The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Wahimiza Ufikishwaji Elimu ya Uzazi kwa Vijana Wenye Ulemavu

Wataalamu wanaonya kwamba endapo kama kundi hilo litaendelea kukwepwa kwenye elimu ya afya ya uzazi haki zao za msingi zinaweza zikawa hatarini kukiukwa.

subscribe to our newsletter!

Morogoro. Wadau wanaotoa uangalizi kwa kundi la wasichana na wavulana balehe wenye ulemavu wamebainisha kwamba kundi hili muhimu katika jamii limekuwa likisahaulika linapokuja suala la kuwafikia vijana balehe ili kuwapatia elimu ya afya ya uzazi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya jamii, afya ya uzazi kwa vijana wa rika la balehe ni muhimu mno kwani ni katika kipindi hiki ndipo vijana hukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mimba za utotoni, magonjwa, na utoaji mimba usio salama, ambapo bila elimu muhimu kutolewa zinaweza kuhatarisha maisha na ustawi wa mhusika.

Linda Ngido ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mehayo Centre for Disabled Young People, kituo kinachojihusisha na kuwapatia ujuzi na fursa vijana wenye ulemavu ambaye ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba hajawahi kuona wataalamu wa afya ya uzazi kutoka serikalini au kwenye asasi za kiraia kufika kituoni hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya afya ya uzazi.

“Kuna wakati ambao wasichana wanafikia umri wa kupata hedhi, ukimuelekeza binti mwenye ulemavu kuhusu kutumia vifaa vya kujistiri hawataki,” anaeleza Ngido ambaye ni mwalimu kitaaluma. “Wakati mwingine wanavitupa.”

Ngido haelewi ni kwa nini wadau hawajikiti kwenye kuwapatia vijana wa rika la balehe wenye ulemavu elimu ya afya ya uzazi wakati watu hawa pia ni binadamu kama walivyo watu wengine ambao hukua na kuanzisha familia zao.

“Watoto wenye ulemavu nilioanza kuwa nao kwenye kituo hiki, wavulana na wasichana, sasa hivi ni watu wazima, wameoana wenyewe na wana watoto wanasoma,” anaeleza Ngido ambaye alilazimika kuacha kazi yake ya ualimu kufanya kazi yake ya sasa. “Kwa hiyo, siyo kwamba hawa watu wenye hali hii hawawezi kuwa na familia. Hapana, wanaweza.”

The Chanzo ilitembelea kituo cha Erick Memorial Foundation for Education and Rehabilitation for the Disabled (EMFERD) kilichopo mkoani hapa kinachojihusisha na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.

Vijana wengi walio katika rika la balehe ambao ni walemavu waliopo kituoni hapa walikiri kwa The Chanzo kwamba hawajawahi kufikiwa na kupatiwa elimu ya afya ya uzazi, hali ambayo wanasema inawasononesha.

“Hii huduma tunaihitaji kwa sababu watu wenye ulemavu nao wana haki zote za msingi [kama vile ya] kuoa au kuolewa,” Benedict Mwenyasi, kijana mwenye ulemavu wa viungo kutoka EMFERD, aliiambia The Chanzo.  “[Wadau] sisi wanatusahau [kutupatia elimu hii].”

Wadau wanakubaliana kwamba ipo haja ya Serikali na wadau wengine wa afya ya uzazi nchini Tanzania kuweka mikakati na kuchukua juhudi za pamoja za kuhakikisha kwamba kundi hili nalo linafikiwa kwenye utoaji wa elimu ya uzazi nchini.

Moja kati ya wadau hawa ni Obed Mtagulwa, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Care Youth Foundation, shirika linalojihusisha na kutoa elimu ya uzazi kwa vijana rika balehe.

“Hizo sehemu wanazokaa watu wenye mahitaji maalum huwa tunaenda kwa ajili ya kutoa huduma ya misaada pekee yake, bado hatujafika kupeleka elimu ya uzazi,” anakiri Mtagulwa. “Kuna haja kubwa sana ya kuwapa elimu [watu hawa].”

Naye daktari bingwa wa afya ya uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dk Deodata Ruganuza ameonya kwamba endapo wadau hawataweka kipaumbele kwenye kuwapatia watu wenye ulemavu elimu ya afya ya uzazi haki za msingi za watu hao zitakuwa zipo hatarini kukiukwa.

“Tusipoweka kipaumbele katika hili kundi, [vijana walemavu walio katika rika balehe] watakuwa wanakosa kitu cha muhimu sana kwao na kwa familia zao watakazoanzisha,” Dk Ruganuza aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake.

John Kabambala ni mwandishi wa kujitegemea kutoka Morogoro, anapatikana kupitia kabambalajohn@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *