Azali wa Comoro Anavyoendelea Kumdhibiti Rais wa Zamani Sambi Kifungoni

Utulivu wa kisiasa visiwani humo litakuwa ni suala linaloendelea kupewa kipaumbele na jirani yake Tanzania pamoja na SADC ambao Comoro pia ni mwanachama.

subscribe to our newsletter!

Nchi ya Comoro, ambayo ni muunganiko wa visiwa mbalimbali, imo katika mtanziko mkubwa wa kisiasa ambao, pamoja na mambo mengine, umesababishwa na madai ya wapinzani nchini humo kwamba Rais aliyepo madarakani, Azali Assoumani, anabana demokrasia.

Mgogoro huo wa kisiasa unachagizwa zaidi na hatua ya Azali kumuweka kizuizini Rais wa zamani wa nchi hiyo Ahmed Abdallah Mohamed Sambi, huu ukiwa ni mwaka wa nne sasa tangu Azali achukue hatua hiyo inayoendelea kusababisha taharuki nchini Comoro.

Uamuzi huo wa Azali, aliyeingia madarakani mwaka 2016, ulikuja licha ya ukweli kwamba Sambi, na maafisa wengi kutoka kwenye chama chake, walimuunga mkono Azali kwenye kinyang’anyiro cha urais, hatua iliyokaribia kukipasua chama hicho.

Hii ilitokana na ukweli kwamba baadhi ya maafisa kutoka kwenye chama cha Sambi walikuwa na mashaka kwamba Azali, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Taifa, aliyetwaa madaraka kwa mara ya kwanza kwa njia ya mapinduzi mnamo mwaka 1999, angekuwa kitisho kwa utawala wa sheria.

Huenda hawakukosea sana. Baada tu ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Comoro, Azali alianza kuzidhibiti taasisi za dola, ikiwemo Mahakama, ikiwemo ni pamoja na kuzuia kazi zote za  Mahakama ya Katiba na kupiga marufuku maandamano.

Kiongozi huyo amejiimarisha zaidi madarakani baada ya  kura ya maoni iliyoitishwa mnamo Julai 2019 na kususiwa na upinzani. Tume ya Uchaguzi aliyoiteuwa mwenyewe ilitangaza kura hiyo imekubali mabadiliko yaliopendekezwa na Rais Azali.

Kimsingi, madaraka yake yalikuwa yamalizike 2021 lakini baada ya ushindi wake uliotarajiwa kutokana na mazingira yaliojitokeza, akajiunga na mtindo mpya uliozuka barani Afrika wa viongozi kubadili Katiba muda wao unapokaribia ili wabakie madarakani.

Azali ameufuta utaratibu wa Rais wa Umoja wa visiwa hivyo  kuwa wadhifa unaozunguka baina ya visiwa vitatu: kisiwa kikuu Grande Comores (Ngazija), Anjouan (Nzuwani), kisiwa cha pili kikuu, na kile kidogo cha Moheli (Mwali) ambapo mwaka 2021 ingekuwa zamu ya Anjouan.

Sambi anatoka kisiwa cha Anjouan na kutokana na umaarufu wake wengi wakiamini kwamba akama angegombea tena basi angeshinda. Rais Azali anadai kwamba mfumo wa kila kisiwa kuwa na Rais wake na halafu Rais wa  Dola, ni gharama isiyo ya lazima katika nchi ambayo ni masikini. Badala yake kuweko tuna gavana atakayesimamia shughuli za utawala.

Azali aliwabadili magavana wa visiwa mara baada ya mabadiliko ya Katiba ya 2018 na kuwateuwa wafuasi wake. Wadadisi wanasema  alikuwa hasa anamlenga gavana wa Anjouan Dk Salami Abdou, mtu wa karibu sana na Rais wa zamani Sambi.

Wakati Sambi alipokamatwa  na kuwekwa kizuizini, hatua sawa na hiyo ikamkumba Dk Salami ambaye tangu wakati huo naye anazuiliwa katika gereza la kikosi maalum cha polisi (Gendermerie) huko Anjouan.

Dk Salami aliyechaguliwa kwa kishindo mwaka 2016 alikuwa akitarajiwa kugombea Urais 2021 na kushinda pindi Sambi asingegombea. Wapinzani wa Azali wanasema hatua ya kumuweka korokoroni ni kumdhibiti baada ya kukataa kujiunga na Serikali yake.

Wanasiasa kadhaa waliokuwa katika Serikali ya Sambi wamempa kisogo na kujiunga na Azali, akiwemo aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Ahmed Jaffar ambaye  baada ya kushika kuongoza wizara kadhaa katika Serikali ya Azali sasa ni balozi wa  Comoro nchini Senegal.

Azali anavyowagawa wapinzani

Pamoja na yote, mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani humo hauelekei kumtia hofu Rais Azali. Sababu kubwa ni  kwamba wapinzani wake wamegawanyika sana kuanzia ndani hadi nje.

Miongoni mwa wapinzani wa ndani ni pamoja na makamu wa rais wa zamani katika  Serikali ya  Dk Ikililou Dhoinine, Mohamed Soilihi, na aliyekuwa Gavana wa Grande Comores, Moigne Baraka. Soilihi ndiye alishindana na Azali katika duru ya pili ya uchaguzi 2016.

Wapinzani walioko nje wakipiga kambi mjini Paris nao wamekumbwa na mivutano. Kundi kubwa miongoni ni lile linalojiita ‘Dola ya Haki.’ Kundi hilo linapigania kurejeshwa kwa demokrasia na utawala bora nchini mwao. Sambamba na hayo kuna Serikali mbili zilizoundwa uhamishoni.

