Kauli ya Samia Kwamba Alitofautiana na Magufuli Kwenye Mambo Mengi Inatufundisha Nini?

Kauli hiyo inamaanisha kwamba Samia ameweza kujijenga na kuonekana kwamba amemudu kuyahodhi madaraka ndani na nje ya chama chake cha CCM

Siku chache zilizopita, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alirejea nyumbani kutoka ziara ya juma zima nchini Marekani. Katika ratiba yake nchini humo, miongoni mwa mambo mengine, ziara yake ilikuwa na lengo la kuwavutia watalii kutembelea Tanzania, akiizindua filamu iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ya Tanzania: The Royal Tour

Lakini, pamoja na hayo, kilichosababisha gumzo nchini Tanzania ni matamshi yake kwamba  alitofautiana na  mtangulizi wake marehemu Rais John Pombe Magufuli wakati huo yeye Bi Samia akiwa ni Makamu wa Rais.

Mnamo Aprili 15, 2022, gazeti la nchini Marekani la The New York Times lilimnukuu Rais Samia akisema kwamba ilikuwa ni “vigumu” kufanya kazi na Rais Magufuli baadhi ya wakati, na kwamba alikuwa akibishana sana na kiongozi huyo aliyefariki Machi 17, 2021, hususan lilipokuja suala la kukabiliana na janga la UVIKO-19.

Rais Samia aliyeingia madarakani mnamo Machi 19, 2021, akijaza nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba, amefanya marekebisho makubwa yaliowasuta waliofikiri kwamba  asingeweza kuliongoza taifa hilo. Lakini  ameacha swali zito na gumzo. Wadadisi wanahoji: Je, kauli yake hiyo aliyoitoa kwa mwandishi wa habari ni ya dhati  na kwa nini atoe kauli hiyo kwa chombo cha habari cha nje ya nchi? 

Kuyamudu madaraka

Mimi nadhani Samia amekuwa na nia safi kwa sababu amekwishaona hasara na jina baya ambalo Tanzania ililipata ilipokuwa chini ya utawala wa Rais John Magufuli, khasa katika nchi za Magharibi. 

Na nahisi huu ni wakati muafaka kwake kutoa matamshi hayo kwa sababu kufikia sasa ni wazi kwamba ameweza kujijenga na kuonekana kwamba amemudu kuyahodhi madaraka ndani na nje ya chama chake Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Ni muhimu kwake kujitambulisha kwamba ni mtu mwenye muelekeo (na pengine hata sera) tofauti na ule wa aliyemtangulia. Tangu arithi madaraka Rais Samia ameweza kuvivuka vizingiti vingi ndani na nje ya chama kinachotawala. Vingi ya vizingiti hivyo aliwekewa na baadhi ya viongozi wenzake waliokamia kumtega ili aanguke. 

Miongoni mwao walikuwa wale waliofikiri kwamba asingeweza kuwa kiongozi madhubuti kwa sababu tu kuwa yeye ni mwanamke na pia kwa maumbile yake ya upole. 

Lakini kwa vitendo vyake kupitia hatua mbalimbali alizozichukua ameonesha kwamba siyo tu kwamba ni kiongozi madhubuti lakini aliye macho na aliyeziona mapema sana njama za mahasimu wake waliokuwa wamekaa chonjo kama mamba wammeze. 

Kinyume chake ameibuka kuwa ni yeye aliyeweza kuwapiga chenga na hata kuwameza baadhi ya hao mahasimu wake. 

Mambo mawili Samia alipaswa kufanya

Mara baada ya Rais Samia kuushika uongozi wa taifa alikuwa na mambo mawili makuu aliyohisi lazima ayafanye. Mosi, kuwahakikishia wananchi wenzake kwamba yeye ndiye Rais wa taifa lao na pili, kuwahakikishia wawekezaji, hasa wa nje, kwamba mtindo wake wa uongozi ni tofauti na ule wa Magufuli, kwamba yeye yuko tayari kushirikiana nao katika shughuli za maendeleo ya nchi. 

Hilo lengo la pili ndilo lililomfanya atoe kauli yake iliyowashangaza wengi kwamba yeye amekuwa akitofautiana na Rais Magufuli. 

Ukiziangalia baadhi ya hatua za Rais Samia utaona kwamba nyingi ya hatua hizo zimekuwa zikikinzana na zile za Rais wa Awamu ya Tano. 

Nazo zinahusika na sera za ndani ya taifa, za kiuchumi na kisiasa, na hali kadhalika na sera za kutega rasilmali na uwekezaji kutoka nje, hususan kutoka mataifa ya Magharibi. 

Rais Samia ameona umuhimu wa kuyaweka sawa mazingira ya kisiasa na ya kiuchumi kwa mustakbali wa Tanzania. 

Na ndiyo maana ameona bora aitoe kauli yake kupitia chombo cha habari cha Marekani, ambako anatambua kwamba itawafurahisha wakubwa wa huko, itapokelewa vyema na wenye nguvu za kisiasa na za kiuchumi duniani. 

Kwa hakika, ziara yake hii ya Marekani alikokwenda kuzindua filamu hiyo ya Tanzania: The Royal Tour imezidi kumjenga kimataifa kutokana na kauli kadha wa kadha anazozitoa, ikiwa ni pamoja na ile aliyosema kwamba haikuwa rahisi kufanya kazi na Rais Magufuli na kuonesha kwamba hakuwa akikubaliana na yote aliyokuwa akiyasema na kuyafanya Magufuli. 

Kwa kujaribu kuyafanya yote hayo hamna shaka yoyote kwamba nia yake imekuwa safi kuhakikisha kwamba Tanzania inafungua ukurasa mpya katika maisha yake ya kisiasa na kiuchumi. Ametambua kwamba ni kwa kujitenga na hatua zilizokuwa na utata za Rais Magufuli ndipo ulimwengu utapoamini kwamba kweli Tanzania inajenga uongozi mpya. 

Ukinzani kutoka kwa wahafidhina

Changamoto kubwa alizokumbana nazo Rais Samia zilitoka kwenye mapande matatu ya CCM. Kwanza, na za hatari, zilitoka kwenye lile kundi lililokuwa likimuunga mkono Rais Magufuli kwa dhamira za kujipendekeza wao wenyewe na kulinda maslahi yao. 

Nyingine zilitoka kwenye kundi la wanasiasa wa Tanzania Bara lenye kuamini kwamba CCM ina wenyewe na wao ndiyo warithi halali wa chama hicho. Changamoto za tatu ni zile zitokazo kutoka kundi linalojihisi kwamba wao ndiyo warithi wa CCM ya Baba wa Taifa Julius Nyerere.  

Kwa mkato hawa huitwa “wahafidhina” kwa sababu hawataki kubadilika na kuufuata upepo mpya unaovuma chamani na nchini. 

Wachambuzi na wadadidi wa siasa za Tanzania wanahisi kwamba Rais Samia ataifungua zaidi nchi na siyo ukurasa tu pale ataporidhia pafanywe mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini. 

Pengine hizi kauli anazozitupa hapa na pale akiwa katika ziara zake mbalimbali ni ishara kwamba ndani ya nafsi yake anakubali umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya kwa kuanzia na uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi. 

Bila ya shaka hapawezekani kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi chini ya mfumo wa sasa ambapo wajumbe wa tume hiyo wanateuliwa na Rais. 

Ili kuonesha kuwa ana nia safi, Rais Samia anahitajika kuandaa mkakati mpya wa kulipatia taifa tume mpya ya uchaguzi, iliyo huru na yenye wajumbe wenye sifa za kutetea haki na demokrasia. 

Tume Huru ya Uchaguzi ni kipengele kimoja tu katika kuandaa Katiba Mpya ya nchi. Lengo kuu liwe ni kulipatia taifa Katiba Mpya na, kwa kufanya hivyo, kukidhi matakwa ya demokrasia halisi nchini. 

Kuna nchi kadha wa kadha barani Afrika ambazo zimefanikiwa kutunga Katiba Mpya au kuzirekebisha zile zilizopo ili kuimarisha kanuni za kidemokrasia. 

Tumeyashuhudia hayo Afrika Magharibi katika nchi kama Benin, wakati wa  mtawala  aliyekuwa mfuasi wa falsafa ya Ujamaa wa kisayansi, Mathieu Kerekou na vile vile Afrika Mashariki katika nchi kama Kenya. 

Kwa nini Katiba Mpya ni muhimu kwa Samia?

Rais Samia atakuwa amechukua hatua ya ujasiri mkubwa atakaporidhia Tanzania iwe na Katiba Mpya. Atazidi kuuonesha ujasiri wake kwa sababu Katiba inayotakiwa na wengi ni ile itayoyapunguza madaraka makubwa aliyo nayo sasa Rais wa taifa hilo. 

Pamoja na kuyapunguza madaraka ya Rais, Katiba hiyo pia itahitaji kuhakikisha kwamba vyama vyote vya siasa nchini humo vinaangaliwa kwa jicho sawa la Serikali, kwamba hakuna chama kinachopendelewa zaidi ya kingine. 

Msimamo huo utakuwa ni pigo kwa CCM, chama ambacho hasa katika awamu ya tano, kimeonekana kikibebwa na Serikali ya Tanzania.

Vyama vya upinzani  havina budi kujishirikisha katika mazungumzo na kumpa nafasi Rais Samia, kwani mabadiliko  ya demokrasia ni mchakato wenye milima na mabonde.

Ikiwa Rais  Samia  atafanikiwa, pia atakuwa ameacha alama ya uongozi wa kutukuka wakati wowote atakapomaliza kipindi chake cha kuliongoza taifa la Tanzania. Kwa upande mwengine,  utakuwa ni ushindi kwa Watanzania wote, kama taifa na mfano kwa wengi barani Afrika na kwengineko nje ya bara hilo.

Mohamed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Mohammed AbdulRahman

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved