaa vijiweni usikie vichekesho vya kutukana Uafrika na kujidharau. Kuonesha Wazungu ni watu makini. Mtaniani mmoja akaandika eti wakati Mzungu akiamka anakuna kichwa, Mwafrika akiamka mkono moja kwa moja unagusa sehemu za siri kuhakikisha kama zipo!

Katika mazingira haya kukataa lugha yetu tunayoijua wote kutumika kufundishia si jambo la kushangaza, bali ni sehemu ndogo ya changamoto kubwa ya kijamii: kujidharau.

Hivi hatujiulizi iweje Mwenyezi Mungu wa haki abague lugha baadhi ziwe za kisomi na nyingine ziwe za kusambazia umbea? Halafu ni lugha za jamii zilizoendelea kiuchumi tu Mungu aliamua kuzibariki uwezo huo wa kubeba dhana ngumu za kiuanazuoni?

Kiswahili kama lugha ya kufundishia

Nikiona hali hii nakumbuka kaka zangu wawili, wahitimu wa darasa la saba tu wa karibu rika langu wenye gereji zao kubwa za magari.

Kaka zangu hawa hawajui kutamka hata kifaa kimoja cha gari kwa usahihi wa lugha asili ya maneno hayo yaani Kiingereza lakini wanazijua gari kindakindaki.

Kwa kweli hakupaswi kuwa na mjadala  juu ya ipi ni lugha bora ya kufundishia. Ni wazi kabisa Kiswahili kinakidhi mahitaji, iwapo tukiachana na hiyo kasumba ya kujidharau  na kukosa kujiamini na kuanza  kutafuta kila aina ya visingizi vya kuhalalisha Kiingereza.

Nakaa nawaza siku itakapofika Kiswahili kupewa nafasi yake inayostahili na kuwa lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu, tutakapoacha kupimana usomi kwa kigezo cha uwezo wa kuzungumza lugha ya kigeni na tutakapoachana na haya matabaka ya wenye fedha za kununulia watoto wao Kiingereza kwenye shule za ‘english medium’ dhidi ya wale wengi wa shule za kata.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *