The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania

Hatua kubwa kati ya hizi ni utashi wa kisiasa kutoka kwa watu waliopewa dhima ya kuendesha nchi.

subscribe to our newsletter!

Kitajwapo Kiswahili, itambulike kuwa inatajwa moja kati ya lugha chache duniani zenye hadhi ya kimataifa. Jambo la kuzingatia ni kwamba Kiswahili ndiyo lugha pekee ya asili ya Afrika inayoiwakilisha Afrika kimataifa. Hapa ndipo unapoonekana ulazima kwa Tanzania kuitumia lugha hii katika kiwango cha juu zaidi kuliko nchi yoyote duniani.

Kwa namna yoyote ile, Tanzania kwa sasa ndiyo nchi inayonasibiana kwa ukaribu zaidi na Kiswahili. Unasaba huu si tu wa kukitumia zaidi Kiswahili, bali pia kule kukitumia kwake kwa ufasaha na usanifu zaidi. Kwa mnasaba huu, Tanzania inapaswa kukitendea haki zaidi Kiswahili kuliko mataifa mengine.

Lugha ndiyo chombo kikuu cha kuenezea maarifa. Dunia imetudhihirishia kuwa ukitaka maendeleo ya haraka na endelevu, tumia lugha yako kuingiza maarifa katika akili za raia wako. Jamii itumiapo lugha ya kigeni katika kuchota maarifa yao, inatengeneza makasuku.

Kukariri kwao kutazidi kiwango cha ubunifu wao. Hii ni kwa sababu, ubunifu ni zao la maarifa, maarifa ambayo hupatikana kwa kufahamu. Unapomfundisha mtu kwa ulimi (lugha) wake atakielewa anachofundishwa katika kiwango cha juu zaidi.

China, Utaliano, Ufaransa, Ureno, Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yaliyoudhihirishia ulimwengu kuwa maendeleo bora hutokana na namna unavyoitumia lugha ya taifa kama chombo rasmi cha kuchotea taaluma na maarifa yatokanayo na malengo ya taifa kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na hata kijamiii na kidiplomasia.

Hapa tunakutana ana kwa ana na ukweli kwamba umeshafika wakati wa kufanyiwa kazi mikakati ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia Tanzania. Jambo zuri zaidi ni kwamba tafiti nyingi zimefanywa na wataalamu na taasisi kubwa za Kiswahili zinazoonesha umuhimu wa jambo hili na kupendekeza njia za kuliendea na kulikamilisha.

Kila lugha ni bora katika kufundishia

Je, kila lugha inapaswa kuwa lugha ya kufundishia? Hapa kuna jambo kubwa la kuzingatia. Wapo wanaotumia kasumba kuwa si kila lugha inapaswa kuwa lugha ya kufundishia ili kudhoofisha uwezo wa Kiswahili wa kubeba dhima hiyo.

Pamoja na kwamba Kiswahili kimeshaonesha chenyewe uwezo wake huo na kushinda hila za kasumba hii, bado ipo haja ya kufahamu kitaalamu juu ya dhana ya lugha kuwa lugha ya kufundishia.

Utaalamu na uzoefu unaonesha kwamba kila lugha ni bora zaidi katika kufundishia taaluma na maarifa ya jamii zawa ya lugha hiyo. Wasichokifahamu wengi ni kwamba kiwango cha taaluma na kitakachofundishwa kitategemea mipaka ya lugha hiyo.

Vifungu hivi vinne vinaonesha namna lugha inavyojipambanua kutumiwa katika kufundishia kulingana na mipaka na mawanda yake:

Lugha ya kikabila itakuwa lugha bora zaidi kufundishia mila, desturi, amali, fasihi, silka na utamaduni wa kabila husika. Yaani, Kinyamwezi ni lugha bora zaidi kufundishia unyamwezi; Kisukuma – Usukuma; Kizigua – Uzigua na nyenginezo katika mfano huo.

Lugha inapokuwa ya taifa itakuwa lugha bora zaidi kufundishia taaluma zinazohusu malengo ya taifa husika. Lugha hii hutumika katika kufundishia mtaala rasmi wa elimu.

Lugha inapokuwa ya kimataifa itakuwa bora lugha hiyo kufundishiwa jamii yake maarifa na taaluma za taifa lao na mataifa mengine. Yaani, mtaala wa taifa na maarifa ya kigeni.

Lugha ikiwa rasmi itakuwa bora lugha hiyo kutumika katika kila mfumo rasmi wa taifa, hususan katika mfumo wa elimu na uendeshaji wa shughuli rasmi za nchi.

Je, kwa Tanzania, Kiswahili tunakiweka katika fungu lipi kati ya hayo? Ukiweka nadharini utagundua kuwa Kiswahili kimeifungulia Tanzania mipaka na mawanda yake yote kwa asilimia 100. Ni lugha ya taifa, lugha rasmi, lugha ya kimataifa. Wapi kuna upenyu wa kutokea katika ulazima wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia?

Tunaweza kuwa na ukakasi kidogo pale tunapoona hadi sasa mapendekezo ya wataalamu wa lugha na elimu, taasisi za Kiswahili, vyuo vikuu, wanasiasa na wadau wa elimu ya kikifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu, hayajatiwa maanani na mamlaka husika. Je, hatuna imani na wataalamu na taasisi zetu?

Hoja dhidi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia

Zipo hoja kadhaa zitolewazo na baadhi ya wataalamu na wadau wengine zinazodai kuwa Kiswahili hakina uwezo wa kuwa lugha ya kufundishia.

Baadhi ya hoja hizo ni utoshelevu mdogo wa lugha kimsamiati na kitaaluma; umuhimu wa lugha ya Kiingereza kama lugha kuu ya kimataifa; mitaala na vyanzo vyengine vya maarifa hasa ya masomo ya sayansi ni ya Kiingereza pamoja na sababu nyengine nyingi.

Lakini kimsingi hoja hizi hazina mashiko thabiti. Hivi nchi kama China, Korea, Ureno na nyenginezo zinazotumia lugha zao kufundishia zimewezaje kuwa na manufaa makubwa katika sayansi na teknolojia?

Suala la umuhimu wa Kiingereza halipingiki. Ila umuhimu wake ni katika mawasiliano zaidi. Jambo ambalo halitegemei ulazima wa lugha hiyo kutumika kufundishia.

Tunao wataalamu na wazungumzaji wengi wa lugha za kigeni: Kiarabu, Kijerumani, Kireno na hata Kihispaniola wakati hatutumii lugha hizo kufundishia.

Kutumiwa kwa lugha ya Kiswahili kufundishia hakudumazi lugha ya Kiingereza endapo kama kutakuwa na mikakati imara katika ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kama moja ya somo la lazima kwa ngazi ya msingi na sekondari.

Mitaala na maandiko (vitabu) ya masomo kuwa katika lugha ya Kiingereza ni suala la kuandaa tu mkakati imara wa kutafsiri vyanzo hivyo vya maarifa ya kielimu kwa Kiswahili.

Madai ya Kiswahili kutojitosheleza

Bila ya shaka Kiswahili kinajitosheleza kwa ukamilifu wake kuwa lugha ya kufundishia.

Kiswahili kina msamiati wa kutosha. Kinatumika katika vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa (BBC, DW, VOA, Sauti ya China, Sauti ya Japan). Kiswahili ni lugha rasmi katika jumuia za kimataifa (AU, EAU, SADC, UNESCO). Kiswahili kinatumiwa katika shughuli za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kitaaluma na kidiplomasia ndani na nje ya bara la Afrika.

Kiswahili kina maandiko mengi yanayosomwa ndani na nje ya Afrika. Ni lugha inayowaunganisha Waafrika. Kiswahili kinafundishwa katika ngazi zote za elimu kwenye skuli na vyuo mbalimbali duniani. Kiswahili kimataifa kina hadhi ya juu kuliko Kichina na Kitaliano, ilihali lugha hizo hutumiwa kufundishia katika mataifa husika.

Ukitanabahi hadhi na uwezo huu wa Kiswahili utapata wapi ujasiri wa kusema Kiswahili hakina utoshelevu wa kuwa lugha ya kufundishia? Hii ni dhima ndogo sana miongoni mwa dhima zinazoweza kubebwa na lugha ya Kiswahili. Kiswahili kimeshajibainisha hivyo. Labda tuseme uzungu umetukabili katika kila nyanja.

Yapo madai kuwa baadhi ya dhana za kitaaluma, hususan za masomo ya Sayansi, Biashara na Geografia hazielezeki kwa Kiswahili. Madai haya hayana mashiko. Dhana zenyewe zinazodaiwa hazielezeki kwa Kiswahili zinahitaji ufafanuzi katika lugha hiyo hiyo inayodaiwa kuwa ndio msingi wa masomo hayo!

Jambo la msingi hapa ni kuwa hakuna dhana hata moja isiyowezekana kufafanuliwa kwa lugha yoyote ile kwa matlaba ya kupata maarifa juu ya dhana hiyo. Ingawa kwa upande mwengine zipo baadhi ya dhana chache ambazo hazina istilahi za Kiswahili. Hii ni kwa sababu hatujaamua kuziundia istilahi.

Kiswahili kina kanuni kadhaa za uundaji wa msamiati na istilahi. Ni kuamua tu kuwatumia wataalamu wetu kuziundia dhana hizo istilahi za Kiswahili. Kwa zile dhana zitakazoshindikana kuundiwa msamiati wa Kiswahili fasaha, mbinu ya utohoaji inaweza kutumika kama iliovyo katika istilahi fizikia, kemia, elementi, oksijini, kompyuta nakadhalika.

Ukiangalia dhana kama fasihi, tamthiliya, riwaya, hadithi, tarikhi, sarufi, lughawiya, tamathali, ubeti, mizani, tashbiha, sitiari, tash-hisi, mubalagha, takriri, tanakali na nyingi nyenginezo ni istilahi za taaluma ya lugha ya Kiswahili lakini zinatokana na lugha ya Kirabu.

Je, hatuzifafanui kwa lugha ya Kiswahili? Kwa nini hatufundishi fasihi ya Kiswahili kwa kutumia Kiarabu kwa vile istilahi zake nyingi zinozorejelea dhana mbalimbali ni za Kiarabu?

Utashi wa kisiasa

Kuhusu Kiswahili kujitosheleza kuwa lugha ya kufundishia na umuhimu wake kwa taifa, ni jambo lisilo na kigugumizi. Halikadhalika, madhara ya kitaaluma, kifikra na kimaendeleo yatokanayo na matumizi ya lugha ya kigeni katika ufundishaji na ujifunzaji yapo wazi.

Ni vyema kuondoa ukakasi katika kutumia lugha yetu kufundishia mtaala wa elimu yetu. Hizi zinaweza kuwa hatua muhimu zilizobaki ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu.

Kwanza ni suala la umuhimu wa utayari wa kisiasa. Jambo lolote hufanikiwa kwa haraka ikiwa lina mwamko thabiti wa kisiasa.

Baadhi ya wajumbe wa mamlaka za kisiasa, hususan mamlaka ya bunge, mara kwa mara wamekuwa wakitahadharisha juu ya athari za kutumia Kiingereza katika kufundishia, huku wakizishauri mamlaka zenye maamuzi katika elimu kuona umuhimu wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia.

Hata hivyo, bado mawazo na fikra zao hazijatiliwa maanani. Tunaamini kuwa utayari wa mamlaka za kisiasa ni hatua muhimu miongoni mwa hatua zilizobaki ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia.

Wizara inayoshughulikia elimu, pamoja na taasisi zake, zina nafasi kubwa katika kuamsha ari ya mwamko wa kisiasa ili Kiswahili kitumike kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.

Kufanyia kazi mapendekezo ya wataalamu

Jambo jengine ni umuhimu wa kuyafanyia kazi mapendekezo ya wataalamu na taasisi

kuhusu umuhimu wa lugha ya Kiswahili kutumiwa katika kufundishia.

Kwa kupitia ripoti za tafiti zao na maazimio yaliyotolewa katika makongamano mbalimbali ya vyama vya Kiswahili ndani na nje ya nchi, twaweza kupata vyanzo imara vitakavyosaidia katika utekelezaji.

Hakuhitajiki tena tafiti wala ukusanyaji wa maoni. Kilichobaki sasa ni kuamua tu kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo ya wataalamu na wadau hao kama njia muafaka ya kuanzia ili mchakato huu ukamilike.

Hatua hii itapaswa kuenda sambamba na na kutafsiri vyanzo vya maarifa kutoka Kiingereza kwenda kwenye Kiswahili. Ni vigumu kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia huku mitaala, mihutasari, vitabu na vyanzo vyengine vimeelezwa kwa Kiingereza.

Vyanzo hivi vinapaswa kutafsiriwa kwa Kiswahili ili kila dhana na ufafanuzi wake uwepo katika lugha lengwa. Wizara husika kupitia Taasisi ya Elimu inaweza kuandaa mradi maalumu ili kukamilisha hatua hii.

Taasisi inaweza kuandaa kikosi kazi kitakachoshirikisha wataalamu na wadau kutoka taasisi za Serikali, taasisi binafsii na hata wataalamu wa kujitegemea (wasio na taasisi).

Hawa ni pamoja na waandishi wa vitabu, wataalamu wa mfumo wa elimu, walimu, taasisi na vyama vya Kiswahili pamoja na watalamu wa Kiingereza na Kiswahili waliyojaa nchini Tanzania.

Jopo hili litakuwa na kazi ya kutafsiri vyanzo vya maarifa kwa Kiswahili baada ya mpango madhubuti kuratibiwa na mamlaka husika.

Ni muhimu kukatolewa mafunzo maalumu kwa walimu ili kujiandaa vyema kabla ya mpango huu kuanza kutumiwa rasmi darasani. Kadhalika, mpango unaweza kuanza kutekelezwa kwa ngazi ya sekondari ya awali (kidato cha 1 na 2) kabla ya kwenda juu zaidi, ingawa mpango wenyewe utakuwa umekamilika kwa ajili ya ngazi zote.

Katika hatua ya awali tunaweza kuhusisha baadhi tu ya masomo kama vile Civics, History, Geography, Maarifa ya Dini na masomo ya biashara kabla ya masomo ya Sayansi na Hisabati. Matokeo ya utekelezaji huo yatatoa dira angavu ya kuendelea na madarasa ya juu na masomo yote kwani yataonesha mafanikio na changamoto zake na hivyo kufanyiwa kazi kabla ya kuendelea kwa ujumla wake.

Penye nia pana njia

Waswahili husema penye nia pana njia. Kama suala la Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia litatiwa maanani ipasavyo na kuratibiwa kitaalamu, bila shaka linawezekana pasi na ukakasi wowote.

Ni muhimu kuzingatia kuwa uzalendo, uelewa, umahiri na ubunifu hutokana na maarifa waliyonayo raia wa taifa husika.

Marifa yakitolewa kwa lugha ya taifa husika, maarifa hayo yatapatikana kwa urahisi na kwa kiwango stahiki. Yakipatikana hayo ni rahisi sana kwa taifa kusonga mbele kwa haraka katika mafanikio si tu ya kijamii bali hata ya kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia.

Vyenginevyo tutabaki kwenye mitatago. Waswahili wanayo misemo maarufu ikiwemo ule usemao mkataa kwao mtumwa, au taifa lisilozingatia utamaduni wake ni taifa butu, au mcheza kwao hutunzwa.

Tuspozingatia ukweli na umuhimu uliyofumbatwa katika mbavu za kauli na semi hizi, bila shaka tutakuwa tunageukia msemo usemao nabii hakubaliki kwao.

Leo tunashuhudia mataifa ya ughaibuni yanavyojifunza kwa juhudi zote lugha ya Kiswahili kwa kutambua thamani yake. Madhara ya kutothamini cha kwetu na hatimaye kikathaminiwa na wengine yameanza kuonekana na yatashuhudiwa zaidi katika vipindi vijavyo vya maisha.

Hapo ndipo tutakapoinamisha vichwa kusikitika na kukiri kuwa majuto ni mjukuu daima huja mwishoni. Inatosha sasa kutanabahi kuwa tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Hivyo, ni vyema kuupatiza udongo ungali maji!

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *