Dar es Salaam. Dhana ya ufeminia ni moja kati ya dhana zinazoibua tafsiri mbalimbali kwa watu tofauti tofauti. Pengine hakuna mtu sahihi zaidi wa kuongea naye kuhusiana na dhana hiyo inayoendelea kushika kasi ulimwenguni kote ukiachana na yule aliyeamua kujitokeza hadharani na kusema yeye ni mfeminia.
Mwanahamisi Singano ni mfeminia ambaye harakati zake zimejikita kwenye kuangazia ni kwa namna gani mapambano ya usawa wa kijinsia katika jamii yanaingiliana na mapambano dhidi ya athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwenye mahojiano yafuatayo kati ya The Chanzo na mwanaharakati huyo, Singano anautaja mfumo dume kama chanzo kikuu cha matatizo mengi katika jamii kwani unalenga kuifanya jamii kuwa yenye manufaa kwa jinsia moja (ya wanaume) kwa gharama ya jinsia nyengine (ya wanawake).
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake, Singano pia anatoa tathmini yake ya ujio wa Samia Suluhu Hassan kama rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na endapo kama hatua hiyo ni chanya au hasi kwenye mapambano ya kupigania jamii yenye usawa wa kijamii Tanzania na kwengineko. Endelea …
The Chanzo: Labda tuanze pale ambapo tunapaswa kuanzia. Wewe ni moja kati ya watu ambao mmejitokeza hadharani na kusema kwamba mimi ni mfeminia, na labda pengine tungeanzia hapo, labda pengine kusema mfeminia ni nani na kwa nini wewe ni mfeminia pia?
Mwanahamisi Singano: Mimi ni mfeminia kama ninavyosema kila siku. Tunaita ufeminia kwa Kiswahili, [kwani hili neno ‘feminism’] tumelitohoa kwa sababu sidhani kama kuna jina zuri zaidi hili. Lakini pia linaleta ule uhalisia wa ufeminia.
Na nimejiweka hadharani kama mimi ni mfeminia kwa sababu kwanza sidhani kama kuna sababu ya kujificha, moja. Lakini pili, katika zile kanuni za ufeminia tunasema moja ya kitu muhimu sana katika ufeminia ni kutambua kama wewe ni mfeminia na kujitambulisha kama wewe ni mfeminia.
Kwa hiyo, tunasema ni muhimu kujitambulisha kama mfeminia kwa sababu jina katika harakati za ufeminia, jina lina maana kubwa. Uchaguzi wa jina kwamba mimi nijiite nani ina maana kubwa sana.
Mfeminia ni mtu ambaye, kwa tafsiri yangu mimi, ni mtu ambaye anapigania dunia iliyo sawa. Dunia ambayo haina ubaguzi. Dunia ambayo haina unyanyasaji. Dunia ambayo hakuna uporaji. Dunia ambayo ni salama. Dunia ambayo ni nzuri kwa kila mtu kuishi lakini pia siyo tu mtu, mtu na vitu vilivyoumbwa kwenye dunia.
Kwa hiyo, kwetu sisi ukiwa mfeminia maana yake umepigania haki katika usawa. Lakini muhimu zaidi pia katika ufeminia ni kujua kwamba si kitu kimoja ambacho ni tatizo. Ni kwenda kwenye mizizi ya tatizo ni nini na mimi hilo hasa ndio lililonifanya nikataka kujifunza zaidi kuhusu ufeminia.
Kwa sababu mara nyingi tunaangalia vitu kwenye matawi, kwamba sijui watoto hawasomi, tumeishia tu hapo, tujenge shule watoto wasome. Lakini hata tunapozijenga watoto hawasomi kwa sababu hatujaenda kwenye chimbuko la kwa nini watoto wa kike hawaendi shule.
Kwa hiyo, ufeminia unatulazimisha sisi twende tukaangalie nadharia, twende tukaangalie vyanzo vya vitu, twende tukaangalie chambuzi mbalimbali. Kwa hiyo, unatupeleka kule kwenye mizizi na jinsi gani tunaweza tukautatua huo mzizi.
Lakini zaidi tunasema ufeminia pia unatupa sisi zana kusema sio tu mimi napigania haki za mtoto wa kike, kwa mfano, haki za mwanamke lakini jinsi gani yale mapigano umeyawekea dhamira, umeyafanya kuwa ya kwako, umeyafanya kuwa yanakuhusu kwamba hiki si kitu cha nje.
Yaani si kwa sababu mtoto wa Khalifa [Said, mwandishi] au si kwa sababu au tumeona kwamba watu wengi wanasema kwamba mimi napenda usawa kwa sababu nina mtoto wa kike. Je, [kama] usingekuwa na mtoto wa kike usingekuwa unafanya masuala ya usawa?
Au mimi napenda kwa sababu mimi nimezaliwa na mwanamke. Sasa sisi tunasema tunataka usawa kwa sababu sisi wote tuna haki ya kuwa sawa. Iwe nimezaliwa, nimetoka mtini, iwe nina mtoto wa kike sina mtoto wa kike hilo ndio jambo la msingi, hilo ndio suala kuu.
Kwa hiyo, ufeminia unatuletea hiyo dhamira kwa nini tunafanya tunachokifanya, tunawezaje kwenda kwenye mizizi, na tunawezaje kwenda kutengeneza jamii ambayo ni salama kwa kila mtu na vitu vilivyomo.
The Chanzo: Labda ni katika hatua gani ya maisha yako uliweza kupata hiyo aina ya uelewa, au hiyo aina ya uchambuzi, na mpaka ukafikia hatua ya kusema kwamba mimi napaswa kuwa mfeminia au mimi ni mfeminia, labda kwa ufupi kama unaweza kutushirikisha na sisi?
Mwanahamisi Singano: Kulijua jina ni hapa tayari nishakuwa mkubwa. Lakini mimi nimezaliwa Tanga, na sisi tumezaliwa watoto wa kike wote, kwa hiyo nakumbuka siku mdogo wangu wa mwisho anazaliwa, kwa sababu sisi tumeachana sana, kwa hiyo siku mdogo wangu anazaliwa mama alikuwa hospitali tunajua mama amekwenda hospitali kujifungua, mimi nilikuwa na miaka kama 12 hivi, [au] 13.
Anarudi baba anaulizwa kwamba, mama yangu mdogo anamuuliza dada amejifungua mtoto gani, baba akasema hao hao. Na unaelewa hata mapambano ya mama alivyokuwa na hamu kwa hiyo mdogo wangu yule wa mwisho alijifungua mama akiwa ameshajiandaa na vikaptura, sijui na vinini kwa sababu alikuwa anajua kwamba huyu ndio atakuwa mtoto wangu wa kiume, huyu ndiyo atakuwa mrithi, huyu ndiyo atakuwa mbeba jina la ukoo, huyu ndiyo atakuwa atakaye tuhifadhi yaani vitu vyote hivyo na sisi huku tulikuwa hatuonekani.
Kwa hiyo, tangu nimezaliwa nimekuwa naiona hiyo na mtoto wa kike niliyezaliwa na kukulia kwenye familia ambayo sisi tumekuwa tunalindwa sana, yaani wewe unaonekana nafasi ipo hivyo. Kwa hiyo, kuna vitu nilikuwa nataka kufanya, nataka kwenda nje kucheza, siendi kwa sababu ni mtoto wa kike.
Nataka kwenda kufanya hivi, kwa hiyo nilikuwa naona kwamba kwa nini siwezi kuwa. Sasa tangu nipo mdogo nikawa nasema kila siku mimi nataka kuwa mtoto wa kiume wa baba yangu.
Kwa sababu nilikuwa nataka kuwathibitishia kuwa si sahihi kwamba sasa hujapata mtoto wa kiume haimaanishi kwamba hautasaidiwa, haimaanishi kwamba hautakuwa na mtu anayekujali, haimaanishi kwamba ndoto ulizokuwa nazo kwa watoto wako haziwezi kufanyika sio.
Kwa hiyo, nikataka kuwa hiyo kwamba inabidi nimthibitishie baba yangu kuwa si sahihi, sisi tupo watoto wa kike na tutafika huko. Kwa hiyo, kuanzia tu mwanzo udogoni nilikuwa nataka kufanya vile vitu vya kiume vya kiume lakini baadae nikaja nikajua sina sababu ya kumthibitishia kwa sababu hivi vitu si kwa sababu wanaume wanafanya kwa sababu ya vinasaba.
Ni kwa sababu jamii imejenga kwamba mimi nafasi yangu nikishakua, nikishabalehe, nikaolewe, nizae, nikashatoka kwenye familia nitaitwa jina jingine nitafanya hivi nitakuwa tena sipo huku. Kwa hiyo, nikaanza kuziona hizo dalili mapema na nikaanza kutaka kutoa na kuvaa uhusika ambao kijamii sio uhusika wangu.
Na nilipokuwa mkubwa sasa nikaja kujua kumbe kwenye hili sipambani peke yangu. Ni mapambano ambayo wanawake wengi wanayapitia kutaka kuleta nafasi yao kwenye jamii kutambulika, kutaka kuwafanya wazazi kutaka kuifanya jamii wajue kwamba si mtoto wa aina moja ambaye anathamani zaidi kuliko mwingine na baadae nilikuja kujua kwamba kuna ufeminia, nikajua kumbe nilichokuwa nakiwaza, nakifikiri, nakifanya ni sehemu ya hii kweli. Kwa hiyo, nikajiona nipo nyumbani.
The Chanzo: Kwa hiyo ilikuwa ni …
Mwanahamisi Singano: Ilikuwa ni safari.
The Chanzo: Ilikuwa ni safari ndio lakini pia ilikuwa ni kitu binafsi.
Mwanahamisi Singano: Ilikuwa ni kitu binafsi mpaka kesho ni kwangu mimi binafsi kwa sababu moja ya kitu ambacho ni cha kufurahisha, kwa mfano, mzazi wangu mimi ni baba yangu ni mkubwa, bila shaka ana wakubwa zake wa kiume wengine lakini kwa wale ambao tayari wamebaki Tanga ambao ndio nyumbani ukitokea msiba tutapeleka Tanga yeye ndio mkubwa wa kiume.
Na katika familia zetu yeye ndio inabidi sasa kukiwa kuna msiba yeye ndiyo kaka mkubwa inabidi aende. Lakini bahati mbaya sana yeye hana mtoto wa kiume. Kwa hiyo, yule mtoto wake wa kiume angekuwepo ndiyo ingekuwa inabidi abebe yale majukumu ya familia.
Kwa hiyo, katika harakati mimi imenibidi nibebe yale majukumu ya kiume, tukifiwa lazima niseme kwamba sawa sasa tunapanga kufanya nini?
The Chanzo: Maisha ya mfeminia yanaonekanaje?
Mwanahamisi Singano: Ni jambo la kusisimua sana. Ni mazuri kwangu mimi nayapenda kwa sababu ni maisha ambayo yanakupa uhakika wa kitu unachokifanya ambayo mimi najua kile ni kitu cha tofauti kwa mtu mwingine yoyote.
Lakini mimi binafsi napenda kufanya kitu ambacho najua chimbuko lake ni nini. Napenda kufanya kitu ambacho kina athari, yaani sitaki kufanya kitu ambacho kwa sababu tu nimefanya ambavyo tunaona watu wengi tu wanafanya, yaani hata katika kiwango cha kawaida tumemuona.
Umemuona mtoto yupo barabarani anaomba tunona tu tutampatia shilingi kumi lakini hatujiulizi kwa nini yupo barabarani? Yupo salama? Alifikaje barabarani na vitu vingine kama hivyo. Kwa hiyo, maisha ya ufeminia yananifanya nafikiria, najua kwamba kwa nini hiki kinatokea na nini nifanye.
Lakini pia ni maisha ambayo yanachangamoto sana, sana, sana, sana. Hasa katika jamii zetu ambazo bado kuwa mfeminia ni kama wewe umefukuzwa, yaani kama wewe umelaaniwa, wewe unataka vitu ambavyo haviwezekaniki wewe, ni mtu ambaye unachukia wanaume, wewe ni mtu ambaye huambiliki, wewe ni mtu ambaye hushauriki, yaani mabaya yote tumewekewa sisi.
Kwa sababu tu tumeamua kusema kwa dhati yetu kwamba dunia tunayoishi sisi ni dunia ambayo siyo ya usawa na tumechukua hatua ya kufikiria dunia ambayo ni mbadala na watu wengi wameamua kuwa kwenye faraja ya dunia tuliyokuwepo kwamba hivi ndivyo nilivyoikuta basi na mimi nitafanya haya haya niliyoyakuta bila kuangalia njia nyingine bora zaidi.
Kwa hiyo, ile dhamira yetu ya kutengeneza dunia mbadala inafanya tunaonekana kuwa hivyo. Kwa hiyo, ni maisha ambayo yanachangamoto kubwa sana. Na mara nyingi mtu anaponiambia mimi nataka kuwa kama wewe, mimi namwambia usione tu mazuri ya kuwa kama mimi, je, utaweza kuubeba mzigo na miba na matusi na dharau na kejeli ya kuwa mfeminia?
The Chanzo: Samahani nataka kukuuliza hivi na umegusia hapo kidogo. Kwa hiyo, unataka kumaanisha kwamba wewe haujawahi kuolewa wala haujawahi kuwa na watoto?
Mwanahamisi Singano: Hapana, niliwahi kuolewa [na] nina watoto watatu ni watoto wazuri Alhamdulillah!
The Chanzo: Kwa sababu hiyo ndiyo dhana …
Mwanahamisi Singano: Siku hizi ndiyo wanasema kwamba tunaolewa lakini hatukai kwenye ndoa.
The Chanzo: Na hii inakufanya ujisikieje wewe kama mfeminia, unapigania kitu ambacho ni kizuri lakini kwenye jamii watu wanatafsiri tofauti ya kile ambacho unakifanya lakini na wewe mwenyewe binafsi?
Mwanahamisi Singano: Sishangai kwa sababu katika mapambano mimi ninayopambana nafikiri kama watu wa kawaida wangekuwa hawaguswi kwa jinsi wanavyoguswa mimi ningejua kuna kitu sifanyi sawa sawa.
Lakini ukweli kwamba watu wanaguswa unajua kwamba umegusa mahali ambapo hapaguswi ndio maana kuna huo mwitikio. Wanasema ukichukua tindikali ukiweka tu hapa ambapo hapana kitu utasikia tu ubaridi lakini kama pana mchubuko utasikia inaanza kuwasha.
Kwa hiyo, ni alama kwamba tunafanya kazi si kubwa japokuwa muda mwingine inakuja na hasara kwenye sifa zako, hasara kwenye amani yako, matusi. Kuna siku mtu anakwambia kitu, unachapisha kitu kutoka sehemu nzuri katika moyo wako, mtu anakutukana matusi mpaka usiku unaamka unasema hivi huyu mtu ananijua, yaani hata hayo majina yangu matatu mpaka akanitukana matusi ya kiasi hiki?
Kwa hiyo, ni changamoto na hiyo inawafanya watu wengi sana ama wanaacha hata kama mtu akitaka anawaza kwamba nitapigania usawa lakini nitapigania usawa kwa hasara gani. Kwa hiyo, matokeo yake wameachwa wachache ambao wanafanya hiki kitu au ambao wanaona kwamba liwalo na liwe nitafanya, nitasema.
Lakini wengi wameacha na kwa sababu wengi wanaacha hawa wachache wanaendelea kusonga mbele kwa sababu ni wachache ambao wanajulikana, ambao kila mtu sasa ndio anafanya mfuko wa kupiga. Kwa hiyo, inatengeneza hali kama hiyo.
The Chanzo: Unadhani mnapokea ukinzani, nyinyi mafeminia, mnapokea ukinzani kutoka kwa makundi gani kwa kiasi kikubwa?
Mwanahamisi Singano: Yote, yote. Wanawake na wanaume kwa sababu kwenye ufeminia, ufeminia upo wazi kwamba dhana ya mfumo dume ni dhana ambayo bila shaka inawanufaisha wanaume na kuna wanawake ambao wananufaika lakini ni dhana ambayo inabebwa na inahamishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na wote wanawake na wanaume.
Mimi nimekua walionifundisha katika eneo langu kwenye jamii ni kwamba mwanamke awaje walikuwa wengi ni wanawake ndio wanakufundisha kwamba wewe ndio mwanamke unatakiwa kuwa hivi.
Kwa hiyo, wale ni moja ya mfumo. Kwa hiyo, mimi nikiwaona wanawake wanavyopika kwa sababu najua kwa hiyo sishangai na moja ya kitu ambacho mimi kinanifikirisha, au kinanifanya siko na amani, ni watu ambao wanataka kuamini kwamba ukiwa mwanamke unatakiwa uwe mfeminia au unatakiwa uzijue haki za wanawake.
Matokeo yake tunaambiwa kwamba tunapopigania haki za wanawake unaambiwa umeshampata kiongozi mwanamke mbona mwanamke mwenzenu, mbona yaani hatuoni kwamba huyu ndio ni mwanamke.
Kwa hiyo, tunapata upinzani kutoka pande zote. Bahati mbaya ni kwamba ukipata upinzani kutoka kwa wanaume unauwanja mkubwa wa kupambana nao. Ukipata upinzani kutoka kwa wanawake, hata mimi binafsi najitahidi kwa uangalifu mkubwa kwa sababu sitaki ionekane kwamba wanawake wanagombana.
Kwa sababu, kuna hiyo dhana kwamba sisi tukipishana maneno ni ile wanawake hampendani lakini wanaume wakipishana unaonekan na majadiliano.
The Chanzo: Unadhani kwa mtazamo wako na kwa muktadha wa Kitanzania ukinzani ambao nyinyi mafeminia mnaupata unasababishwa na kitu gani?
Mwanahamisi Singano: Mfumo dume, mzizi mkubwa ni mfumo dume kwa sababu …
The Chanzo: Mfumo dume lakini ni dhana ya dhahania sana.
Mwanahamisi Singano: Yaani ni mfumo dume ambao umejikita kwenye ama dini zetu, kwenye mila zetu, kwenye miundo na sera za Serikali zetu, kwenye sheria. Kwa hiyo, ni mfumo dume kwa sababu ulijiingiza ukajikita kila mahali.
Kwa hiyo, utapambana na ukinzani kutoka kwa wapiga debe wa mfumo dume wa dini, kwa mfano, utapambana na ukinzani kutoka kwenye mila, utaambiwa siyo mila zetu, wewe mtoto wa kike hutakiwi kufanya hiki.
Kwa hiyo, unajikuta kwenye kila pembe, yaani akitoka shangazi anakwambia kwamba wewe hizi siyo mila zetu, hatukukuzaa hatujakulea hivyo. Utakuja kwa baba kutuambia dini haitaki hiki. Utakuja Serikali tutakapo kwambia nafasi yako ni hii. Kwa hiyo, kwote tunabanwa na ni ngumu kwa sababu kuvunja sasa hiyo kutoboa kwenye hizo zote inataka nguvu za ziada.
The Chanzo: Vipi kuhusu hofu? Kwa mfano, vile mafeminia mnaonekana ni kwamba hampiganii tu haki za wanawake kama ulivyozungumza. Umezungumza kwamba kwamba mafeminia ajenda yenu ni kutengeneza dunia ya usawa. Dunia ambayo inatoa haki na fursa sawa kwa kila mtu na hiyo inaenda mpaka haki za watu ambao wanashabikia mapenzi ya jinsia moja na vitu vingine ambavyo kwa kwetu sisi kama Tanzania tunaviona ni vitu ambavyo ni hovyo, vitu ambavyo ni vya ajabu. Hudhani hiyo pengine inachochea kwa kiasi fulani? Kwanza labda pengine nikuulize ni kweli kwamba ukiwa feminia ni lazima ushiriki mapambano ya makundi kama haya mengine, na hudhani kwamba hiyo inaweza ikawa pengine inachangia kutokupata mapokezi yale ambayo mnayategemea kutoka kwenye jamii?
Mwanahamisi Singano: Kwanza ni muhimu sana nadhani kama mafeminia sisi kama nilivyosema tunaangalia vitu kutoka kwenye mizizi kwa sababu tunataka kutengeneza dunia yenye usawa, yaani kwenye chata kuu ya mafeminia wa Kiafrika imesema kabisa kwamba sisi ni mafeminia iwe hakuna kama, iwe lakini na hata hivyo sisi ni mafeminia mwisho.
Sasa huwezi ukawa ni mfeminia ukasema mimi ni mfeminia lakini haki za walemavu hapana. Mimi ni mfeminia lakini haki za wanaonyang’anywa ardhi yao hapana. Mimi ni mfeminia wa hiki tu, hapo wewe sio mfeminia.
Kwa hiyo, kuwa mfeminia ni kujua kwamba majukumu yetu yanaingiliana. Mimi kama Mwanahamisi nimepewa nafasi ya upendeleo kwa kila namna. Nimesoma, nimekaa darasani, nimesafiri nimeangalia dunia. Kwa hiyo, hata ukinichukua mimi Mwanahamisi na ukandamizaji ambao yule dada nimemuacha Usagarabangi niliyemaliza naye darasa la saba kuna tofauti.
Kwa hiyo, nikujua kwamba huo muingiliano pia upo katika jinsi sisi tunavyoona au kwa jinsi tunavyosimama kutoka kwenye mhimili mkuu wa madaraka ni tofauti. Kwa hiyo, kuna watu ambao wanakaribia pale katikati, yaani kwenye ule mfumo dume kuna watu wameshirikishwa hapo wapo na kuna kina sisi wengine tunaokuja kuja lakini kuna wale wengine ambao nguvu ya madaraka ipo hapa na wao wenyewe wapo kule kabisa.
Kwa hiyo, hali yao ni tofauti kabisa na ndiyo maana tunasema kwamba lazima ukiwa mfeminia lazima uweke hiyo lenzi ya jinsi gani hizo hali zinakutana kwa kuangalia rangi, jinsia, tabaka, maeneo, uwezo, ujinsia na hivyo vitu vingine kwa sababu hivyo vyote vinaamua wewe upo wapi kwenye jamii.
Kwa hiyo, kwangu mimi jibu rahisi ni kwamba huwezi ukawa mfeminia ukawa unachagua. Bila shaka kila mtu anaweza akakipa kipaumbele kwamba mimi nitafanyia eneo hili lakini natambua kwamba ukweli wa watu wengine.
Kwa hiyo, mimi ninaweza nikasema mimi najikita kupigania, kwa mfano, mazingira, unakijita kupigania haki za kusoma lakini haimaanishi kwamba sijui kwamba hata hapa kwenye elimu watu Wamaasai uwezo wao kupata elimu unakuwa tofauti na watu wengine. Kwa hiyo, hiyo tunasema inatusaidia kwenda kwenye mzizi wa jambo.
Lakini kwa swali lako la hofu, hofu ipo sana, sana, sana, sana. Kwa sababu amini kwamba hakuna mfumo ambao una usanifi kwenye kutoa zawadi na adhabu kama mfumo dume. Mfumo dume ni mfumo ambao upo na ufanisi kwa asilimia mia moja, ukiubeba unakubeba, ukiutikisa utakuadhibu.
Ndiyo maana leo kesi zinazosema kwamba mafeminia hawaolewi ni adhabu za mfumo dume na hata, kwa mfano, unaona wadada sasa hivi kumeingia kundi kubwa la wamama ambao wanasema unaweza kuwa na mafanikio lakini ukampigia mmeo magoti.
Hao wanainuliwa, yaani unaona ni jinsi gani wanakua kwa sababu mfumo dume unawabeba, unawashikilia. Kwa hiyo, hizo hofu zipo kwa sababu tu vitisho vya kufa ambavyo tunaviona sana kwa nchi za wenzetu na hata hapa watu ambao wanapigania usawa wanapoteza maisha yao, wengine wananyanyaswa, wanateswa kesi zipo nyingi dunia nzima.
Lakini pia ukiachia hizo kesi za kutengwa zilizokithiri, kesi za kushushwa thamani, kesi za kuumizwa hisia zako, yaani watu hawakuoni wewe kama mtu, watu wanakuona wewe ni mfeminia ni kitu tu ambacho anaweza akakipiga mateke, akakitukana. Kuna siku unaingia tu Twitter mtu anakutukana matusi yaani wewe huwezi wewe unayeyasoma huwezi kusoma kwa sauti, unajiuliza kwa nini hili limetokea?
The Chanzo: Je, hali hiyo inakuumiza?
Mwanahamisi Singano: Ndiyo inaniumiza. Kwa sababu mwisho wa siku sisi ni binadamu. Unajua kama nilivyosema mwanzo kwamba linapokuja kovu moja unajua kabisa kwamba nafanya kitu sahihi, unasonga mbele maisha yanaendelea. Kwa sababu kila siku mimi naamini wanasema kwamba mimi nipo radhi haya maumivu niyapitie mimi asije akayapitia binti yangu.
Kwa hiyo, afadhali niendelee kupata hayo maumivu, matusi ili ifike mahali watu wajue kwamba hatukupoteza muda. Kizazi kinachokuja kiwe kizazi ambacho wanaweza kujieleza kuwa mimi ni mfeminia halafu kila mtu akaona ni sawa.
The Chanzo: Je, unadhani ni kwa kiasi gani ufeminia unakubalika kwenye dini kama za za Kikristo na Kiislamu. Naamanisha inawezekana kwa mfano kwangu mimi, au mtu yeyote ambaye ni Muislamu au Mkristo, na akawa mfeminia? Kwa sababu kama nilivyokusikiliza kwa kiasi fulani zinaweza zikakinzana, namaanisha ufeminia na imani za dini zinaweza zikakinzana. Kwa mfano, Uislamu kwenye suala la mirathi mwanaume anatakiwa apewe hiki mwanamke anatakiwa apewe hiki. Je, unafikiri ni vigumu kiasi gani kwa hivi vitu viwili, ufeminia na masuala ya dini, kukaa pamoja.
Mwanahamisi Singano: Dini zote zimejengeka kwenye mfumo dume, hakuna ubishi kwenye hilo. Kwa hiyo, dini zetu zimetengeneza jamii yenye huu mfumo dume ambayo tunayo na kwa hiyo kujibu swali lako ni vigumu kwa ufeminia na dini kukaa pamoja.
Lakini binafsi sasa nazungumza kwa sababu bado najitambulisha kama Muislamu kwa sababu mimi naamini dini ni kitambulisho na najua kuna watu wengi kama mimi ambao wanaamini kwenye huo utambulisho na ni kitu kimoja kusema kwamba tutawaacha wenyewe.
Kwa hiyo, kuna vitu ambavyo labda kwenye dini unaweza ukaviona kwamba hivi vilikuwa tofauti tofauti. Nikutolee mfano. Mimi ni kama Muislamu ukiangalia habari labda ya Bi Khadija unaweza kutengeneza kesi kwamba Bi Khadija alikuwa mfeminia, yaani vile vitu ambavyo alikuwa anavifanya yeye enzi hizo ni mwanamke alikuwa anamiliki mamali, yeye mwenyewe ndio alichagua nani amuoe na vitu vingine kama hivyo ambavyo hata katika jamii zetu za sasa ni vigumu, hata katika Uislamu si kitu ambacho kinapewa sifa japokuwa kilitokea huko zamani.
Na mimi nawaambia, kwa mfano, kama kaka zangu nasema sasa wewe mwanaume uoe wanawake wanne, kila mara huwa natania kwamba unaweza kufanya hivyo kama mkewe sio yeye anayekulisha kwa sababu kwenye maisha ya Mtume [Muhammad] kipindi chote alichokuwa na Bi Khadija hakuwahi kuoa. Kwa hiyo, alijua kwamba kaoa mwanamke mwenye kipato alitulia akawa na ndoa moja.
Kwa hiyo, kwa nini wewe unataka kuoa mwanamke mwenye kipato halafu umuolee wake wengine hata nyendo za Mtume hazikuwa hivyo. Kwa hiyo, unaweza kukuta mambo kama hayo hivyo dini zetu zote za Kiislamu, za Kikristo ni dini za mfumo dume.
Na zinatumika sana kuendeleza mfumo dume na moja ya kitu ambacho dini inakuwa ngumu sana kwa sababu dini zote zinafundisha kitu kimoja: usihoji. Kwa hiyo, hata hizi za kukaa na watu kujiuliza maswali kwamba mahusiano ya Khadija na mtume yalikuwaje na tunajifunza nini kutoka kwao inakuwa ngumu kwa sababu tayari tumeshaambiwa tusiulize.
The Chanzo: Kutokana na ukweli kwamba Tanzania ni jamii ya kidini haswa, unadhani hiyo inaweza ikawa inachangia kwenye ile hofu ya kupigania ufeminia, kwamba ni sehemu inayowajengea watu hofu kuweza kukubali kile ambacho mnakipigania ninyi?
Mwanahamisi Singano: Ufeminia unapingwa kila sehemu ya dunia, haukuwa na mapokeo rahisi duniani kote, iwe ni kwenye jamii za Kikristo au huko Magharibi [ufeminia] haukuingia kwa rahisi duniani kote.
Na kwa Tanzania dini haipelekei huo ugumu lakini ni moja pia kitu kingine ambacho kinapelekea kuwa vigumu kwa jamii zetu za huku kwa sababu wanaamini kwamba [ufeminia] ni utamaduni wa nchi za nje, ni ajenda ya nchi za nje na kuna kazi kubwa ambayo sisi tunatakiwa tufanye kuwaambia watu kuwa sio ajenda za nchi za nje.
Bibi zetu walishanza kupigania usawa kabla hawajajua kwamba kuna nchi inaitwa Marekani, kabla hawajaanza kuingiliana na hao watu wa huko, kabla hawajajua kwamba kuna hiki.
Ukisoma historia nyuma kabla ya ukoloni kuna wanawake ambao tayari walikuwa wenyewe wanafanya kazi wenyewe, ilikuwa ni dunia ya kushirikiana katika majukumu, kuna kuheshimiana, kuna fursa kwa kila mtu, huu unyanyasaji ulikuwa haupo.
Mimi nimesoma kitabu cha The Africans: Triple Heritage cha Ali Mazrui na filamu yake ameeleza kwamba jamii za kabla ya ujio wa ukoloni hapa Afrika zilikuwa ni jamii ambazo wanawake ndiyo wanaenda kufanya biashara, na jeshi la kwanza la wanawake tu lilikuwa Afrika.
Kwa hiyo, tumechukua kipindi cha ukoloni tukakifanya ndio kigezo cha maisha ya Mwafrika. Baada ya hapo kila kitu tunakiona kwamba ni muhimu na hiyo imefanywa makusudi kwenye kuvunja ule ukombozi uliokuwepo Afrika kabla kuona kwamba sisi tulikuwa hatuna ukombozi.
Kwa hiyo, moja ya kazi kubwa ambayo sisi kama mafeminia ambao si wengi tunaoifanya ni kuleta kwamba hili siyo jambo geni, lilitoka kwetu na siyo sawa hata sisi kujipambanua kwamba tumepokea ufeminia. Inabidi kama Waafrika tuone kwamba haya mapambano yalianza kwetu na mimi mwenyewe nimesimama hapa kwa sababu bibi zangu walipambana kunifanyia mimi leo niwe hapa.
The Chanzo: Tukibaki hapo hapo kwenye suala la ukinzani, hudhani pia kwamba baadhi ya watu wanasukumwa kupingana na kile ambacho nyinyi mnakipigania kwa sababu tu ya kutokuwa na imani kwamba hicho unachokipigania kinawezekana au hata kama kinawezekana sio kwa muda huu wa sasa kwamba usawa wa wanawake na wanaume ni hauwezekani? Kwa sababu yeye anaona haiwezekani badala ya kukaa kimya anaona bora apingane na hilo. Unadhani kwamba hii niliyoitoa ni hoja kwenye ukinzani ambao mnaupata, kwamba hivi ndivyo dunia ilivyo?
Mwanahamisi Singano: Inasaidia lakini tumeona mabadiliko, tumeona mageuzi yanayofanyika, kwa mfano, miaka mia moja iliyopita ni mageuzi ambayo ni makubwa sana. Miaka mia moja iliyopita wanawake walikuwa hawapigi kura, haki ya kufanya kazi kulikuwa hakuna, haki ya kuchaguliwa ilikuwa hakuna. Vitu vingi vimetokea.
Kwa hiyo, kwangu mimi bila shaka watu wanasema haiwezekani lakini kwa miaka kumi iliyopita hatukutegemea wote Tanzania ingekuwa na Rais wa kwanza mwanamke lakini vinatokea. Kwa hiyo, hatua zote hizi zinatufanya sisi zinatupa nguvu kwamba inawezekana kufanyika.
Na kwangu mimi haijalishi kama itafanyika kwenye kizazi hiki au kijacho, ikiwa mimi natamani mimi kizazi chetu kikiondoka haki tulizozipata kizazi kinachokuja kiwe na haki zaidi ya kizazi chetu, kiwe na machaguo mazuri, kiwe na maisha mazuri kuliko sisi.
Kwa hiyo, tunaweka msingi kama sisi tuliorithishwa tulisimama kwenye mabega ya waliotoka nyuma yetu na sisi tufanye kazi nzuri ya kusimamisha mabega yetu kuwa imara ili wanaokuja na wenyewe wapande wafike mahali.
Kwa hiyo, hoja ya kwamba kama hatujakamilisha ni moja ya uchoyo, kama mimi sitaki kuona matunda yake basi sikifanyi ni hoja yenye choyo kikubwa.
The Chanzo: Kwa sababu umemtaja Rais Samia Suluhu Hassan, unadhani ujio wake kama Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania unarahisisha katika hali yoyote kazi zenu nyinyi kama mafeminia? Unadhani kwamba ni maendeleo chanya kwenu nyinyi kama mafeminia?
Mwanahamisi Singano: Mimi nilisema, na ninaamini, kwamba Urais wa Samia utakuwa mgumu sana kwa mafeminia kwa sababu kwanza tunasherekea kuwa na mwanamke kama kiongozi mkuu wa nchi.
Hilo hatuwezi kulipuuza, ni jambo kubwa. Kuna mtu watoto wanakua wanamuona mwanamke akiwa kiongozi mkuu wa nchi ambayo siyo dhana ambayo mimi nilikuwa nimekua nayo. Mimi nilivyokuwa mdogo ukiniambia nichore Rais nitamchora mwanaume mwenye suti.
Hiyo ndiyo ilikuwa picha pekee ambayo nilikuwa nayo kichwani kwangu kwa sababu hicho ndicho kitu pekee nilichokuwa nakiona. Kwa hiyo, ameleta picha mbadala kwa Watanzania siyo tu mtoto wa kike hata watoto wa kiume hata kila mtu anajua kwamba inawezekana.
Kwa hiyo, kwa picha hiyo mbadala ni muhimu sana katika uwakilishwaji wa mwanamke wa Kizanzibar, Muislamu anavaa hijabu, picha zote hizo ambazo kwa muda mrefu tulikuwa tunajua kwamba wanawake wa aina hiyo ni wakukaa tu ndani, wakuhudumia tu waume zao wa kufanya hivi.
Kwa hiyo, ni mabadiliko makubwa kwenye jinsi ya tunazitengenezaje jamii zetu kwa sababu tuna huo ubaguzi jamii ile, kabila lile ndio wahusika, kabila lile ni hivi. Kwa hiyo, inaondoa huo ubaguzi kwa ukubwa.
Lakini changamoto inakuja kwamba kuwa mwanamke hakukufanyi uwe mfeminia. Kuwa mfeminia ni safari ambayo unahitaji kuichukua wewe binafsi, unatakiwa kujitolea na wewe mwenyewe ujitolee kujifunza kwa sababu siyo vitu ambavyo vinakuja kwa sababu nimezaliwa na mwili wa mwanamke hivyo moja kwa moja mimi nitakuwa najua kwamba ni kwa namna gani ubaguzi upo, naweza kukwambia ni jinsi gani kuna mambo nayapitia lakini ni kwa sababu nina uelewa na ninajua.
Kwa hiyo, kuwa mwanamke haimfanyi yeye kuwa mfeminia. Hicho ni kitu cha kwanza. Lakini pia atakayoyafanya kwenye kwenye uongozi ni yeye peke yake ni mfumo dume, kuna matarajio mengi kwake lakini anaweza kufanya kile ambacho yeye anaweza. Sasa ugumu unakuja kwamba katika hatua gani kama mafeminia tunatakiwa tusimame tuseme kile unachokifanya sio sahihi bila kuonekana kwamba tuna chuki. Na ni katika hatua gani tuseme kwamba kuna kufanya vizuri bila kuonekana kwamba tuna huruma.
The Chanzo: Mimi nilidhani kwamba pengine uliposema kwamba Urais wa Samia utakuwa mgumu kwa mafeminia nilijua, nilidhani, unakwenda kuongea kwamba atakachokifanya akakosea yaani makosa yake yatahusishwa na uwanauke wake?
Mwanahamisi Singano: Ndiyo, lakini hiyo ni hoja kwa watu wengi ambao siyo mafeminia. Lakini kwangu mimi siyo hoja kwa sababu hakuna makosa yanayofanyika kwa wanaume yakahusishwa na wanaume wote.
Kwa hiyo, si hoja ambayo hata napenda kuirudia kuisema kwa sababu tunatengeneza hiyo dhana kwamba akifanya yeye itahusishwa na [wanawake] wote kwa sababu kwangu mimi katika hatua hiyo tusingekuwa na Rais.
Kwa sababu, marais wote waliopita Tanzania wamefanya makosa mengi sana lakini haijawahi kuwa kwamba sababu tumeongozwa na Rais mwanaume amefanya makosa wanaume wote hawafai tena kuongoza Tanzania.
The Chanzo: Kuna njia yoyote ambayo Samia anaweza kurahisisha kazi yako kama mfeminia?
Mwanahamisi Singano: Ndiyo.
The Chanzo: Kivipi?
Mwanahamisi Singano: Kwanza, yeye kuamini yeye mwenyewe kwamba ana mengi ya kujifunza. Hasa kwenye harakati za wanawake. Pili, kujua kwamba nani wanaweza wakamsaidia kwenye kufanya hizi kazi za wanawake kwa sababu si tu kila mwanamke, yaani sisi pia na ufeminia wangu kuna vitu nimelishwa tangu zamani, yaani mpaka nikifanye ndio najua hapa nimejihusisha na mfumo dume.
Kwa sababu vitu hivyo vimewekwa kwenye makuzi yetu, kwenye mitazamo yetu na hivyo vitu vingine. Sasa ni yeye kujua kwamba nahitaji kuwa na watu sahihi kwa ajili ya kazi, yaani haitoshi tu kwamba hawa nimewapa Wizara ya Wanawake na Watoto lakini pia hiyo Wizara inafanya nini, wanaleta maendeleo?
Kuna watu ambao ni manguli kwa sababu Tanzania hatuna uhaba wa manguli wa mafeminia, unajua wakati ufeminia unakuja Afrika ulianzia Tanzania. Kwa hiyo, hatuna uhaba huo wa watu ambao wanaweza wakasema kabisa kwamba hii ni njia ambayo tunahitaji kwenda nayo lakini bahati mbaya sana tunakwenda kwa watetezi wa mauala ya kijinsia ambao wao wanasema tu kwamba tatizo hapa ni madarasa tujenge madarasa.
The Chanzo: Safi. Je, unadhani kuna uamuzi au hatua yoyote ya kisera ambayo ungependa Rais Samia aifanyie kazi ambao unaamini utasaidia kupeleka mbele harakati za ufeminia Tanzania?
Mwanahamisi Singano: Kwa mfano, kuna nchi nyingi duniani ambazo wanajitabulisha wenyewe kama Serikali za kifeminia. Kwa mfano, Canada, Sweden, Mexico na sasa hivi kuna harakati za kufanya kuwe na sera za kigeni za ufeminia.
Kwa hiyo, ufeminia siyo tena neno ambalo linatakiwa liwe na ukakasi kiasi hicho na hata haimpungizii Samia chochote kwamba Tanzania ni nchi yenye mfumo dume ukilinganisha na Canada lakini haimpungizii yeye chochote kusema kwamba tunataka mabadiliko ya kweli na hili litakuja kama tutaukumbatia ufeminia na kama tutafanya kazi na mafeminia.
Kwa sababu hao ndiyo watamsaidia kwenda kwenye mzizi wa jambo zaidi ya hapo tutakuwa tu tunapaka upepo rangi.
The Chanzo: Labda tukirudi kwenye ule mfumo dume. Labda kwa kutumia lugha ambayo mtoto wa miaka minne anaweza kuielewa, unaweza ukanielezea mfumo dume ni nini haswa?
Mwanahamisi Singano: Mfumo dume ni mfumo ambao umetengenezwa kuwapendelea jinsia moja katika jamii, kwa maana kwamba ni mfumo ambao umefanya mwanaume awe ndiyo anabeba upendeleo wote huo ndio tunaouita mfumo dume.
Sasa huo mfumo dume unakuwa unapewa nguvu na mifumo mingi sana bahati mbaya kwa mfano mifumo yetu ya kiuchumi ni mifumo dume pia. Kwa hiyo, unakuta tukiangalia sisi kwenye ufeminia, ukiangalia ule uongozi wa upendeleo unakuta kule juu kabisa ni wanaume weupe, kwa mfano, kwa sababu tuna huo muingilianao kwamba si tu mwanaume lakini ni nani mwenye nguvu zaidi kati ya hao wanaume kwa hiyo utamkuta ni mwanaume mweupe wa bepari.
Kwa hiyo, tunaweza kutumia hiyo hali kusema kabisa nguvu ipo wapi, nani anayemiliki madaraka na ni kwa namna gani hayo madaraka yanagawanywa na ni muhimu pia kushika kwamba watu wanaposema kwenye mfumo dume tunachokipigania sana ni kwamba sio tu mtu ni nguvu ya madaraka.
Lakini kuna mahusiano kati ya nguvu ya madaraka na kutokuwa na nguvu ya madaraka na haya mahusiano ni mahusiano ya kinyonyaji na hilo ndio linakuwa tatizo kwamba ili huyu aendelee kuwepo hapa lazima amnyonye huyu.
Sasa tunataka kukata ile mirija ya unyonyaji ili huyu asinyonywe kwa sababu yule awepo pale. Hiyo ndiyo dhana ya mfumo dume. Jamii zetu zimejengwa kwamba sisi wanawake tunanyonywa ili wanaume wawe pale. Nitakutolea mfano.
Tumekaa kwenye jamii ambayo tulimuondolea mwanaume majukumu yote ya kifamilia, mwanaume alikuwa akitoka asubuhi anakuta ameandaliwa chai, nguo zake zimeandaliwa, anakula, yeye ataacha tu fedha atakwenda kufanya kazi. Haulizwi huku nyumbani hali, hajui watoto wameamka, wameogeshwa, nyumba imesafishwa, nyumba sijui.
Kila kitu kinafanywa na akirudi mwanamke anakuwa amepewa mafunzo kwamba akirudi yule mume ametoka kwenye kazi unamfariji. Kwa hiyo, akirudi atakuta chakula kizuri, atakuta hiki, atakuta hiki kila kitu mapenzi na mahaba na kila kitu.
Kwa hiyo, mafanikio ya mwanaume kule nje kwenda kutafuta ilitengenezewa msingi kwamba kuna mtu huku ndani ambaye amechukua majukumu mengine yote ili yeye azingatie kwenye masuala mengine.
Ndiyo maana hata kwenye jamii zetu ilikuwa labda sijui kuna harusi, sijui ya ndugu kwa mkweo, yaani wanaume hawana hilo deni kwamba lazima niende ukweni kwenye harusi, lazima sijui niende nini. Lakini kwa mwanamke kulikuwa kuna huo mzigo kwamba lazima nikamwakilishe mume wangu, mjomba sijui anaumwa, mke ndio ataenda kuwakilisha, atasema kaenda kazini yeye ndio ataenda kumwakilisha kumwangalia mgonjwa hospitali ili tumpe ile nafasi mwanaume aende akatafute riziki.
Kwa hiyo, yale majukumu yalibebwa na jinsia moja, sasa imefika mahala yale majukumu hayaonekani tu kwamba yalikuwa ni mgawanyo wa kazi, nafanya yote haya ili kwamba uende ukafanye hicho unachokifanya kwa uzuri, imeonekana ni jambo la kitamaduni.
Sasa hivi mimi nikitoka kwenda kufanya kazi hakuna mtu anayeyachukua majukumu yangu ili nikafanye kile kitu pale basi, natakiwa nifanye kila kitu jumulisha kwenda kutafuta riziki na ninapohoji kwamba hii kutafuta riziki wewe mwenzangu ulifika pale kwa sababu tulibeba haya majukumu unaonekana kwamba hujaweza kuleta kinachotakiwa.
Sasa unamkuta mwanamke ambaye anamajukumu yote ambayo anafanya na mwanaume ambaye hana jukumu lolote na anakwenda kushindana ni kitu ambacho hakiwezekani.
Sasa inapofika hapo na ninakuja kwenye lile suala uliniuliza mwanzo kwamba tunaonekana hatuolewi au ndoa hazidumu, kwa sababu inafika mahali inakuwa haiwezekani kama binadamu kufanya yote. Kwa hiyo, inabidi uchague kwamba nibaki hapa au niondoke.
Kwa hiyo, dhana ya kwamba wanawake wasomi hawaoleki au hawakai kwenye ndoa wao wanawake ndio tatizo, nadhani turudi kwenye mfumo wetu. Mimi nahisi jamii haijatengeneza mfumo mpya wa kuishi na wanawake ambao wanafanya kazi kwa sababu kila mtu anamasaa 24, kila mtu anamwili huo huo, kiwango cha nguvu ni sawa huwezi kufanya kila kitu.
The Chanzo: Turudi kwenye zile hoja umesema zinasukuma mfumo dume, ulitaja rangi na ulitaja mfumo wa kiuchumi. Sina uhakika kama rangi ya watu zinahusika kwa kiwango kikubwa kwa muktadha wetu wa Tanzania. Lakini ni kwa kiwango gani unadhani mfumo wetu wa kiuchumi kwa jinsi tulivyouunda mfumo wetu wa kiuchumi, mfumo wetu wa kijamii, unasukuma huu mfumo dume na pengine mfumo wetu wa kiuchumi sisi ni upi labda?
Mwanahamisi Singano: Nafikiri mfumo wetu wa kiuchumi nahisi ukiwapata wataalamu wa siasa-uchumi watakwambia zaidi. Lakini nadhani ni kwa kiasi kikubwa tupo na ubepari japo kuwa mioyoni mwetu tunahisia bado za kuwa wajamaa lakini tunaona Mheshimiwa Samia Suluhu amejipambanua kwamba yeye anavutiwa na wawekezaji kwa hiyo tunakwenda kwenye jamii ya ubepari.
Na bahati mbaya kwenye ubepari ni kwamba inabinafishsa na kufanya uone ni wewe peke yako ndio umefanya, ni juhudi zako ni kila kitu chamgu yaani kila kitu kinakuwa binafsi, maarifa yanakuwa ya kwako, kila kitu kinakuwa cha kwako hata mafanikio yanakuwa ya kwako.
Na tunaona leo sasa hivi ukiangalia mandhari yetu kuna neno kulia, kushoto na katikati kwa wanawake, kwa nini ni kwa sababu tunajihisi kwamba ni wewe na wewe peke yenu huwezi kusikia habari za nani kaongoza kujenga huu msingi, ni kwa namna gani tunafanya kwa ajili ya vizazi vijavyo, hakuna tena kufanya kazi kwa kwa pamoja ni mimi peke yangu.
Matokeo yake hiyo inatengeneza hali kubwa yakutokuwa na usawa kati ya walionacho na wasionacho. Kwa hiyo, hali ya kutokuwa na usawa inakuwa kubwa kwenye jamii yetu, kiwango cha kutokuwa na usawa kwenye harakati hasa za wanawake kinakuwa kikubwa wanawake wengi wanakuwa kuchagua wakishapata mafanikio wakishaanza kuona ndoto zao.
Wanawake wengi wapo tayari kufanya kazi kwa ajili ya kuukumbatia mfumo dume ili wafikie hiyo ndoto, huwa tunaambiana kwenye makundi wewe mtumikie shetani upate ujira wako. Kwa hiyo, tunawatengenezea mabepari vibarua wa kulipwa ujira kidogo, tunautengenezea mfumo dume ukuu wake na mwisho tunarudi pale pale kuwa ni mfumo ambao unakulipa.
Kwa hiyo, kwa wale ambao wameukumbatia wamepata biashara nzuri na maisha mazuri, wamepata mume ambaye wanamsujudia na baada ya hapo wanakuwa ndiyo sura ya wanawake waliofanikiwa katika karne hii ya 21 wanatakiwa aweje na wengine wote tunakuwa tunabaki kutamani na mwisho wote tunaingia katika mfumo huo.
The Chanzo: Hiyo ni safi sana, umeelezea vizuri. Tuhame kwenye ufeminia tuje kwenye suala jingine kabla hatuja malizia. Wewe ni moja kati ya watu ambao kupitia harakati zenu mnaonesha mwingiliano uliopo katika ya mapambano ya kupigania haki za wanawake, lakini kusema ukweli siyo kusema haki za wanawake, ni usawa wa kijinsia, na mapambano ya kupambana na mabadiliko ya tabia za nchi. Labda kwa ufupi unaweza kutueleza ni kwa namna gani haya mapambano mawili yanaingiliana?
Mwanahamisi Singano: Na kabla sijaelezea hilo, nirudi hapo kwenye hoja ambayo umeisema vizuri sana kwamba tunapigania usawa wa kijinsia kwa sababu japo kuwa watu wengi wanaamini bila shaka tunapigania sana kwa sababu wao ndio wanaonyanyaswa lakini mfumo dume hauwasaidii pia wanaume.
Kaka zetu sasa hivi wapo kwenye mkanganyiko kwa sababu viwango vilivyowekwa na mfumo dume vinataka wanaume wawe wamefanikiwa kuliko mwanamke, unatakiwa uwe na nguvu, hautakiwi kuhisi maumivu, unatakiwa ufanikiwe kupata hiki, yaani kuna mambo mengi ambayo unatakiwa kuyapata.
Lakini mtu anakuumiza unaumia, lakini unaona kabisa kwamba mtu anafiwa lakini unaambiwa kwamba usilie ndiyo uanaume. Kama hivyo ni kwa namna gani tunaua hisia za wanaume tunawafanya hivyo kwa sababu dunia tuliyokuwa tunaishi sasa hivi kila mtu ana riziki yake, kila mtu anapambana.
Hivyo unakuja unanipenda labda mimi Mishy lakini unajua kabisa kwa kiwango cha mfumo dume mimi inatakiwa niwe na kipato zaidi ya Mishy, unawezaje kupata kipato zaidi yangu kwa mfano hujui mapambano yangu, hujui nafanya nini.
Kwa hiyo, unajikuta kwamba kigezo mimi nilichokiweka labda wewe hukifikii kitu ambacho kinakuumiza wewe. Badala ya kuwaya kufurahia uwepo wangu inakuumiza kwa sababu unatakiwa kuwa vizuri na ndio hapo sasa tunakuja kwenye ukatili [dhidi ya wanawake] ili mwanamke ajione mdogo na wewe uwe mkubwa kwa sababu ukimuachia atakupita na baada ya hapo itakuwa haina maana.
Kwa hiyo, sisi tunaamini mfumo dume hauwasaidii pia wanaume. Kaka zetu wengi wanalalamika kwamba lazima utume ya kutolea sijui, nani kasema kwamba unatakiwa ufanye hivyo, nani kasema?
Kwenye dini walikuwa wanasema kwamba katika dini tumeumbiwa lazima mwanaume ndio atunze familia lakini ukiangalia kwenye dini Bi Khadija siyo ndiyo alikuwa na hela kwa miaka yote waliyoishi? Yeye ndio alikuwa anatoa.
Kwa hiyo, tunatoa wapi hilo suala, labda tungekuwa tunasema kwamba inategemeana na nani anakipato kikubwa. Kwa hiyo, tunafanya unawasukuma wanaume kwamba unapaswa kufanya hiki na kile kitu ambacho kinawaumiza wanawake na jamii nzima. Kwa hiyo, sisi tunapigania usawa wa kusema kila mtu anahaki ya kuwa sawa kwenye hii dunia.
Na ukirudi kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi, mabadiliko ya tabia ya nchi kwa imani yangu, na kwa imani ya mafeminia wengi, yanaoana sana, sana na mfumo dume lakini pia mfumo wa uchumi wetu wa kibepari.
Kwa nini? Kwa sababu ubepari na mfumo dume zote zimejingwa kwenye msingi wa unyonyaji, kunyonya nguvu kazi kwa ajili ya manufaa ya wachache. Kwa hiyo, tumefikia kwenye dunia ambapo mfumo wa kibepari wa watu weupe unainyonya dunia, umetengenezwa janga.
Na kwa sababu umetengeneza janga wale ambao hawana nguvu, ambao wengi ni wanawake, kwa sababu hawa ndio wanakuwa wananyonywa na kwenye mfumo dume hawa ndiyo wanaonyonywa na mfumo wa ubepari ndiyo unaobeba mzigo wa yale mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa hiyo, kwetu sisi hatuwezi kuzungumzia mabadiliko ya tabia ya nchi kabla hatujabadilisha mfumo wetu, hatuja ukataa ubepari, hatuja ondoa mfumo dume, tunatakiwa tufanye hivi vyote.
The Chanzo: Ukiondoa mfumo wetu wa kiuchumi uliopo sasa hivi mnalenga kuuweka mfumo upi?
Mwanahamisi Singano: Mfumo ambao ni sawa kwa sababu moja kati ya tatizo kubwa kwenye hili dunia tunaamini tu kwamba mifumo ndio lazima tuitumie ile ile kwamba lazima kuwe na ukabaila, sijui kuwe na ujamaa na ubepari.
Lakini kwa nini hatutengenezi mfumo wa hekima ya kibinadamu ambao utakuwa na haki sawa katika karne hii ya 21? Swali mara nyingi linapokuja ni kwamba kama ubepari haufai turudi tena kwenye ujamaa, nani kasema turudi tena kwenye ujamaa?
Kwa sababu hiyo ni kusema kwamba kizazi hiki hatuna uwezo wa kutengeneza kitu kipya kwa sababu mifumo tuliyonayo yote ilitengenezewa. Kwa hiyo, sisi tunasema tunahitaji kubadilisha mfumo, tunahitaji kutengeneza mfumo mbadala wa kiuchumi, mfumo mbadala wa kijamii ambao utatufanya sisi tuishi kwa maelewano na kila mmoja, lakini pia kutengeneza jamii ambayo ina usalama, inafuraha na inaishi kwa maelewano.
The Chanzo: Mishi Tanzania ni taifa linaloendelea na kama taifa lolote lile linaloendelea linachukua hatua, juhudi, ambazo zinalenga kuisukuma mbele liwe taifa ambalo limeendelea. Unadhani inawezekana kwa taifa kama Tanzania kuchukua hatua hizi na wakati huo huo bila kuyafanya mabadiliko ya tabia ya nchi yazidi kuwa makali?
Mwanahamisi Singano: Inawezekana.
The Chanzo: Kivipi?
Mwanahamisi Singano: Moja, tunashida sana kwenye kutafsiri maendeleo ni nini kwa sababu sisi tunaelezea maendeleo ni maghorofa, maendeleo ni ukataji miti, maendeleo ni kujenga nyumba kubwa. Hivyo ndivyo tunavyoelezea maendeleo kwamba haya ndio maendeleo.
Ndiyo maana sisi kwenye ufeminia hayo mabadiliko ya kimfumo tunasema lazima kwanza tubadilishe tafsiri ya maendeleo. Tufike mahali tusione maendeleo lazima yawe vitu ambavyo siyo endelevu, kwa sababu tuna vitu vingi sana ambavyo ni sehemu ya maendeleo.
Kwenye nchi zilizoendelea sasa hivi wameanza harakati za kujenga nyumba ndogo. Maana yake ni kwamba kama nyumba nakaa tu mimi peke yangu, kuna mtu mmoja kwa nini niwe na jumba la vyumba 10 ili tu niseme kwamba kwa hivi sasa nimeendelea, haina maana.
Kwa hiyo, tunaweza tukawa tunaendelea kwa sababu maendeleo ni ustawi na ndiyo maana kuna maendeleo mengi yanafanyika sasa hivi. Mimi ninaamini sasa hivi hakuna msuguano kati ya maendeleo na kukabiliana na tabia ya nchi, kama kuna kitu naamini mataifa yetu sisi yana fursa ya kubalisha njia ya maendeleo ambazo wenzetu wamefanya.
Hatutakiwi kwenda kule kwa sababu kuna njia mbadala sasa hivi ni sawa sawa Khalifa useme kwamba wote tunaona kwamba kwenye ile nyumba kuna nyoka wameingia watu tumepanga foleni, wameingia watu 10 kila anaeingia mle katoka na kilema, katoka kafa, sasa wewe unasema kwa sababu nyinyi mmetoka kule na vilema na mimi lazima niingie nipate, lazima niingie nivunjike mguu, lazima niingie nijeruhiwe. Hiyo haiwi akili sasa kwa sababu tunatakiwa kujifunza kwa waliotangulia.
Unajifunza wenzetu wameanza na hiyo mifumo yao ya maendeleo na ndiyo imetuletea haya majanga. Hatuna haja ya kusema kwamba na sisi lazima twende kule kule. Sasa, kwa mfano, Tanzania tuna shida ya nishati, nishati haijafika sehemu yote hatuna haja ya kwenda sehemu yoyote kwa sababu nishati kwa sasa ndiyo imekuwa rahisi kwa hiyo tunaweza kufanya hilo.
Nahisi nchi ipo kwenye wakati mzuri kukubaliana kwamba sisi timegundua mafuta, tumegundua tuna makaa ya mawe hivyo tuna furaha kwamba hatuhitaji kutumia hivyo hata kama mnatupatia hizo fedha, sisi twende kwenye umeme wa jua.
Kwa hiyo, mimi naamini kama kwenye nishati, nishati mbadala kwa hivi sasa zinapatikana kwa urahisi, kuweka umeme wa jua, kubuni nishati mbadala ambazo zitatengeneza ajira kwa watu wetu.
Mfano mwingine, mpaka leo watu wanakaa kwenye nyumba za nyasi, siyo? Sehemu kubwa ya Watanzania. Lakini je, tunaweza kuyatumia haya mabadiliko ya tabia ya nchi kusema kwamba tubadilishe mtazamo kwa hawa wasanifu wafanye ni aina gani ya nyumba ambazo ni ndogo ambazo tunaweza kujenga kwa watu wetu badala ya watu kuona kwamba tunahitaji kuiga kila kitu maghorofa ya New York kuyaleta Dar es Salaam kwa ajili ya kusema kwamba tumeendelea.
Kwa hiyo, hivyo ndio tunaweza kutengeneza dhana ya maendeleo lakini pia sisi tunawezaje kuacha hivi vyote vibaya maana yake tumepata bahati ya kujua kitu gani wenzetu walifanya ambacho si kizuri, kitu gani ambacho wamefanya kizuri na tunawezaje kuchukua vile vizuri tu tukavipeleka.
Kwa hiyo, kwangu mimi mjadala wa kwamba kuwa uhifadhi mazingira unakinzana na maendeleo ni mjadala ambao umeshakufa, ni mjadala sasa hivi hatuzungumzii tunazungumzia kwamba unaweza kuendelea wakati huo huo unapambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kulinda mazingira yako.
The Chanzo: Na haya mageuzi au njia mbadala ni lazima yatokee kwa wakati mmoja, ni lazima yaguse sekta zote?
Mwanahamisi Singano: Ndiyo kosa ambalo tunalifanya kwa sababu tumeyafanya mabadiliko ya tabia ya nchi, kwanza tumeyapeleka Ofisi ya Makamu wa Rais, yaani nafikiri ni wizara ambayo ilitakiwa iwe wizara yenye nguvu kwa sababu wao wanabidi watwambie madaraja tunayojenga ni endelevu, haya machaguo tunayoyafanya ya kununua hiki na miradi yote, tunatakiwa twende mbinu zote za Serikali na jamii kwamba ni kitu ambacho kinatakiwa kiwe kila kitu sio tu mradi.
Kwamba tunapanda miti hapa 20,000, tunapanda miti hapa 100,000. Miti inasaidia ndiyo kwa kiasi kikubwa, lakini miti peke yake haiwezi kubadilisha mabadiliko ya tabia ya nchi. Kuna ripoti mbili za IPPC [Intergovernmental Panel on Climate Change] zimetoka Februari na iliyotoka juzi ambayo ya Februari imezungumzia madhara ya mabadiliko ya tabia ya nchi, hakuna ambaye hajaathirika imetupa picha kwamba zaidi ya watu wa dunia tayari wanishi katika hali ya hatari, siyo?
Mvua sasa hivi zinanyesha mafuriko, athari kwenye miondombinu ni kubwa mno unajenga, tunaweka mabilioni, tunakopa yanapiga mafuriko barabara imeenda. Kwa hiyo, siyo tu watu wanaathirika hata Serikali inaathirika.
Pesa zetu zinazotolewa kwenye kodi unaweka kwenye miondombinu ambayo kesho kutwa inaondoka lakini bado huko deni tunalipa. Lakini pia IPPC wametoa ripoti ya kupunguza mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo inaonesha njia mbadala na zinazofanya kazi hivyo tuna njia nyingi za kuchagua na vitu gani vya kufanya kwa jamii yote ikituhisisha na sisi pia.
Kuona kwamba hili si suala la watu wengine ni suala la kwangu. Wote sisi tunawajibu wa kuhakikisha kwamba hii dunia tumeipokea siy dunia ambayo tumeirithi kwa sababu ukirithi ni cha kwako.
Na Kuna huo msemo kwamba sisi tumerithi dunia mimi natamani niwaambie Watanzania tutoke kwenye kurithi tuseme kwamba hii ni dunia tumeikopa kwa watoto wetu tuwarejeshee dunia yao ikiwa katika hali nzuri.
The Chanzo: Katika miaka yako yote hii ya mapambano umejifunza nini wewe binafsi?
Mwanahamisi Singano: Kwanza, imenifundisha mimi kwamba watu waliopita walikuwa ni watu walioheshimika sana kwa sababu walifanya kazi kubwa mpaka kufikia hapa. Nadhani wao wamefanya vitu vingi sana.
Kila siku nasema hata aliyegundua ndizi inaliwa kwa sababu sisi tumekuta tu kwamba chakula ni ndizi ni mihogo, alianzaje mpaka akafikia hapo akasema hiki kinafanywa hivi na hiki kinafanywa hivi kinaliwa hiki hakiliwi.
Kwa hiyo, naamini kwamba watu waliokuwa nyuma walikuwa maalumu kwa kazi yao kwenye jamii na nikijilinganisha wao na mimi yaani kila siku nafikiria kwamba hivi mimi nafanya nini ili jamii inayokuja iseme kwamba kizazi kile kilichopita kilifanya nini mpaka kikafanya haya ambayo sisi sasa hivi tunanufaika nayo.
Kwa hiyo, ninachokifanya ni kujisukuma mwenyewe, kutokuogopa kwa sababu mtu aliyegundua ndizi inaliwa alianza kwa kujaribu kujua kwamba hii inaliwa katika hatua nyingine unatakiwa ujaribu uyoga huu unasumu na huu unaliwa unatakiwa ujaribu.
The Chanzo: Unatakiwa ujitoe sadaka.
Mwanahamisi Singano: Ndiyo. Vitu ambavyo kama vingeenda tu kawaida kwamba mimi nafanya hiki kitu tu tungejikuta wote tunakula chakula cha aina moja. Kwa hiyo, inatakiwa ujaribu, ujisukume, usiogope, nafasi zipo lakini pia hatari zipo.
The Chanzo: Mishy, mimi ninakushukuru sana kwa muda wako na ni maarifa makubwa sana ambayo umejaribu kunishirikisha, bila shaka na kwa watazamaji kupitia The Chanzo. Lakini nilikuwa nataka nimalizie mazungumzo yetu na swali hili. Kule mwanzo tulizungumza kuhusiana na ukinzani ambao nyinyi kama mafeminia mnakumbana nao. Na kusema ukweli unajua Tanzania ni jamii ya mfumo dume kitu ambacho watu wote tunakubaliana na pia kwenye masula ya mabadiliko ya tabia ya nchi kuna mashaka makubwa. Lakini kuna kitu kinachonifurahisha na nahitaji kufahamu kutoka kwako kwamba ni kitu gani kinachokufanya uendelee na hizo harakati licha ya haya yote? Ni kitu gani kinachokusukuma, unajua, kuna ukinzani unajua kuna watu hawakubaliani na unachokifanya, unajua kuna watu hawaamini kwamba unachokipigania ni sahihi lakini bado unaendelea kufanya. Ni kitu gani hicho kinachokufanya uendelee kufanya hivyo unavyofanya?
Mwanahamisi Singano: Mapenzi. Mimi sifanyi harakati kutoka kwenye sehemu ya hasira. Nafanya harakati kutoka sehemu ya mapenzi. Nafanya kwa sababu nawapenda watoto wangu sana na nawatakia kilicho chema, kwa sababu naipenda jamii yangu, kwa sababu naipenda nchi yangu, kwa sababu nawapenda watu wote.
Yaani hakuna kitu ambacho kitanifanya kitakuwa kikubwa zaidi ya kwamba niache kufanya kutoka sehemu ya mapenzi. Bahati mbaya sana kile utakachokifanya watu wanafikiria unachuki lakini kama ningekuwa nafanya kwa kumkomoa mtu ningekuwa nishachoka.
Kwa hiyo, kila siku nasema kitu pekee ambacho kinanifanya niendelee kufanya ni kwa sababu nafanya kutoka sehemu ya mapenzi. Kwa sababu nataka, natamani kuona kwamba watoto wangu wanakuja kuishi kwenye dunia ambayo ni salama.
Natamani kuona dunia ambayo mimi nisimwambie [binti yangu] Shamimu usiende club kwa sababu siyo salama. Mimi sitaki [kijana wangu] Salim akue aumie aambiwe asilie, anatakiwa alie ili kutoa machungu yake nje.
Kwa hiyo, natamani kuona hivyo na siwezi nikaacha mtu mwingine afanye kwa sababu ni wajibu wangu kama mzazi, ni wajibu wangu kama Mtanzania kuishi vizuri. Kwa hiyo, tunapigana siyo kwa sababu havifanyiki lakini mnaamini tunaweza kufanya zaidi ya hapo. Kwa hiyo, nafanya hivyo kutoka kwenye sehemu ya mapenzi.
Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
One Response
Very true