Azali ameutumia mchafukoge huo kuonyesha  kwamba wapinzani hawafai. Katika kile kisichotarajiwa, Azali alitoa msamaha kwa aliyekuwa Makamu wake wa Rais Jaffar Ahmed Said Hassani aliyekimbilia uhamishoni baada ya kuupinga mpango wa Azali kubadili Katiba ili abakie madarakani.

Tangu aliporejea nyumbani, Said Hassani amebakia kimya kama alivyokuwa uhamishoni.

Raia walioko ndani nao wana maoni tafauti. Wale wanaomuunga mkono Azali wanadai anapaswa kuendelea ili kuvunja ule utamaduni wa kuwa na wanasiasa wale wale wenye tabia ya kujikomba kwa Serikali, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa maendeleo.

Wanaompinga nao wanamshutumu kuwa alikiuka misingi ya kidemokrasia na utawala bora na sasa anatawala kidikteta.

Kongamano la mageuzi

Mnamo mwezi Machi 2022, Azali aliandaa Kongamano la Kitaifa la siku 28 kujadili mustakbali wa  visiwa vya Comoro, lakini  kwa mara nyengine likasusiwa na vyama vya upinzani.

Hata hivyo, kuna walioshiriki kwa jina la upinzani kutoka Comoro na nchi za nje, ikiwemo Ufaransa, ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wake waliovaa sare za upinzani. Yaliopitishwa katika kongamano hilo  yanatoa sura ya kuhakikisha Azali anadhibiti madaraka.

Mapendekezo hayo yatajadiliwa na Bunge, katika kile kinachoonekana kitakuwa ni kuyapitisha bila kupingwa kwa kuwa mhimili huo wa utungaji sheria unadaiwa kudhibitiwa na wanaoiunga mkono Serikali.

Miongoni mwa yaliyomo katika waraka huo ni nafasi ya Tume ya Uchaguzi ambayo wajumbe wake watakuwa wakichaguliwa kama kawaida na Rais na kusimamiwa na wizara ya mambo ya ndani.

Kuanzia sasa lakini nguvu za tume zinaimarishwa na kuwa na mamlaka ya kuteuwa mawakala katika vituo vya uchaguzi, ikiwa na maana hakutakuweko na mawakala wa vyama.

Kwa mujibu wa wadadisi, ilitegemewa kongamano hilo lingekuwa jukwaa la upatanishi wa taifa ikiwa ni pamoja na kuachiwa huru wafungwa kisiasa akiwemo Rais wa zamani Sambi lakini hilo halikutokea.

Je, visiwa hivyo vimejifunza?

Hali ya kisiasa katika visiwa hivyo inazidi kutokota. Bado viko mbali na kujifunza janga lililovikumba la mivutano ya kisiasa, yakiwemo mapinduzi na majaribio kadhaa ya mapinduzi tokea vilipojitangazia uhuru kutoka kwa mkoloni Ufaransa mwaka 1975.

Kuna wanaoamini matukio hayo yana mkono  wa nguvu ya kisiasa ya mkoloni wa zamani anayeendelea kukikalia kisiwa cha nne, Mayotte, kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa  na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla, ikiwemo Umoja wa Afrika.

Ufaransa inadai wakazi wa Mayotte wameamua kuwa sehemu ya Ufaransa.

Wafuasi wa Sambi, aliyesoma Iran na Saudi Arabia, wanasema kujitenga kwake na Ufaransa na kuziegemea nchi za Kiarabu ni sababu moja wapo ya kuadhibiwa na Azali anayetajwa kuwa kipenzi  cha Ufaransa.

Sambi alipokuwa madarakani alisimama kidete na kuzusha suala la kisiwa cha Mayotte mbele ya hadhara kuu  ya Umoja wa Mataifa.

Juhudi za upatanishi

Juhudi za Umoja wa Afrika (AU) kujaribu kuutafutia suluhisho mgogoro mpya wa kisiasa kati ya Rais Azali na wapinzani wake mpaka sasa hazijafanikiwa, huku Azali akiashiria kwamba atakuwa tayari kuzungumza moja kwa moja na  wapinzani ambao wanasisitiza mazungumzo yoyote lazima yaongozwe na mpatanishi.

Ujumbe wa AU, ukiwemo ule ulioongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Algeria, Ramtane Lamamra, aliojaribu kuleta suluhu visiwani humo, ulirudi Addis Ababa ukiwa mikono mitupu.

Mnamo Agosti  2021, Rais Samia Suluhu Hassan alimtuma Rais wa zamani Jakaya Kikwete kwenda Moroni akiwa na ujumbe maalum kwa Rais Azali, ikisemekana ulihusiana na hali ya kisiasa na ombi la kutaka Rais wa zamani Sambi aachiwe huru.

Hakuna kilichoelezwa baada ya Kikwete kuwasilisha ujumbe huo.

Tanzania, nchi iliyoshiriki katika zoezi la kukikomboa kisiwa cha Anjouan kilipotangaza kujitenga, itakuwa inafuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa yanavyoendelea visiwani Comoro.

Kushiriki kwa Tanzania kijeshi kulifuatia ombi la Rais Sambi ambaye ni kutoka Anjouan. Sambi alisisitiza hatokubali kwamwe kusambaratika kwa umoja wa visiwa hivyo.

Utulivu wa kisiasa visiwani humo litakuwa ni suala linaloendelea kupewa kipaumbele na jirani yake Tanzania, AU na Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambao Comoro pia ni mwanachama.

Haifahamiki Sambi atabakia kizuizini kwa muda gani zaidi. Lakini kinachojulikana ni kwamba Rais Azali amejizatiti kubakia madarakani angalau mpaka 2030.

Mohamed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Anuani yake ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia Twitter @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts