Tutafakari Namna Bora ya Kuhakikisha Afya za Watu Wetu

Kama ilivyo ni wajibu wa Serikali kuelimisha watu wake ili waweze kutoa mchango stahiki katika ujenzi wa taifa, vivyo hivyo Serikali inapaswa kuwajibika na kuwatibu watu wake pale wanapoogua.

subscribe to our newsletter!

Ipo haja ya kufanya mageuzi makubwa, ya kisheria, kwenye namna Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatoa huduma zake kwa Watanzania kama kweli tumedhamiria kuimarisha afya za watu wetu kwa kuwakinga na kuwaepusha na maradhi mbalimbali.

Hili ni muhimu zaidi pia kama kweli tuna nia ya dhati ya kuwafanya wananchi wengi wajiunge na mfuko huo.

Kwa siku nyingi sasa, watumiaji wa mfuko huo wamekuwa na malalamiko lukuki juu ya utaratibu wa namna unavyotoa huduma zake kwa wanufaika wake, hali ambayo siyo tu inawaathiri Watanzania waliojiunga na mfuko bali pia wale ambao hawajajiunga kwa kukataa kabisa kufanya hivyo.

Malalamiko ni mengi lakini moja ni lile linalohusu uwepo wa ukomo wa umri wa mtegemezi ambapo mwisho wa umri wa mtegemezi unapaswa kuwa ni miaka 21. Kigezo hiki cha umri kimekuwa kikwazo cha watu wengi kuweza kupata haki ya huduma za matibabu.

Niliwahi kukutana na kesi moja kwenye hospitali moja jijini Dar es Salaam, ambapo dada mmoja alienda hospitali kupata huduma akiwa bado ni mtegemezi, lakini umri wake kwa mujibu wa sheria ulikuwa umepita kizingiti kilichowekwa na hivyo hospitali kushindwa kumpatia huduma.

Hii tukio lilinifikirisha sana. Inakuwaje, kama lengo ni kila mtu apate huduma, tunaanza kuwachagulia Watanzania wategemezi umri wa kuumwa? Maana hii ni sawa na mtu kukuchagulia uumwe katika umri gani.

Vifurushi vya matajiri na masikini

Eneo jingine linalozalisha malalamiko ni lile linalohusu vifurushi ambapo mwenye pesa nyingi ndiyo hupata kifurushi kinachomuwezesha kupata huduma nyingi na nzuri za kiafya wakati yule asiye na pesa huishia kupata vifurushi vinavyomuwezesha kupata huduma hafifu na duni.

Huku ni kuwagawa wananchi kimatabaka. Kama lengo ni kila mtu apate huduma ya afya, kwa nini tunaanza kuwatenga watu? Kwa nini isiwe kwamba muhimu ni mtu achangie kwenye mfuko na kupata fursa ya kupata matibabu kulingana na ugonjwa alionao kuliko kulingana na aina ya kifurushi alichonacho?

Au chukulia hili la kuweka ukomo wa mwanachama kuwaingiza wanaomtegemea. Kwa mujibu wa sheria, mteja ana fursa ya kuingiza wategemezi wane ambao ni lazima wawe ni watoto, mke/mume na wazazi.

Lakini tunafahamu kwamba wategemezi kwa Watanzania wengi wanaotoka kwenye familia kubwa (extended families) siyo lazima watoke kwenye makundi hayo. Unaweza ukakuta mtegemezi wangu mimi ni shangazi yangu au ni bibi yangu.

Hivi ni vitu vya kawaida sana kwenye familia nyingi za Kitanzania. Muda mwingine mtegemezi wako anaweza asiwe ni ndugu yako wa damu kabisa.

Huu ni utaratibu mbaya ambao unahitaji kubadilishwa ili kuwawezesha wanachama kuwa na uhuru wa kuweka wategemezi ambao kweli ni wategemezi wao na si watu ambao wanalazimika tu kuwaweka kukidhi matakwa ya kisheria japo hawahitaji msaada wake.

Ukiachana na malalamiko haya ya kimfumo, wanachama pia wanalalamika kukosa matibabu wanapokwenda hospitali, huku wakiambiwa kwamba tatizo walilonalo bima yake haiwezi kutibu. Wengine wanalazimika kutumia fedha zao za mfukoni kulipia huduma ambazo zinapaswa kushughulikiwa na bima zao.

Ni muhimu sana malalamiko haya yakafanyiwa kazi ili NHIF iwe kweli ni mfuko wenye lengo la kutoa huduma za kiafya kwa Watanzania kwa gharama ambazo wananchi wanaweza kuzimudu.

Tutafakari upya utoaji huduma za afya 

Kimsingi, wananchi ambao wanafanya kazi ya kujenga taifa na kulipa kodi zinazoendesha shughuli za Serikali yao hawapaswi kutozwa pesa pale wanapougua ili waweze kupata matibabu.

Hivyo, ni muhimu kwa Serikali kuanza kufikiria ni kwa namna gani inaweza kufanikisha hilo kwa kuwapatia wananchi wake bima za afya bila ya uwepo wa gharama yoyote.

Kama ilivyo ni wajibu wa Serikali kuelimisha watu wake ili waweze kutoa mchango stahiki katika ujenzi wa taifa, vivyo hivyo Serikali inapaswa kuwajibika na kuwatibu watu wake pale wanapoogua ili wapone warudi kwenye shughuli za ujenzi wa taifa.

Wako watu ambao wanaweza kudai kwamba Serikali kutoa huduma za afya bure kwa watu wote ni jambo ambalo haliwezekani kwa nchi kama Tanzania.

Kujaribu kujibu wasiwasi wao, naweza tu kuwasihi watu hawa kwenda kuangalia ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia ni fedha kiasi gani za walipa kodi zimetafunwa hiholela bila ya kuwepo kwa uwajibikaji wowote.

Tunaweza kuwa na fedha na kufanyia ufisadi lakini tukakosa fedha za kutibia watu wetu, watu ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu!

Pia, ni muhimu kutambua kuwa kutoa huduma za afya bure kwa wananchi hakutowezekana endapo kama tutaendelea kuangalia ugonjwa wa watu kama chanzo cha kujitengenezea faida binafsi.

Hii yote maana yake ni kwamba ili kuweza kufanikisha lengo la kuwapatia watu wetu huduma bora za afya bila ya gharama yoyote kwanza ni muhimu kuhakikisha usimamizi mzuri wa pesa za walipa kodi ili zisifisidiwe.

Lakini pia, ambalo ni muhimu zaidi, ni kubadilisha namna tunavyotazama mambo, labda kwa kutanguliza huduma mbele kabla ya faida.

Nassoro Kitunda ni mhadhiri msaidizi wa sosholojia, Mwenge Catholic University. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts