Ben Ishabakaki: Katiba Mpya Italeta Mageuzi Kwenye Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Wakili huyo hata hivyo anaonya kwamba Katiba na sheria nzuri havitoi uhakika kwamba mfumo wa haki utaimarika. Anasema mageuzi ya kisheria ni lazima yaambatane na mageuzi ya kitabia na kimatendo miongoni wato haki.
Na Mwandishi Wetu5 May 202218 min

Dar es Salaam. Machache sana yanajulikana kuhusiana na utaratibu wa maridhiano kati ya mshitakiwa na waendesha mashitaka nje ya mijumuiko ya mawakili na wanasheria tangu utaratibu huo uanzishwe kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mnamo mwaka 2019.

Huu ndiyo msingi wa hatua ya The Chanzo kumtafuta wakili maarufu nchini Tanzania ambaye ni moja kati ya mawakili ambao wameshughulika na kesi nyingi za wateja wao kukubali kuingia maridhiano na waendesha mashitaka ili waweze kupata uhuru wao.

Huyu siyo mwengine bali ni wakili Benedict Ishabakaki ambaye katika mahojiano maalumu yafuatayo na The Chanzo anashindwa kujizuia kuelezea mchango wa utaratibu huo katika mchakato mzima wa uboreshaji wa haki jinai nchini Tanzania.

Ben, hata hivyo, ana mawazo kadhaa ambayo anadhani kama mamlaka husika zitayafanyia kazi siyo yatauboresha utaratibu huo wa maridhiano bali pia yataenda mbali kwenye kuboresha haki jinai nchini Tanzania na upatikanaji wa haki kwa ujumla, likiwemo lile la kufufuliwa kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Endelea …

The Chanzo: Ben, wewe ni moja kati ya mawakili ambao kwa kiwango kikubwa sana wameshughulika na kesi za wateja ambao wametaka kuingia kwenye utaratibu wa maridhiano [na waendesha mashitaka] ili waweze kuachiwa huru au watoke gerezani. Kwanza, kwa kuanzia tu, kwa niaba ya watazamaji wetu, ungejaribu kutuelezea kwa lugha rahisi utaratibu wa maridhiano ni nini na ni nini maoni yako ya ujumla kuhusiana na utaratibu huo.

Ben Ishabakaki. Asante. Utaratibu wa maridhiano, yaani kwa Kiswahili [plea bargaining] tunasema ni maridhiano na DPP [Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali]. [Utaratibu huu] ulianzishwa rasmi mwaka 2019. Kuna mabadiliko ya sheria ambayo yalifanyika mwaka 2019 [kuleta utaratibu huu].

Lakini kabla ya mwaka 2019 kama mtakumbuka, [wakati wa] awamu ya Mheshimiwa [Rais John] Magufuli ilikuwa ni awamu ambayo makosa ya jinai ya kiuchumi yalikuwa ni mengi sana. Kwa hiyo, kabla hata ya mwaka 2019 watu walikuwa wanafanya kitu kinachoitwa maridhiano na DPP lakini katika njia isiyo rasmi.

Sasa baadaye baada ya kuona kwamba ni njia nzuri ya watu kutoka magereza, kwa sababu magereza zilikuwa zimejaa sana kama mtakumbuka, kama ulikuwa huwezi kulipa kodi unapelekwa ndani. Kama umeingiza mzigo bandarini bila kuidhinisha unapelekwa ndani. Kama ulifanya jinai yoyote ambayo inahusu uchumi na mambo mengine na jinai zingine za kawaida ulikuwa unapelekwa ndani.

Kwa hiyo, kipindi cha Mheshimiwa Hayati Magufuli watu wengi walikuwa wapo ndani. Kwa hiyo, ikatokea njia isiyo rasmi ya mtu kwenda kwa DPP [na] kumwambia bwana mimi kweli hizo pesa sijazilipia kodi au kweli hilo kosa nimelifanya naomba nilipe hicho kiwango niweze kuachiwa.

Kwa hiyo, hiyo imekuwa ikifanyika kabla ya mwaka 2019 lakini baadaye baada ya watu kuona kwamba ni kitu kinafanyika siyo kisheria lakini hizi harakati za kuwa na hayo makubaliano zilianza toka kipindi cha nyuma.

Nakumbuka kuanzia mwaka 2015 wanasema kuna mswada ambao ulikuwa unajadiliwa bungeni lakini ulisahaulika. Kwa hiyo, baada ya 2019 kuleta ile sheria ndio Mheshimiwa Magufuli, kama mtakumbuka, siku moja Ikulu akasema kwamba tunapitisha sheria ya kusamehe watu.

Na kwa bahati mbaya sana, tafsiri [iliyopo] kwenye umma, [watu] ambao watu siyo wanasheria, waliichukulia vibaya [huu utaratibu] kwa sababu walijua labda ni msamaha wa Rais, ama ni kitu ambacho Rais amesema kwamba watu waandike barua kuomba msamaha ndani ya siku saba.

Lakini kuwaelewesha Watanzania ili waweze kuelewa hili siyo kuomba msamaha. [Kinachofanyika] ni kwamba unahisi kuna kosa fulani ambalo Serikali au DPP anasema umefanya. Wewe unamwandikia barua DPP kwamba nipo tayari tukae mezani tujaribu kumaliza [hiyo kesi].

Kwa hiyo, kama Mamlaka ya Mapato [TRA] wanasema hujalipa kodi ya [Shilingi] bilioni tano lakini wewe kwenye rekodi zako inaonesha kuna kodi ya bilioni mbili umelipa, mnakaa mezani mnakubaliana kwamba kwenye ile kodi ya bilioni tano kuna mbili nililipa.

Kwa hiyo, mnaingia kwenye muafaka [wewe na DPP], anakufutia yale makosa mengine yote ambayo unadhani walikufungulia ndivyo sivyo, ama unadhani hayakuwa yamefunguliwa sawa baada ya hapo wewe unaridhia kwamba utalipa kiwango fulani cha pesa na unakuwa unaachiwa huru.

Kwa hiyo, ni mchakato ambao baada ya kupitishwa kwa sheria [mnamo] mwaka 2019 ulitumika sana. Sina idadi kamili kwa sababu sina takwimu [ya kesi nilizoshughulika nazo]. Lakini mimi binafsi naweza nikasema nimesimamia hayo makubaliano siyo chini ya 20, wateja wakubwa na wengine wadogo.

The Chanzo: Na hapo nilikuuliza pia yaani kwa ujumla unauchukuliaje utaratibu huu wa [mshitakiwa kuingia] maridhiano [na waendesha mashitaka]?

Ben Ishabakaki: Kwa ujumla utaratibu wa maridhiano nauchukulia vizuri, [nauchukulia] kwa upande chanya sana. Kwa sababu ukiangalia dunia ya sasa na nchi nyingine ambazo zimeendelea na nchi nyingine jirani, [kwa] mfano ukiangalia Kenya wanao huo mfumo na wameanza kuutumia zamani.

Kwa hiyo, ni mfumo ambao ulichelewa kuja Tanzania. Ni mfumo mzuri kwa sababu unapunguza watu magereza. Lakini pia unawapa watu haki ya kusema, kukaa na kufanya majadiliano kwamba wewe unasema mimi nimeiba kiasi fulani au unasema nimefanya kosa fulani hili kosa mimi nilifanya kwa kiwango fulani, kwa hiyo mnakubaliana.

Lakini siyo makosa yote kwa Tanzania ambayo yana makubaliano hayo, lakini pia kuna baadhi ya mipaka ambayo ipo kwenye baadhi ya makosa yenye makubaliano hayo. Kwa hiyo, mimi kwa ujumla nasema ni mfumo mzuri sana na ninauhimiza.

Na kwa Tanzania tena, tuna [huo utaratibu wa maridhiano] lakini kwa wenzetu, nchi kama Marekani na nchi za Afrika Kusini ambazo zimeendelea, uchumi unavyozidi kukua wa nchi, uhitaji wao wa kuendana na sheria za nchi unazidi kuongezeka, kwa mfano makampuni ya simu, makampuni makubwa ya uchimbaji wa mafuta na gesi.

Ikitokea tu wamechafua mazingira kisheria lile ni kosa la jinai. Sasa makampuni makubwa ambayo yameendelea, na nchi ambazo zimeendelea, tunasema kuna kitu kinaitwa deferred prosecution, yaani tusiende hata kukukamata, tukae chini mezani, tukwambie bwana Khalifa [Said, mwandishi] wewe umefanya hili kosa. Je, unakiri? Ndiyo mimi hili kosa nimefanya ama kwa uzembe au makusudi nakiri na nipo tayari kuwalipa fidia hawa watu.

Kwa hiyo, mwisho wa siku unaona kwamba hutapelekwa mahakamani. Lakini kwa Tanzania sheria tuliyonayo haina hiyo sheria ya deferred prosecution, yaani kwamba tuuache tusikushtaki. Ya Tanzania jinsi ilivyo ya plea bargaining lazima upelekwe kwanza mahakamani halafu ndiyo unakwenda kwa Mwendesha Mashtaka kwamba hili kosa ni kweli nililifanya na ninaomba tukae chini tumalizane.

Kwa hiyo, [utaratibu wa maridhiano] ni mfumo mzuri kwanza unapunguza watu magerezani lakini pili unawapa watu haki yakusema ukweli wa suala ambalo ametuhumiwa nalo.

Pia, upande wa Serikali kwa namna moja au nyingine inaiongeza kipato Serikali kwa sababu kama mtu alikwepa kodi akafunguliwa kesi ya jinai na ameenda amekiri atalipa ile kodi kwa hiyo Serikali inapata fedha zake.

Lakini pia upande ambao sio wa Serikali, yaani mshtakiwa, labda leo mimi nimekutapeli, nikakuibia [Shilingi] milioni 400 nikashtakiwa na Serikali nikakiri kwamba nilikuibia ile pesa kwa kawaida kimsingi inabidi irudi kwako wewe kama muathirika. Kwa hiyo, pia mfumo huu unasaidia Serikali, unasaidia waathirika lakini pia inamsaidia na mtuhumiwa.

Tatizo tu kwa Tanzania ni kwamba mfumo ulikuja kipindi ambacho kuna shinikizo sana, watu [walikuwa] wanataka kutoka nje [ya magereza]. Kwa hiyo, kuna makosa mengine mtu unakuta alituhumiwa nalo ambalo siyo hata kweli, labda alibambikiziwa, lakini kwa sababu anataka kutoka nje inabidi aende akubali atoke nje.

Na kwa sababu kwa bahati mbaya sana kwa nchi yetu kama Tanzania tuna makosa mengi sana ambayo hayana dhamana, na kama utakumbuka awamu iliyopita kila kosa utasikia kuna utakatishaji, sasa kuweka usawa kati ya mtu anayetaka kwenda kwenye maridhiano kwa kuwa tu amekosa dhamana tunasema hapo ili kuweka usawa kwamba je, ameridhia kwenda kwenye maridhiano, inakuwa ni ngumu.

Kwa sababu huyu mtu nia yake labda ni kutoka tu ndani kwa sababu kosa lake ni utakatishaji wa fedha, hana dhamana na unakuta hana nia ya kweli ya kwenda kwenye maridhiano.

Na ndiyo maana unaona kwa sasa hivi [kesi za washtakiwa] kuomba kuingia maridhiano na DPP zimeshuka kabisa. Tunazungumzia [kesi] moja au mbili. Ukienda ofisi ya DPP sasa hivi unakuta mtu mmoja au wawili [wanataka kuingia maridhiano].

Lakini zamani kulikuwa kuna msururu ofisi ya DPP. Kwa sababu gani? Makosa mengi yalikuwa hayana dhamana. Lakini mtaona DPP mpya aliyekuja sasa hivi makosa mengi yana dhamana. Na mpaka akukamate akupeleke mahakamani lazima uchunguzi uwe umekamilika. Kwa hiyo, utaona huu utaratibu wa kuingia maridhiano upo lakini hautumiki tena [sana].

The Chanzo: Nataka kufahamu kidogo. Pale mwanzo umezungumzia uwepo wa deferred prosecution na hapa sisi tuna utaratibu wa plea bargaining. Labda pengine unaweza kujaribu kutofautisha labda, yaani hizi [taratibu mbili] zinatofautiana vipi kimsingi kabisa?

Ben Ishabakaki: Kimsingi zinatofauti kubwa sana. Kwa mfano, kwenye plea bargaining mwisho wa siku kama lazima kwanza ukamatwe na lazima ushtakiwe na lazima uende ndani kama kosa halina dhamana au kosa lina dhamana utakaa nje. Kwa hiyo, lazima msingi wa kwanza ukamatwe na lazima ushtakiwe na lazima utakuja kukiri baadhi ya makosa.

Kwa hiyo, kama umeshtakiwa na makosa kumi, mkishakubaliana, ndiyo maana tunasema plea, unajua maana ya plea ni kukiri, yaani kwenda kukiri mbele ya Mahakama. Kwa hiyo, lazima utakwenda mbele ya Mahakama ukiri baadhi ya makosa ndiyo maana ya plea bargaining, yaani kwamba tumekushtaki na makosa mia, au makosa kumi, mnakubalinana, ukakiri makosa mangapi, hiyo ndiyo maana ya plea bargaining.

Lakini kwenye deferred prosecution tumegundua wewe tayari ushafanya kosa wakati tunachunguza. Wewe mwenyewe unakiri kwamba ni kweli hili kosa nimelifanya na mara nyingi inakuja kwenye makosa kama ya mabenki, makosa ya uchafuzi wa mazingira na makampuni makubwa.

Kwamba ni kweli tumechafua mazingira, ama ni kweli tulishindwa kukata hii kodi, ama ni kweli miamala ya simu hii tumeifanya ndivyo sivyo, au ni kweli hizi data za watu tumeziuza kwa kampuni nyingine. Kwa hiyo, kabla DPP hata hajakukamata wewe mwenyewe mtuhumiwa unakua unakiri.

Kwa hiyo, DPP mnakuwa mnaingia kwenye makubaliano kwamba mimi sitakushtaki lakini kwa sababu mimi sitakushtaki na wewe ukiri kwamba utafanya kitu fulani, labda hutafanya hilo kosa kwa miaka kumi, au utailipa hasara ile jamii ambayo imepata kama labda ni uchafuzi wa mazingira, au kama labda umeiba data za watu kiasi fulani.

Kwa hiyo, kwenye deferred prosecution yaani huendi kumshtaki mtu mnaingia kwenye makubaliano kwamba sitakushtaki ila wewe utafanya hiki na hiki na hiki. Na mkishamaliza kawaida mnaipeleka ile hati mahakamani.

Uzuri wa deferred prosecution kwa nchi ambazo zinaendelea na nchi zenye uchumi mzuri ni kwamba kunakuwa hakuna kumbukumbu za kijinai. Kwa sababu hujashtakiwa lakini kwenye plea bargaining kumbukumbu za kijinai zinakuwepo kwa sababu kuna baadhi ya makosa ambayo tayari umeshakwenda mahakamani na umekiri.

Kwa hiyo, kwa nchi kama Tanzania kwa kipindi kama sasa hivi ambapo tunaona Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu Hassan] anahamasisha watu kulipa kodi, nadhani njia mbadala ya plea bargaining, kwa sababu pia imekuwa ikilalamikiwa sana, ni deferred prosecution.

Na kwa sababu uchumi unakua [huu utaratibu ni muhimu sana]. Leo hii huwezi ukaileta kampuni ya uchimbaji wa mafuta ipo Mtwara, inachimba mafuta, unawakamata wakurugenzi wake wote unawaweka ndani, kampuni inakwenda kuanguka.

Tumeona kwenye baadhi ya makampuni hapa Tanzania kipindi kilichopita, wakurugenzi wote [wa kampuni] wanapelekwa ndani. Kwa hiyo, kampuni inaweza ikayumba. Kwa hiyo, kwa wenzetu walioendelea wanaona kwa nini tumpeleke mtu ndani? Tukae chini tukubaliane naye. Mnakubaliana hatukupeleki ndani lakini hii hasara ambayo umeisababishia Serikali utailipa.

The Chanzo: Utaratibu wa deferred prosecution na plea bargaining zinaweza kuwepo kwa pamoja, au ni moja iwepo nyingine isiwepo?

Ben Ishabakaki: Zinaweza kuwepo zote kwa pamoja. Ukiangalia nchi kama Marekani wana plea bargaining lakini pia [wako na] deferred prosecution. Lakini mara nyingi kwenye nchi kama hizo ukishakuwa na plea bargaining na deferred prosecution watu wataenda kwenye deferred prosecution kwamba sitaki kuwa na kumbukumbu wa kijinai.

Kwa sababu kama nilivyokwambia kwenye plea bargaining kwenye maridhiano lazima utakwenda kukiri baadhi ya makosa. Kwa hiyo, tayari unakuwa na ushahidi wa kijinai.

The Chanzo: Hizi hoja nyinyi kama mawakili, au kama wadau wa sheria, mmeshaziwasilisha kwa mamalaka husika. Yaani kusisitiza uwepo wa huo utaratibu wa deferred prosecution badala ya kuwepo au nyongeza ya mfumo wa plea bargaining.

Ben Ishabakaki: Binafsi, kama law firm ya kwangu Victory Attorneys, tumewasilisha. Hata hii plea bargaining moja kati ya watu waliyoipigania ni sisi. Tumekuwa tukiandika makala nyingi sana kwa sababu law firm ya kwetu tunachoamini [ni kwamba] tunavyozidi kuandika unaleta hamasa.

Hii deferred prosecution ukiingia kwenye google kwa Tanzania utaikuta makala ambayo tumeiandika sisi na tumeshawasilisha kwa DPP na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa hiyo, tunadhani jinsi uchumi unavyokua hakuna namna itabidi waje na huu mfumo ambao kidogo utakuwa umepunguza watu magerezani. Lakini pia unapunguza ushahidi wa kijinai na machungu ambayo watu wamekuwa wakilalamikia ya mfumo wa jinai hapa Tanzania.

The Chanzo: Turudi kwenye plea bargaining. Huu utaratibu unafanya kazi tu endapo kama mimi nimekosana na Jamhuri au hata kama mimi nimekosana na wewe Benedict? Kwa sababu vile nimesikia ni kwamba kesi nyingi, sina uhakika, wewe umefanya hizi kesi, kesi nyingi ni zile ambazo zimemhusisha mtu na Serikali, amekwepa kodi, amefanya hivi. Huu utaratibu wa plea bargaining unafanyaje kazi katika mazingira ambayo mimi na wewe ndio tunadaiana au tumekosana?

Ben Ishabakaki: Kwanza tu ujue kesi za madai siyo [za] jinai ila kama nimekutapeli ina maana hapo kuna fraud ndiyo inakuja jinai. Kwa hiyo, kama nilikuwa nimekutapeli [Shilingi] bilioni mbili, na kuna kesi ambayo mimi nimeifanya wakati was kipindi cha nyuma, mtu alimtapeli mtu na tukaingia kwenye maridhiano na akamlipa yule mhusika.

Kwa hiyo, inawezekana. Hizi kesi zinakuwa ni kwa upande wowote. Yaani plea bargaining inatumika kwa upande wowote. Mimi na wewe kama umenitapeli nitakurudishia tutamalizana. Mimi na Serikali vivo hivyo.

Lakini kama nilivyokwambia katika utawala was Mheshimiwa Magufuli ulikuwa ni utawala uliosisitiza sana kufuatwa kwa sheria na kanuni. Kiasi ya kwamba makosa mengi sana yaliyokuwa yanakuja pale yalikuwa ni makaosa ya Serikali na ndiyo maana plea bargaining nyingi zilikuwa ni za Serikali.

Lakini pia hii sheria imesema kuna baadhi ya makosa huwezi ukafanya plea bargaining. Kwa mfano, makosa ya ubakaji hiyo huwezi ukasema [unaingia kwenye plea bargaining], hakuna mjadala. Makosa ya ugaidi.

Makosa ya madawa ya kulevya ambayo yanazidi gramu fulani. Bangi ambayo inazidi kiwango fulani. Makosa ya ujangili. [Makosa] hayo tunasema hakuna mjadala. Umekutwa na kosa nenda mahakamani ukahukumiwe kwa sababu lengo ni kuwafanya watu wasifanye hayo makosa.

Lakini tunasema makosa haya ya kiuchumi, haya ambayo leo Khalifa ameshindwa kulipa kodi, baadaye tunaweza tukamwadhibu akarudi mtaani akafanya biashara, tuyawekee plea bargaining.

Kwa hiyo, kuna baadhi ya makosa hakuna mjadala lakini kuna baadhi ya makosa mjadala upo, iwe umeitendea Serikali au umemtendea mtu wa kawaida.

The Chanzo: Katika muktadha wa upatikanaji haki, unadhani utaratibu wa plea bargaining unachagiza upatikanaji wa haki au unakwamisha?

Ben Ishabakaki: Naweza nikasema, nahofia sana kusema unachagiza upatikanaji wa haki kwa sababu ya hali [iliyopo huko chini]. Kesi nyingi ambazo nimefanya unakuta mtu anasema twende tu, twende tu yaani kwamba kwa sababu yupo ndani.

Laiti kama tungekuwa na makosa yote ambayo yana dhamana Tanzania halafu mtu anakwenda kukiri ningesema upatikanaji wa haki unakuwepo. Lakini kwa sababu mtu tu yupo ndani, hana dhamana, na unaona kabisa wewe kama wakili kwamba anakwambia twende tu kwa sababu nipo ndani, sidhani kama kimsingi ni haki.

Lakini kwa sasa hivi kama kungekuwa na plea bargaining naona haki ipo kwa sababu kama nilivyokwambia sheria imepitishwa, utapelekwa ndani kama uchunguzi umeisha, kitu ambacho ina maanisha DPP atakuwa na ushahidi kabisa kwamba hapa mimi nakwenda kukufunga. Kwa hiyo, ukikiri umekiri mwenyewe.

Lakini kipindi cha nyuma tulikuwa tunakwenda kwenye plea bargaining hata uchunguzi haujalamilika. Sasa unashindwa kuelewa kwamba huyu mtu je, kama uchunguzi haujakamilika [anakiri vipi hili kosa?]

Lakini anakiri hili kosa kwa sababu mtu alikuwa mtu anasema kwamba mimi nipo ndani leo siwezi kusubiri mwaka mzima mpaka uchunguzi ukamilike, ngoja nifanye plea bargaining.

Kwa hiyo, katika haki unakuta kuna haki ambayo inanyimwa hapo kwamba mtu anataka kukiri kosa ambalo uchunguzi haujakamilika.

The Chanzo: Sijui, kwa mfano, kama wewe pia unakuwa na huu wasiwasi, mimi nimeongea na baadhi ya wanasheria vijana wanokua, wengine ni mawakili na wao wanahofu kwamba endapo huu utaratibu wa plea bargaining ukiendelea kutumika ni kama vile pengine kuna aina fulani ya wanasheria watakosekana, unajua sasa hivi nyinyi kuna watu ambao mnawaangalia kama mfano wakuigwa. Lakini sasa hivi hamuendi mahakamani, unajua ile kumtetea mteja, hivyo baadhi ya mawakili wana wasiwasi pengine baada kama vile miaka ishirini au miaka inayokuja mawakili kama waliopo sasa hivi wazee wanaweza wasiwepo tena kwenye hizo siku za mbele. Wewe pia una huo wasiwasi au hiyo hofu?

Ben Ishabakaki: Nimekuelewa sana kwa sababu wanasema kila kizazi kina kizazi ambacho inakiangalia. Kwa mfano, sisi wakati tunasoma tuna mawakili tulikuwa tunawaangalia ambao walikuwa vizuri kwenye yanapokuja masuala ya mfumo wa jinai jinsi ya kupitia hayo masuala.

