Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kwamba kuanzia Julai 1, 2022, Serikali itaanza kutoa ruzuku ya mbolea za viwandani kwa wakulima wa mazao yote nchini ili kupunguza maumivu kwa wakulima hao yaliyotokana na kupanda kwa bei za mbolea, hususani katika msimu wa kilimo wa 2021/2022.
Bashe aliyasema hayo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2022/2023 ambapo Serikali inatarajia kutumia Shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku, sawa na asilimia 20 ya matumizi yote ya wizara ambayo ni jumla ya Shilingi bilioni 751.1.
“Heri tusifanye jambo lolote, lakini tulinde wakulima wetu na uchumi wetu,” Bashe ameliambia Bunge hii jana, Mei 17, 2022. “Utaratibu wa namna ruzuku hizo zitakavyotolewa utawekwa wazi wakati wa uwasilishaji wa bajeti kuu.”
Kupanda kwa bei ya mbolea
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022, wakulima walinunua mbolea za kukuzia kama UREA kwa Sh110,000 kutoka Sh50,000 msimu wa 2020/21, huku mbolea nyingine za kupandia kama DAP ikinunuliwa kwa Sh120,000 kutoka Sh60,000.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, katika msimu wa mwaka 2021/2022 hadi kufika Aprili 2022, jumla ya tani 436,452 za mbolea zilipatikana ambapo kati ya hizo ni tani 43,579 tu ndizo zilizalishwa nchini na kiasi kilichobaki kiliagizwa nje ya nchi.
Katika msimu wa mwaka 2022/2023, Serikali imesema inategemewa tani 650,000 za mbolea zitaagizwa kutoka nje ya nchi, hivyo kuwepo kwa uezekeano mkubwa wa bei za mbolea kuendelea kuathiriwa na bei za soko la dunia.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 2020 na mwaka 2022, bei ya mbolea kama ya UREA kwa tani moja zilipanda kutoka Dola za Marekani 251 hadi Dola za Marekani 1,214.
Hivyo, kutengwa kwa ruzuku kunaweza kusaidia kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya bei za mbolea kwenye soko la dunia, hivyo kuwanufaisha wakulima.
Kwenye wasilisho lake, Bashe amesema anatambua maumivu waliyopitia wakulima katika msimu huu wa kilimo, kitu kilichoifanya Serikali kuamua kutenga kiasi kikubwa cha fedha kitakachotolewa kama ruzuku ya mbolea.
“Niwape pole [wakulima] kwa maumivu waliyoyapata kwa msimu huu ulioisha kwa gharama za pembejeo kupanda,” alisema Bashe, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM). “Ninafahamu wamebeba mzigo mkubwa sana.”
Sehemu tu ya misaada
Ruzuku za pembejeo ni sehemu tu ya misaada ya Serikali kwa wakulima hususani wadogo ambao ndiyo wanaunda sehemu kubwa ya uzalishaji wa mazao nchini. Kwa sehemu kubwa ruzuku zimewezesha matumizi ya pembejeo za kilimo na hivyo kuongeza tija kwenye kilimo maeneo ambayo walengwa walinufaika nayo.
Katika vipindi tofauti kuanzia mwaka 2003/2004, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwenye kilimo kwa njia tofauti tofauti, ikiwemo mfumo wa ruzuku zilizohusisha Serikali kuingia mikataba na makapuni ya mbegu ili kuchangia gharama za usafiri na kugharamia sehemu ya bei za pembejeo, matumizi ya vocha na kutoa mikopo kwa ushirika na vikundi vya wakulima ili waweze kujipatia pembejeo.
Serikali imekuwa ikichukua hatua hizo baada ya kurudishwa kwa mfumo wa ruzuku za kilimo ambao awali uliondolewa miaka ya mwishoni mwa 1980 kutokana na masharti ya programu ya urekebishaji uchumi ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Katika kipindi cha mwaka 2008/2009 hadi 2010/2011 ilishuhudiwa Serikali ikitenga wastani wa takribani Shilingi bilioni 120 kwa ajili ya ruzuku ya kilimo iliyotolewa kwa njia ya vocha kwa wakulima waliochaguliwa kununua pembejeo kwa bei nafuu kisha mgavi wa pembejeo hubadili vocha kwa pesa taslimu toka serikalini au taasisi ya fedha iliyokubaliana na serikali.
Kiasi hiki kikubwa cha ruzuku kilisitishwa mwaka 2013/2014 baada ya wahisani kuacha kuendelea kuchangia, hivyo Serikali ikapunguza kiasi cha ruzuku na namna ya utolewaji wake.
Ufanisi mdogo
Hata hivyo, mfumo huu ulikosolewa kutokana na kuwa na changamoto nyingi, ikiwemo ufanisi mdogo uliopelekea vocha kutolewa kwa kuchelewa, wakulima kuuza vocha kutokana na kushindwa gharama za ziada, ubaguzi katika uchaguzi wa wakulima waliopewa vocha kwani zoezi hili lilitumiwa kama njia ya viongozi wa ngazi za chini kulipa fadhila au kuwaadhibu mahasimu wao wa kisiasa.
Hii ni licha ya ukweli kwamba mfumo huu ulileta mafanikio mengi ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula nchini (mahindi na mpunga) katika kipindi cha mwaka 2008/2009 mpaka 2010/2011
Pia, mfumo huu ulikuwa na mapungufu yaliyopelekea kuwanufaisha zaidi wakulima wachache ambao tayari walikuwa na hali nzuri kiuchumi, rushwa za wazi wazi pamoja na kuyapa nguvu makampuni makubwa kuwa na udhibiti wa mnyororo wa thamani wa pembejeo za kilimo.
Katika hotuba yake bungeni, Bashe amesema ruzuku hii siyo ya kudumu bali itatolewa kwa kipindi maalum, hususan wakati yanapotokea majanga au mdororo wa kiuchumi.
Kauli hii bado inaibua maswali mengi kutokana na ukweli kwamba bado Serikali haija ainisha ni kwa namna gani ruzuku hizi zitatolewa ili kuwasaidia wakulima nchini ambao kwa kauli yake Bashe amekiri kuwa wameumizwa sana na bei za mbolea msimu huu.
Ingawaje haijasema ni njia gani itatumika hadi hapo bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2022/2023 itakaposomwa bungeni, wadau wanahimiza Serikali kushirikiana na wahusika na kuwasikiliza wakulima wadogo ili iweze kuwa na picha halisi ya changamoto zilizojitokeza katika mifumo iliyokuwa ikitumika huko nyuma.
Hii itasaidia fedha zinazotolewa kuwanufaisha wakulima wengi, hususani wakulima wadogo ambao wanatajwa kuwa ndiyo sehemu kubwa ya uzalishaji wa mazao chakula na biashara nchini.
One Response
Asante waziri Bashe Kwa kutukumbuka wakulima wadogo.