[Lakini] hiyo haiwezi kuondoka kwa sababu kama ninavyokwambia tunaidadi kubwa sana ya makosa ambayo bado yanafanyika Tanzania na bado yapo ambayo hayana plea bargaining. [Kesi zinazohusu] masuala ya mauaji, ugaidi. Tukiangalia masuala ya ubakaji bado haya yatakuwepo.

Katika hali ambayo kama mtu anapenda vijana wadogo wanaokua wanapenda kufanya kesi za jinai sijaona kwamba suala la plea bargaining linaeweza likaondoa hao wanasheria ambao wanataka kwenda kwenye sheria za jinai.

Bila shaka hiyo inaweza ikapunguza lakini haiwezi kuondoka kabisa. Kwa mfano, kama leo hii kuna mawakili wapo maarufu ambao ni wazuri kwenye makosa ya jinai, kuna kesi nyingi za jinai ambazo zinaendelea Mahakama Kuu.

Lakini pia hata nchi ambazo nimekutajia, mfano Afrika Kusini, Marekani, [na] Kenya, bado kuna mawakili wazuri sana kwenye mfumo wa jinai. Hizi nchi bado zinafanya deferred prosecution na bado zina hiyo plea bargaining.

Ni mabadiliko lakini pia kama nilivyokwambia sio makosa yote [yanaweza kumalizwa kwa plea baragaining]. Lakini pia dunia inabadilika. Uchumi wa nchi unakua. Kwa nini uwe na watu wengi magereza kisa kutengeneza wanasheria mahiri ambao wanafanya haki jinai? Kwa hiyo siamini, siamini kwenye hilo.

The Chanzo: Pale mwanzo umezungumzia kwamba hutaki kusema kwamba utaratibu wa plea bargaining unachagiza upatikanaji haki kwa sababu watu wengi wanaolazimika kuingia kwenye plea bargaining ni watu ambao wanakuwa wapo ramande, wapo ndani na wanakuwa wanataka kutoka. Na hiyo inanipelekea mimi kukuuliza kwamba unadhani ule utaratibu wa plea bargaining uweze kufanya kazi vizuri, unatakiwa uunganishwe na nini, yaani uambatanishwe na mageuzi gani?

Ben Ishabakaki: Kwanza ni mfumo mzuri kama nilivyokwambia. Sasa hilo suala lako bila shaka nililikwepa kwa sababu kama nilivyokwambia yaani tujihusishe sana kwenye uzoefu.

Kwanza wakati hii sheria [iliyoleta utaratibu wa plea bargaining] inatungwa mwaka 2019 kulikuwa hakuna kanuni. Kanuni zimekuja mwaka 2021, sijui umenielewa? Kanuni ni ile ambayo inakwambia utaandika barua wapi, ndani ya siku ngapi plea bargaining iwe imekamilika.

Kwa hiyo, zamani ulikuwa unafanya plea bargaining hata kwa mwezi, miezi minne, miezi sita, mwaka mzima upo bize unamtafuta DPP. Lakini kwa mimi hilo swali lako ni zuri sana.

Nadhani mfumo uendelee kuwepo, watuongezee mfumo mwingine huo wa deferred prosecution baada ya hapo sasa kuwe tunasema mfumo wa haki jinai wa Tanzania uwe wa usawa, makosa karibia yote yawe na dhamana.

Kama leo Khalifa anaamua kwenda kwenye plea bargaining, yupo nyumbani ameamua kwenda, ameamua yeye. Lakini tusimsukume mtu, tukamuweka ndani, amekosa dhamana na akija kwenye chaguo la kuomba plea bargaining tunamruhusu.

Lakini pili tayari nimeona Serikali imeanza kufanya mabadiliko kama nilivyokwambia. Sasa hivi mtu hapelekwi ndani, sheria inasema, nimeona juzi kuna kesi mbili tatu [Mahakama ya Hakimu Mkazi] Kisutu watu wameshapelekwa halafu DPP anasema uchunguzi bado unaendelea, lakini sheria haisemi hivyo.

Kwa hiyo, kwa sababu uchunguzi umeshakamilika ndiyo mtu anakamtwa sasa hivi, au [ndiyo] anapelekwa ndani, naona inaweza ikasaidia kiasi. Kwamba upo ndani lakini unajua kabisa kwamba nakwenda kukubaliana kwenye kitu ambacho ushahidi nauona kabisa kuna makosa nimeyafanya.

The Chanzo: Nataka kukuuliza kwa sababu nadhani hilo ni tatizo kubwa sana Tanzania. Wewe kama mwanasheria inakushangaza kuona kwamba sheria inasema hivi lakini watekelezaji, au mamlaka husika inayopaswa kutekeleza hiyo sheria, inafanya vinginevyo? Labda pengine inakushangaza, pengine inakusikitisha labda kwa namna yoyote?

Ben Ishabakaki: Inanisikitisha na ndiyo maana tunaposema ujue nchi ya kidemokrasia au kama ulishawahi kusikia neno utawala wa kisheria yaani unapofanya mambo yako lazima yaendane na sheria.

Mheshimiwa Rais [Samia] amekuwa akizungumza kwamba sheria [ichukue] asilimia sabini [ya matendo yako] na utu wako, utashi wako, uendeshaji wa kawaida [uchukue zilizobaki]. Lakini unapokuja kwenye masuala ya jinai kumbuka hii ni haki ya mtu.

Kwa mfano, ukimchukua kijana wa miaka 25, wakili mdogo au mwanaharakati, au mtu tu yeyote, ukampeleka ndani akakaa miaka mitatu. Hapa tayari unakuwa umeshaharibu maisha yake. Kama alitakiwa awe na familia, kama alitakiwa awe na watoto, kama alitakiwa akue kwenye kazi yake, umeshaharibu [huo mpangilio wake].

Kwa hiyo, kwenye masuala ambayo yanagusia haki jinai pale hatutakiwi tutumie utashi, kwamba tumkamate huyu kwa sababu [fulani]. Hapana, tunatakiwa tutumie sheria. Na ndiyo maana sheria wakati imepitishwa ilisema kwa baadhi vya makosa unaweza ukakamtwa hata kama upelelezi haujakamilika.

Mfano, mauaji hatuwezi tukasema tunakushtumu kwa kuua sasa tusubiri upelelezi ukamilike. Lakini kwa baadhi ya haya makosa mengine tusubiri upelelezi ukamilike na ndiyo maana sheria ililitambua hilo.

Kwa hiyo, nadhani tunapokuja kwenye mfumo wa haki jinai hakuna suala la kusema utashi wa mtu. Inabidi twende kwenye sheria kwa sababu tunagusa haki ya mtu.

The Chanzo: Na kama sheria ina matatizo tuipeleke [bungeni] tuiboreshe.

Ben Ishabakaki: Kabisa. Kwa hiyo, ninaumia, na sipendi, kuona watu wanatumia utashi zaidi ya sheria unapokuja kwenye suala la mfumo wa haki. Tungekuwa tunazungumzia sheria za biashara, kwa mfano wewe ni mwekezaji umekuja Tanzania kuwekeza nakwambia labda inatakiwa labda kitu kidogo tuseme uwe na ofisi ya kufanya kazi lakini wewe unafanya kazi ya mfumo kama hii ya televisheni ambayo siyo lazima uwe na ofisi naweza nikasema sheria inasema hivi lakini ngoja nipindishe kidogo ili nimkaribishe huyu mwekezaji.

Lakini kwenye suala la haki jinai ni kuwa makini sana kwa sababu tunacheza na uhai wa mtu, tunacheza na maisha ya mtu na kumbuka tunaishi mara moja hapa duniani. Kwa hiyo, nikishachukua miaka yako mitatu [au] minne ukiwa ndani ndio basi tena.

The Chanzo: Utaratibu wa plea bargaining unaweza kutumika ndivyo sivyo au kutumiwa vibya na watu wenye mamlaka pengine kufanikisha malengo yao fulani ambayo yanaweza yakawa hayajulikani kwa umma?

Ben Ishabakaki: Kwa maoni yangu, na kutokana na wadau wengi ambao wemekuwa wakizungumza, kuna mkutano tulikuwa nao juzi, tamasha la mambo ya plea bargaining, wadau wengi wanalalamikia kwamba huu mchakato umejawa na rushwa, umejawa na watu kuja kujifanya kwamba wao ndiyo wanafanya haya mambo.

Kwa hiyo, bila shaka wakati mwingine inaweza ikaleta shida kwa sababu mtu anataka atoke. Au wakati mnapokubaliana shilingi ngapi ilipwe pale, mtu anaweza akatumia faida zake kwenye kufanya mambo mengine, mwanya huo unaweza ukawepo, lakini kwa chochote hata bila plea bargaining nchi yoyote ambayo haina maadili, haina misingi rushwa inaweza ikatokea muda wowote iwe una plea bargaining au hauna plea bargaining.

Haya ni mambo ambayo inabidi tujihusishe na misingi ya malezi yanaenda mbali. Kwa hiyo, hata uwe na sheria nzuri namna gani mambo ya rushwa yanaweza yakawepo tu.

The Chanzo: Ukiangalia kwa ujumla picha ya mageuzi ya mfumo wa haki jinai na hapo umezungumzia kwamba kuna moja kati ya vitu ambavyo unavipigania nyinyi kama wanasheria, mawakili ni kuhakikisha kwamba makosa yote yanakuwa na dhamana. Unadhani hiyo inawezekana, unadhani inaweza ikafika wakati Tanzania tukawa na makosa yote yanadhamana, unadhani inawezekana?

Ben Ishabakaki: Inawezekana sana. Zanzibar tu hapo makosa karibia yote yana dhamana. Kenya, ambao ndio majirani zetu, ambao tunasema [tuko nao kwenye] Jumuiya ya Afrika Mashariki tunaopambana nao, makosa yote yana dhamana. Kwa nini Tanzania tushindwe?

Siyo kwamba Watanzania ni watukutu sana, au kuna utakatishaji wa pesa sana, ni utashi [tu]. Tukiwa na kiongozi mwenye utashi, tukiwa na watu wenye uelewa tutafika. Naamini tutafika tena mapema sana. Siyo suala kusema kwamba ni kubwa kama Katiba ambayo inahusisha mambo mengi. Ni utashi tu. Leo mtu anaweza akasema nataka Tanzania makosa yote yawe na dhamana tutafika.

The Chanzo: Kwa hiyo, makosa yote yakiwa na dhamana mahakama ndiyo inabaki kuwa muamuzi wa nani apewe nani asipewe kabisa?

Ben Ishabakaki: Na ndiyo wenzetu Zanzibar wanafanya [na] wenzetu Kenya wanafanya. Sasa Mahakama ndiyo itasema kutokana na tabia ambazo huyu mtu ameonesha tukimuachia atakuwa anaathari kwenye jamii, kwa hiyo tunamnyima [dhamana].

Lakini sasa ukishaifunga kwenye sheria, hata kama Jaji anaona huyu mtu hana athari kwenye jamii, hawezi kukuachia, kwa sababu sheria inamfunga.

The Chanzo: Na hapo maana yake mabadiliko makubwa yanapaswa yafanyike kwenye sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Ben Ishabakaki: Kabisa.

The Chanzo. Tumalizie wito wako labda kwa ujumla, kwa sababu kule mwanzo tumezungumza masuala ya kufuata sheria kwa mamlaka husika, wito wako labda, yaani dira yako ya Tanzania ya haki labda ikoje kwa mtazamo wako? Wewe ni kipi labda pengine unapaswa ukione ili kuweza kusema kwamba kweli sisi Tanzania sasa tumekuwa nchi ya wenye kujali haki na masula ya utawala wa kisheria na vitu kama hivyo?

Ben Ishabakaki: Dira yangu ni kubwa kidogo na ianatisha kwa sababu nadhani mfumo wa haki jinai unaanzia kwanza kwenye mageuzi na mageuzi yanaanzia pakubwa zaidi, yanaanzia kwenye sheria mama ambayo ni Katiba ya nchi.

Kwa hiyo, maadamu ni mjadala ambao unaendelea kitaifa, nadhani inabidi tuanzie huko [kwenye kutengeneza Katiba Mpya]. Lakini sisemi kwamba mfumo wa haki jinai lazima uende kwenye Katiba. Hata Katiba ya sasa hivi tuliyonayo inatosheleza, ina haki nyingi sana ambazo zinaweza zikaleta haki jinai.

Lakini kuna mambo mengi sana ya [kufanya kuboresha utoaji haki jinai Tanzania]. Kuna matendo, yaani yale matendo ya kila siku tu ya Jeshi la Polisi inabidi yaboreshwe. Kuna matendo ya wale wachunguzi pia.

Kwa hiyo, unaweza ukaishia kuwa na Katiba nzuri, sheria nzuri, mfumo wa haki jinai mzuri, lakini matendo yakawa mabaya. Kwa hiyo, dira yangu ni kwamba ni bora tuwe na sheria hizi lakini matendo ya Jeshi la Polisi, matendo ya wachunguzi, matendo ya waendesha mashtaka wa Serikali, yabadilike.

The Chanzo: Na Tunawezaje kufanikisha hilo?

Ben Ishabakaki: Sasa hilo ni suala la utashi. Ni suala la uongozi wa juu [kuamua]. Uongozi wa juu ukisema labda tunataka watu, mfumo wa jinai, kwamba uwe namna hii, utakuwa namna hiyo.

Naamini nchi yoyote, bila shaka kuna mambo mengine huwezi ukayabadilisha, mfano utashi wa watu kulipa kodi, hiyo lazima uanze na watoto, nchi za wenzetu unapewa ice cream wanaikata kidogo halafu wanakupa nusu, ukiuliza nini wanakwambia hicho cha juu ni kodi ya Serikali.

Kwa hiyo, kuna mambo mengine lazima yaanzie mbali sana kuanzia kwenye utashi, uelewa wa watu maofisini na wapi. Lakini kwenye mambo kama haya ya mfumo wa haki jinai ni mambo ambayo, mfano leo Mkuu wa Jeshi la Polisi akisema sitaki askari wangu yoyote afanye vitendo hivi na hivi na hivi hayatafanyika kwa sababu yeye ndio mwajiri, Rais wa nchi akisema hiki na hiki [sitaki kuviona] yatafanyika.

Baada ya muda watu watajua kwamba kumbe matendo yapo hivi. Kwa hiyo, baada ya muda tutafika.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved